Ukuaji wa mtoto tumboni kwa mama mjamzito mwenye mimba ya miezi sita.
Mimba ni mchakato wa asili wa muda mrefu kwa binadamu, inachukua takribani siku 280 au wiki 40 ambayo pia inakadiriwa miezi 9 mpaka mtoto kuzaliwa na kuwa na uwezo wa kuyaishi mazingira ya nje ya tumbo la mama.
Mchakato huu kwa mtoto huanzia kwenye seli moja tu ambayo ni mchanganyiko wa yai la mama na mbegu ya baba.
Seli hiyo hugawanyika mpaka kupata mamilioni mengine ya seli ambazo huunda viungo mbalimbali ndani na nje ya mwili wa mtoto.
Kuna hatua mbalimbali ambazo mtoto tumboni anazipitia kutoka yai la mama kurutubishwa mpaka wakati wa kujifungua.
Tufahamu nini kinachoendelea tumboni kwa mama mjamzito katika miezi yake yote 9 mpaka kujifungua.
Kwenye mwezi wa sita ukuaji wa mtoto tumboni unaongezeka kwa kasi mpaka kufikia makadirio ya urefu wa inchi 12 na uzito wa gramu 800.
Ngozi ya mtoto bado inakuwa na uangavu pia ngozi yake bado inaendelea kuzalisha vinywele vingi pamoja na uteute
mweupe unaoifunika ngozi kuilinda ngozi isiharibiwe na hali ya majimaji kwenye mfuko wa kizazi.
Pia vinasaidia kuzuia ngozi ya mtoto isipoteze joto la mwili.
Katika kipindi hiki kope za mtoto ndipo zinaanza kufunguka na kuruhusu mboni za macho ya mtoto kujitokeza.
Kutoka kwenye mwezi wa tano ambapo alama za vidole vya mtoto zilianza kujitengeneza, mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi wa sita alama za vidole vya mkononi na miguuni zinakuwa tayari zimekamilika.
Usikivu wa mtoto nao unakuwa umeimarika kiasi ambacho anaweza kusikia mapigo ya moyo ya mama yake, kusikia sauti za upumuaji
wa mama yake pamoja na miungurumu ndani ya tumbo la chakula kwa mama yake.
Pia anaweza kushituliwa na sauti nje ya tumbo la mama.
Mtoto tumboni anaweza kupata kwikwi na mama anaweza kuhisi mishituko ya mtoto tumboni kama ana kwikwi.
Mapafu ya mtoto yanakuwa tayari yameshajitengeneza ila uwezo wa mapafu wa kuweza kupokea hewa kutoka nje ya tumbo la mama
unakuwa bado ni mdogo sana.
Hivyo ikitokea mtoto atazaliwa katika kipindi hiki anaweza kuendelea kukua endapo atakuwa chini ya uangalizi wa
karibu sana wa madaktari.
Mwili wa mtoto katika kipindi hiki unaendelea kuzalisha mafuta na kuyaifadhi mafuta hayo mwilini kwaajili ya shughulu mbalimbali za mwili.
Kwasababu ya upungufu wa mafuta ngozi ya mtoto inaonekana kuwa na mikunjo sana.
Kwa mama mjamzito katika kipindi hiki cha miezi sita anaendelea kupata dalili za kawaida kama vile kiungulia, kuhisi joto kali mwilini na
maumivu ya mgogo.
Na wakati mwingine mama mjamzito anaweza kupata hali ya kuvimba miguu.
Unaweza pia kusoma: