Real Love - Episode 01 
Ilikuwa taarifa ya kushitusha sana kwa kila mtanzania.
Vilio vilitawala kila sehemu, hapakuwa na historia ya tukio la aina hiyo kuwahi kutokea.
Hofu zilitanda ndani ya mioyo ya watu wengi.
Mamia ya watu walioko mkoani Dar es salaam walimiminika mahali pale ili kupata taarifa yoyote ile, wengine waliopo mbali au ambao walishindwa kuhudhuria
walikuwa karibu na televisheni zao kuhakikisha hawapitwi na wengine walikua bize na simu zao wakifuatilia.
Katika mkoa wa Dar es salaam hapakuonekana magari ya watu wala watu barabarani zaidi ya magari machache yaliyokuwa yakienda kwa mwendo
mkali huku yakiambatana na kelele nyingi, kila mtu alijitahidi kujificha vyema akiwa mahali alipo.
Aliyekuwa kazini alijificha hapohapo, aliyekuwa shuleni au dukani naye alifanya hivyo.
Hakuna aliyethubutu kutoka mahali alipokuwepo.
Eneo la tukio lilikuwa kimya sana kana kwamba hakukuwa na watu wengi muda mchache uliopita, sasa makundi ya watu yalihamia sehemu nyingine kabisa huku
sura zao zikiwa zimehamanika sana.
“Hiiiihiiiiiii”
Sauti ya kiume ilisikika ikilia kilio kwa uchungu, machozi yalimmiminika Charles huku uso wake ukionesha ushirikiano kwenye uchungu uliomkabili.
Alilia kwa mengi sana, lawama, uchungu, majuto, hatia na ukiwa vyote vilimuandama.
Wakati akiwa amesimama nje ya geti la hospitali ya taifa Muhimbili alikuwa akilia kama mtoto.
Hakuna aliyemjali kwa sababu watu wengi waliokuwepo hapo nje walikuwa wakilia pia.
Wengi kati ya watu waliokuwepo hapo nje hawakutaka kuingia tofauti na Charles yeye alikuwa akiogopa kuingia.
Alikuwa na mawazo mengi yaliyoifanya miguu yake kumuwia vigumu kuingia.
Alijilaani sana, alijilaumu, alijipa kesi nzito ambayo hukumu yake ni kunyongwa.
Makundi ya watu waliosimama nje ya geti la Hospitali ya taifa yalikuwa yamejitengezea kwa kuacha njia ya kutosha gari kupita.
Magari yalikuwa yakitoka na kuingia muda wote kwa mwendokasi sana, magari hayo yalikuwa ya hospitali, mengine ya serikali na mengine ya watu binafsi.
Ving’ora vilikuwa vikipiga kelele kwa nguvu eneo hilo lilijaa msongamano na vurugu pamoja na kelele zilizochanganyikana na vilio, mayowe, na hata maongezi mengine,
hakika watu waliguswa.
Simu ya Charles iliita, alisita kuipokea.
Watu waliosimama pembeni yake walikuwa wakimuangalia kwa jicho la “pokea simu” nayeye aliwaangalia kwa jicho la “kwani inawahusu?” Au “simu ya kwenu?”
Simu iliita mpaka kukatika na kisha ikaanza kuita tena, ikaita ikaita.
Pale alipokumbuka kuwa hata yeye ni mhanga aliamua kuitoa simu mfukoni.
Lahaulaah!!!
“Mama Happy.”
Ndivyo ilivyosomeka simu ya Charles.
Macho yalimtoka pima.
Watu pia waliomzunguka walikuwa wakimuangalia kwa macho ya “si upokee.”
Bila hata kuambiwa, alijua ni nini ataambiwa punde atakapopokea simu hiyo.
Moyo ulimuuma na nafsi ilizimia.
Simu ikakatika kisha ikaanza tena kuita.
Safari hii alipiga moyo konde akapokea.
“Uko wapi baba.”
Mama Happy alisema kwa haraka.
“Eeer...seem....”
Alishindwa cha kuongea.
“Naomba msaada baba yangu...tunahitaji damu.”
Mama Happy aliongea kwa namna ya huzuni na upole.
Wala Charles hakusubiri kupigiwa filimbi wala kuongezewa neno lolote, alichomoka mbio kali, walinzi walimpigia kelele asimame na hakuwa na mawazo nao
wala hakusimama.
Alikwenda moja kwa moja mpaka jengo la emergency.
Alimkuta mama Happy amesimama hapo akiwa amechanganyikiwa.
Ndani ya hilo jengo watu walikuwa ni wengi na walikuwa wakikimbia hapa na pale, kila mtu alikuwa bize hakuna aliyesimama bila muelekeo
wala hapakuwa na watu waliokuwa wakiongea ongea.
Bila kupoteza muda mama Happy alimshika mkono Charles na kumuongoza kwenye vyumba vya madaktari.
Huduma zilikuwa zikitolewa hapo, huku wengine wakipelekwa katika wodi za wagonjwa mahututi.
Walipofika hakuna aliyeongea daktari alianza kushughulika na Charles.
Jambo ambalo lilimpa amani Charles kiasi cha kuweza kutoa tabasamu bila kujali eneo alilokuwepo na jambo lililompata.
Dakika tano zilitosha kuthibitisha kuwa anaweza kumtolea damu mgonjwa wa mama Happy na hapo alianza kutoa damu kuokoa maisha.
Asubuhi ya siku hiyo Charles alikuwa kama aliyechanganyikiwa.
Kila mara alikuwa akiitazama simu yake akidhania atapokea ujumbe wowote kutoka kwa Happy lakini mpaka saa nne ya asubuhi hakukuwa na ujumbe
wowote ulioingia kwenye simu yake kutoka kwa Happy.
Ni usiku uliopita walikuwa na mzozo mzito juu ya mdada aliyetambulika kama Yvonne.
Ilionesha ni kiasi gani Happy alikasirishwa na jumbe alizozikuta kwenye simu ya Charles.
Tangu waachane usiku wa jana yake saa mbili hakujibu jumbe yoyote kati ya nyingi ambazo Charles alimtumia kupitia mtandao wa
WhatsApp na meseji za kawaida.
Akiwa bado amekaa kitandani Charles alifikiria mengi.
“Yvonne huyu...msieeew (anasonya) wacha nimpigie Happy wangu.”
Anapiga na simu inaita bila kupokelewa mpaka inakata, anapiga tena inapokelewa.
“Hallo baby.”
Anaongea Charles kwa kiherehere.
“Yes Karls.”
Sauti nzuri ya Happy inaongea ikitaja jina ambalo Happy alipendelea kumuita Charles.
Charles anahisi faraja.
“Mbona nimekupigia sana hujapokea.”
“Sorry nlikuwa nje kidogo.”
“Well can we go out for some snacks and drinks.”
Kimya.
“Pliz Happy naomba usikatae nataka tuongee sweetie.”
“Okay, wapi?”
“Mlimani city saa kumi na moja.”
“Kwanini isiwe saa tisa halafu saa kumi nirudi zangu nyumbani.”
“Come on baby..”
Charles alibembeleza.
“Okay, baadae.”
Happy alikata simu.
Kwa upande mwingine Charles alipanga kuenda kumuomba msamaha Happy na kumhakikishia kuwa hana mahusiano na Yvonne.
Tangu wamalize chuo ni mwaka sasa umepita.
Wakati Happy akiwa amesomea ualimu chuo kikuu cha mzumbe na Charles amesomea procurement and logistic kutoka chuo cha ushirika Kilimanjaro.
Ingawa walikuwa wakisoma mikoa tofauti lakini walikuwa na mahusiano waliyoyaanzisha wakiwa mwaka wa pili chuoni baada ya kukutana wakiwa
mkoani Dar es salaam ambapo ndipo yalipokuwa makazi yao wote wawili.
Charles alikuwa akiishi Mikocheni pamoja na wazazi wake wote wawili pamoja na mdogo wake wa kike Careen huku akiwa ameajiriwa mara baada ya
kumaliza chuo katika kampuni binafsi ya Kennys Ltd na alikuwa akilipwa mshahara mzuri tu na Happy alikuwa akiishi Changanyikeni.
Na mama yake baada ya baba yake kumtelekeza mama yake na kwenda kuishi na mwanamke mwingine. Maisha yao akina Charles hayakuwa mabaya walikuwa na
maisha mazuri sana.
Wazazi wake walikuwa waajiriwa serikalini na wenye wadhifa mzuri tu.
Mama wa Happy alikuwa ni mwalimu wa sekondari hivyo maisha yao hayakuwa mabaya japo pia sio mazuri.
Mama happy aliweza kujenga nyumba yake hapo Changanyikeni na kujenga nyumba ya wapangaji ambapo wote walikuwa wakiishi hapo.
Mama Happy alikuwa akimtambua Charles kama mchumba wa mwanaye ila familia ya Charles haikuwa imewahi kutambulishwa kwa Happy
kwahiyo ilikuwa haimtambui.
Nafsi ilikuwa ikimuambia asiende hata hivyo alimpenda sana mchumba wake Charles na alimwamini sana hivyo aliona bora aendelee
kumsikiliza.
Moyo wake ulijawa shaka na huzuni ambazo hakuelewa zinapotokea.
Alijikaza hivyohivyo ili awahi japo aliona anaishiwa nguvu.
Alivaa vizuri akapendeza, gauni zuri jeusi ambalo alilifunga na mkanda juu kidogo ya tumbo lake dogo, gauni hilo lilichanua kuanzia tumboni na kuishia juu
kidogo ya goti lake huku likimchora vizuri umbo lake na kuacha miguu yake mizuri wazi.
Chini alivalia kiatu kilichoinuka kidogo ili kisimchoshe na kichwani aliamua kuziachia nywele zake nyingi kwenda nyuma.
Hakika alivutia sana uzuri wote aliupata kutoka kwa mama yake.
Alipita sebuleni na kumuona mama yake akiwa anaangalia televisheni.
Alienda kukaa kando yake na kumuelezea kiini cha safari yake bila kumficha, bila hiyana mama yake alimruhusu kwenda.
Happy alinyanyuka na kupiga hatua za kivivu jambo ambalo hata mama yake alilihisi.
“Happy....unajisikiaje mamaangu.”
“Hamna mama nipo vizuri tuu.”
“Kama hujisikii vizuri ubaki tu ukimuelezea Charles ataelewa.”
“Hamna mama acha niende.”
“Natamani ungebaki.....ila nenda na urudi salama mama.”
“Sawa mama ubaki salama.....nikuletee nini?”
“Ukirejea salama ni furaha yangu.”
Aliongea mama Happy huku Happy akitoka nje, alihisi kizunguzungu lakini alijipa moyo.
“Utapumzika nikirudi.”
Akatoka na kupanda bajaji ambapo alishukia eneo la chuo kikuu na kupanda daladala iliyomfikisha mlimani city.
Aliposhuka mlimani city ndipo alipotoa simu yake na kukuta meseji nyingi kutoka kwa Charles.
“Baby.”
“Njoo hapa KFC.”
“Nakusubiri.”
“Uko Wapi.”
Hakujibu bali aliongoza njia kuingia getini alipofika mkabala na KFC alimuona Charles kwa ndani na Charles nae alimuona na kumtabasamulia.
Happy hakuhangaika kutabasamu bali aliongeza hatua kuelekea alipo Charles.
Alifika na kuketi.
“Mambo baby.”
Charles aliondoa ukimya.
“Poa.”
Alijibu Happy huku akijilazimisha kutabasamu tabasamu lililomfanya apendeze sana.
Charles alianza kumuomba msamaha Happy na kisha kumueleza kuwa Yvonne ni mfanyakazi mwenzao anayemsumbua tu na wala hana mahusiano naye.
Alimuonesha pia maongezi yao kwenye simu pamoja na picha zilizomuonesha Yvonne akiwa amekaa kihasara ambapo ilionekana wazi kuwa Yvonne ndiye
anayemtaka Charles na Happy alimuamini.
“Sasa utafanyaje ili asikusumbue sipendi ukaribu nae.”
Alisema Happy kwahiyo sauti ya kudeka.
“Najua jinsi ya kudeal naye, relax my queen wewe ndo mtu pekee uliyeuteka moyo wangu.”
Aliongea Charles na kumfanya Happy atabasamu.
Punde chakula kililetwa, kuku za KFC na chips na cocacola bonge pamoja na ice cream kama ambavyo alivyokuwa anapenda Happy.
Walianza kula kwa furaha huku Charles akijitahidi kumchekesha Happy kadri ya alivyoweza kwa vile aligundua kuwa Happy amekuwa mnyonge sana,
na sio siri aliweza kwa kiasi chake.
“Guess...”
Alitokea mdada na kumziba macho Charles.
Happy alibaki amekodoa tu macho kama fundi kushona akitafuta kupenyeza uzi kwenye tundu la sindano.
Charles alikua akijaribu kuitoa ile mikono iliyombana vyema usoni.
Mdada yule alikuwa akimtazama Happy huku akitabasamu Happy alimshangaa.
Yule dada baada ya kuona Charles anaelekea kuiondoa mikono yake aliinama na kumbusu sikioni na kuachia mikono.
Happy aliachama mdomo huku akijitahidi kuizuia hasira yake.
“Yvonne...kwann umefanya hivyo?”
“Aren’t we lovers?? Au hutaki huyo dada ajue?”
“Eeeh........wwwwee.....Yvvone!”
Aliita kwa hamaki huku akiishiwa maneno mdomoni.
Happy alibaki amefura kwa hasira.
“Sipendi mahusiano ya kufichaficha actually kwahiyo uliniitia nini hapa? I thought unakuja kunitambulisha sijui kwa dadaako huyu sasa
nini unanifokea?”
Yvonne aliongea kwa ashuo huku akibinua mdomo na kumtazama Happy kwa dharau.
Happy alinyanyuka kwa hasira na kuanza kupiga hatua za haraka kutoka nje.
“Happy....Happy...”
Aliita Charles huku akikimbia kumfata nje alikoelekea.
Siku hiyo ya Jumamosi Mlimani city palikuwa na watu wengi ambao walianza kuangalia sinema hiyo ya kikorea ya bure kabisa.
Happy alifanikiwa kutoka mpaka nje na wakati huo Charles alifika na kumzuia, Yvonne naye hakubaki nyuma alitoka kuwafuata ingawa
hakufika walipokuwa wamesimama.
“Happy kwanini unafanya hivyo can’t you see kuwa anataka kuniharibia kwako mbona tumeshayaongea yameisha kwanini huniamini?”
Alilalamika Charles.
“Niamini nini sasa Charles??”
“Nimeshakuonesha kila kitu huoni anafanya makusudi uchukie uniache hebu acha utoto Happy unajua nakupenda wewe pekeako.”
Happy alibaki kimya wakati huo alijiona mjinga sana.
“Naomba turudi ndani Happy tukamalizie siku yetu vizuri tafadhali.”
Happy hakuwa na la kubisha alianza kuondoka bila kusema neno lolote kuelekea ndani ya jengo la mlimani city.
Yvonne aliyaona hayo yote na alikasirika sana.
Aligeuka kwa hasira na kuiendea gari yake.
Happy alitembea akijua kuwa ameongozana na mchumba wake Charles kumbe Charles alibaki palepale akimtazama mwanamke yule aliyempenda na ambaye hakuwa
tayari kumpoteza mawazo mengi yalipita juu yake.
“Sitakuacha Happy katika hali zote.”
Alinong’ona tu mwenyewe na hapo aligundua kuwa Happy amesimama anamtazama.
“I love you.”
Alisema Charles bila kutoa sauti.
Happy alielewa na alitabasamu na kisha kugeuka kuendelea kuingia ndani huku Charles naye akianza kupiga hatua kuelekea alipo mchumba wake.
Ghafla wakati Happy akiwa anakaribia kulifikia lango la mlimani city, ndani ya sekunde jengo la Mlimani city linasambaratika.
Moto mkali ukizuka na sauti kubwa na moshi mwingi ukitanda.
Yvonne aliyekuwa akifungua mlango wa gari yake alishtuka na kupiga kelele.
Sasa eneo lilitawaliwa na vilio na kelele zisizo na mpangilio.
Moto ulizidi kuwaka haikutegemewa mtu yeyote aliyepo ndani ya jengo hilo kutoka salama Shambulio la kigaidi.
Akiwa ameanguka chini kutokana na nguvu ya shambulio hilo Charles alikuwa akilia kama mtoto.
“Happy.....”
Alizubaa kidogo huku akiwa haamini anachokiona.
Unaweza pia kusoma: