Muonekano wa Giza:

Msaada

Picha inaonesha hatua mbalimbali za ukuaji wa mtoto tumboni kwa mama mjamzito

Ukuaji wa mtoto tumboni kwa mama mjamzito mwenye mimba ya mwezi mmoja.

Mimba ni mchakato wa asili wa muda mrefu kwa binadamu, inachukua takribani siku 280 au wiki 40 ambayo pia inakadiriwa miezi 9 mpaka mtoto kuzaliwa na kuwa na uwezo wa kuyaishi mazingira ya nje ya tumbo la mama.

Mchakato huu kwa mtoto huanzia kwenye seli moja tu ambayo ni mchanganyiko wa yai la mama na mbegu ya baba.
Seli hiyo hugawanyika mpaka kupata mamilioni mengine ya seli ambazo huunda viungo mbalimbali ndani na nje ya mwili wa mtoto.

Kuna hatua mbalimbali ambazo mtoto tumboni anazipitia kutoka yai la mama kurutubishwa mpaka wakati wa kujifungua.
Tufahamu nini kinachoendelea tumboni kwa mama mjamzito katika miezi yake yote 9 mpaka kujifungua.

Katika mwezi wa kwanza wa ujauzito.
Safari huanzia katika mirija ya uzazi (Fallopian Tube).
Kwenye mirija ya uzazi ambapo yai la mama hukutana na mbegu za baba.
Ndani ya masaa 24 toka kukutana kwa yai na mbegu, yai hilo huanza kugawanyika kutoa seli nyingine nyingi ambazo zinaanza kumtengeneza mtoto.

Wakati yai hilo likiendelea kugawanyika hushuka taratibu kutoka kwenye mirija ya uzazi kushuka kuelekea kwenye mfuko wa kizazi.

Kuna sababu kadhaa zinaweza kusababisha yai hilo kushindwa kushuka na kubakia kwenye mirija ya uzazi.
Hali hiyo husababisha mimba kutunga nje ya mfuko wa kizazi, hali ambayo si salama kwa mama mjamzito.
Mimba kutunga nje ya kizazi inaweza kumsababishia mama mjamzito maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu, kutokwa na damu ukeni na maumivu ya bega.

Kama ni mjamzito na ukaona dalili hizo ni vizuri kuwahi hospitali kwa msaada zaidi.

Inachukua siku 3 mpaka 5 seli hizo za mtoto kushuka kutoka kwenye mirija ya uzazi mpaka kwenye kwenye mfuko wa kizazi.
Seli hizo baada ya kufika kwenye mfuko wa uzazi huendelea kugawanyika zaidi na kujichimbia ndani ya kuta za mfuko wa kizazi.

Mifumo mbalimbali ya kumkinga na kumlisha mtoto akiwa tumboni inaanza kujitengeneza kwenye mwezi wa kwanza wa ujauzito.
Hata kondo nalo huanza kujitengeneza mwezi wa kwanza kumsaidia mtoto kupata virutubisho vyake kutoka kwa mama.

Japokuwa katika mwezi wa kwanza wa ujauzito mtoto tumboni anakuwa katika umbile dogo sana kuliko hata punje ya mchele, lakini uso na macho yake yanaanza kujitengeneza.
Pia moyo wa mtoto unajitengeneza na kuanza kudunda na kusukuma damu kwenye mishipa mikuu ya damu kwenye mwezi huu wa kwanza wa ujauzito.

Katika kipindi hiki cha mimba changa ndio kipindi ambacho mama mjamzito anashauriwa kuzingatia matumizi ya vidonge vya vitamini anavyopewa kliniki.
Vitamini hivyo kama vile vitamini B6 na Folic acid ni muhimu sana kwa ukuaji huu wa mwanzo wa mtoto.

Kipindi hiki cha ukuaji hutokea kwa wajawazito asilimia kubwa wakiwa hawana taarifa kuwa ni wajawazito.
Ili kuongeza usalama kwa mama mjamzito na mtoto wake tumboni inashauriwa kutumia vidonge hivyo vya vitamini kipindi anachojiandaa kubeba mimba.

0
0
1