Wakati Nilipokufa - Episode 02 
Nilikumbuka miaka sita iliyopita.
Wakati ndiyo kwanza nimeanza kufanya kazi pale nilipokuwa nikifanya kazi.
Alikuwa akileta chakula kila siku kazini kwetu.
Alikuwa akifanya kazi kwenye moja kati ya migahawa iliyokuwa nje ya ofisi yetu pale mwananchi.
Wakati wa mchana ulipofika alikuja kuchukua oda na kisha kutuletea chakula.
Nilivutiwa nae alikuwa ni mkarimu sana na mwenye kuhudumu kwa upole.
Sauti yake na jinsi alivyokuwa mzuri alinivutia sana.
Mweupe mwenye macho makubwa na nywele zake nzuri ambazo mara nyingi alikuwa akizifunga.
Mrefu hakuwa mnene wala hakuwa mwembamba hakika alivutia mbele ya kila macho ya mwanaume aliyekuwa akimtazama.
Nilijaribu bahati yangu.
Baada ya kunikataa mara kadhaa hatimaye aliweza kukubaliana na mimi.
Mahusiano yetu yalianzia hapo.
Nilikuja kugundua stori ya kusikitisha sana ya Aisha.
Alikuwa ni yatima na yule mama mwenye mgahawa wake ndiye ambaye alikuwa akiishi naye.
Wazazi wake walifariki akiwa mdogo.
Mama huyu alimchukua na kisha kuishi naye kama mwanae.
Hata hivyo hakubahatika kupata elimu nzuri.
Alipomaliza darasa la saba elimu yake iliishia hapohapo.
Mama mwenye mgahawa ambaye tulikuwa tukimjua kwa jina la mama K alikuwa ana watoto watatu.
Na kwa maelezo yake ni kwamba alishindwa kumsomesha aisha kwasababu alikuwa bize kuwasomesha watoto wake.
Watoto wenyewe hata hawakuweza kufikia mbali kielimu.
Tangu alipomaliza shule Aisha alikuwa akimsaidia mama K shughuli zake za mgahawa.
Nilitokea kumpenda sana katika miezi mitatu tu ya mahusiano yetu tayari Aisha alikuwa amebeba ujauzito hilo
lilinikasirisha sana ukizingatia sikuwa na muda mrefu tangu nimeanza kazi wala sikuwa nimejiandaa kuwa na familia.
Nilihisi ni kama amenitegeshea ili nimkomboe na maisha magumu aliyokuwa akiishi hii ilifanya nimchukie.
Sikuwa ma jinsi mama K alinisusia mtoto wake kwasababu alikuwa ni mjamzito.
Yeye mwenyewe alikuwa ameshakata tama kabisa kwa upande mwingine.
Huruma iliniingia kumchukua.
Nilimchukua huku nikimtunza vizuri kabisa.
Na hakika na yeye pia alinitunza vizuri kama mume wake wala hata sikujutia.
Kwa upande mwingine ingawa nilipata mtoto mapema sana tofauti na matarajio yangu maisha yaliendelea kubarikiwa sana.
Pamoja na kuongezeka kwa familia lakini bado mshahara wangu ulinitoshea huku nikiweza kujiendeleza na kupanua biashara.
Niliweza kufungua maduka mawili ambayo hata hivyo mke wangu alikuwa hajui kama nilikuwa nikimiliki maduka hayo
sikutaka kumshirikisha kwasababu tukio la kubeba mimba mwanzoni kabisa mwa mahusiano yetu lilinitisha hivyo sikuwa
nikimuamini sana.
Wazazi wangu walifariki tukiwa tayari tumeshakuwa wakubwa.
Ni takribani mwaka mmoja kabla sijakutana na Aisha.
Kwetu tulikuwa mimi na dada yangu.
Na pesa ambazo tuliachiwa na wazazi wetu kama urithi ndizo ambazo nilitumia kuanzisha biashara.
Maduka yangu mawili yalikuwa yakifanya biashara nzuri kabisa.
Dada yangu Salma ndiyo mtu pekee aliyekuea akijua na yalinipa jeuri mbele ya mke wangu.
Pamoja na mikogo yote niliyokuwa nikimfanyia wala hakuonesha kushituka aliridhika kabisa na maisha ambayo alikuwa
akiishi hakujali tulikuwa tunakula nini wala amevaa amependeza ilimradi tunakula na ilimradi ana mavazi mwilini mwake
mengine yote hakuyajali.
Hakuwa mtu wa starehe wala nini.
Kila mara nilipotaka kumuumiza moyo yeye kwanza hakuonekana kuumizwa.
Jambo hili lilinikasirisha sana na hii ndiyo ilipelekea kukutana na Ester na
kuanzisha naye mahusiano.
Mara kwa mara Dada yangu ambaye alikuwa ni wa kwanza kuzaliwa,Salma alikuwa akinisisitiza kwamba mke wangu hapaswi
kujua kila kitu changu.
Na nilimuamini sana dada yangu kuliko mke wangu na kwa kiasi fulani dada yangu alikuwa hampendi mke wangu.
Ijapokuwa kila mara alipokuja kunitembelea nyumbani mke wangu alimhudumia vizuri sana huku akimfungashia zawadi
wakati akiondoka.
Mara zote Dada Salma hakuonyesha chuki wakiwa pamoja hii ilinifanya niamini kuwa hamchukii.
Mke wangu alijaliwa ukarimu kwa ndugu zangu wote na majirani hakika walimpenda sana.
Tulikaa miaka mitano mpaka mke wangu alipokuja kubeba tena mimba nyingine.
Na hapo ndipo tulipompata mtoto wetu mwingine Abdul.
Nilimuwaza mke wangu na nikaamua kukurupuka.
“Unaenda wapi?”
Ester aliniambia.
“Naenda nyumbani kwangu.”
“Unapoondoka hapa na usirudi tena.”
Alisema.
“Huyo mkeo si umemuaga unarudi baada ya wiki moja.”
Niliona anaongea ujinga.
Hapo ndipo nilipokumbuka kwamba simu yangu ilikuwa imezimwa tangu nilipofika hapo.
Niliwaza kutoa taarifa ofisini kwangu ya kwamba sijafa bado niko hai.
Niliamua kuwasha simu wakati niko njiani kuelekea nyumbani kwangu.
Wakati huo ilikuwa ni takribani saa nane.
Niliogopa kumpigia bosi simu.
Niliogopa kumpigia mtu yoyote yule simu.
Nilikuwa nikiangalia simu yangu kana kwamba nimeshika bomu hakika ilikuwa ya kuogopesha sana.
Niliwaza hali ambayo alikuwa nayo mke wangu kwa wakati huo.
“Hata hivyo familia itakuwa inamfariji.”
Niliwaza.
“Marafiki zangu wote watakuwa wapo nyumbani sasa hivi.
Usikute hata bosi wangu yupo nyumbani.”
Niliwaza.
“Kazini kwangu watakuwa wanasikitika sana watoto wangu je? Watakuwa wanawaza wataishije bila baba.
Ila nina hakika hamna kitu kitakachobadilika.”
Niliwaza na kuwazua mpaka wakati mwingine nilianza kutabasamu mimi mwenyewe.
Kuonesha jinsi gani mimi binafsi nilikuwa nikiogopa kifo changu.
“Utasema nimekufa kweli bwana.”
Nilisema huku nikiachia kicheko.
Niliamua kufungua data.
Na kilichonifanya nifungue data ni wazo la kwamba ofisini kwetu tulikuwa tuna group letu la whatsapp.
Nilitaka kutoa taarifa kupitia ujumbe mfupi wa whatsapp.
Na ilikuwa ni baada ya kukuta sikuwa na salio la kutuma meseji.
Nilitaka kutoa taarifa kwa pamoja na imfikie kila mtu kwamba mimi sijafa endapo nikikuta taarifa tayari zimeshafika ofisini.
“R.I.P MUDI.”
Mara baada ya kufungua whatsapp yangu ndicho kichwa cha habari nilichokutana nacho.
Asilimia kubwa ya magroup yangu yalikuwa yameandikwa hivyo huku yakiwa yamepambwa na picha yangu.
Siyo siri nilichanganyikiwa nilitoa mguno ambao ulimshitua kila mtu ndani ya daladala niliyokuwepo.
Nilivuta pumzi na kushusha.
“Pagumu.”
Hali hiyo ilinishinda kutofautisha kati ya group la kazini na magroup mengine ambayo nilikuwepo.
Nilianza kufungua group moja mpaka lingine.
Na mwishowe nilifika katika group ambalo nilikuwa nikilitafuta.
Nilifungua.
Bosi ndiye aliyetoa taarifa ya msiba wangu ndani ya group.
Nilimjua fika bwana Bakili alikuwa akipendezewa sana na uchapakazi wangu.
Na mara kwa mara alikuwa akijivunia mimi kuwa mmoja ya wafanyakazi katika ofisi yake.
“Tunasikitika kutangaza kifo cha Mudi ambaye alipata ajali ya gari wakati akielekea Mwanza. Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi.”
Zilifuatiwa na meseji za watu wengi ambao ni wafanyakazi wenzangu waliokuwa wakiandika R.I.P huku wakiambatanisha na emoji za
machozi na kulia.
Wakati nikiendelea kushusha nikisoma meseji mbalimbali huku nyingine zikinifurahisha katika group hilo watu mbalimbali
walikuwa wakisifia uchapakazi wangu huku wakionesha kusikitishwa sana na kifo changu hicho bandia.
“Mmmh.”
Mguno wa fadhaa ulinitoka.
Nilikutana na picha ambayo niliifungua na kukuta ni tangazo la kazi huku bosi akiwa ametangaza nafasi yangu ya kazi
kwaajili ya kutafuta mtu wa kuikaimu.
“Jitahidini tushare hili tangazo ili tupate mbadala wa bwana mudi ambaye ametangulia mbele za haki.”
“Yani siku moja tu tayari wameshaanza kutafuta mtu wa kunireplace?!”
Mawazo yalipita akilini mwangu.
“Mmmhhh…”
Niliguna.
“Sasa wakipata mtu mwingine…”
Huku upande wa pili ukiniambia kwamba lazima umtafute mfanyakazi mwingine kazi haziwezi kusimama kwasababu mimi nimekufa.
Nilitoka upande wa magroup na kuamia kwa upande wa hadhi.
Picha yangu ilikuwa imejaa katikati ya karibia kila namba yangu ya simu iliyokuwepo.
Watu waliandika maneno mbalimbali hata watu ambao nilikuwa nawadai na walikataa kunilipa siku hiyo walinipost
na kisha kuandika maneno ya kuonesha jinsi gani wameguswa na msiba wangu.
“Aaanh watu wanafiki bwana.”
Hadi wale watu ambao tulikuwa hatuongei siku hiyo walinipost huku wakielezea kiasi gani wameumia.
Nilipitia baadhi ya status huku nikicheka.
“Duuuh naushuhudia msiba wangu mimi mwenyewe.”
Siyo kwamba nilicheka kwa kufurahi hapana lakini nilicheka kwa kuumia.
Mambo yamekuwa ndivyo sivyo kila kitu nilichokiona kilinishitusha.
Nilikuja kushituliwa gari likiondoka kituoni pale Tabata hata sikujua ni saa ngapi tumefika.
Gari tayari lishaanza kutembea.
“Nishushe nishushe please…”
Nilipiga kelele kwa sauti watu walianza kucheka.
“Wewe umesinzia?”
Konda aliniambia.
Gari lilisimama na kisha nilikurupuka na kushuka.
Nilikuwa nimevaa suruali yangu ambayo niliondoka nayo nyumbani na shati.
Niliogopa kwenda nyumbani kwangu hivyo nilitoa wallet yangu iliyokuwa mfukoni na kisha kuangalia mule ndani nilikuta
nina kiasi kizuri tu cha pesa.
Nilitoka na kisha kuelekea moja kati ya maduka yaliyokuwepo hapo karibu.
Nilivutiwa na duka la nguo za kiislamu lililokuwepo hapo nilienda na kisha kununua kanzu, kibarakashee pamoja na kimtandio.
Nilivivaa vyote hapohapo mpaka muuzaji alinishangaa.
“Salama?”
Aliniuliza.
“Ndiyo salama.”
Nilijibu kwa harakaharaka na kisha kuondoka.
Haikuwa rahisi mtu kunijua kama ni mimi.
Nilitafuta na miwani zilizokuwa zikiuzwa na wamachinga waliokuwepo maeneo hayo ya stendi ya Tabata na kisha kujipachika usoni.
Niliita usafiri wa bodaboda na kisha kupanda kuelekea maeneo ya nyumbani kwangu.
Jioni tayari ilikuwa imeshafika.
Kama nilivyotegemea nyumbani kwangu kulikuwa na watu wengi sana.
Kilio kilisikika kutoka ndani sikuwa na shaka huyo alikuwa ni mke wangu ilikuwa ni sauti pekee iliyovuma kwa nguvu
na niliisikia kutoka mbali sana.
“Huyu mwanamke analia na mengi.”
Niliwaza.
Nilishukia mbali na nyumbani ili nisiweze kutambulika.
Nilianza kutembea kwa mwendo wa kusuasua mpaka nilipokaribia nyumbani kwangu nilienda kukaa viti vya nyuma upande ambao wanaume
walikuwa wamekaa.
Kwa upande wa wanaume walipokuwa wamekaa kulikuwa na wanawake kadhaa walikuwepo maeneo hayo.
Minong’ono mingi ilisikika.
Nilijaribu kutafuta watu ambao nilikuwa nikifahamiana nao sikuona hata mmoja.
Hakukuwa na mfanyakazi yeyote kutoka ofisini kwangu.
Kwa mbali niliweza kuona marafiki zangu wachache, wachache sana tofauti na wale ambao nilikuwa nimewazoea.
Wamama kadhaa walionekana kushughulika.
Nilisikia wababa wakiongea.
Na mimi nilivuta sikio langu ili nisikie ni nini walichokuwa wakikiongea.
“Inasemekana bwana huyu mwanamke ndiyo kamuua mumewe ili arithi mali.”
“Mmmh kamuua mumewe si ajali hiyo?!”
“Mimi nimewasikia wamama kule jikoni walikuwa wanaongea wakati natoka msalani.”
“Hawa wamama nao, mtu kabisa amepata ajali watu wote kwenye gari wamekufa sasa amemuuaje?”
“Huwezi jua duniani kuna mambo mengi.”
Alisema mwingine.
“Aaah nyie achaneni na stori za kina mama bwana.”
Alijitokeza mbaba mtu mzima ambye kiukweli ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona.
Alirekebisha koo lake huku akimaanisha watu waanze kumsikiliza.
Hata wakina mama waliokuwa wanashughulika hapa nyumbani waliacha shughuli zao wote na kumsikiliza yule mzee.
“Napenda nishukuru kila mmoja wenu kwa kuja mahali hapa.”
Aliongea kwa sauti ya kukwaruza.
“Lakini kutokana na ukweli kwamba mwili wa marehemu ulishindwa kupatikana na asilimia kubwa ya miili imeharibika vibaya mno hivyo
kunalazimika kuzikwa katika kabuli la pamoja hukohuko.
Ni kwamba mara baada ya chakula cha jioni tunaanua matanga hivyo watu wote wanaruhusiwa kuondoka.
Wanafamilia tu pekee watabakia kwaajili ya kujadili mambo machache, tunashukuru sana kwaajili ya uwepo wenu mahali hapa.”
Aliongea na watu kuachia miguno mbalimbali.
“Mmmh aisee.”
Huku wakinionea huruma sana.
Niliketi tu upande wa nyuma.
Ilipofika saa kumi na mbili vyakula vilianza kugaiwa.
Ilikuwa tu wali na maharage ambayo hata haukupikwa vizuri.
Nilitegemea kwenye msiba wangu watu wangekula sana hata hivyo ilikuwa kinyume.
Kwanini lakini inamaanisha dada ameshindwa kuandaa chakula kizuri.
Mawazo mengi yalinipitia nilijikuta tu nikitikisa kichwa change huku nikisonya.
“Vipi bro…”
Aliniuliza kijana ambaye alikuwa pale mbele yangu.
“Aaanh nimesikitika sana.”
Nilimuambia.
“Kazi ya Mungu bwana.”
Hakuonekana kunigundua kabisaa.
Mara baada ya kumaliza chakula ni kweli watu walianza kupungua mpaka kufikia kiasi cha saa mbili usiku asilimia
kubwa ya watu walikuwa wameishaondoka wakina mama wachache waliobakia kuosha vyombo walikuwa wakimalizia na mara baada
ya kumaliza waliondoka.
Walibaki watu wachache sana.
Niliona kati yao akinyanyuka na kisha kuelekea ndani ya nyumba yangu.
Nilibaki nimejibanza tu ukutani haikuwa rahisi sana kuniona.
“Sasa naingiaje humu ndani?!”
Nilikuwa nikiwaza.
“Ila afadhali watu wamepungua.”
Nilijiambia.
“Heeee hapa sasa naweza nikaingia, dada yangu yupo na mke wangu yupo nijioneshe kwanza kwao.
Nifanye utaratabu wa kuwasiliana na ofisini kwangu ila wale hata wakipata mtu mwingine hawaniumizi kichwa
kwanza nina biashara zangu zimesimama vizuri kabisa.”
Niliwaza nikiwa nimesimama pale ukutani.
Nilivuta pumzi na kuzishusha.
“Ngoja niende sasa.”
Nilijiambia.
Nilipiga hatua mbili na kisha kusimama ghafla.
Unaweza pia kusoma: