Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Hyung Nim - Episode 01

Aliniomba urafiki katika mtandao wa kijamii wa Facebook.
Ilikuwa ni wakati niko likizo ya mwisho kabla sijamaliza elimu yangu ya sekondari kidato cha sita katika shule ya wasichana ya Ruvu iliyoko mkoani Pwani.
Nilikubali ombi lake kama nilivyokuwa nikikubali maombi ya watu wengine nilijua ni moja kati ya marafiki wengi niliokuwa nao.
Alikuja sehemu ya ujumbe mfupi akanisalimia.
“Mambo Jenny.”
“Poa.”
Nilimjibu kiuchangamfu tu.
“Mzima?”
“Mzima, sijui wewe.”
Nilijibu.
“Pande za wapi?”
Aliuliza.
“Nipo Kilwa, uwanja wa taifa.”
Nilimjibu.
“Aaah, nipo Dar karibu.”
“Ahsante.”
Nilijibu.
“Mishe zipi?”
Aliuliza.
“Nasoma.”
“Unasoma wapi?”
“Ruvu, Pwani, HGE.”
Nilimjibu kwa mkato.
Nilianza kutopendezwa na maswali yake mengi yasiyo na maana.
“Anataka nini huyu?!”
Niliwaza.
“Sawa karibu Dar, mimi niko pale chuo kikuu cha Dar es salaam nasomea Accounting.”
“Wooow! Hongera ni ndoto yangu pia.”
Hatimaye kati ya mambo yote ambayo alikua akiniongelesha hilo la kwanza alinifurahisha.
“Nilikuwa na ndoto ya kufika chuo kikuu cha Dar es salaam na kusomea mambo ya Accounting.”
Kwa hilo nilimpenda.
“Naomba basi namba yako ya simu.”
Alisema.
Nilipoisoma hiyo meseji nilikasirika.
“Fyuuu.”
Nikasonya.
“Kumbe walewale tu.”
Alikuwa ni moja wapo kati ya wanaume wengi ambao walikuwa hawaishi kuniomba namba ya simu katika mtandao wa Facebook.
Nikamuambia.
“Hivi karibuni nitarejea shuleni kwahiyo haitakuwa na maana.”
“We nipe tu nikae nayo ukirudi shuleni nitakutafuta.”
Aliongea kiunyonge.
Nikaamua tu kumpa kwani nilijua mpaka nitakaporudi shuleni angekuwa amekwisha ipoteza.
“Ahsante.”
Alishukuru.
Na kisha akanitumia meseji kwenye namba yangu.
“Ni mimi Gibson.”
Nikamjibu kiufupi.
“poa.”
Siku iliyofuata nilienda shuleni.

MIEZI MITANO BAAADAE.

Nilirejea shuleni baada ya kuhitimu elimu yangu ya sekondari, nilikaa nyumbani nikisubiria matokeo yangu ya kidato cha sita kwa ajili ya kujiunga na chuo.
Nilipofika mama yangu alinikabithi simu nzuri kabisa aina ya huawei.
Nilifungua simu yangu na kisha nikajiunga na mtandao wa whatsapp.
Nilikuta namba nyingi za marafiki zangu, nikaanza kuchati nao.
Mara ghafla iliingia meseji katika namba ambayo sikuijua.
“Hello Jenny mambo?”
Aliandika.
“Poa, nani mwenzangu?”
Niliuliza.
“Mara hii ushanisahau au namba yangu umefuta?”
Alinitumia text hiyo.
“Sikujui naomba uniambie wewe ni nani.”
Nilimjibu kwa dharau.
“Aaah bwana! Mimi Gib.”
Aliniandikia.
“Gib! Mbona sikujui.”
“Gibson, Gibson Jude.”
“Aaah! Gibson niambie za siku.”
Nilijibu kiunyonge wala sikupendezwa kuwa na mawasiliano nae.
“Poa tu, naona ukafuta namba yangu.”
“Aanh, hamna sikufuta.”
Nilimjibu.
“Sawa niambie.”
Alionekana kuchukulia kawaida tu.
“Poa, hongera kwa kumaliza shule.”
Aliniambia.
“Aaaah ahsante.”
“Mtihani ulikuaje?”
“Kawaida tu.”
“kwahiyo utafaulu si ndio.”
“Yaah kufaulu lazima.”
Nilijibu.
“Hongera bwana, una ndoto za kwenda kusomea wapi?”
Sikutaka kumuambia nia yangu ya kwenda kusoma chuo kikuu cha Dar es salaam.
“Nataka niende kusoma chuo kikuu cha Dodoma.”
“Kwanini umechagua chuo kikuu cha Dodoma.”
“Nimepapenda tu Dodoma sitaki kuishi sehemu nyingine zaidi ya Dodoma.”
Nilimuambia.
“Sawa kama unapendelea iwe hivyo.”
Tuliendelea na urafiki wa karibu.

Hatimaye siku moja aliniambia kitu cha kunikera.
“Jenny nakupenda naomba uwe mpenzi wangu.”
Nilishangaa huyu mkaka vipi hanijui hata hajawahi kuniona anaanza kuleta mambo yake ya ajabu ajabu.
Kanikuta tu Facebook.
“Fyuuu.”
Nilisonya.
“Sorry nina boyfriend wangu.”
Nilimwambia.
“Jenny unaniumiza, nakupenda sana nimekusubiri kwa muda wote huo.”
“Am sorry nampenda sana Tony siwezi kumwacha nampenda sana na siwezi kumsaliti naomba tu tuwe marafiki.”
Nilimuambia.
Alikubali kwa shingo upande.
Tuliendelea kuwasiliana kama marafiki wa kawaida.
Niliwaonyesha marafiki zangu Maria, Angel na Lily picha zake na hata dada yangu Jackline.
Kila nilipowaonesha picha zake hawakutaka kuongea kitu chochote, nilijua wamempuuzia kwa sababu ni wakawaida sana hata mimi nikaanza kumchukulia wa kawaida.
Hakuchoka kuendelea kuwasiliana na mimi mara kwa mara tuliendelea kuwasiliana.
Siku moja nilimuazima dada yangu simu yake.
“Dada naomba simu yako mara moja.”
“Unataka ya nini bwana?”
Aliniambia.
“Aaah we nipe tu mara moja.”
“Halafu simu yangu mbovu unajua whatsapp yangu haidownload picha wala audio yani haidownload kitu chochote vile naomba nitengenezee.”
Dada yangu hakuwa mtundu kama nilivyokuwa mimi, niliweza kuchezea simu na kuzitengeneza.
Hivyo alinikabidhi simu yake nimtengenezee.
Nilipofungua upande wa jumbe fupi nilikuta namba niliyoifahamu ilikuwa ni ya Gibson.
“Gibson anawasiliana na dada yangu!”
Nilishangaa.
“Amemjuaje?”
Nilibaki najiuliza.
“Aaah! Kumbe ndiyo tabia yake huyu Gibson kaniomba mimi namba Facebook akamuomba namba na dada yangu na usikute anatutaka wote.”
“Fyuuu.”
Nilisonya.
“Pumbavu na kuanzia saa hizi sitawasiliana na yeye tena.”
Nilisema.
Mara kwa mara Gibsona alijaribu kunipigia simu sikupokea alituma jumbe zake nilisoma na kisha kuzifuta.
“Kaa mbali na mimi Gibson.”
Niliwaza.
Muda mrefu ulipita bila kuwasiliana na Gibson.
Siku moja nilipokea ujume katika namba nisiyoifahamu.
“Mambo.”
“Poa.”
Nilijibu.
“Nani?”
Niliuliza.
“Gibson!”
Nilishaanza kumsahahu.
“Gib ndiyo nani?”
Niliuliza kwa ukali.
“Aaah Gibson, umenisahau Gibson Jude.”
“Aaah Gibson, Oooh sory.”
Nilisema ingawa sikuwa namaanisha wala sikutaka kumuomba msamaha sikutaka kuwasiliana naye kabisa.
“Usijali vipi?”
“Poa.”
“Tokeo limeshatoka umepata ngapi?”
Aliniuliza.
Sikupenda.
“Nimepata One.”
“Aaah Hongera, hongera sana.”
“One ya ngapi?”
“Nimepata One ya tisa.”
“Aaaah! hongera sana aisee kumbe una akili.”
Nilicheka tu.
“Aaah! Jenny bado una mpango wa kwenda kusoma chuo Dodoma?”
Aliniambia.
Katika maisha yangu hakuna kitu ambacho siwezi kama kumdanganya mtu, nilishindwa kumdanganya.
“Hapana sitaki kwenda kusoma chuo cha vilaza?”
Akacheka.
“Chuo kikuu cha Dodoma siyo chuo cha vilaza Bwana.”
“Just joke.”
Nilimuambia.
“Kwahiyo unataka kwenda chuo gani?”
“Nataka kusoma chuo chochote kilichopo Dar es salaam sitaki kutoka nje ya Dar.”
“Wooow! Karibu sana chuo kikuu cha Dar es salaam.”
“Ahsante ila sijui kozi za kuchagua.”
“Usijali.”
“Mimi sifahamu kozi nyingi sana lakini nitakuunganisha na dada yangu atakusaidia kuchagua kozi.”
“Wooow! nitafurahi sana Gibson.”
Nilimuambia.
Hakika alikuwa mtu mzuri sana Gibson nilipenda ukarimu wake.

Nilikaa nikisubiria anitumie namba ya simu ya dada yake lakini ghafla nilitumiwa ujumbe mfupi wa maandishi.
“Mambo Jenny, mimi naitwa Grace ni dada yake na Gibson ameniambia nije nikupe maelekezo kuhusu kozi za kuchagua katika chuo kikuu cha Dar es salaam.”
Nilifurahi sana.
“Yaah ahsante.”
Aliniorodheshea kozi akinipa na maelezo ya kozi nzuri za kuchagua, nilifurahi sana hakika alinisaidia sana kuchagua kozi nzuri.
Niliweza kuchagua kozi na kumaliza maombi ya vyuo vikuu.
“Karibu sana chuo kikuu cha Dar es salaam.”
Aliniambia.
“Aaah tuombe Mungu tu nichaguliwe hapo.”

Siku zilienda na marafiki zake waliweza kunifahamu, alinitambulisha kwa marafiki zake watatu Wilson, Jose na Albert.
Walikuwa wakinipenda sana hao marafiki zake ingawa hatukuwahi kukutana nao hata siku moja.
Tuliwasiliana katika mitandao mbalimbali, mara nyingi tulipigiana kwa video Call na tulitumia muda mwingi sana kuongea nao.
Familia yangu zima walijikuta wakimfahamu kwa maana kila mara wakinikuta naongea na simu kwa video Call nilikuwa naongea na yeye.
Mama aliniuliza siku moja.
“Huyu mtu ni nani?”
“Ni rafiki yangu mama anaitwa Gibson.”
Mama alicheka.
“Ni rafiki yako kweli?”
Mama aliuliza.
“Ndiyo mama ni rafiki yangu.”
“Sawa kama ni rafiki yako.”
Mama alitilia shaka urafiki wetu.
Nilicheka tu.

Sehemu 2
0
0