Wakati Nilipokufa - Episode 01 
“Nimepata safari ya kikazi naelekea Mwanza ni safari ya siku tano.”
Niliongea huku uso wangu ukiwa mkavu kabisa.
“Sawa.”
Aliitikia kiupole mke wangu Aisha.
Wakati huo alikuwa akimnyonyesha mtoto wetu mdogo Abdul, huku akimsaidia homework mtoto wetu ambaye kidogo alikuwa
mkubwamkubwa, Hasan.
Nilinyanyuka hapo sikutaka hata kumuangalia.
Siku za hivi karibuni mke wangu alikuwa siyo mtu wa maneno mengi na mimi kwa kiasi fulani nilifurahia sikutaka sana
kujibujibu maswali ambayo yangenipelekea kunikasirisha.
Nilipenda sana kuwa na mke ambaye haongei na hakika Mungu alinijalia.
“Utaondoka lini?”
Nilisikia sauti ya mke wangu ikitokea sebuleni wakati tayari nimeshaenda chumbani kwetu.
“Kesho kutwaaa.”
Nilijibu kwa kelele huku nikichukua simu yangu.
Nilifungua ujumbe mfupi ulioingia huku nikitabasamu.
Wala sikujua ni nini mke wangu anafanya huko sebuleni niliendelea kuchati huku nikifurahia.
Niseme tu ukweli kwamba pamoja na kwamba nilikuwa ni mtu mzima tayari na nimeajiriwa lakini bado nilikuwa na mambo mengi ya kitoto.
Siku ilipita.
Kesho yake ilikuwa ni Jumapili siku ambayo nilikuwa napumzika nyumbani.
Sikutoka kitandani mpaka ilipofika saa tano.
Mke wangu alikuja kuniambia.
“Chai tayari haunywi?”
Nilivuta pumzi.
“Nakunywa.”
“Amka basi uoge uje unywe chai.”
Aliniambia kwa upole.
Siyo siri nilijaliwa mke mzuri mpole na mnyenyekevu sana.
Ni mara chache sana kumkuta amekasirika na hata akikasirika haiwezi kuzuia yeye kutimiza majukumu yake kama mke
kwa maana hiyo basi niseme tu kwamba hakuwahi kukasirika.
Nilioga na kisha kwenda sebuleni ambapo watoto wangu walinisubiri pamoja na mke wangu.
Nilikunywa chai tamu ambayo iliandaliwa na mke wangu.
“Kesho ndiyo unasafiri?”
Alisema.
“Ndiyo.”
Niliongea huku nikichezacheza na mtoto wangu Hasan.
Wala hakuongeza neno jingine lolote.
Mara baada ya kupata chai nilirudi kitandani nikimuacha mke wangu akihangaika na watoto wawili mmoja mwenye miaka sita
ambaye tulimpata kabla sijaanza kuishi na mke wangu na mwingine alikuwa na miezi tisa ndiyo kwanza alikuwa akikaa chini.
Jioni ilipofika mke wangu aliingia chumbani baada ya shughuli nyingi.
Alikuwa amembeba Abdul mgongoni.
“Vipi?”
Nilimuuliza mara baada ya kuingia.
“Hamna kitu.”
Nilimuuliza mara baada ya kuona amevuta begi langu.
“Nimeshapanga.”
Nilisema.
Aligeuka na kuniangalia.
Ni kama alitamani kuongea neno lolote lile la kunilaumu lakini alishindwa.
“Sawa.”
Alijibu kwa unyonge na kisha kukaa kitandani.
“Naomba nisaidie kumshika Abdul nikaandae chakula.”
“Amelala?”
Nilimuambia.
“Hapana.”
Alisema.
“Poa.”
Alimshusha Abdul na kisha kuondoka nilibaki nikicheza na mtoto wangu yule.
“Chuchuchu tototoo…”
Nilimbembeleza wakati Abdul alipoanza kulia.
“We mama Hasan mtoto analia bwana njoo umchukue.”
Alikuja mara moja kumchukua.
“Umemaliza kupika?”
Nilimuuliza.
“Bado.”
Alisema.
Hata hivyo nilishindwa kumuambia aendelee na shughuli zake mimi niendelee kumbembeleza mtoto.
Alimchukua na kisha kumuweka mgongoni na kutoka nje.
Nilichukua simu yangu na kisha kufungua meseji zilizokuwepo katika mtandao wa whatsapp na kuendelea kuchati
kana kwamba hakuna kitu chochote kilichotokea.
Asubuhi ya siku iliyofuata ndiyo siku ambayo nilikuwa niko safarini.
Mke wangu aliamka mapema sana alimtayarisha Hasan kwaajili ya kwenda shule.
“Utaondoka nae.”
Nilimuangalia.
“Mimi nasafiri nitaondokaje nae.”
“Sawa.”
Hatukuwa na usafiri wowote mimi nilipanga kuondoka na pikipiki.
Nilitoa tiketi yangu huku nikiiweka mezani kuonesha kwamba safari imeiva.
Nilitoa begi langu pia na kuliweka sebuleni.
Hasan tayari alikuwa amejiandaa kwaajili ya kwenda shuleni.
Mama yake alimuwekea kila kitu ambacho alikihitaji kwaajili ya kwenda shuleni na kisha kutoka nae nje.
"Bye baba."
Alisema Hassan wakati akiondoka, nilimpungia tu bila kusema lolote.
Baada ya muda alirejea kumaanisha kwamba tayari Hassan alikuwa ameondoka kwenda shuleni.
“Vipi ameshaenda?”
“Eee ameenda, nimekutana na watoto wenzie wanaenda shuleni nikamuagiza na yeye aende nao.”
Alisema.
Nilimuangalia kwa upole sana huku nikimuhurumia majukumu mengi aliyokuwa nayo.
“Hata hivyo si mwanamke tu wa nyumbani anayaweza mbona hajawahi kulalamika.”
Nilisema.
Aliniandalia kifungua kinywa ambacho nilikinywa harakaharaka na baada ya muda pikipiki ambayo niliita kwaajili ya kunipeleka
stendi ilifika nilichukua mizigo yangu na kisha kuondoka.
“Bye mke wangu tutaonana baada ya siku tano.”
Nilisema.
“Sawa ufike salama na urudi salama.”
Alisema Aisha.
Taratibu nilipotea kwenye mboni za macho yake kuelekea stendi kwaajili ya kusafiri.
Nilifika salama kabisa nilipokuwa naenda.
Nilipokelewa na mwenyeji wangu ambaye safari yetu tuliipanga kwa muda mrefu kidogo.
“Karibu baby…”
Aliniambia mara baada ya kufika nyumbani kwake.
Tofauti na matarajio ya mke wangu safari yangu haikuwa ya kuelekea Mwanza ndiyo kwanza nilikuwa naelekea Kigamboni kutoka
nyumbani kwetu Tabata.
“Umemuagaje yule mwanamke?”
Alisema Ester.
“Nimemuambia nina safari ya siku tano kuelekea Mwanza.”
“Ungemuambia ya wiki mbili kabisa.”
Alisema Ester huku akicheka na mimi nilicheka.
“Karibu mpenzi.”
Alisema Ester nilikaribia ndani.
Siyo mara yangu ya kwanza kufika hapo kulikuwa ni kama nyumbani kwangu, mimi ndiye niliyempangishia chumba Ester.
Alionekana mwanamke mwenye kuvutia sana.
Nilikuwa kila mara nikijilaumu kwanini niliwahi kumuoa mke wangu Aisha.
Niliona Ester alifaa sana kuwa mke wangu.
Hata hivyo yeye mwenyewe alionekana kuridhika na nafasi ya mchepuko mara kwa mara alikuwa akimcheka mke wangu.
Mwanamke huyu wa kitanga alionekana kuiteka akili yangu sana.
Nilisahau kabisa familia yangu alinipetipeti kama ambavyo ilitakiwa.
Nilizima simu ili kuepusha usumbufu wowote ule utakaopelekea kuniharibia starehe yangu.
Na kama ambavyo nilikuwa nimetegemea nilikandwa, alinimassage mwili mzima, aliniogesha, alinipikia chakula kitamu sana.
Sikupanga kutoka nyumbani kwake mpaka siku ya kurudi nyumbani kwangu, mambo aliyokuwa akinipa yalinichanganya kabisa akili.
Baada ya hayo yote tulienda raundi mbili kali kabisa ambazo ziliniacha hoi kwa usingizi mzito.
Nililala kama pono.
Nilikuja kuamka mwili wote ukiwa umechoka sikujua hata ni saa ngapi wakati huo ila nilichokuja kugundua ni kwamba taa ilikuwa
imewaka na mapazia yote yalikuwa yameshushwa.
Nilichelewa kujua kama wakati huo ni usiku au ni mchana.
Nilinyanyuka kiuvivu nikitoka kuelekea sebuleni nilimkuta Ester wangu amekaa akiangalia taarifa ya habari nilienda kukaa pembeni yake.
Aliniangalia tu huku akitabasamu bila kuongea kitu chochote na mimi nilirudisha tabasamu kwa tabasamu na kisha kuendelea kukaa
kuangalia taarifa ya habari huku nikimvutia Ester kwangu na yeye bila hiyana aliniegamia kwenye mabega yangu.
“Basi la abiria la kampuni ya SUTCO lililokuwa likifanya safari zake kutoka Dar es salaam kuelekea Mwanza limepata ajali
mbaya sana katika mlima senkenke.
Gari hilo lililokuwa limebeba abiria hamsini na sita lilitumbukia katika daraja lililokuwepo katikati ya mlima senkenke na
kuua abiria wote.”
Habari hiyo ilinishitua sana.
Hilo ndilo gari ambalo nilimdanganya mke wangu kwamba nasafiri.
Ndilo gari hilo nilikata tiketi ya uongouongo kwaajili ya kumuaminisha mke wangu kwamba kweli nilikuwa nikisafiri.
Na sasa gari hilo lilikuwa limepata ajali na kuua abiria wote.
Ester alionekana kusikitika.
“Jamani watu wanakufa siku hizi.”
Akilini kwangu nilishachanganyikiwa kabisa.
Kwa takribani kwa dakika mbili sikuelewa mahali nilipokuwa akili yangu ilikuwa ikizunguka sana niliona kichwa changu kikiwa chepesi.
“Mungu wangu.”
Niliita kwa sauti.
“Nini?”
Alisema Ester.
Macho nilikuwa nimeyatoa pima kuonesha kiasi gani nilikuwa nimechanganyikiwa.
“Yesu wangu.”
Nilijikuta nimeita hilo jina ambalo halikuwa hata kwenye imani yangu.
“Ni nini wewe?”
Alisema.
“Hili ndilo basi nililomdanganya mke wangu nasafiria.”
“Eeenh!”
Hata yeye pia alishituka halafu ghafla aliangua kicheko.
“Unacheka?!”
Alicheka sana.
Nilimshangaa.
“Kinachokufurahisha wewe ni nini hasa?”
Nilikuwa nikiwaza sana narejeaje nyumbani kwangu.
Hapo ndipo nilipoanza kufikiria umuhimu wa familia yangu.
“Si utabaki tu hapa.”
Alisema Ester.
Niliona ananichanganya.
“Hivi huyu mwanamke anafikiria kweli.”
Niliwaza na kuwazua.
“Mungu wangu nyumbani kwangu kwahiyo saa hizi kuna msiba.”
Nilisema.
Nilinyanyuka na kisha kuelekea chumbani.
Nilibaki tu nimesimama nikikiangalia kitanda kana kwamba ni kipya kwangu.
“Unachochanganyikiwa ni nini?”
Alisema Ester.
“Familia yangu, mke wangu, watoto wangu!”
Nilisema kwa kuchanganyikiwa.
“Kwahiyo hao ni wa muhimu sana kuliko mimi?”
Alisema Ester.
“Hivi Ester umechanganyikiwa?!”
Niligeuka nikiwa na hasira sana.
“Yani badala ya kufikiria namna ya kusolve hili tatizo unaanza kufikiria kwamba nani ni muhimu kati yenu.”
“Kwahiyo mimi nikae nianze kukutatulia matatizo yako na mkeo una akili kweli wewe?”
Hapo nilijiona kweli sina akili.
Na hakika nilikuwa sina akili kwa kukubali kwangu kuwa na uhusiano na mwanamke mwingine nje ya ndoa yangu,
hakika alinichanganya.
“Ukiwa hapa kwangu unatakiwa usahau kwanza habari za mkeo.”
“Kaa hapa mpaka siku zako za kukaa hapa zitakapoisha halafu ndiyo utakapoenda kwenu utakavyojua namna ya kuhangaika
wewe na mkeo, mimi mambo ya kuhangaika na mkeo mimi siwezi kukusaidia.”
Alisema Ester huku akija kukaa kitandani.
Akili yangu haikuwepo kabisa.
Ester alinishika kiuno na kunivutia kwake, nilimsukuma.
“Acha ujinga Ester!”
“Kama unajihisi umechanganyikiwa sana ondoka kwangu.”
Niliwaza hata hivyo saa hiyo saa mbili ningeondokaje kigamboni na kisha kuelekea mpaka kwangu ambapo sikuwa na shaka
kwamba nyumbani kwangu tayari walikuwa wameshapata taarifa na wakati huohuo kuna msiba.
Nilikumbuka kwamba tangu nilipofika kwa Ester nilizima simu.
Nilivuta mto na kulala kisha kujiegesha pale kitandani.
Mawazo mengi sana yalipita akilini mwangu.
Usingizi mzito ulinichukua.
Nilikuja kuamka siku iliyofuata asubuhi ya saa nne.
Ester alikuwa akiendelea na shughuli zake.
Hata hivyo kulala kwangu kote hakukunifanya nisahau madhila yaliyonikuta.
Bado akili yangu ilikuwa haijaamua njia yoyote ya kunitatulia tatizo hili hakika nilijutia kuchepuka kwangu.
Nilivuta pumzi na kuzishusha.
Ester alikuwa akiingia chumbani kwake na kutoka.
Wala hakujishughulisha kuniuliza hali yangu wala nini aliendelea kufanya mambo yake.
“Ester… Ester…”
Niliita.
Ester alinipita kana kwamba hanisikii.
“We Ester si nakuita.”
Aligeuka huku akinikata jicho kali na kisha kuendelea na mambo yake.
“Yani mimi nina matatizo hapa lakini yeye hata ajali anakazania mambo yake, angekuwa mke wangu hapa asingenifanyia hivi.”
Nilimkumbuka mke wangu.
Unaweza pia kusoma: