Muonekano wa Giza:

Msaada

Kuchudi - Sehemu ya Tatu (03)

Alichoropoka mbio na kisha kukimbia wale wachawi hawakumuacha nyuma.
“Huyu ameshajua siri zetu ameshaona na sura zetu hatuwezi kumuacha.”
Walikuwa wakimkimbiza huku wakiongea kwa kupiga kelele.
Wakati wanafika barabarani wachawi hao walikutana na wale wavuta bangi waliungana na kutengeneza kundi kubwa ilihali kila mmoja akiwa hajui juu ya uwepo wa mwenzie.
Walimuungia tela na kisha kumkimbiza.

Kuchudi alikimbia huku akiomba Mungu.
“Mungu mimi ukinivusha salama kwenye hili janga sitarudia tena kutembea usiku yani hata sehemu yenye giza sitatembea ikifika saa moja tu mimi nitakuwa nimelala.”
Aliendelea kusali sara ambayo hakujua kama ilisikilizwa ama vipi huku akikimbia.
“Naomba unisaidie, naomba unisaidie Mungu kweli mimi nitamsikiliza baba yangu kila anachokiongea.”
Huku akiendelea kukimbia alikatiza hadi sehemu ambayo aliona Kanisa.
Bila kuulizwa aliingia ndani ya kanisa hilo.
Mlinzi aliyekuwa amesimama getini alijaribu kumzuia hata hivyo Kuchudi tayari alikuwa ameshaingia ndani.
Aliingia moja kwa moja hadi kwenye lango la kanisa ambalo lilikuwa wazi.

“Mchungaji…”
Alianza kupiga kelele.
Mchungaji aliyekuwa ofisini kwake pamoja na baadhi ya viongozi wengine ambao walikuwa wakifanya maombi walitoka.
“Vipi?”
Kuchudi alikimbia moja kwa moja na kwenda kumkumbatia mchungaji.
“Mchungaji niokoe.”
Alikuwa akimbembeleza mchungaji.
“Niokoe mimi, niokoe roho yangu, kweli mimi ukinisaidia nitakuwa mkristo mzuri, nitakuwa nahudhuria kanisani, nitakuwa mwana maombi, nitaanza hadi kuimba na kwaya.”
Aliongea.
“Kuna nini?”
“Wananikimbiza wanataka kuniua.”
“Kina nani?”
“Kuna watu wananikimbiza mimi siwajui.”
“Basi ongea vizuri tukuelewe.”
Wazee wa kanisa walimzingira na mchungaji pamoja nao.

Hata hivyo lile kundi kubwa la watu lililokuwa likimkimbiza Kuchudi liliingia hapo na moja kwa moja walienda kusimama pale alipokuwa amesimama mchungaji pamoja na wazee wake wa kanisa.
Kuchudi alijificha nyuma ya mchungaji.
“Vipi?”
Mchungaji na wazee wa kanisa waliogopa.
Wazee wa kanisa walirudi nyuma.
Mchungaji alibaki amesimama mbele ya wale watu huku kwenye mgongo wake Kuchudi alikuwa amejificha.
“Vipi?”
Aliwauliza.
“Kuna kijana tunamtafuta ameingia hapa.”
Alijibu mvuta bangi mmoja.

Wale wachawi walishituka na kisha kumgeukia yule mvuta bangi.
“Nani?”
“Kuna kijana tulikuwa tunamkimbiza alikuja kutuchunguza.”
Wale wachawi waligeukiana.
“Kwahiyo huyo aliyekuja kuwachunguza nyie ndiye huyo aliyekuja kwetu sisi?”
Wachungaji bila kuambiwa walianza kushusha maombi.

Na mara wakati huo polisi wawili waliingia wakiwa na gari yao.
Kufumba na kufumbua polisi tayari walikuwa wameshawafikia wale wavuta bangi.
“Nyie wavuta bangi ndiyo tunaowatafuta.”
Walimkamata mmoja baada ya mwingine na kisha kuwaweka kwenye gari.
Wale wachawi walikuwa wakiungua na moto uliokuwa ukitokana na yale maombi.

Kwa kufanya hivyo Kuchudi alikuwa ameponyeka kwenye mikono ya wote waliokuwa wakimtafuta.
Na tangu hapo Kuchudi alibadilisha namna yake ya kuishi.
Hakuwa tena akitembea usiku na aliheshimu miiko aliyokuwa anaambiwa na wakubwa wake.

MWISHO

Sehemu 2
0
0