Muonekano wa Giza:

Msaada

Angel - Sehemu ya Ishirini na Nne (24)

Kuanzia siku hiyo geto hilo likawa limeota meno!
Hakuna alierudi tena walikwenda moja kwa moja!

Angel baada ya kukoswa koswa tena kwa mara ya pili katika balaa hakutamani tena kuchepukia popote.
“Nitatembea mpaka kunakucha, siingii popote.”
Alijisemea.
Aliendelea kukata mitaa wakati huo ikiwa imetimu saa kumi kamili alfajiri.
Tayari majogoo yalianza kuwika majumbani mwa watu kuashiria sasa utawala wa giza unakaribia kikomo.
Angel bado aliendelea kuranda randa huku akijitahidi kukwepana na walinzi wa mji.
Hatimae mwenyezi Mungu alisaidia.
Mwanga wa jua ukamkuta Angel akiwa salama salmini.
Angel mwenyewe hakuamini.
Kwanza alitafuta sehemu iliyotulia akapiga magoti na kusali akimshukuru muumba wake kwa kuufanya usiku huo uliokuwa na mabalaa ya kila aina kumwacha akiwa salama japokuwa kapitia magumu na hatarishi mno usiku huo.

Saa 2:00 asubuhi.
Bado Angel aliendelea kuranda randa mitaani pasipokuwa na ramani yoyote kichwani yaani ilimradi tu alikuwa akizurura na begi lake mgongoni.
Mara...
Anakutana na mama mmoja hivi akiwa kajitwisha kapu la karanga kichwani kwake.
Huku mkononi akiwa na kifuko kidogo alichobebea karanga chache za kuonjesha.
“Shikamoo!”
Alimsalimia kwa heshima zake zote.
“Marahabaa! Haujambo?”
Yule mama akaitikia kwa uchangamfu wa hali ya juu!
“Sijambo mama.”
“Karibu ninauza karanga!”
“Asante sana.”
Angel alijibu huku akitua begi lake kana kwamba alikuwa anataka kununua.
Yule mama akataka kumchotea karanga tatu za kuonja ili amwonjeshe kwanza.
“Hapana mama wewe nipimie tu wala usihangaike.”
Basi yule mama akatua kapu lake wakati huo Angel akifungua begi lake na kulipekenyua kwa ndani ndani huko.
Anakumbuka kuna hela humo.
Akaiona...
Ilikuwa ni pesa ya muda mrefu sana, anakumbuka aliweka humo kipindi yupo Mbalizi na mama yake alikuwa bado yu hai.
“Shilingi ngapi kikombe?”
Akauliza bei.
“Ni shilingi mia tano tu.”
Akajibu mama huyo.
Angel akatoa hiyo mia tano kisha akapimiwa karanga zake bada ya hapo wakaachana na huyo mama huku akimuaga kuwa anawahi kwenye eneo la biashara.
Nae Angel akatafuta sehemu tulivu kwaajili ya kupata kifungua kinywa chake ambacho ni hizo karanga...

Wazo moja tu alikuwa nalo Angel kichwani kwake wakati anaendelea kula karanga zake.
Wazo hilo lilikuwa ni kufika ubungo tu, hata hakuwa na nauli aliamini iwapo angeomba msaada basi asingekosa.
“Nitaomba msaada wa lifti kwenye mabasi, mwenyezi Mungu atanisaidia watanipa lifti tu.”
Aliendelea kujiwazia hivyo Angel huku akiendelea kula karanga zake taratibu.
Sekunde ikazaa dakika, dakika nayo ikazaa saa moja, hatimae inatimu saa tatu kamili asubuhi.
Angel anamaliza kupata kifungua kinywa chake, anamshukuru Mungu kwa hilo, taratibu anabeba begi lake na kuainza upya safari ya kuitafuta stendi ya mabasi (Ubungo).
Hakutaka kujiuliza kwa mtu yeyote na hakutaka kuonekana ni kama mtu asie sawa.
Alijitahidi kujiweka kawaida sana ili asijulikane kama ni msafiri.
Na pia hakutaka kuishi Dar es salaam kwa kuhofia wenda siku moja angekutana na Rebeca.

Katika kuzunguka zunguka kwake alifanikiwa kukutana tena na yule mama muuza karanga.
“Hee! Mwanangu tumekutana tena?”
Akauliza mama huyo kwa uchangamfu.
“Hahaha.. Ndiyo nafikiri ni kutokana na mizunguko zunguko!”
Akajibu Angel kwa staili ile ya uchangamfu.
“Ni kweli kabisa.. Aah mi bado pia nazunguka zunguka lakini nakaribia kuzimalizia hizi karanga zimebaki kidogo.”
“Sawa.... sasa mama.”
“Oooh.”
“Hapa njia ya kutokea Ubungo wapi maana mi ni mgeni na huu mtaa.”
“Ahaa.. Pita hapa hiviii mpaka palee kwenye ile nguzo unaiona?”
“Ndiyo.”
“Ukifika pale kata kulia utakuta barabara ya lami hiyo itakupeleka mpaka ubungo sawa ee.”
“Nashukuru.. Ila si mbali?”
“Kuna haisi tele tu humo barabarani zitakufikisha.”
“Asante mama angu nashukuru sana.”
“Asante pia mwanangu.”
Wakaachana pale.
Angel akafuata maelekezo ya yule mama muuza karanga mpaka akafika barabarani.
Bado alikuwa na akiba yake ndogo ya pesa, akatoa kiasi kidogo cha pesa ambacho aliamini kingetumika kama nauli ya kumfikisha Ubungo akaishika mkononi pesa hiyo kwa uangalifu mkubwa sana.

Mda mfupi baadae ilitokea Haisi...
“Ubungo! Ubungo! Ubungo! Oraaaaaa!! Oya dada wapi jaa ndani twende.”
Alikuwa ni kondakta ndiyo alikuwa akiinadi kazi yake.
Angel alipanda haisi hiyo na safari ikaendelea.
Angel alijitahidi kuwa makini sana na kila mtu, alijua ni lazima Rebeca angemtafuta tu.
Akafika mpaka Ubungo ambapo alishuka yeye na abiria wengine wote waliokuwa wamesafiri na haisi hile kisha akalipa nauli kama ilivyo kawaida.
Wapiga debe nao walimwandama sana lakini hakutaka kuongea nao, majibu yake yalikuwa ni,
“Mimi sisafiri kwenda popote nipo hapa tu.”
Hilo ndiyo lilikuwa jibu lake…
Mwishowe wapiga debe hao waliamua kuachana nae.
Angel akatoka pale na kwenda kando hakutaka kampani na mtu yeyote.
Lengo lake lilikuwa ni kutafuta basi lililoandikwa DAR - MORO.

Sasa wakati ametoka pale anatembea kuelekea sehemu yanapopakiwa mabasi ya kwenda mikoni, kuna kitu alishtukia.
Kuna mwanaume alikuwa akimfuata nyuma nyuma huku asitake kuonesha dalili zozote kama alikuwa anamfuatilia.
Angel alimshtukia mtu huyo kwani takribani hatua karibia kumi hivi alikuwa akimfuatilia kwa nyuma ila si karibu sana.
Mkononi akiwa ameshika simu ndogo ya batani.
“Huyu mtu ananifatiliaa au najishtukia?”
Alijiuliza Angel huku akizidisha umakini nae pili hakutaka mtu huyo agundue kama amekwisha muona na alichokuwa anapania ni kumuuza ndani ya umati mkubwa wa watu na si vinginevyo.
Lengo la Angel lilifanikiwa...
Akafika sehemu kulikuwa na mlundikano wa watu ambao aliamini kama angejichanganya pale bila mwanaume huyo kumuona basi angekuwa amekwisha mpoteza.
Kabla ya kufanya hivyo kwanza alimtizama mtu huyo kwa macho ya wizi, akagundua muda huo alikuwa akibofya bofya simu yake mkononi.
Pale pale akajipoteza kwenye ule umati...
Baadae akazungukia upande mwingine na kurudi maeneo yale yale.
Alikuta yule mwanaume ameanza kuangaza macho huku na kule huku akiwa kaweka simu sikioni.
“Anapiga simu!”
Akajisemea Angel huku akizidi kumsogelea mwanaume huyo kwa nyuma akiwa na watu wengine kadhaa waliokuwa wakielekea upande huo.
“Ndiyo upo wapi?”
Alianza kuongea na simu...
Angel akatega masikio vyema huku akiwa makini.
“Ndiyo yupo ubungo hapa...
Kavaa tisheti nyeupe, suruali nyeusi na begi mgongoni kama ulivyosema.”