Ukuaji wa mtoto tumboni kwa mama mjamzito mwenye mimba ya miezi miwili.
Mimba ni mchakato wa asili wa muda mrefu kwa binadamu, inachukua takribani siku 280 au wiki 40 ambayo pia inakadiriwa miezi 9 mpaka mtoto kuzaliwa na kuwa na uwezo wa kuyaishi mazingira ya nje ya tumbo la mama.
Mchakato huu kwa mtoto huanzia kwenye seli moja tu ambayo ni mchanganyiko wa yai la mama na mbegu ya baba.
Seli hiyo hugawanyika mpaka kupata mamilioni mengine ya seli ambazo huunda viungo mbalimbali ndani na nje ya mwili wa mtoto.
Kuna hatua mbalimbali ambazo mtoto tumboni anazipitia kutoka yai la mama kurutubishwa mpaka wakati wa kujifungua.
Tufahamu nini kinachoendelea tumboni kwa mama mjamzito katika miezi yake yote 9 mpaka kujifungua.
Kwenye mimba ya miezi miwili, sura ya mtoto inaendelea kujitengeneza na masikio yanaanza kuchomoza pembezoni ya kichwa.
Mikono na miguu inaanza kuchomoza pamoja na vidole vya mkono na miguu vinaanza kuchomoza kwenye mwezi huu wa pili wa ujauzito.
Pia katika mwezi huu wa pili mrija unaounda ubongo, uti wa mgongo na mishipa kadhaa ya fahamu unakuwa tayari umejitengeneza.
Mfumo wa umeng'enyaji wa chakula na milango ya fahamu inaanza kujitengeneza.
Kitovu cha mtoto nacho kinaanza kukua kutoka tumboni kwa mtoto mpaka kwenye kondo.
Pia baadhi ya mifupa inaanza kuimarika hali inayoweza kukifanya kijusi hicho kuanza kucheza tumboni ila kwasababu ni bado kidogo sana mama hawezi kuhisi chochote.
Katika mwezi wa pili wa ujauzito kijusi hakina jinsia, haiwezekani kutofautisha wa kiume wala wa kike.
Mara nyingi kwenye mwezi huu wa pili wa ujauzito wajawazito wanaanza kupata dalili kadhaa za ujauzito kama vile maumivu kwenye matiti, kuhisi uchovu kuliko kawaida, kukojoa mara kwa mara kuliko kawaida, kupata kiungulia, kuhisi kichefuchefu na wakati mwingine kutapika.
Mwili nao unaanza kuzalisha damu nyingi ili kukidhi mahitaji ya kiumbe kipya, hali hiyo husababisha kasi ya mapigo ya moyo ya mama kuongezeka ili kusukuma damu ya ziada.
Unaweza pia kusoma: