Ufahamu ugonjwa wa Bawasili, Madhara yake na Jinsi ya kujikinga.
Bawasili, hii ni hali ya kuvimba kwa mishipa ya damu kwenye njia ya haja kubwa.
Hali hii inaweza kutokea kwenye ngozi ya ndani au ngozi ya nje kwenye njia ya haja kubwa.
- Kuwashwa sehemu ya haja kubwa.
- Kupata maumivu sehemu ya haja kubwa.
- Kupata viuvimbe sehemu ya haja kubwa.
- Kutokwa na damu sehemu ya haja kubwa.
Hizo ni dalili kwa mtu mwenye bawasili.
Unapoona bawasili haiponi kwa zaidi ya wiki moja, au unapoona damu zinatoka mfululizo kwenye
njia ya haja kubwa au kuambatana na matatizo mengine kama vile kuhisi kizunguzungu au kuhisi kuzimia
ni muhimu kumuona daktari kwa uchunguzi zaidi.
Kwasababu kutokwa na damu kwenye njia ya haya kubwa kunaweza kusababishwa na magonjwa mengine pia.
Kuna sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha mishipa ya damu kuvimba kwenye njia ya haja kubwa kama vile:
- Unapotumia nguvu kubwa kusukuma haja wakati wa kujisaidia.
- Kukaa kwa muda mrefu chooni.
- Kuharisha au kupata choo kigumu kwa muda mrefu.
- Kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi.
- Kushiriki mapenzi kinyume na maumbile.
- Kukosa ulaji wa vyakula vyenye nyuzi lishe kwa wingi.
- Na Kama unanyanyua vitu vizito mara kwa mara.
Kadri ya umri unavyoenda tishu kwenye njia ya haja kubwa zinakosa nguvu, hivyo kuwa na umri mkubwa kunaongeza hatari ya mtu kupata bawasili.
Pia hali hii inaweza kuwakuta wajawazito kwasababu mtoto tumboni huiminya mishipa ya damu inayopita kwenye njia ya haja kubwa na hali hiyo inaweza kuisha mara baada ya kujifungua.
Njia nzuri na salama ya kujikinga kupata bawasili ni kuhakikisha choo chako ni laini ili usitumie nguvu kubwa wakati wa kujisaidia.
Ili kuhakikisha choo chako kinakuwa kilaini unashauriwa kufanya mambo yafuatayo.
Kula vyakula vyenye nyuzi lishe kwa wingi.
Kula matunda, mboga za majani, na vyakula vya nafaka kwawingi vina nyuzi lishe ambazo hubakia tumboni bila kumeng’enywa na kufanya choo kuwa kilaini.
Kunywa maji ya kutosha.
Inashauriwa kunywa glasi 6 mpaka 8 za maji kwa siku inasaidia kukifanya choo chako kuwa kilaini, pia inashauriwa kuepukana na matumizi ya pombe.
Epuka kutumia nguvu kubwa wakati wa kujisaidia na kubana pumzi ili kulazimisha haja kutoka.
Kufanya mazoezi ya viungo.
Kufanya mazoezi mara kwa mara ni muhimu kwasababu inasaidia kuzuia kupata choo kigumu pia inapunguza uzito mkubwa unaweza kukuweka katika hatari ya kupata bawasili.
Mwisho unatakiwa kuepuka kukaa chooni kwa muda mrefu ili kuepuka kuminya mishipa ya damu kwenye njia ya haja kubwa kwa muda mrefu.
Unaweza pia kusoma: