Muonekano wa Giza:

Msaada

Kuchudi - Sehemu ya Kwanza (01)

Kuchudi ni kijana mwenye umri wa miaka 21.
Yeye alikuwa akiishi na baba yake mwenye umri wa takribani miaka kenda uliokaribiana na uzee.
Kuchudi na baba yake walikuwa wakiishi kwenye nyumba yao maeneo ya Magomeni.
Nyumba hiyo ilikuwa na baadhi ya wapangaji ambao ndiyo walikuwa wakiisaidia kuipatia familia yao mapato kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Mama yake na Kuchudi alikwishafariki miaka mingi iliyopita, hivyo alikuwa akiishi na baba yake tu akiwa kama mtoto wa pekee.
Baba yake ambaye hakuwa na kazi yoyote ya kufanya mara baada ya kustaafu alikuwa akitegemea pato la kodi ya nyumba kwa ajili ya kupata mahitaji yao ya kila siku.

Mara baada ya kumaliza kidato cha nne na kushindwa kuendelea Kuchudi hakuwa akifanya kitu chochote.
Hakuwa akifanya kazi wala hakutaka kujiendeleza kimasomo.
Alikuwa hajajiunga na vijana wa mtaani, alikuwa hachezi mpira, alikuwa habet alikuwa hana marafiki mtaani.
Yeye alikuwa akipenda kushinda nyumbani huku akifanya kazi mbalimbali kwa vile familia ilikuwa na watu wawili tu.
Alifanya kazi zote kwa muda wa mchana na kila ilipofika saa mbili ya usiku alipenda kutoka na kutembea.
Mara nyingi alipenda kutembea wakati wa usiku kwa sababu wakati huo hakukuwa na kelele nyingi wala jua halikuwa kali.
Mara nyingi baba yake alikuwa akimuonya kuhusu swala hilo la kutembea usiku hata hivyo Kuchudi hakutaka kuelewa.

“Baba mchana jua kali.”
Alikuwa akitoa visingizio.
“Kwanini usitembee mida ya jioni?”
“Aanh kwani nikitembea usiku kuna nini?”
“Sawa kama unaona kutembea usiku ni sawa tembea miguu si yako tembea.”
Baba yake alimuambia.
“Ila asiyesikia la mkubwa yatampata makubwa.”

Aliyasikia maneno ya baba yake hata hivyo hakutaka kuyatilia maanani.
Aliendelea kufanya kazi za nyumbani na ilipofika jioni aliondoka.

Siku hiyo baba yake hakuwepo nyumbani.
Alienda kumsalimia mzee mwenzie nyumba ya jirani.
Ilipofika saa tatu ya usiku baba yake na Kuchudi alikuwa akirejea nyumbani na hapo ndipo alipopishana na Kuchudi alikuwa akitoka.

“Unaenda wapi?”
“Kutembea baba.”
“Kuchudi kwanini mwanangu hutaki kunielewa mara ngapi nakuambia kuhusu swala la kutembea usiku?”
Kuchudi alishachoshwa sana na mawosia ya baba yake.
“Wewe hapo ulipo ni mchana? Bwana baba mimi nachelewa utaniambia nikirudi.”
Baba yake alimuambia.
“Sawa mwanangu nenda, safari njema.”
“Aya baba nawe ubaki salama.”

Kuchudi aliondoka kuelekea katika mizunguko yake.
Alipita mtaa wa kwanza wa pili na wa tatu hapo aliamua kugeuza na kurudi nyumbani.
Wakati akipiga hatua chache ghafla taa zilimmulika usoni.
Alisimama kwa muda ili kuzuia mwanga wa zile taa uliokuwa ukimpiga usoni.
Alipokuja kufumbua macho yake aliwakuta watu wawili wamesimama mbele yake hata hivyo alishindwa kuwatambua kutokana na mwanga mkali uliokuwa ukimpiga usoni.
“Kwanini unatembea usiku?”
“Kwani wewe hapo ulipo ni mchana nije nitembee hapo?”
“Haaa unatujibu nini?!”

Sehemu 2
0
0