Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Nataka Kuzaa - Episode 04

Patrick ni mtu ambaye ananisikiliza sana na kunijali na alikuwa akinipenda sana na zaidi ya yote alikuwa ana malengo mazuri tu na mimi ila ubize wake ulinikera sana.
“Niambie Sociolah shida ni nini mama?”
“Patrick kuna mambo yananichanganya sana nilikuwa nahitaji faraja kutoka kwako ingawa uko bize sana.
Hata hivyo nilikuwa nahitaji pesa maana nimeibiwa hela zangu na siwezi kumuambia mama.”

“Unahitaji kama shilingi ngapi?”
“Yoyote tu mimi siwezi kukupangia.”
“Umeibiwa shilingi ngapi?”
“Nimeibiwa kama laki tano hivi.”
“Pole, nitakutumia.”
“Nitashukuru sana.”
“Aya, usiku mwema.”
“Patrick hautaki hata kuongea na mimi kidogo.”
“Kuna kazi nafanya hapa mama, nitakupigia nikimaliza.”
Nilijua kwamba hatonipigia kwa maana hamalizagi kazi zake.
“Sawa usiku mwema.”
Alikata simu yake.
Kwa kiasi Fulani nilijihisi afueni.
Haikupita dakika kadhaa Patrick alinitumia laki tano, nilifurahi sana.

Siku ya Jumapili nilirejea bwenini kwetu Mabibo na siku ya Jumatatu tuliingia kwenye vipindi kama kawaida.
Melania bado hakuwa amepata simu yake hivyo alikuwa mtu mwenye Hasira muda wote na manung’uniko.
“Usijali utapata.”

Ilipofika saa sita kasoro dakika tano tuliingia kwenye semina.
Kiongozi wa semina ile alitupa maelekezo machache kuhusu semina yetu na kisha akatugawa katika makundi kwa ajili ya kazi ya kuwasilisha.
Daktari Kisayeye alianza kwa kuongea.
“Makundi yapo matano kundi la kwanza mtawasilisha Jumatatu ijayo, kundi hili lina watu wanne, Sociolah Kindamba.”
“Mmmh..!”
Kwanza nilishituka lakini pia nilifurahi kuwa wa kwanza kuwasilisha kazi bila kuwa na uzoefu wowote ilikuwa siyo jambo dogo.
“Melania Petro.”
“Woow...!”
Nilifurahi sana…. Nilifurahi kuwa na Melania katika kundi moja.
“Innocent Chande.”
Hata sikuwa nikimfahamu ni kwa mara ya kwanza nimekutana naye.
Watu wote tuliotajwa ilibidi tusimame ili tufahamiane alisimama huyo Innocent, alikuwa ni mkaka mzuri sana nilifurahi kuwa naye Kundi moja alikuwa mtanashati mno.
“Na wa mwisho atakuwa ni Franklin Kazimana.”
Nilihisi kuzimia.
“Frank tena?!”
Melania ambaye uso wake ulipambwa na Tabasamu ulibadilika ghafla, alichukia kupita maelezo nilishindwa hata kumtazama usoni.
Daktari Kisayeye aliendelea kutaja watu katika makundi yao tofauti tofauti.
Kiukweli nilianza kuichukia ile semina yetu.
Kiongozi wetu alipoondoka tu Melania alikuwa wa kwanza kutoka darasani.
Innocent aliniita.
“Sociolah.”
Niligeuka na kumfuata.
“Unajua tuna kama siku chache tu hivi kabla hatujawasilisha kazi yetu inabidi tukutane tuanze kupanga mikakati, mbona mwenzio amekimbia.”
“Aanh.. atakuwa hajisikii vizuri, tunakutana lini?”
“Kwani nyie mnakaa wapi?”
Aliuliza.
“Tunakaa Mabibo.”
“Basi tukutane leo saa moja Mabibo.”
“Sawa.”
Niliongea na kuondoka, nyuma yake nilimuacha Frank akipiga hatua kumkaribia Innocent, niliwaacha waendelee na maongezi yao na mimi niliondoka.
Baada ya kumaliza vipindi vyote tulirejea Mabibo.

Saa moja kamili ya siku hiyo ilitukuta katika Vimbweta vya Block A.
Melania alikuwa bado amenuna.
“Huyu mwalimu shetani kweli akachagua watu akaona bora atuweke na huyu chizi.”
“Melania acha bwana aaah.”
“Mimi sijui kama nitakuwa Comfortable kwa kweli na huyu taahira huyu.”
Frank na Innocent walikuwa wakipiga hatua wakijongea upande wetu.
Melania alivuta mdomo baada ya kumuona Franklin, hakika alikuwa akimchukia sana.
Franklin na Innocent walijongea mpaka kwenye vimbweta ambapo sisi tulikuwa tumekaa na kisha wakaketi.
Franklin alibakia kimya tu wakati Innocent alitusalimia kwa uchangamfu wote na sisi tuliitikia kwa kuchangamka pia.
Mara zote Innocent alikuwa ni mcheshi sana, Melania hakuishiwa kucheka lakini kila tu alipogeuka na kukutana na Frank alivuta tena mdomo.

Tulianza kujadiliana swali letu tulilopewa na mwalimu.
Hapo niligundua kitu kingine kuhusiana na Frank hakika huyu kaka alikuwa ni jiniazi sana, alikuwa anamuelewa mwalimu zaidi ambavyo ni kawaida, aliweza kuyakumbuka maneno yote ambayo mwalimu alikuwa akiyaongea darasani nilimuelewa zaidi Frank kuliko nilivyokuwa nikimuelewa mwalimu alipenda kuongea kwa mifano, alielezea swali zima peke yake wala hakuna aliyekuwa akichangia na alielezea kila kitu kwa kweli ilikuwa ni ajabu sana.
Mara zote Melania alikuwa amekasirika.
Mara ghafla Melania alikunja sura nikashangaa.
“Kwanini?”
Kumbe aliona mabaki ya maharage kwenye meno ya Frank wakati Frank akiongea, nilishangaa sana kwanini Melania anamchunguza sana huyo mkaka wa watu.
Melania alikaa katikati yangu na Innocent wakati Frank alikaa katikati yangu na Innocent.
Tuliendelea kujadiliana hadi tulipofikia mwisho, baada ya hapo tuliagana na kila mtu kupewa kazi ya kufanya.

Simu yangu iliita alikuwa ni Daktari Kisayeye.
“Hujambo Sociolah.”
“Sijambo, shikamoo Daktari.”
Nilimsalimia.
“Marhabaa, najua mnajiandaa na kazi niliyowapa.”
“Ndiyo.”
“Sasa ili kuweka urahisi za kupata taarifa zote za kitaaluma ungetengeneza kikundi cha WhatsApp ili taarifa ziweze kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja, fanya hivyo mwanangu.”
Aliongea Daktari Kisayeye.
“Sawa mwalimu nitafanya hivyo.”
“Aya usiku mwema binti yangu.”
“Ahsante na kwako pia.”
Nilishukuru na kukata samu.
Wakati huo Melania hakuwepo, Frank alikuwa tu amesimama kana kwamba hajui aelekee wapi.
Innocent aliniita.
“Sociolah kwani Melania ana nini?”
“Kafanyaje kwani?”
Niliuliza.
“Kamsonya mkaka wa watu kiasi kwamba mpaka watu wote wameshituka wakamgeukia.”
“Achana naye ana matatizo yake.”
Niliongea kisha nikamuangalia Frank alibakia tu amenitolea macho kana kwamba hajui anaongeleshwa nini, nilimuangalia tu huku nikishindwa cha kuongea na mimi nikaondoka.

Nilifika chumbani kwangu Melania alikuwa ana hasira bado nilijua sababu kubwa ni kwamba bado hakuwa amepata simu yake.
Nilitengeneza kikundi cha WhatsApp kama nilivyoelekezwa na daktari Kisayeye, niliweza kuwaunga wanafunzi nilikuwa nikisoma nao darasa moja wale wachache ambao nilikuwa na namba zao na kisha nikaweza kuwaunga wengine waliobakia kwa kutumiwa namba zao.
Kikundi kilikamilika, mtu mmoja tu hakuwepo kwenye kikundi naye alikuwa ni Franklin na Melania ambaye simu yake ilipotea ingawa nilimuunga.
Mara baada ya kuwaunga wanafunzi kutoka katika darasa letu kila mtu alikuwa akimuulizia Franklin.
“Yuko wapi matranka.”
Mtu mmoja aliandika meseji, mtu huyo alikuwa akipenda sana utani, kila mtu alicheka.
“Aah usikute atakuwa anapaka rangi tranka lake.”
Mtu mwingine alituma meseji, watu waliendelea kucheka, kiukweli mimi iliniuzi sana nilichukia mno.
“Hebu kuweni na heshima nyie.”
Nilituma hiyo meseji.
“Aah CR unamtetea mtu wako.”
“Sio kwamba namtetea mjifunze kuheshimu hali za watu nyie ni watu wazima kwanini mnakuwa mnafanya mambo kama watoto wa sekondari hebu kueni basi.”
Niliongea.
Innocent naye alikuja juu.
“Acheni mambo ya ajabu nyie yule ni mtu tena kawazidi vingi tu, msimchukulie kirahisirahisi kama mnavyomuona achaneni naye fanyeni mambo yenu.”
Innocent alimtetea.
“Sawa tumemsikia CR na handsome wa darasa.”
Alionge msichana mmoja ambaye alikuwa anapenda sana utani na kisha watu wakaacha kumjadili Frank.

Siku zilienda hatimaye siku ya kuwasilisha kwetu iliwadia tuliwasilisha vizuri. Daktari Kisayeye alimfurahia sana Franklin, hakusita kuelezea sifa zake mbele ya darasa.
“Huyu mwanafunzi ni mwanafunzi bora na hajawahi kutokea hapa chuoni nitakupa zawadi kwa maana umeweza kuongelea kila kitu ambacho ninachokitaka umegusa maeneo nyeti sana, hakika wewe ni bora.”
Alimsifia.
Hakuna aliyejishughulisha kupiga makofi, hata nilipoanzisha hakuna mwingine aliyenifuatia, niliamua kuacha.
Mara baada ya kuweza kuwasilisha tulitoka darasani Melania hakuwa katika hali ya kawaida, aliniita.
“Sociolah, mimi bila simu yangu kwa kweli maisha hayaendi.”
“Usijali nitakufanyia mpango upate simu nyingine, usijali.”
“Mama hawezi kunielewa nimepoteza simu nzuri hivi.”
“Usijali utapata simu nyingine.”
“Sawa mimi nataka tu nirudi bwenini Mabibo.”
“Turudi tu hata mimi nimechoka.”

Tulianza safari ya kutoka darasani hadi Shuttle Point kwa ajili ya kusubiri magari ya kuendea Mabibo.
Tulitembea kwa hatua za kichovu sana hatimaye tulifika Shuttle Point. Wakati tukisubiri gari na hapo ndipo tulipomuona mwizi wa vitu vyetu, alikuwa ameshikilia simu ya Melania pamoja na wallet yangu mkononi akituijia mbele yetu.
“Mwiziiii……”
Ghafla bila kutarajia Melania aliita.
Watu waligeuka na kutazama ni nani aliyekuwa mwizi wetu. Bila kuchelewa mwizi alishikwa na watu na muda si muda akaanza kupigwa.
Mambo yalikuwa yakitokea harakaharaka kiasi kwamba sikuweza hata kunyanyua mdomo, nilibaki tu nikiwa nimetoa macho.
Melania aliendelea kupayuka.
“Mwizii… Mwizi…”
Watu walifika na kumvuta Shati Frank, nilishangaa vitu vyetu vimefikaje kwenye mikono ya Frank.
Wakati nikiwa bado sielewi nini kimetokea ghafla alitokea Innocent alipangua watu waliokuwa wamemshika Frank na kisha akamvutia mikononi mwake.
“Nini…. Kuna nini?”
Aliwauliza.
“Huyu jamaa ameiba vitu vya watu.”
Akamgeukia Frank na kumtazama.
“Mna uhakika kwamba ameiba?”
“Ndiyo si hivyo hapo kavishika mkononi.”
Wakati sisi tukitokea madarasani kwetu kwa ajili ya kuelekea Shuttle Point kupanda gari Frank alikuwa akija mbele yetu huku akiwa ameshikilia wallet yangu na simu ya Melania.
“Mna uhakika na wewe unamuitia mwizi mtu kabla hujamuuliza.”
Innocent aliendelea kufoka.
Melania alinyamaza, tulishindwa cha kuongea tukabaki tukitazamana.
Na wale watu waliokuwa tayari wameshamshika Frank na kutaka kumpiga walibaki wameduwaa.
“Mmemsikiliza alichowaambia hivi unafikiria angekuwa ameiba angekuwa amevishikilia tu hivi anatembeatembea navyo.”
Innocent aliongea hakuna aliyejibu.
“Kwani amevipaje vitu vyetu.”
Niliweza kuuliza.
“Waambie Frank.”
Alisema.
Alishikwa na kigugumizi Frank, nilishangaa Frank huyu mwenye kuweza kuongea ameshikwaje na kigugumizi.
Mwishowe aliweza kuongea.
“Sociolah siku ile wakati ulivyokaa pale mbele halafu ukanyanyuka kwa hasira na kuelekea nyuma ulidodosha wallet yako.”
Nilishangaa sana wala sikuwahi kuhisi kama ningeweza kuwa nimedondosha wallet yangu pale.
“Jioni ya siku ile nilikufata pale mgahawani ili nikukabithi wallet yako lakini mlinitukana na kisha mkaondoka kabla sijakukabithi wallet yako na baada ya hapo mliondoka wote Melania alisahahu simu yake pale mezani, niliichukua siku ile na nikaja pale mgahawani na nikataka kuwakabidhi mkanimwagia juisi.”
Kwa kweli ilikuwa ni aibu kubwa sana mbele za watu kila mtu alitutazama kwa jicho kali tulishindwa kunyanyua sura zetu.
“Nimeamua kuwakabidhi kwa maana kila wakati nikitaka kuwakabidhi huwa hamtaki. Bahati mbaya simu ya Melania ilizima mda mrefu tu, nikaichaji kwa chaja ya mwenzangu kule chumbani lakini wala mimi sijui kuifungua simu yake, ningeweza kuwajulisha kwamba simu ninayo lakini ilishindikana.”
Nilishindwa cha kuongea kwa kweli ilikuwa ni aibu sana nilitazama kando.
“Wallet yako hii hapa hakikisha kama iko salama na Melania simu yako hii hapa iangalie pia.”
Aliipokea kwa fujo na papara zote aliikagua simu yake ilikuwa kama ilivyokuwa cha zaidi alikuwa ameichaji.
Aliifungua na kukuta kila kitu kiko salama wala havikufunguliwa, kwa kweli nilishindwa hata kufungua wallet yangu.
“Fungua Sociolah uangalie.”
Nilifungua, nilikuta fedha taslimu shilingi laki tano kama zilivyokuwa kila kitu changu kilikuwepo na hakuna kitu kilichopunguka wala kuongezeka, nilishangaa sana.
Melania alishindwa hata kumshukuru Frank alihisi aibu aliondoka ghafla huku akilia na kukimbilia kwenye gari.
Watu waliokuwepo wameanza kukusanyika pale walianza kuondoka na mwishowe tulibaki mimi, Frank na Innocent.
Innocent alinitazama tu nilinyanyua uso na kuwakuta wamesimama mbele yangu kana kwamba hawana mahali pa kwenda.
“Ahsante Frank, and am sorry for everything.”
Niliweza kusema.
“Usijali.”
Alivyomaliza kusema aliondoka.
Innocent alibaki akinitazama tu.
“Kuwa makini.”
Aliongea na kisha kuondoka.
Niliwaangalia hadi walipoishilia kwa aibu nilitoka pale na kuingia kwenye gari sikutaka hata kwenda kukaa karibu na Melania.
Gari lilipojaa dereva alikuja na tulianza safari ya kuelekea Mabibo.
Tulipofika Mabibo habari ile ilikuwa gumzo katika kikundi chetu cha WhatsApp.

Sehemu 3 Sehemu 5
0
0