Muonekano wa Giza:

Msaada

Faida za kula mwani kiafya

Mwani ni aina ya mimea inayoota na kukua kwenye maji chumvi (bahari) na maji baridi (mito, maziwa na mabwawa).

Tofauti iliyopo kati ya mwani na mimea mingine inayokua kwenye nchi kavu ni kwamba mwani hautegemei mizizi kufyonza maji na virutubisho vingine bali hutumia sehemu zote za mmea kuvyonza virutubisho vinavohitajika kutoka kwenye maji.

Kwa Tanzania, Zanzibar ndiyo inayoongoza kwa kilimo cha mwani.

Kuna aina mbalimbali za mwani, kuna mwani mwekundu, kahawia na mwani wa kijani.
Mwani wa kijani ndio unatumiwa na wengi kwa kula.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kisayansi mwani umegundulika kuwa na faida mbalimbali za kiafya kwa binadamu.
Kwa sababu hiyo ulaji wa mwani umeongezeka duniani, na kwa mujibu wa takwimu za duniani ulaji wa mwani unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 9.7 kati ya mwaka 2020 mpaka 2025.
Ongezeko hilo la ulaji wa mwani duniani limeongezeka kwasababu ya faida hizi za kiafya kwa binadamu.

Mwani una madini ya iodine na kirutubisho cha tyrosine kwa wingi ambavyo vinasaidia utendaji kazi wa tezi ya thyroid.
Tezi ya thyroid huzalisha homoni mbalimbali mwilini ambazo zinasaidia ukuaji wa mwili, uzalishaji wa nguvu mwilini, kuzalisha na kuzikarabati seli zilizoharibika mwilini.
Madini ya iodine ni muhimu mwilini ndiyo maana madini hayo huongezwa kwenye chumvi tunazotumia majumbani.

Mwani una viondoa sumu ambavyo husaidia kuondoa sumu mbalimbali mwilini ambazo zinaweza kusababisha uharibifu kwenye seli za mwili hivyo kusaidia kuukinga mwili na magonjwa ya muda mrefu kama vile kisukari na magonjwa ya moyo.

Mwani una nyuzi lishe ambazo zinasaidia kuimarisha afya ya mfumo wa chakula.

Mwani unaweza kusaidia kupunguza uzito.
Kutokana na wingi wa nyuzi lishe kwenye mwani, ukila mwani unakaa muda mrefu tumboni bila kuhisi njaa.
Hali hiyo inakufanya kutokulakula hovyo na kukusaidia kupunguza uzito wa mwili.

Mwani husaidia kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo.
Kuongezeka wa kiwango cha cholesterol mwilini ni moja ya kisababishi cha magonjwa ya moyo.
Tafiti zimeonesha mwani kuna uwezekano ukasaidia kupunguza mafuta ya cholesterol mwilini.

Pia mwani unasaidia kupunguza shinikizo la damu mwilini na kuzuia ugandaji wa damu kwenye mishipa ya damu.
Mwani husaidia kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu hasa kwa wenye aina ya 2 ya kisukari.

Jinsi ya kula mwani.

Unaweza kukaanga mwani na mafuta kidogo pamoja na chumvi kwa wale wanaopenda chumvi.
Pia unaweza kuupika mwani kama mboga na kuuchanganya na chakula kama vile wali na ugali.
Pia kwa watu ambao hawafurahii ladha ya mwani unaweza kuchanga mwani na mboga nyingine ya majani unayoipenda kuepuka ladha ya mwani.

Kuna baadhi ya tahadhari unazopaswa kuzifahamu unapokula mwani.
Kuzidi kwa kiwango cha madini ya iodine mwilini.
Kwasababu ya wingi wa madini ya iodine kwenye mwani inashauriwa kula mwani angalau mara moja au mbili kwa wiki.
Madini ya iodine yanapozidi mwilini husababisha tezi ya thyroid kushindwa kufanya kazi vizuri.

Hatari ya kupata sumu za metali nzito.
Risasi na zebaki ni baadhi ya metali nzito ambazo zinaweza kufyonzwa na mwani kutoka baharini, metali hizo ni sumu kwa binadamu.
Hivyo unashauriwa kununua mwani kutoka kwenye chanzo kinachooaminika.

0
0
1