High School - Episode 04 
Nililia hadi nilipopitiwa na usingizi nilikuja kushituka ilikuwa ni asubuhi siku ya pili.
Roho iliniuma sana, sikuweza kunyanyuka kuelekea darasani nilibaki nimejilaza tu chumbani.
Nikiwa nimezama kwenye fikra huku nikidondokwa na machozi nilihisi mlango wa chumba chetu umefunguliwa nilijuwa ni
Candy.
Cha kushangaza alikuwa ni Martin.
Nilipomuona machozi mfululizo yalianza kunidondoka, Martin alijongea kitandani nilipokuwa nimelala akanikumbatia.
“Cathe pole.”
Aliongea kwa upole.
Nilishindwa kuongea.
“Pole sana yote ni mambo ya kidunia usijali Mungu yupo pamoja nawe.”
Aliendelea kunifariji na kunitia moyo, nilijitahidi kurudia katika hali yangu ya kawaida ingawa kwa kiasi fulani
nilishindwa baada ya muda alitoka kwa sababu aliingia kwa makosa.
“Dunia sasa imeniacha peke yangu, mama ambaye nilikuwa nikimtegemea na nikimpenda kuliko watu wote ndio huyo ameniacha.”
Nililia sana kwa kweli.
Baada ya muda kupita nilirejea katika hali yangu ya kawaida lakini haikuwa kawaida kama kawaida.
Nilikonda nilipungua mara zote nilikuwa mwenye huzuni machozi yakinidondoka.
Sikupenda kujiunga na watu katika makundi nilipenda kukaa peke yangu.
Sikupenda kula chakula nilikula pale tu niliposikia njaa.
Usiku iliniwia vigumu sana kupata usingizi kila nilipolala sura ya mama yangu ilinijia, sikuwa na wakati hata wa
wakusoma kila niliposoma machozi yalinibubujika nilipenda kusoma ili nitimize ndoto zangu.
Kutimia kwa ndoto zangu ilikuwa ni furaha ya mama yangu, sasa mama yangu hayupo ninasoma kwa ajili ya nani?
Nilikata tamaa ya kusoma nilikata tamaa ya kuishi.
Walimu walijitahidi sana kunifariji, na kunipa nasaha mbalimbali.
Haikusaidia kitu.
Martin naye hakuacha kunihusia kwamba hayo yote ni mambo ya dunia yapasa kujipa moyo.
Ilikuwa ni siku ya Jumanne asubuhi, tukiwa kwenye mkusanyiko jina langu liliitwa mbele kiukweli saikolojia yangu
haikuwa vizuri kabisa nilijuwa tu tayari nina kesi nyingine hapo shuleni nilikuwa tayari kwa kila kitu.
Hata kama nikiambiwa kwamba leo nimefukuzwa shule ningepokea kwa kawaida kabisa, nilishachoshwa na mambo yaliyokuwa
yakinikuta.
Nilijongea mbele kiunyonge zaidi.
Shule nzima walinyamaza kimya, wakitegemea kusikia ni tukio gani tena nimelifanya maana nilishazoelekea kuwa
mtu wa matukio hapo shuleni.
Nilipanda mpaka mbele.
Mwalimu alichomoa barua na kunikabidhi nilibaki nimeshangaa imetoaka wapi, nilijiuliza.
Nilirudi huku nikiwa na mshawasha wa kuifungua barua ili nione ni nini kilichoandikwa ndani yake nilifika
darasani hata sikukaa sana nilinyenyuka na kuelekea bwenini nikaifungua barua hiyo na kuanza kuisoma.
Nilichokutana nacho kilichoandikwa kwenye hiyo barua kilinifanya nilie upya.
Iliibua huzuni na simanzi ndani ya moyo wangu.
Iliua kabisa tumaini langu na furaha yangu.
Matumaini yangu ya kuwa na furaha yalikatizwa na barua ile.
Ilikuwa ni barua kutoka kwa mama yangu.
“Kwako mwanagu mpendwa na wa pekee naandika barua hii kwa huzuni nyingi nikijua kuwa sitaweza kukuona tena.
Wewe ni kipenzi cha moyo wangu Cathe.
Mama yako anakupenda sana na siku zote nilitamani ufike pale ambapo ulitaka kufikia, najua unajua tumaini langu kwako kuwa
natamani utimize ndoto zako lakini moyo wangu unaumia sana kujuwa kwamba utatimiza ndoto zako ingawa sitoshuhudia.
Naomba ujipe moyo mama yako natangulia na wewe utafata.
Mpendwa wangu ujaposoma barua hii sitaki ujenge chuki yoyote na mtu yoyote bali uzidishe upendo.
Mwanangu kilichokupeleka shuleni ndicho unachotakiwa kukizingatia usiangaike na vitu ambavyo siyo lengo lako wala la kwetu
sisi kama wazazi wako kukufikisha shuleni, soma sana mwanangu.
Wala usisahau kumkumbuka Mungu wako kwa maana ndiye atakuwa kiongozi wa maisha yako mwanangu.
Napenda ujue hiki kitu nitakuwa na furaha sana endapo barua hii itakufikia na kuifungua na kuisoma.
Mwanangu Cathe, nilipokuzaa wewe ukiwa na miezi minne tu nilikuwa na ujauzito mwingine baba yako alinishawishi kuutoa
ingawa nilikataa aliniambia kwamba sitakupa muda wa wewe kukua vizuri kama nitakuwa na ujauzito mwingine.
Baaada ya ushawishi wa muda mrefu nilikubali kuitoa hiyo mimba ambayo ilikuwa ni ya mdogo wako, nilifanikiwa kuitoa lakini
ilitoka vibaya, iliharabu mfuko wangu wa uzazi.
Baada ya muda, nilianza kusikia maumivu ya tumbo yasiyoisha nilipoenda hospitali niliambiwa mfuko wangu wa uzazi umeharibika
haufai tena hivyo napaswa kutolewa.
Hapo ndipo nilopohakikishiwa kuwa mgumba maisha yangu yote, baba yako alibadilika sana kila mara tulikuwa tukizozana kwasababu
alikuwa anataka kupata mtoto mwingine aliniambia endapo sitaweza kumpatia mtoto mwingine basi ataenda kuzaa nje ya ndoa.
Niliumia sana kwa maana sio mimi niliyetaka kutoa ujauzito bali ni yeye aliyeniamasisha sikuwa na jinsi nilivumilia hayo
yote huku nikiweka juhudi kuomba mwanangu.
Cathe tukio lililotokea shuleni kwako ingawa sina imani kama ni kweli umefanya hivyo lilimkasirisha sana baba yako,
mara zote alijuwa kwamba mimi ni mtu wako wa karibu sana kuliko yeye, kwa maana hiyo kosa lolote wewe ambalo ukifanya
lawama zote nilibeba mimi, nashukuru katika kipindi chote katika uhai wangu nilibeba majukumu yangu sawasawa na hata sasa
naelekea mwisho wa maisha yangu nimekupigania wewe kama mtoto wangu na naamini utafika sehemu ambayo unatamani kufika.
Baba yako alinipiga sana kwa kosa lako ulilolifanya shuleni.
Na baada ya hapo aliondoka hadi ninapoandika waraka huu sijui yuko wapi, nahisi maumivu makali mwilini na hakuna mtu wa kunisaidia.
Sitamani tena kuendelea kuishi katika mateso kiasi hiki acha tu nife mwanangu.
Nilimwomba tu kijana wa hapo jirani anisaidie kukutumia hii barua ili mwanangu ujue baba yako ni mtu wa aina gani.
Sio kwamba umchukie bali umpende na kuishi naye vizuri katika tabia aliyokuwa nayo baba yako ni mkatili sana.
Mwanangu naona nafsi yangu haina mda mrefu sana nitakufa wakati wowote ule.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kutimiza ndoto zako usiache kusomea kile unachokipenda mkumbuke sana Mungu usiache
kusali kila unapoingia katika tatizo lolote.
Mimi ni mama yako mpendwa nakutakia maisha mema binti yangu.”
Nilijikuta nimekaa sakafuni bila kujua.
Nilikosa nguvu ya kufanya kitu chochote nilianza kulia upya niliumia sana na kitu alichokifanya baba yangu,
furaha yangu ilikuwa imetoweka kabisa kiukweli nilimchukia sana baba yangu, alikuwa ni zaidi ya shetani kwangu,
kwa upande mwingine niliilaumu nafsi yangu kwa kusababisha kifo cha mama yangu nilijiona sina thamani tena nililia na nafsi yangu.
“Nisamehe mama nisamehe kwa kusababisha kifo chako popote ulipo mama naomba unisikie naomba unisamehe mama yangu.”
Nililia sana.
Maisha yaliendelea ingawa kiakili nilikuwa siko sawa.
Taaluma yangu ilishuka sana wala sikujali katika hilo niliishi tu ili mradi siku zisogee mbele.
Maisha yangu yalibadilika kwa kiasi kikubwa nilikuwa nina hasira muda wote hata hivyo sikupenda tena
kuonewa nilipanga mtu yoyote atakaye nifanyia kitu chochote nitalipiza kisasi.
Kisasi kilitawala ndani ya moyo wangu.
Mtu wa kwanza niliye muwazia alikuwa ni baba.
“Lazima nitakaporudi nyumbani nilipizie kwa kifo cha mama.”
Nilisema.
Niliwaza kumlipizia Candy endapo angenifanyia tukio lolote lile.
Sikumhofia tena Maloya.
Sikuhofia kupigwa kwasababu nilishakuwa sugu nilipigwa sana.
Sikuogopa kufanya tukio lolote lile kwa kuhofia adhabu au kutangazwa mbele za watu, nilijikuta nimekuwa sugu sikuogopa chochote.
Adhabu kwa upande wangu zilizidi mara nyingi.
Maloya alikuwa akinisingizia mambo mbalimbali, nilikuwa nikipokea adhabu mara kwa mara kutoka kwa Maloya kwa makosa ya kusingiziwa
nilifanya tu sikuwa nahisi chochote katika moyo wangu.
Candy alizidi kunionea kutokana na kwamba yeye alikuwa ni kiongozi mara kwa mara alikuwa akinisingizia makosa na kupewa adhabu.
Niliona kawaida tu na mara nyingi nilimdharau sikusita kumwonesha dharau kila tulipokutana naye sikulihofia tena kundi lake.
Chuki zao na dharau zao kwangu zilikuwa ni kawaida sana maisha yangu yaliendelea vizuri na hata ufaulu wangu ulianza kuongezeka.
Mawasiliano na baba yalipungua, mara kwa mara alikuwa anajaribu kunitafuta lakini sikuweza kuitikia simu zake alipokuwa
akipiga simu ofisini nilipoitwa kwa ajili ya kuongea naye nilikataa.
Martin alikuwa akinionea huruma sana kutokana na adhabu nilizokuwa nikipata pale shule.
Siku yake alinitafuta.
“Cathe sijakuona mda mrefu sana.”
Nilitabasamu nikamwambia.
“Niko busy sana.”
“Busy na nin?”
Aliuliza.
“Jamani kwani hapa shuleni tunafanya nini, niko busy na kusoma.”
Alicheka kisha akaniangalia kwa muda nilijisikia aibu.
“Aaaah, yaah niko busy na kusoma sasa hivi sitaki kukutwa na matukio yoyote yale ya ajabu.”
“Uamuzi mzuri sana kwa maana ufaulu ulikuwa umeshuka sana.”
Alisema.
“Cathe najisikia vibaya sana kwa ajili yako mara nyingi nakuona katika adhabu inaniumiza sana.”
Nilitoa tabasamu jepesi kisha nikamwangalia usoni.
“Martin usijali kuhusu yote haya ninachoangalia sasa ni kufanya kile kitu ambacho kimenileta hapa shuleni kwa sababu hilo
ndio lililokuwa tamanio la mama yangu na ameondoka kabla sijalitimiza ni lazima nilitimize ili hata uko alipo apumzike kwa amani.”
Aliniangalia sana kana kwamba sio mimi niliyekuwa nikiongea hivyo.
“Cathe umeongea kitu kizuri sana lakini hujui kuwa hizo adhabu zinaweza zikakuathiri kisaikolojia na kimasomo pia?”
“Martin siwezi kuruhusu kitu chochote kikaniharibu tena najua kwamba nikiwa mpole nikiwa mkali haya matukio kwangu ndiyo
yameshakuwa yangu na hayawezi kuondoka vyovyote vile niwavyo lazima yatanijia, siwezi kumkimbia Candy siwezi kumkimbia Maloya
siwezi kuikimbia shule nitaendelea kupambana hivyo hivyo.”
Niliongea.
Alifurahi sana alinivuta na kunikumbatia nililihisi joto lake tulibaki tumekumbatiana kama dakika mbili hivi ilikuwa ni
wakati mzuri sana kwangu ambao sikuwahi kuwa nao katika maisha yangu yaliyopita.
Tuliachiana huku tukitweta, aliachia tabasamu na mimi pia.
“Uwe na wakati mwema Cathe.”
Alisema na kuondoka.
Tukio hilo liligoma kufutika katika akili yangu kabisa kila mara nilikuwa nikifikiria liwazo kutoka kwa Martin.
Nilihisi nampenda sana Martin.
“Huyu mkaka.”
Niliwaza na kisha nikatabasamu na kuondoka eneo hilo na kuelekea bwenini.
Nilipofika bwenini nilipanda kitandani kwangu nikiwa na tabasamu.
“Hatimaye katika maisha yangu nimepata liwazo, mtu ambaye anaweza akarejesha furaha yangu katika mazingira
magumu kama haya.”
Nilifikiria.
Niliamua kwenda kumwambia wakati tutakapokutana tena baada ya kufikia uamuzi huo nilikuwa nikitabasamu kila wakati,
ulipofika wakati wa kuhudhuria kipindi cha dini alikuwepo pia, aliimba vizuri sana moyo wangu ulijawa na furaha na amani tele
kila mara nilikuwa nikimwangalia.
Tulipotoka kwenye kipindi nilienda nilimshika mkono tukaongozana darasani alikuwa na furaha sana.
Tulipofika darasani nilimwambia.
“Martin baada ya hapa nilikuwa nahitaji kuongea na wewe.”
Aliachia tabasamu.
“Usijali bibie.”
Aliongea kwa sauti yake tamu.
Kisha akaendelea kusoma na mimi nikachukua madaftari yangu na kuanza kusoma.
Baada ya muda wa prepare kuisha wanafunzi walianza kutoka madarasani na kuondoka, aliniangalia kisha
akanibinyia jicho nikaachia tabasamu tu.
Mara baada ya watu wote kutoka alinigeukia na kunitazama.
“Haya niambie bibie.”
Alisema nilitabasamu.
Alitabasamu pia.
“Martin.”
Niliita kwa sauti nzuri ya kike.
“Naam.”
“Unajisikiaje tunavyoonewa kwa kosa lisilo la kwetu?”
“Hamuna mtu ambaye angeweza kujisikia vizuri Cathe kila mtu lazima angeumia na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu.”
Aliniambia.
“Pole.”
Nilisema.
“Na naomba nisamehe kwa kuwa chanzo cha mambo haya yote kutokea kwa upande wako.”
“Usijali Cathe hata mimi pia napaswa kusema sorry kwako kwasababu hata mimi ni chanzo cha haya yote kutokea kwako.”
“Aaah kwahiyo kila mtu amwombe msamaha mwenzie si ndiyo?”
Nilisema.
“Mmmh.”
Alicheka.
“Ndio nisamehe pia na mimi.”
Tulicheka wote kwa pamoja.
“Cathe.”
Aliniita.
Nilimwangalia, nilishindwa kumtizama moja kwa moja machoni.
“Uliniambia kuna kitu unataka kuniambia nakusikia na utakapomaliza kuniambia unachotaka kuniambia na mimi
kuna kitu nataka nikwambie.”
“Asa kwanini hukuniambia toka saa zile?”
Nilimuuliza.
“Kimenijia ghafla.”
Alisema na kisha akacheka.
Na mi nikacheka pia.
“Ok Martin mara zote huwa najisikia vibaya sana kusemwa au kuhukumiwa kwa kosa ambalo kweli sijalifanya na
najua kabisa kwamba sijafanya.”
“Ni kweli inaumiza.”
Alisema Martin kwa utulivu.
“Martin sorry kama nitakukwaza kwa nitakacho kwambia.”
Nilimuambia.
“Lakini nimeona kwamba tusiache ibaki midomoni kwa watu nataka iwe kweli kwasababu wewe ni mzuri kwangu.”
Aliniangalia sana.
“Cathe are you serious?”
“Nataka kuwa na uhusiano na wewe.”
“Ngoja na mimi nikwambie ambacho ninataka nikuambie.”
Alisema Martin.
Niliishiwa nguvu mwili mzima ulikuwa ukitetemeka nikiwaza Martin anataka kuniambia nini.
Akili yangu haikutulia niliwaza sana nimewezaje leo kumwambia mwanaume kuwa nakupenda kitu ambacho sikuwahi
kufikiria katika maisha yangu.
Akili yangu haikuwa sawa kabisa.
“Cathe.”
Sauti yake ilinitoa kwenye wimbi la mawazo, niliongea kwa kitetemeshi.
“Nakusikia Martin.”
“Mawazo yetu yanafanana.”
Nilibaki namshangaa nisijue akimaanisha nini.
“Una maana gani Martin?”
Nilimuuliza.
Alivuta pumzi ndefu na kisha kuishusha.
“Ulichokuwa unakiwaza ndicho kilichokuwa akilini mwangu.”
Alisema.
Sentensi yake fupi ilitosha kuufanya moyo wangu ujae na furaha sana niliruka kwa furaha na kumkumbatia.
Kila mtu akiwa na furaha moyoni mwake na huo ndio mwanzo wa mahusiano kati yangu na Martin.
Unaweza pia kusoma: