Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Nataka Kuzaa - Episode 02

Ratiba za chuo zinaanza kwa uwepo wa semina elekezi mbalimbali.
Kila siku mama yangu alikuwa akiondoka na mimi kutoka nyumbani hadi chuoni aliniacha mahali husika na kisha kuelekea ofisini kwake.
Nilikuwa nikiangalia mazingira mbalimbali ya pale chuoni kwetu, nilizunguka sehemu moja hadi nyingine ili kuweza kuyafahamu mazingira vizuri.
Katika kipindi hicho cha semina elekezi ndipo nilipokutana na Melania na Fety wasichana tuliopangiwa nao chumba kimoja katika mabweni ya Mabibo.
Niliweza kufahamiana nao pale nilipoenda hapo kwa ajili ya kukabidhiwa chumba kwa kuwa wao walikuwa wamekwishahamia kwenye mabweni ya Mabibo wakati mimi nilitokea nyumbani katika kipindi chote cha semina elekezi.
Melania na Fety niliona wanafaa kuwa marafiki zangu, hakika walikuwa wasichana warembo sana kwenye macho yangu niliona ni wao tu hakukuwa na wengine zaidi yao.
Walipenda kutabasamu wakati wote iliwafanya wazipendezeshe sura zao nzuri sana niliwapenda sana.
Wasichana hao hawakuonesha kuringa na hao ndio wakawa marafiki zangu.
Mimi na Melania tulikuwa tukisoma kozi moja wakati Fety alikuwa akisomea uchumi.
Melania alikuwa akitokea hapa hapa Dar lakini Fety alikuwa akitokea Morogoro.

Siku ya Jumapili nilihamia rasmi katika mabweni ya Mabibo.
Siku ya Jumatatu tulianza masomo rasmi siku hiyo ilikuwa ya kufurahiwa sana, nilifurahia kila kitu tulichokuwa tukifundishwa darasani.
Siku ya Jumanne tulikuwa na kipindi saa mbili asubuhi.
Niliwahi kuondoka Mabibo nikiwa na Melania na kisha tukaingia darasani.
Nilikuwa napenda sana kukaa mbele ili niweze kuelewa vizuri kile mwalimu alichokuwa akifundisha.
Tulipofika mlangoni Melania alianza kucheka.
“Anacheka nini huyu.”
Nilimshangaa nilimuona kama mwendawazimu.
“Gosh… kuingia darasani tu anacheka.”
Tuliwahi dakika kadhaa kabla mhadhiri hajaingia nikaachana naye kwa kuwa yeye hakupenda kukaa mbele, nikaelekeza macho yangu kwenye viti vya mbele ili kupata nafasi na hapo ndipo niligundua kwa nini Melania alikuwa anacheka.
Kwanza sikuamini macho yangu kile nilichokiona mbele yangu kilinichekesha na kisha kilinishitusha.
Alikuwa ni yule mkaka ambaye nilikutana naye siku ya kwanza nilipofika hapa chuoni.
“Haa inamaana na huyu anasoma udaktari, mbona makubwa.”
Alikuwa bize kuangalia mbele kana kwamba mwalimu alikuwa tayari ameingia na anafundisha.
Alionekana kituko kwa maana huko nyuma watu wengi walikuwa wakimuongelea yeye na kumcheka.
Siku hiyo alivaa tshirt kubwa jeupe ambayo rangi yake ilionekana kufifia, alivaa suruali nyeusi iliyopauka pamoja na makubazi miguuuni, hakuacha ile kofia yake.
Alikuwa ni mzuri wa sura lakini vituko vyake kwa kweli vilinichosha.
“Huyu mkaka anashida sana.”
Ilikuwa imebaki siti moja tu pembeni yake nafikiri watu hawakupenda kukaa karibu naye kwa vile nilikuwa nikipenda sana kukaa mbele nilienda kukaa palepale.
“Hi.”
Nilimsalimia.
“Hallo.”
Aliongea.
Alikuwa na sauti nzuri sana tofauti na muonekano wake ilinibidi kucheka.
Alitabasamu tu na kisha kuendelea kuangalia mbele, nilivutiwa kufanya naye maongezi.
“Unaonekana kufurahia sana kuwepo hapa.”
Alivua kofia yake na hapo niliushuhudia uzuri wake mwingine, alikuwa na nywele nzuri ambazo ziliupamba uso wake.
“Huyu mkaka ni mzuri au anafanya kusudi ili watu wasijue kwamba yeye ni mzuri.”
Niliongea mwenyewe na nafsi yangu nilionesha tu tabasamu.
Alilamba midomo yake na kisha akanigeukia kwa tabasamu pana.
“Naitwa Franklin.”
Aliniambia.
“Ooh Frank nice name.”
Nilimjibu kwa aibu.
“Ni ndoto yangu ya muda mrefu sana kuja kusomea udaktari lazima niwe na furaha.”
Alinijibu kwa ufupi huku jibu lake likiwa limejitosheleza niliachia tu tabasamu.

Mara ghafla meseji iliingia kwenye simu yangu, alikuwa ni Melania.
“Sociolah umechanganyikiwa hujui kama unajiharibia CV yako kila mtu anakucheka huku nyuma.”
Na muda huo ndipo mhadhiri aliingia, nilishindwa kumjibu nikatoa madaftari yangu na kisha kuanza kumsikiliza mhadhiri.
Mhadhiri alianza kufundisha.
Mkaka yule ambaye nilimtambua kwa jina la Frank alionekana kuwa makini darasani, alisikiliza kila pointi ambayo mwalimu alikuwa akiongea na alionekana kuelewa sana.
Nilitumia muda mwingi kumuangalia.
Mhadhara ule ulinipita kwani sikuelewa vitu vingi.
Baada ya kipindi kuisha nilibaki tu nikimshangaa, alikusanya vitu vyake huku akionekana akijivuta vuta sana.
Watu walianza kutoka nje.
Melania alikuja na kusimama pembeni yangu.
Frank alikusanya vitu vyake na kisha akasimama aliachia tabasamu na kuvaa kofia yake.
“See you.”
Aliongea huku akiachia tabasamu.
Nilitabasamu tu na kushindwa kumjibu na kisha alitoka.
Nilisimama kwa ajili ya kutoka nje Melania alinivuta na kunikalisha chini kisha akakaa pembeni yangu.
“Sociolah unapatwa na ugonjwa wa akili wewe ni wa kuongea na huyu mtu aliyekuja na matranka hapa chuoni.”
Aliniongelesha kwa ukali akionesha kuwa yuko siriazi.
“Aah, Melania sio kwamba… Sio kwamba…”
Nilishindwa cha kuongea.
“Sio kwamba nini kila mtu huko nyuma anasema kuhusu wewe kweli Sociolah unafikiri una hadhi ya kuongea na huyo mkaka, kwani ulikosa sehemu za kukaa mpaka ukae hapo si ungekuja hata ukae kule nyuma.”
“Melania huyu mtu ni mwanadarasa mwenzetu swala la kukaa naye karibu na kuongea naye nadhani hayo ni maamuzi yangu binafsi uniache kwani kuongea naye nimepungiwa nini acha watu waongee kwani wao wakiongea mimi napungukiwa na nini sitaki mtu afuatilie maisha yangu.
Melania niko huru kuongea na mtu yoyote ambaye mimi namtaka kwahiyo kwa hili naomba uniache.”

Niliongea kwa msisitizo sana.
“Kwa hilo naomba uniache.”
Alifuatilizia maneno yangu huku akibana pua.
“Unafikiri kwamba muonekano wako ni rahisi sana kwa hicho unachokifanya utapata shida hapa ni chuoni Sociolah.”
Aliongea.
“Haaa...”
Nilivuta pumzi tu nikishindwa nini cha kumjibu.
“Twende tukale.”
Nilimjibu.
“Fikiria sana nilichokwambia hupaswi kuwa na ukaribu na huyo mtu.”
Aliongea.
Ni kweli hatukuendana kabisa na Frank lakini hata hivyo Frank alionekana alikuwa ni mtu mpole na asiye na hatia, kwanini astahili hivi, kwanini kila mtu anamtenga alionekana kukosa marafiki hapa chuoni nadhani kisa kikiwa ni kuja na tranka, nadhani taarifa zake zilienea chuo kizima, ilinitia huzuni sana huyu mtu anahitaji faraja ingawa mwenyewe anaonesha kutokujali kabisa.

Niliondoka nikiwa na mawazo mengi tulimkuta Fety akitusubiri kwa ajili ya kuelekea cafe.
Tuliingia cafe na kuagiza chakula.
Wakati naendelea kula nikiwa na mawazo mengi nilishitukia kumuona Fety na Melania wakicheka huku wakioneshana kitu.
“Nyie mbona mnachekacheka si mniambie na mimi nicheke.”
Niliwambia.
Melania alicheka kwa sauti mpaka alipaliwa Fety alichukua maji na kumpa.
“Fety what’s wrong.”
Nilimuuliza Fety.
“Kushoto kwako.”
Aliniambia.
Nilibaki tu nikishindwa kumuelewa.
“Kuna nini huko kushoto kwangu.”
“Geuka uangalie.”
Niligeuka, nilishindwa kujizuia nikacheka hakika kilikuwa ni kituko cha mwaka.
Kwa kweli nilishindwa kujizuia kucheka, hakika kilikuwa ni kitu cha kuchekesha kuliko vyote ambavyo niliwahi kukutana navyo katika maisha yangu. Nilicheka sana lakini mwishowe niliingiwa na huruma.
“Hivi huyu mtu ana akili kweli? Hajui kama anafanya haya mambo mbele za watu ona watu wanavyomuangalia.”
Niliongea kwa sauti.
Fety na Melania walinigeukia na kunitazama wakiwa wameduwaa.
Kushoto kwangu alikuwa Frank, alikuwa akinywa chai pamoja na sahani ya matunda.
Matunda yale yalikuwa ni mchanganyiko wa matikiti, machungwa, mananasi na maparachichi.
Lilikuwa ni tukio la kushangaza sana mtu kunywa chai na matunda.
Kila mtu alikuwa akimtazama yeye na kumuongelea yeye.
Tukio langu la kukaa naye mbele darasani na kisha kuongea naye mawili matatu lilikuwa kama gumzo pale chuoni.
Watu wote walikuwa wakiongea wakimtazama na kisha walinigeukia mimi na kucheka, hakuonekana kujali kwani alikuwa akilamba michuzi ya matunda iliyokuwa ikichuruzika mikononi mwake bila haya wala aibu huku akipigia miruzi kana kwamba yuko peke yake.
“Ooh gosh hii ni aibu.”
Niliwaza.
Nilinyanyuka kwa hasira sana.
Melania aliongea kwa kupaniki.
“Kwani wewe ni ndugu yako?”
Nilimuangalia kwa jicho kali na kisha nikaenda nilipokuwa nataka kwenda.
Nilijongea moja kwa moja hadi kaunta walipokuwa wakiuza vitafunwa, niliagiza chapati mbili na andazi moja na kisha nikampelekea mezani kwake nikamuwekea kwa hasira na kurudi kukaa kwenye meza yangu.
Hata sikujua ni nini kilichonivuta kufanya hivyo ingawa aibu yake ilikuwa kama yangu pia kwa maana tu nilijiweka karibu naye asubuhi ya siku hiyo.
Moyoni mwangu nilijisikia vibaya sana kwa nini nilikaa karibu yake asubuhi ya siku hiyo.
Aliniangalia na kisha akatabasamu tu.

Dakika mbili si nyingi chapati zile zilikuwa zimeishia mdomoni mwake, alizikunja chapati zile mbili na kuzitafuna kwa mikupuo miwili tu zikawa zimeisha.
Kicheko cha watu kiliongezeka sasa hivi walishindwa kujizuia kucheka kisirisiri walicheka kwa sauti kubwa.
Nilinyanyuka kwa hasira na kuondoka.
“Kwa kweli nimejiingiza kwenye mkenge, mama yangu akisikia kwamba nafanya mambo ya ajabu hapa chuoni hakika baba hatonielewa anaweza akachukua hatua kali.”

Niliondoka nikiwa na mvurugiko wa mawazo kutoka cafe mpaka kwenye madarasa yetu, nilichagua darasa ambalo halina watu na kisha nikakaa.
“Oooh my god! Huyu ni mtu wa aina gani hivi hajui kama yuko katika jamii ya watu anapaswa kuwa na heshima na adabu mbele za watu.
Kwanini anafanya mambo kama chizi alafu ananiingiza mimi kwenye mkenge huu, Shiit…”

Nilijawa na hasira sana kuwa karibu naye nilikumbuka maneno ya Melania.
“Utajutia hapa ni chuoni.”
Ningejua ningemsikiliza Melania, sijui kwanini niliruhusu kuwa karibu na huyu mkaka.
Watu walianza kuingia darasani kila mtu akiliongelea tukio lile nilibaki kimya nilikuwa nimekaa kwenye siti za mbele kama kawaida na mhadhara ulikuwa unakaribia kuanza.
Watu waliingia, Melania aliiingia darasani pia hakutaka hata kunisemesha alienda kukaa siti za nyuma kabisa.
Nilikuwa nimejiinamia kwenye kiti nikiwa na huzuni, mawazo pamoja na hasira.
Ghafla nilihisi mtu amekaa pembeni yangu.
Sikujushughulisha kumuangalia niliendelea tu kuwaza na kuwazua.
“Hello.”
Sauti yake ilinishitua.
Niligeuka kwa mshituko huku nimetoa macho nikimtizama.
“Ahsante kwa breakfast.”
Aliongea na kisha aligeuka kutazama mbele kama ilivyokuwa kawaida yake kana kwamba anamsikiliza mhadhiri.
Nilishikwa na hasira sana nilinyanyuka kwa hasira nikavuta begi langu na kisha kujongea kuelekea nyuma kila mtu alibaki ananishangaa.
Nilifika mpaka viti vya nyuma ambapo Melania alikuwa amekaa aliniangalia kana kwamba anamuona mwendawazimu.
“Sogea huko.”
Nilimuambia.
Alisogea na kisha nikakaa nikalaza kichwa changu kwenye meza.
Mchanganyiko wa hasira, mawazo ulinifanya nisielewe mhadhara ule.
Mhadhara ulipoisha tu mhadhiri wetu alinichagua kuwa mwakilishi wa darasa ama CR.
Nafikiri ilitokana na kwamba alikuwa akifahamiana na mama yangu hivyo baada ya kujua kwamba niko katika darasa lake aliamua kunichagua mimi kuwa CR.
Kiukweli akili yangu haikuwepo kabisa hapo darasani, mhadhiri alipoondoka tu nilibeba begi langu na kisha kuondoka sikutoa vitu vyangu kabisa tangu tumeingia hapo darasani.
Niliondoka moja kwa moja hadi Shuttle point kwa ajili ya kusubiri gari kuelekea Mabibo.
Gari lilipofika tu nilipanda wa kwanza na kisha nikakaa siti ya mbele kabisa sikutaka kukaa karibu na mtu yoyote.
Melania hakuwepo mbali ingawa hatukuweza kuwa karibu kivile, alikuwa akiniangalia kile nilichokuwa nikifanya huku akinishangaa.
Gari lilipofika Mabibo sikutaka hata kuagiza chakula nilishuka na kisha kuelekea chumbani kwetu mabweni ya Mabibo Block A, Room namba 147.
Nilivyofika tu niliingia na kulala sikuvua hata viatu nililala navyo.
Fety ambaye alikuwa ameshafika bwenini alibaki akinishangaa.
“Una nini wewe we Sociolah… Sociolah…”
Sikutaka kugeuka.
Melania alifika, alifungua mlango na kisha akaenda kukaa kwenye kiti alivuta pumzi na kushusha.
“Kuna nini jamani? Mmepigana nyie? Mmegombana? Kuna nini?”
Fety aliuliza maswali mfululizo sikutaka kuendelea kumsikiliza niliamua kuutafuta usingizi.
Nadhani Melania alimuelezea kila kitu kwa maana nilipokuja kuamka baada ya kuhisi njaa Fety hakuwa tena akiuliza maswali.
Niliamka nikiwa na uchovu sana.
“Nyie mimi nina njaa twendeni tukale.”
“Ndiyo unakumbuka saa hizi kwamba hujala.”
“Aah twendeni bwana tukale.”
Tulijiandaa na kisha kutoka nje.
Tulitoka hadi cafe ambapo walikuwa wanauza chakula, niliagiza chipsi kuku na kisha kukaa nikisubiria chakula changu.

Sehemu 1 Sehemu 3
0
0