Ukuaji wa mtoto tumboni kwa mama mjamzito mwenye mimba ya miezi mitano.
Mimba ni mchakato wa asili wa muda mrefu kwa binadamu, inachukua takribani siku 280 au wiki 40 ambayo pia inakadiriwa miezi 9 mpaka mtoto kuzaliwa na kuwa na uwezo wa kuyaishi mazingira ya nje ya tumbo la mama.
Mchakato huu kwa mtoto huanzia kwenye seli moja tu ambayo ni mchanganyiko wa yai la mama na mbegu ya baba.
Seli hiyo hugawanyika mpaka kupata mamilioni mengine ya seli ambazo huunda viungo mbalimbali ndani na nje ya mwili wa mtoto.
Kuna hatua mbalimbali ambazo mtoto tumboni anazipitia kutoka yai la mama kurutubishwa mpaka wakati wa kujifungua.
Tufahamu nini kinachoendelea tumboni kwa mama mjamzito katika miezi yake yote 9 mpaka kujifungua.
Katika kipindi hiki cha miezi mitano ya ujauzito, ndicho kipindi ambacho asilimia kubwa ya wajawazito huanza kuhisi vizuri mtoto akicheza tumboni.
Katika mwezi wa tano wa ujauzito ukuaji wa mtoto unaenda kwa kasi mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi wa tano urefu wa mtoto unakadiriwa kufikia inchi 10 na uzito wa gramu 400.
Alama za vidole na kucha za mtoto zinaanza kujitengeneza katika kipindi hiki.
Japokuwa ngozi ya mtoto inakuwa nyembaba lakini inakuwa na mafuta mengi ili kumuongezea mtoto joto la mwili.
Pia ngozi yake inakuwa imefunikwa na uteute mweupe mzito ili kuilinda ngozi isiathiriwe na maji ya kwenye mfuko wa kizazi.
Mbali na uteute huo kwenye ngozi pia katika kipindi hiki ngozi inakuwa imefunikwa na vinyweleo ambavyo vinasaidia kuongeza joto la mwili na kuilinda ngozi ya mtoto.
Mtoto anakuwa na utaratibu wake wa kulala na kuamka akiwa tumboni, na makelele nje ya tumbo yanaweza kumshitua akiwa usingizini.
Mifupa na misuli ya mtoto inakuwa imekomaa vya kutosha na ndio katika kipindi hiki mama anaweza kuyahisi mateke na ngumi za mtoto wake vizuri.
Na kwa mtoto wa kike mfuko wa kizazi unaanza kijitengeneza katika kipindi hiki.
Kwa mama mjamzito hali aliyokuwa anapitia kwenye mimba ya miezi minne inaendelea kutokea.
Kiungulia, kupata choo kigumu, mabadiliko kwenye matiti, kizunguzungu, kutokwa na damu puani na kwenye fizi
na wakati mwingine kupata shida ya kupumua ni hali za kawaida kwa mjamzito wa miezi mitano.
Mapigo ya moyo ya mama yanaweza kuongezeka ni hali ya kawaida ili kupeleka damu nyingi kwa mtoto.
Katika kipindi hiki mama mjamzito anashauriwa kulala angalau kwa masaa nane kwa siku, na pia kupata mapumziko wakati wa mchana.
Unaweza pia kusoma: