Kuota meno kwa mtoto (Umri gani? Je yanasababisha homa? Jinsi ya kumsaidia kama anapata maumivu)
Swala la kuota meno kwa mtoto huja tofauti kwa kila mtoto.
Ila ni kawaida mtoto kuota meno ya mwanzo ndani ya mwaka wake wa kwanza wa ukuaji.
Kuna baadhi ya watoto wanazaliwa na meno, wengine uota meno ya kwanza kabla ya kutimiza miezi minne na wengine
uchelewa kuota mpaka baada ya miezi 12.
Ila asilimia kubwa ya watoto huota meno ya kwanza wanapotimiza miezi 6.
Meno yote mdomoni kwa mtoto hukamilika kuota mtoto anapotimiza miaka kati ya 2 mpaka 3.
Kuna baadhi ya watoto meno uota bila kuambatana na maumivu au hali yoyote inayomsumbua mtoto.
Pia kuna wengine hupata dalili hizi meno yanapoanza kuota:
- Kuwa na kidonda na fizi kuwa nyekundu mahali jino linapoota.
- Anakuwa na shavu jekundu.
- Anaweza kuwa na vipele usoni.
- Anakuwa anasugua masikio yake mara kwa mara.
- Mtoto anakuwa anatema sana mate kuliko kawaida.
- Anakuwa nan’gata na kutafuna vitu mara kwa mara kuliko kawaida.
- Mtoto anakuwa mwenye wasiwasi kuliko kawaida.
- Pia mtoto anakuwa hapati usingizi vizuri.
Pia kuna baadhi ya watu wanaaini kuwa kuota meno mtoto kunaweza kumsababishia mtoto kuharisha ila hakuna tafiti za kisayansi zilizothibitisha kama kuna uhusiano wa kuharisha na meno kuota.
Kama mtoto unamuona anateseka na meno wataalamu wanashauri kufanya mambo yafuatayo ili kumpunguzia maumivu.
Kwasababu kila mtoto ana upekee wake unashauriwa kujaribu njia tofauti na kuangalia ipi inamfaa mwanao.
1. Kutumia bangili ya meno.
Kuna vibangili ambayo vimetengenezwa maalumu kwaajili ya mtoto kung’ata ng’ata.
Anapokuwa anang’ata inamsaidia kukanda fidhi zake na kumpunguzia maumivu ya meno yanayoota.
Pia kuna baadhi ya bangili ambazo hupoozwa kwenye friji kwanza ili kupunguza maumivu kwa haraka.
Ila haishauriwi kuweka kwenye friza kwasababu ikipata baridi kali sana inaweza kumuumiza mtoto.
2. Mpe mtoto matunda ya kutafuna.
Kwa mtoto mwenye miezi 6 au zaidi kumpa matunda kama vile tikiti maji akiwa anatafuna inasaidia kumpunguzia mauvu ya fidhi kama meno yanaanza kuota.
Kumfurahisha au kucheza na mwanao pia inasaidia kumpunguzia maumivu ya fizi, pia inashauriwa kumsugua mtoto fizi kwa kidole kisafi kumpunguzia maumivu.
Mwisho kama mbinu hizi zitashindikana inashauriwa kutumia dawa za kutuliza maumivu kwa mtoto kwa kufuata maelekezo utakayopewa na mtaalamu wa dawa.
Na kama maumivu hayo yataendelea kumsumbua mtoto kiasi cha kumfanya ashindwe kula wala kunywa ni muhimu kumuona daktari haraka kwa uchunguzi zaidi.
Unaweza pia kusoma: