Wakati Nilipokufa - Episode 03 
Kutoka ndani ya nyumba yangu niliona begi kubwa ambalo tulikuwa tukilitumia kwa safari za muda mrefu mimi na mke
wangu likitupwa nje.
Sikujua ni nini kilichokuwa kikiendelea nilijionya kuendelea na safari yangu niliyokuwa nayo nilirudi nyuma kidogo na
kujibanza pale nilipokuwa.
Ghafla pia begi la salfeti lilitupwa kutoka mule ndani huku likirusha baadhi ya nguo nje sikuwa na shaka lilikuwa halijafungwa.
“Mmmmh…”
Niliguna.
Kikafuata kikapu.
Nacho kilitupwa nje.
Nilikunja sura kuonesha umakini kidogo katika hilo swala.
“Kuna nini?”
Nilijiuliza.
Na ghafla mke wangu alisukumwa kutoka ndani kwa nguvu sana na kwenda kuangukia mabegi yale.
Alionekana aliumia kidogo.
Alinyanyuka ghafla na kujiangalia mkononi huku akimuangalia mtoto wetu kule nyuma, mgongoni alipokuwa amembeba.
“Ondoka hapa mwanaharamu wewe.”
Ilianza kusikika sauti kabla dada yangu hajaonekana.
Nilitoa macho pima.
“Umeshamuua kaka yetu sasa unataka nini na kama ulitegemea baada ya kumuua kaka yangu utakuja upate mali basi
ndiyo imekwisha hiyo hupati kitu chochote hapa ondoka urudi ulikokuwa malaya mkubwa wewe.”
Alisema dada yangu.
Walitoka ndani wakina dada wawili ambao walikuwa wakilingana rika na dada yangu.
Sikuwa nikiwajua hata hivyo na wao niliona wakimsakama mke wangu pale chini kitendo kile cha ghafla kilinichanganya sana.
“Eenh!”
Niliwaza.
“Mbona mapema sana.”
“Nakwambia hivi hupati kitu chochote kutoka hapa ondoka nisione sura yako.”
“Lakini wifi msiba hata haujaisha.”
Alisema Aisha wangu.
“Msiba gani wewe umemuua kaka yetu tunashindwa hata kuona sura yake ya mwisho msiba gani unaotaka tuendelee kukaa hapa
tukae tusikilize makelele yako?
Unacholia unafiki mtupu unalia unafurahia kupata mali za kaka yangu yani nikwambie hivi
umejindanganya bora hata ungeendelea kukaa naye uendelee kufaidi mali zake kisirisiri lakini kwa kumuua umeenda OP yani
umejindanganya hupati kitu chochote.”
Alisema dada yangu Salma huku akimpasha mke wangu.
Siyo siri moyo wangu ulinipasuka sikuwahi kuwaza kabisa kama hali ingekuwa hivyo nilitegemea mara baada ya kifo
changu hicho feki basi dada yangu angesimama kidete kumtetea mke wangu.
“Daaah.”
Nilisema.
“Nasemaje sitaki kuona sura yako hapa.”
“Wifi mimi nitaenda wapi?”
“Utajua mwenyewe utakapoenda.”
Alisema dada yangu.
“Na hawa watoto? Wifi hebu nihurumie basi.”
“Naomba unikome mimi siyo wifi yako, ungekuwa wifi yangu usingemuua kaka yangu.”
Alisema.
Hapo ndipo nilipopatia picha maneno ambayo yalikuwa yakiongelewa na wale wakaka kule nje.
Kumbe hawakudanganya, tena maneno yenyewe yametoka kwa dada yangu mwenyewe.
“Kweli ameniua amewezaje kusababisha ajali kubwa kiasi kile na kuua kila mtu?!”
Niliendelea kuwaza huku hasira zikiendelea kunikamata polepole.
Salma aliingia ndani huku akiwaacha baadhi ya wadada ambao alitoka nao kule ndani na wakaka kadhaa wakiwa
wamesimama wakimuangalia mke wangu.
Nilitegemea hata wao wangetoa msaada wowote ilikuwa kinyume chake.
Walibaki tu wakimuangalia huku wakiongea wao kwa wao wengine walidiriki hata kucheka baadhi ya watu hao niliwatambua.
Walikuwa ni marafiki wa familia yetu ambao walikuwa karibu sana na mimi na dada yangu.
Mara chache sana waliwahi kuja nyumbani kwangu na kuhudumiwa vizuri tu na mke wangu.
Nilishangaa sana.
“Kweli leo ndiyo wameamua kumlipa mke wangu hivi?”
Baadhi ya ndugu zangu, shangazi zangu, baba zangu wadogo walimuangalia tu mke wangu bila kumsaidia kitu chochote.
Aliendelea kulia mwenyewe pale chini huku akijaribu kukusanya baadhi ya nguo ambazo zimemwagika na kuzirudisha ndani ya begi.
Dada yangu alitoka tena nje.
“Bado tu hujaondoka?”
Alisema.
Nilivuta umakini zaidi.
“Hivi ni amechanganyikiwa au vipi?”
Nilijiuliza.
Mke wangu hakujibu chochote sauti ya kwikwi tu ulisikika alikusanya nguo zake na kisha kuondoka.
“Kama unaona huwezi kuwalea hao watoto waache hapa mimi mwenyewe nitawalea.”
Aliongea huku akimvuta mkono mwanangu Hasan.
Hasani aliangua kilio cha nguvu.
“Niache sitaki.”
Alisema.
“Naenda na mama.”
Aliendelea kulia kwa nguvu.
“Nenda na wewe.”
Alimsukuma mwanangu ambaye alienda kumkumbatia mke wangu na wote walianguka chini.
Kwakuwa mke wangu hakuwa amesimama mbali alikuwa amepiga magoti akikusanya nguo pale chini wote walianguka.
Mwanangu mdogo Abdul alianza kulia kwa nguvu.
Ni kana kwamba mama yake alihisi pengine amemuumiza alinyanyuka haraka sana na kisha kumuangalia mwanae akimkagua
maeneo mbalimbali.
“Ondokeni bwana mnatuchelewesha sisi.”
Alisema dada yangu.
Wote watatu walikuwa wakilia sasa.
Baada ya kuhakikisha kwamba Abdul hajaumia popote mke wangu alinyanyuka huku akijaribu kukusanya yale mabegi.
Yalionekana ni mazito sana kwake kiasi kwamba nilimuonea huruma.
Begi moja lilikuwa la kuburuza.
Alimpa mtoto wangu mdogo kipochi chake akibebe.
Hasan alibeba huku akilia.
“Mama tunaenda wapi?”
Alilia kwa nguvu.
Machozi ya uchungu yalinitoka niliumia sana.
“Kweli dada yangu anaweza kumfanyia mke wangu kitendo hiki?”
Niliumia kwasababu hayo mengine yote nimeyasababisha mimi mwenyewe.
Hata siku moja mbele ya dada yangu sikuwahi kuonesha kumkubali mke wangu, mara nyingi tulikuwa tukikaa tukimsema huku
nikionekana kufurahia sana na sasa dada ameendeleza kile kitu ambacho mimi nilikuwa nimekianzisha.
“Aaanh bora hata angewaonea huruma watoto wangu jamani kweli watoto wangu wakaanze kuhangaika hivi utasema baba
yao nilikuwa masikini.”
Niliumia sana na wakati huo niliona kiasi gani nilikuwa nikimpenda mke wangu.
Ni mke wangu tu ndiye aliyesimama na mimi wakati wote.
Mara mlango ulifunguliwa alitoka dada yangu huku akiwa amebeba sufuria ambalo alimmwagia moja kwa moja mke
wangu sikujua hasa ni kitu gani kilichokuwepo pale lakini mke wangu wala hakulia.
Hasan ndiye aliyekuwa akilia huku akilitaja jina la mama.
“Mamaaaaa…”
Mke wangu alipiga magoti kana kwamba hakuna kitu chochote kilichokuwa kikimtokea.
Alijipangusa yale maji na kisha kumgeukia mtoto wetu Hasan.
Aliongea nae kwa kifupi tu kwa sauti ambayo sikuweza kuisikia na kisha alilibeba lile begi la salfeti almaarufu
kama shangazi kaja kichwani huku akiliburuza lile begi lenye matairi na mkono mwingine akiwa amebeba kikapu.
Hasan akiwa amebeba kipochi chake ambacho mara nyingi alikuwa akibeba vitu vya mtoto akiwa safarini au akienda
mahali popote pale.
Walianza kuondoka nyumbani kwa upole sana.
Kiukweli nilishindwa kuendelea kusimama mwili uliniisha nguvu sikuamini kilichokuwa kikitokea mbele ya macho yangu.
Nilikaa chini, mke wangu alinipita pale bila kunitambua.
Aliondoka.
Machozi yalinitoka sana, nililia mno.
Nilipokuja kushituka niliona muda kama umeenda sana.
“Mke wangu atakuwa ameondoka sasa ameenda wapi?”
Niliendelea kujiuliza.
Nilinyanyuka kama chizi na kuanza kumkimbilia.
Hata hivyo sikuona alipokuwa ameenda wala sikujua amepitia njia gani.
Nilikimbia tu.
Nilikimbia mpaka nilipofika kwenye kituo cha daladala.
Hata hivyo hawakuwepo.
Nilikaa hapo kituoni.
“Sasa ameenda wapi?”
Nilianza kurudi huku machozi yakinitoka.
Nilikuwa kama mwehu.
Nilipita kando ya barabara mpaka sehemu ambayo barabara ya kuelekea mtaani kwetu ilikuwa ikiingia.
Nilivua kile kibakarashee na ule mtandio niliokuwa nao kichwani kwa maana nilihisi kulowa jasho sana.
Nilitoa na ile miwani ambayo niliibandika usoni.
Huku nikipiga hatua za kichovu sana.
“Babaaaaa…”
Nilisikia sauti ya nguvu.
Niligeuka kule sauti ilikokuwa ikitokea kwasababu nilijua hakika ni kwamba ile sauti inanihusu.
Ilikuwa ni sauti ya mwanangu Hasan.
Niligeuka na kisha kuangalia kule ambapo sauti ilitokea.
Hasani alikuwa akiniijia kwa kasi sana huku akiwa ametupa ile begi ambayo mama yake alikuwa amempa aibebe.
Bila shaka Aisha hakuweza kutembea umbali mrefu na yale mabegi alichagua sehemu ambayo ilikuwa na utulivu
pembeni ya barabara na kisha kupumzika.
Alionekana kushituka sana.
Alirudi kinyumenyume.
“Hasan…”
Alimuita Hasan kwa nguvu.
Nadhani pia ile kanzu nyeupe ilimchanganya.
“Hasan njooo.”
Aliita.
Ni kana kwamba alikuwa akitaka kunikimbia lakini hata hivyo aliogopa kumuacha mwanae Hasan.
Niliona mapenzi mazito ya mke wangu kwa watoto wetu.
Chozi lilinitoka.
Hasan teyari alikuwa ameshanikaribia.
Alikuja alinurikia kwa nguvu nilimbeba huku machozi yakinitoka.
“Hasan noooo…”
Alisema mke wangu.
“Naomba umuache mtoto wangu.”
Alisema kwa sauti.
Huku akinioneshea kidole ni kiasi gani alikuwa na uwoga hata hivyo alipatwa na ujasiri wa ghafla kwaajili ya
kumuokoa mtoto wake.
“Ni mimi mke wangu.”
Nilisema huku nikimsogelea alirudi kinyumenyume.
“Hapana sio wewe mume wangu ameshakufa.”
Aliongea.
“Ni mimi sijafa naomba ukae chini nikuelezee vizuri.”
"Hapanaaaa."
Aliendelea kupiga makelele kwa nguvu kiasi cha kutaka kuamsha watu ambao kwa wakati huo walikuwa wameshaondoka maeneo
hayo ambayo mara nyingi yalionekana kutumika kibiashara.
“Ni mimi.”
Nilimsogelea kwa ukaribu na kisha kumvutia kwangu.
“Ni mimi.”
Hakuonekana kuamini kile kitu, alitamani kukimbia hata hivyo nilimbana vizuri kabisa.
“Ni mimi mke wangu usiogope.”
Alikuwa akilia kwa nguvu mno.
Tulikaa chini huku nikijaribu kumsimulia kile ambacho kilitokea huku nikimuomba msamaha kwa yote.
Alilia mno, nadhani ni mara mbili zaidi ya ule msiba uliokuwa umemkuta.
Alilia mno.
Alilia sana mjane wangu yule ambaye hakuwa tena mjane kwa wakate ule.
“Mmmh siamini mume wangu kama uko hai.”
Alisema mwishowe mara baada ya kuniamini.
“Mke wangu najutia kila kitu ambacho nimekufanyia mimi ndiyo sababu ya wewe kufika hapa ulipofika naomba unisamehe sana.”
Niliongea.
“Ninacho mshukuru Mungu tu ni kwamba uko hai mengine yote nimeshayasamehe.”
Niliona imani kubwa sana mbele ya macho ya mke wangu.
Nilimnyanyua huku nikimkumbatia.
Watoto wangu sasa walikuwa wameacha kulia walionekana kuwa na furaha sana.
“Twende nyumbani.”
Alionekana kuwa na uwoga.
“Usijali kila kitu kitakuwa sawa.”
Kiukweli mke wangu alikuwa akitoa harufu kali sina shaka ni ule uchafu aliomwagiwa na dada yangu,
roho iliniuma mara mbili.
Nilibeba mabegi yote huku yeye akiwa amembeba mtoto wetu mgongoni pamoja na mwanangu Hasan akiwa amemshikilia mkono.
Safari hii nilidhamiria kumtetea mke wangu.
Mara baada ya muda mfupi tulikuwa tumeshawasili nyumbani.
Nyumba yetu ilikuwa imetawaliwa na vicheko kana kwamba siyo hiyo ambayo watu walikuwa wakilia muda mfupi uliopita.
Nilisogea hadi getini huku mke wangu akiwa anaogopa kusogea.
Ilibidi nishushe mabegi chini na kwenda kumshika mkono huku nikijaribu kumuelezea kitu lakini mke wangu
alionesha ishara ya kukataa nilijaribu kumuambia mara mbili mara tatu nikimuelekeza hatimaye alikubali.
“Cheers…”
Sauti ilisikika kutoka mule ndani.
Huku mazungumzo mbalimbali yakiendelea pamoja na kutawaliwa na vicheko.
Nilifungua mlango na kisha mke wangu alingia.
Aliingiza begi la kwanza huku watu wakimuangalia kana kwamba hawaamini nini kilichokuwa kinatokea.
“Wewe malaya umefuata nini humu ndani si nilishakufukuza.
Hivi unataka nikuvunje miguu ndiyo uondoke humu ndani huna kwenu wewe, wewe yatima wewe.”
Aliongea dada yangu huku akinyanyuka.
Shangazi yangu mmoja alimzuia.
“Tulia Salma tulia.”
Alimvuta.
Unaweza pia kusoma: