Nataka Kuzaa - Episode 03 
Melania na Fety waliagiza chakula na kisha kukaa pamoja.
Tulianza kula huku tukiongea mawili matatu ingawa bado nilihisi uchovu mwingi na kichwa kikiniuma.
“Mungu wangu balaa gani tena hili?!!”
Nilishituka.
Frank alikuwa akija kuelekea upande wetu, watu wote mule ndani ya cafe waligeuka na kutuangalia sisi.
Melania alionesha kuchukia sana, kwa hakika alikuwa hampendi sana Frank.
“Anakuja kufanya nini huyu tena.”
Niliwaza bila majibu.
Frank alisogea hadi upande wetu.
“Haloo.”
Alinisalimia mimi tu.
“Unataka nini?”
Nilimuuliza kwa sauti iliyopoa.
“Samahani dada nilikuwa naomba…”
Melania alisimama na kuanza kumrushia matusi.
“Wewe umechanganyikiwa mbona unapenda kushobokea watu usiowajua eenh yani kuongeleshwa tu kidogo basi ndiyo
unafikiri kama umeunga ukoo kwanini unapenda kumsumbuasumbua rafiki yangu,
samahani wewe hauko kwenye level zetu naomba uachane na sisi tena umkome Sociolah.”
“Aah nilikuwa sijui anaitwa nani kumbe anaitwa Sociolah.”
Frank aliongea, nilizidi kumshangaa.
“Frank kuwa na akili sikia nikuambie sitaki ukaribu na wewe naomba kuanzia leo usinizoee.”
Nilipatwa na ujasiri wa kuongea.
“Usijali.”
Alisema.
Watu wote walikuwa wakituangalia sisi mule ndani.
“Shiit…”
Nilishindwa hata kula nilinyanyuka na kuondoka kuelekea chumbani kwangu.
Nafsi ilinisuta sana kumtukana ingawa nahisi alistahili sana matusi yale.
“Yani yupo kama hayupo sijui kama ana akili sawasawa huyu.”
Nilifika chumbani kwangu na kujilaza, muda haukupita Fety na Melania waliingia nao walikuwa wamepaniki sana.
Ilikuwa ni kwa mara ya kwanza Fety anamuona lakini ilionesha kiasi gani hampendi.
Walikuwa wakiongea maneno ya kulaani kitendo cha kutuijia pale usiku ule.
“Tumemuacha pale mezani maana anatushobokea sijui hata ameona nini, anafikiri sisi ni level sawa na yeye,
fyuu…”
Mwishoni alifyonza.
Niligeukia upande wa pili usiku huo ulipita.
Niliamshwa na pilikapilika za Melania na Fety pamoja na mwanachumba mwenzetu ambaye aliitwa Monica.
Kiukweli nilikuwa nimechoka sana na nilihisi njaa.
“Kuna nini jamani mbona vuruguvurugu?”
Melania alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa, alikuwa akirusharusha nguo huku na kule,
akipangua vitu na kuharibu mpangilio mzima wa chumba chetu.
“Kuna nini?”
Niliuliza bila kujibiwa.
Monica na Fety walikuwa kimya tu. Nilinyanyuka na kukaa.
Nilijinyoosha.
“Aanh…, nasikia njaa hatari.”
Melania alinigeukia na kunitazama kwa jicho kali.
“Unawaza kula tu huwazi hata ni nini kimetokea.”
“Si nimeuliza sipati jibu.”
Niliuliza kwa kupaniki.
“Kama hamtaki kunijibu mimi nifanyeje? Halafu matatizo yenu mimi hayanihusu kama nasikia njaa mbona nyie hamjali.”
Fety alinikonyeza.
“Kwani kuna nini?”
Niliuliza.
“Melania haioni simu yake.”
“Ooh…”
Kwakweli nilishituka sana.
Melania alikuwa akiipenda sana simu yake aina ya Samsung S6 ambayo alipewa zawadi na mama yake
kwa kuchaguliwa kujiunga na chuo kikuu cha Dar Es Salaam, ilikuwa ni simu nzuri na mpya kwahiyo
sikushangaa kuona Melania amechanganyikiwa kuipoteza simu yake ile, ilikuwa ni nzuri sana hata mimi nilikuwa nikiipenda.
“Mmmh… Patamu.”
Nilisema.
Kiukweli Melania alikuwa amechanganyikiwa alitimuatimua vitu vyote na hakufanikiwa kuipata,
ilinibidi tu na mimi nijitahidi kumsaidia kuitafuta kwa maana alikuwa na hasira zisizo za kawaida.
“Simu yangu nani kaiba jamani….?”
Alikuwa akipiga kelele kama chizi.
“Jamani muda wa kipindi umekaribia mnaonaje tukaenda na tukarudi huku kuja kuitafuta,
kwani mara ya mwisho ulikuwa nayo wapi?”
“Hata sikumbuki mimi nimechanganyikiwa kabisa hapa.”
Melania alisema.
“Mimi nakumbuka ilikuwepo hapa jana.”
Fety alisema.
“Basi itakuwepo hapahapa twendeni tukahudhurie kwenye kipindi turudi tuendelee kuitafuta.”
Nilipendekeza.
Melania alikubali ingawa kwa shingo upande.
“Mimi bila simu yangu hata sijihisi kuwa niko vizuri.”
“Mmh…”
Nilitabasamu tu kwa pembeni maana angeniona ingekuwa ni kesi nyingine.
Tuliondoka na kwenda chuoni, muda wote alikuwa amekasirika hakutaka hata kujiongelesha na mtu.
Tulihudhuria kipindi hiko cha saa nne na baada ya hapo tulitoka na kuelekea Café kwa ajili ya kupata kifungua kinywa.
Melania aligoma kuagiza kitu chochote.
“Sasa utakaa bila kula jamani mbona unakuwa hivyo.”
Nilimuongelesha Melania kwa namna ya kumshawaishi.
“Siwezi hata kula chochote, Sociolah simu yangu ni kila kitu kwangu najisikia vibaya sana bila kuwa nayo.”
“Usijali utaipata kula basi.”
Nilimshawishi.
“Usinilazimishe kula Sociolah wewe kwasababu hujapoteza kitu hivi unafikiri
ingekuwa ni ya kwako ungekula wewe, hebu niache usinisumbue.”
Kwa kweli nilinyoosha mikono juu kwa maana Melania alikuwa ni mtu ambaye asiyeshawishika,
akiweka msimamo ni mgumu sana kuubadilisha.
Fety alijaribu.
“Kula basi hata kidogo.”
Alinyanyuka tu na kuondoka hatukujua ameelekea wapi.
“Kuwa makini naye sana Sociolah akiwa na hasira huyo anaweza kummeza mtu.”
Fety aliongea tulicheka.
Hazikupita dakika mbili Melania alirudi akiwa na glasi ya juisi, nilijua ni
juisi ya maembe pamoja na ukwaju, juisi ambayo wote tulikuwa tukiipenda sana.
Wakati huo nilikuwa nikinywa chai yangu na chapati, Fety alikuwa akinywa chai na maandazi.
Tukio la ghafla lilitokea na la kushangaza.
Wakati Melania anafika mezani kwetu Frank naye alifika mezani kwetu,
nilibaki na mshangao nilishindwa kuongea chochote.
“Samahani, mambo.”
Frank alimsalimia Melania.
Nilimuona Melania hasira zikimzidia na ghafla alimmwagia ile juisi aliyokuwa nayo Frank,
alimmwagia juisi yote kwenye shati lake jeupe la mikono mirefu ambalo alilivalia na suruali yake ya bluu,
hakuchomekea na chini alikuwa amevaa malapa bila kusahau kofia yake.
Masikini ya Mungu roho iliniuma sana.
“Melania umefanya nini?”
Melania aliniangalia tu kana kwamba anaongea na mimi kupitia macho na alipokwisha
kumaliza aliondoka bila kusema chochote.
Frank alibakia amejiinamia tu nilimuonea huruma lakini nilishindwa cha kufanya.
Fety alitoka pale alipokuwa amekaa hadi karibu ya Frank.
“Ndiyo ukome.”
Alimuambia na kisha kuondoka.
Nilimuangalia Frank kwa huruma sana, nilishindwa kufanya chochote nikabeba begi langu na kisha kuondoka.
Nilikuwa nikimfuata Fety alipokuwa akielekea, tulienda hadi yalipokuwa madarasa yetu.
Tulikaa eneo la Vibweta.
“Melania kwanini umalizie sasa hasira zako zote kwa Frank? Kakufanya nini lakini?”
Hakunijibu kitu.
“Yani hasira zako za simu ndiyo unakuja kummalizia Frank ona ulivyomuaibisha mkaka wa watu
jamani kwa nini lakini?”
Alisonya tu.
“Angalia sasa sijui hata anakaa wapi masikini, umemmwagia juisi atatembeaje hapa chuoni kumbuka kwamba bado
hatujamaliza vipindi kwanini lakini?”
Niliendelea kufoka tu huku ikionesha kwamba Melania hakuwa akinisikiliza hata kidogo.
“Shiit… Fety tumchangie Melania hela akanunue simu, hata kwa kipindi kifupi tu, mimi nitatoa baadhi ya hela nilizokuwa nazo.”
Niliongea kwa hasira bila kujua.
Nilifungua pochi yangu na kuanza kutafuta wallet yangu ambayo niliyokuwa nikihifadhi kiasi kikubwa cha hela.
Hiyo ilikuwa ni hela ya matumizi ya wiki hili ambayo nilipewa na mama kiasi kama laki tano hivi.
Lahaula..!
Haikuwepo!
Nilichanganyikiwa, nilitupa kila kitu kilichokuwepo kwenye pochi yangu na sikufanikiwa kuiona hiyo wallet.
“Mungu wangu wallet yangu iko wapi?”
Kila mtu alishituka.
“Sioni wallet yangu jamani, nani kachukua?”
“Hapana.”
Kila mtu alijibu.
“Shiit..”
Nilishindwa cha kuongea hasira zilinikaba kooni.
“Nyie au tunaibiana sisi kwa sisi.”
Fety alisema.
“Hata mimi naijiwa na mawazo hayo, haiwezekeni jana simu ya Melania imepotea leo wallet yako imepotea,
kuna nini kati yetu?”
“Mungu wangu nitaishije mimi bila hizi hela, nitamuambia nini mama? Hakika hawezi kunielewa… Hawezi kunielewa kabisa.”
Nilichanganyinkiwa si kidogo.
“Haaa…”
Nilivuta pumzi na kushusha sikuwa nikielewa nini cha kufanya.
Niliingia darasani lakini hakika sikuambulia chochote.
Muda wa vipindi ulipoisha tulirudi bwenini kwetu Mabibo.
Kwa kweli sikuwa na nguvu za kumsaidia Melania kutafuta simu yake kila mtu alichanganyikiwa kwa kiwango chake.
Weekend nilirudi nyumbani, kwa kweli nilikuwa nashindwa jinsi ya kumuanza mama, naanzaje kumuomba mama hela.
Melania naye hakufanikiwa kuipata simu yake hakika alikuwa na majonzi sana.
Weekend kwangu ilikuwa chungu sana maana kila mara nilipokuwa nikijaribu kutafuta njia ya kupata hela nilishindwa,
mwisho wa yote nilimkumbuka mpenzi wangu Patrick, niliamua kumtafuta.
Nilikutana na Patrick kiasi kama miezi sita iliyopita, wakati huo ndiyo nilikuwa tu nimemaliza kidato cha sita
katika shule ya sekondari ya Ifakara Girls iliyopo Ifakara mjini.
Nilikutana na Patrick katika moja ya sherehe ambazo baba alikuwa amealikwa, baba alipenda kuhudhuria na mimi.
Patrick alikuwa ni mhasibu wa TANESCO pale Ubungo mataa na alikuwa akiishi Shekilango.
Alikuwa amepanga nyumba moja kubwa ambayo ilikuwa inajitegemea kwa kila kitu, nilimpenda sana Patrick.
Tatizo moja tu alikuwa nalo Patrick alikuwa ni mtu asiyeishiwa na ubize, kila wakati yuko bize, asipokuwa bize na
kazi basi yupo bize na marafiki, asipokuwa bize na marafiki basi na kitu kingine chochote tu ilimradi yuko bize muda wote.
Siku ya Jumamosi niliamua kwenda kwake.
Patrick alikuwa hafahamiki kwetu hivyo nilidanganya nyumbani kuwa ninaenda kwa rafiki yangu,
mama aliniruhusu.
Niliondoka hadi kwa Patrick sikutaka kumuambia kwamba naenda.
Siku hiyo ya Jumamosi Patrick hakuwepo nyumbani, kwakuwa ninafahamu sehemu ambayo Patrick huwa anaweka funguo yake
nilifungua na kuingia ndani na kisha nikampigia simu.
“Patrick niko kwako nakusubiri.”
“Sociolah mbona umekuja bila kuniambia leo mimi siko nyumbani siku nzima.”
“Patrick you are not serious.”
“Sociolah niko bize sana naomba tu uende nyumbani.”
“Patrick nina shida ndiyo maana nimekuja.”
“Sema unataka shilingi ngapi.”
Kiukweli ilinikera sana.
Mbali na kuwa nilikuwa nikihitaji hela lakini pia nilihitaji faraja kutoka kwake.
“Sawa.”
Nilikata simu.
Sikuwa na pa kwenda niliamua tu kumalizia tu siku yangu hapo, niliingia chumbani kwake na kulala.
Jioni ilifika Patrick hakuwa kweli amerejea niliondoka na kuelekea nyumbani.
Nilipofika sikutaka hata kula niliingia chumbani kwangu na kulala, mama alikuja kuniamsha.
“Sociolah amka uende kula.”
“Mama nimechoka sana.”
“Nimesema amka uende kula, siku hizi umekuwa mvivu sana kula sijui una matatizo gani Sociolah,
utakonda chuo hakihitaji mchezomchezo kula mwanangu.”
Sikutaka kubishana naye nilielekea sebuleni nilikula kidogo na kisha kurudi chumbani kwangu.
Nilipofika tu nilikuta simu yangu inaita alikuwa ni Patrick, nilipotaka tu kupokea ilikata,
nilikuta simu zisizopokelewa saba na meseji tano, zote zilikuwa za Patrick, alipiga tena nilipokea.
“Hello.”
“Am sorry Sociolah nilikuwa niko bize na saa hizi nimerejea nyumbani ulikuwa na tatizo gani.”
“Patrick…”
“Nakusikiliza.”
Aliongea.
Unaweza pia kusoma: