Ukuaji wa mtoto tumboni kwa mama mjamzito mwenye mimba ya miezi mitatu.
Mimba ni mchakato wa asili wa muda mrefu kwa binadamu, inachukua takribani siku 280 au wiki 40 ambayo pia inakadiriwa miezi 9 mpaka mtoto kuzaliwa na kuwa na uwezo wa kuyaishi mazingira ya nje ya tumbo la mama.
Mchakato huu kwa mtoto huanzia kwenye seli moja tu ambayo ni mchanganyiko wa yai la mama na mbegu ya baba.
Seli hiyo hugawanyika mpaka kupata mamilioni mengine ya seli ambazo huunda viungo mbalimbali ndani na nje ya mwili wa mtoto.
Kuna hatua mbalimbali ambazo mtoto tumboni anazipitia kutoka yai la mama kurutubishwa mpaka wakati wa kujifungua.
Tufahamu nini kinachoendelea tumboni kwa mama mjamzito katika miezi yake yote 9 mpaka kujifungua.
Kipindi cha mwezi wa tatu wa ujauzito, viungo mbalimbali ya kijusi vinaendelea kukua.
Mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa tatu wa ujauzito muonekano kamili wa mtoto unakuwa umekamilika.
Muonekano wa kijusi pamoja na mkia wake vinapotea na kuwa na umbile kamili la mtoto la kawaida.
Japokuwa jinsia ya mtoto bado ni ngumu kujulikana hata kwa kipimo cha ultrasound lakini mifumo ya uzazi inaanza kujitengeneza katika kipindi hiki.
Mikono, kiganja na vidole vya mkononi, miguu na vidole yake vinakuwa vimekamilika na sasa mtoto anaweza kukunja ngumi na kufungua.
Mwanzoni vidole vyake vinakuwa kama vidole vya bata na mpaka kufika mwishoni mwa mwezi wa tatu wa ujauzito ngozi hiyo ya katikati inakuwa
imepotea.
Pia ana uwezo wa kufungua na kufumba mdomo wake.
Mifupa ya mtoto inaendelea kukomaa, ngozi na kucha za vidoleni zinaendelea kukua.
Figo za mtoto zimekua na kuanza kutoa mkojo.
Na kwa wakati huu kope za mtoto juu na chini zinakua bado zimejishika na kufunika macho.
Urefu wa mtoto kutoka kichwani mpka kwenye makalio katika kipindi hiki unakadiriwa kuwa sentimita 6 mpaka 7.5.
Kwasababu katika kipindi hiki asilimia kubwa ya viungo vya mtoto vinakuwa vimekamilika, hivyo uwezekano wa mimba kuharibika nao unapungua kwa kiasi kikubwa baada ya miezi hii mitatu ya ujauzito.
Kwa mama mjamzito dalili alizozipata katika mwezi uliopita zitaendelea au kuongezeka zaidi katika mwezi huu mitatu ya ujauzito.
Matiti yanaongezeka ukubwa na kupata mabadiliko mengine kwenye matiti kama vile kuongezeka kwa chuchu na kuwa nyeusi zaidi.
Na kama mjamzito ana ngozi ya chunusi kipindi hiki zinaweza kuongezeka zaidi ya kawaida.
Unaweza pia kusoma: