Muonekano wa Giza:

Msaada

Real Love - Episode 02

Alipogutuka alijaribu kukusanya nguvu huku akijitahidi kuinuka na kukimbilia kule moto ulikokua ukiwaka lakini alidakwa na kikosi cha uokoaji ambacho kilikuwa kimeshafika mahali hapo.
Walimuweka pembeni huku wakijaribu kusaidia watu waliokuwa wapo hai na ambao maiti zao zilionekana pia walichukuliwa.
Baadhi ya watu ambao walikuwa nje ya jengo hilo na kwenye sehemu ya kuegesha magari walijikuta wakipatwa na mshituko na wengine kuzimia na hata kufariki. Kila mtu alikuwa akikimbia kuokoa maisha yake.
“Mchumba wangu jamaniiiiii....”
Akiendelea kulia Charles.
“Yupo Wapi?”
“Alikuwa hapo mlangoni.”
“Itakuwa ameshapelekwa hospitali nenda huko muhimbili ukaangalie.”
Hakuwa hata na nguvu ya kupiga hatua, alitia huruma.
Alipandishwa kwenye moja ya magari ya uokozi na kwenda mpaka muhimbili hata hivyo alishushwa getini kwa vile hapakuwa na mtu aliyeruhusiwa kuingia ama laah hospitali ingetapakaa watu wazima zaidi ya majeruhi.
Habari zilienea kwa kasi ya upepo kwa nchi nzima.
Hali ya hatari ilitangazwa huku taarifa zikificha ama kwa kutokuwa na taarifa sahihi au kwa kuogopa kuwatisha juu ya watu waliopoteza maisha.
Aliendelea kulia akiwa pale mlangoni mpaka alipopigiwa simu na mama wa Happy na kuhakikisha mpenzi wake yupo hai.
Hakutaka kujua mama Happy alifika saa ngapi wala alipataje taarifa.

Damu iliendelea kutiririka kutoka kwenye mishipa yake, hakuwa peke yake watu wengi walijitolea kutoa damu kwa waathirika wa mlipuko huo wengine kwa ajili ya ndugu zao na wengine kwa ajili ya kuguswa na tukio hilo.
Alipomaliza alitoka nje alipomkuta mama Happy akilia kwa uchungu.
“Mama kulia hakusaidii tumshukuru Mungu Happy ni mzima mengine tuyaache yapite.”
Charles alijaribu kumtia moyo.
“Sawa.”
Alisema mama Happy huku akinyanyuka.
Ni kama alikuwa akimkwepa Charles lakini Charles hakulijua hilo.
Kila siku baada ya kazi Charles alikuwa akihudhuria hospitalini hapo na kumkuta mama Happy akiwa nje ya wodi za wagonjwa mahututi.
Alionekana mtu ambaye hayupo sawa nyumbani na kazini.
Alikuwa akionyeshwa dharau na Yvonne waziwazi na wala hakujali.
Bado tukio la ugaidi lililofanyika mlimani city na kikundi cha al-shabaab kupinga majeshi ya Tanzania kupelekwa kulinda amani nchini Kenya walipokuwa wamepiga kambi na kufanya mashambulio kadhaa, lilikuwa halijafutika mioyoni kwa watu.
Mpaka kufikia wiki moja tayari watu 519 waliripotiwa kufariki.
Kila siku maiti kadhaa zilitolewa kutoka katika chumba cha magonjwa mahututi.
Mama happy alikuwa akilia kila siku akiomba asiwe mtoto wake huyo kifungua mimba.
Charles aliumizwa na hali ya mama Happy kukataa kuoga wala kula wala kuondoka hospitali ni hapo.
Alihisi mama huyo anamchukia sana kwa kuona kuwa ndio chanzo cha mwanaye kupata matatizo ingawa kiuhalisia mama huyo hakuwa akimuwazia mabaya Charles.
Haikuwa mpaka wiki ya pili yake ambapo Happy alirejewa na fahamu.
Nje ya wodi alikuwepo mama yake tu naye aliruhusiwa kumuona.
Alipoingia ndani mama Happy pamoja na Happy waliishia kulia tu mpaka mama huyo alipotolewa nje.
Charles hakufika hospitali siku hiyo kwa vile alihisi uchovu.
Nyumbani kwao mama yake alikuwa akimuijia juu kuhusu mahali panapomchelewesha akishatoka kazini.
Siku hiyo aliamua kupumzika na kwa hakika alilala sana kiasi cha kutosikia simu yake iliita wakati mama Happy alipompigia.
Haikuwa mpaka kesho yake alipohudhuria hospitalini pale na kupata habari njema.
Alisubiri mpaka muda wa kuruhusu ndugu wa wagonjwa kuingia lakini mama wa Happy alimkataza kuingia.
“Kwanini?... Kwanini nisimuone mchumba wangu na ameamka? Au yeye ndo amesema hataki kuniona?”
Maswali haya yote yalimtoka Charles ambapo mama Happy alikosa majibu, alibaki akilia tu.
“Nitaingia.”
Alisema huku amekunja sura, hisia zake kwamba mama Happy amemchukia zilidhihirika.
“Hataki niendelee na mwanaye!! me simuachi Happy mpaka aseme yeye mwenyewe kuwa hanitaki.”
Alijiongelesha huku akiingia ndani akimuacha mama Happy akizidiwa na vilio.
Alipewa mavazi maalumu ya kuingilia ndani na baada ya kuyavaa aliruhusiwa kuingia.
“Kitanda namba moja.”
Nesi alisema wakati Charles akiingia ndani ya wodi ile.
Hakuamini alichokiona.
Alifunika mdomo wake kwa viganja vyake huku akipepesuka.
Nesi aliyesimama nyuma yake alimuwahi.
Machozi mfululizo yalimtoka Happy aliyekuwa amelala pale kitandani baada ya kuona kila kitu.
Nesi alimuongoza nje, alimtoa mavazi yake na kumpeleka nje kabisa.
“Haturuhusu mtu mwenye moyo mdogo kuingia humu ndani tafadhali sana mama.”
Alisema Nesi huku akimuacha Charles aliyekuwa akilia karibu na mama Happy ambaye aliongeza sauti ya kilio.

Charles aliondoka bila kuaga huku Machozi yakimuanguka kwa wingi.
Alilifikia gari lake lakini ilimuwia vigumu kulifungua, alijikuta amekaa nje katika mlango wa gari lile.
Sasa watu walimshangaa na yeye alihisi aibu kidogo akijitahidi kunyanyuka na kufungua mlango wa gari lile na kuingia ndani.
Kila mtu alijua kuwa amepata taarifa mbaya.
Charles alilia sana, alilia, akalia kisha akalia tena.
Simu iliita hakuwa na nguvu ya kuipokea alitazama jina la “Dear mama” lililokuwa linasomeka pale juu huku akiongeza kasi ya kulia.
Saa mbili usiku ilimkuta akiwa bado yupo ndani ya gari lake katika maegesho ya magari muhimbili.
Simu yake ilishaita sana na meseji ziliingia nyingi hakuwa hata na nguvu ya kuzifungua.
Mara simu yake ikaanza kuita tena “Best pal” ndivyo ilivyosomeka.
Hakupata shida kujua kuwa ni rafik yake.
“Oi chalii uko Wapi?”
Aliuliza Salimu baada ya kupokelewa simu.
Kimya.
“Umepata tatizo? niambie uko Wapi nije sasa hivi.”
“Parking 3 Muhimbili.”
Alisema Charles na simu ikakatwa.
Ilikua muda wowote kuanzia saa hiyo Salimu angefika.
Salimu alikuwa zaidi ya ndugu kwake.
Charles alimheshimu Salimu kama kaka yake mkubwa.
Nusu saa baadae Salimu aliwasili na aliweza kuitambua gari ya Charles.
Alifungua mlango wa dereva.
“Hamia kule bro.”
Charles hakupinga alishuka huku akitembea kwa msaada wa kulishikilia gari mpaka upande wa pili na kujitupa kwenye siti ya mbele ya abiria.
Salim alikuna kichwa akaingia na kumsaidia Charles kufunga mlango na kisha kumfunga mkanda na yeye akafunga mlango na mkanda na safari ikaanza.
Japo Charles hakuwa akijua mwisho wa safari itakuwa ni wapi lakini hakusema lolote pia kwasababu alimuamini sana rafikiye.
Ni michirizi tu ya Machozi ilijengeka usoni mwake.
Macho yake yalivimba sana na kuingia ndani huku machozi yaliyokaukia yakichora ramani zisizoeleweka usoni mwake.
Salim alijionya kumuuliza chochote.
Safari iliendelea.

Saa nne kasoro Salimu alipiga honi mbele ya geti la nyumbani kwao Charles.
Akiisha kuingia baba na mama yake Charles walitokea kumlaki aliwakabidhi Charles huku akiwahusia kutomuongelesha.
Mama Charles alimuongoza Charles ndani huku Charles akionekana kama mgonjwa na baba Charles alimshukuru Salim na kisha Salim aliondoka akiahidi kurejea kesho yake.
Charles alipelekwa kuoga huku mama yake akimpisha wakati huo akimuandalia chakula baada ya kuoga.
Charles alijitupa kitandani na kupitiwa na usingizi.
Mama Charles alipofika kumletea chakula alimkuta tayari ameshalala.
“Muache tu apumzike atakula akiamka.”
Aliongea baba Charles kutokea mlangoni kwa chumba cha Charles baada ya kuona mkewe akijaribu kumuamsha Charles ili ale.
Kishingo upande mama Charles anamfunika vizuri mwanaye huyo wa kwanza kati ya watoto wake wawili na kisha kumzimia taa na kumuacha apumzike.
Mpaka saa nne asubuhi Charles hakuwa ameamka kitu kilichowatia hofu wazazi wake.
“Hebu kamuamshe.”
Alisema baba Charles, mama Charles aliamka kwenda kumuamsha.
Alinyonga kitasa na kugundua kuwa mlango umefungwa kwa ndani.
“Charles......Charles...Charles hebu fungua mlango jamani.”
Alilalama bila kuitikiwa.
“Charles.......we Charles.....Charles, Mungu wangu.”
Kadri alivyoendelea kuita ndivyo ambavyo sauti yake ilibadilika na kuwa kilio.
Baba Charles alishasogea mlangoni na kumshika mkewe.
Mama Charles akiendelea kuita huku akinyonga kitasa kile kwa nguvu lakini hakukuwa na mtu aliyeitika kutoka ndani.
Baba Charles aliamua kumpigia simu alipiga zaidi ya mara tano haikupokelewa aliporudia tena simu ilikatwa.
Anapiga tena ikakatwa na kuzimwa.
Alipojaribu tena ikawa haipatikani.
“Charles em fungua mlango mwanangu.”
Aliongea baba Charles kwa sauti yake nzito.
Mama Charles alikuwa akilia kwa sauti kubwa.
“Niacheni nataka kupumzika endeleeni na mambo yenu.”
Sauti kutoka ndani ilisikika.
Mama Charles akijaribu kubembeleza lakini hakukuwa na sauti nyingine iliyotoka.
Walikata tamaa na kuamua kurudi kukaa kwenye viti huku mama Charles akimuegemea mumewe kwa masikitiko.
Baba Charles alitoa simu yake na baada ya kubonya hapa na pale aliweka sikioni.
“Hallo....Marhaba....wazima..Charles amegoma kula...sawa mwanangu.”
Alikata simu.
“Nani?”
Mkewe aliuliza.
“Rafiki yake Salim?”
Jioni ya siku ile Salim alikuja kama alivyoongea na baba yake Charles, Mr Katesh.
Charles hakufungua mlango mpaka alipomaizi kuwa ni Salim ndiye aliyekuwa akigonga mlango.
Salimu akiingia na ni kama ni yeye tu ndiye aliyekuwa akijiongelesha kwani Charles hakuwa akijibu chochote.
Baada ya kuona rafikiye hajibu chochote alianza kumshawishi akubali kula na kumwambia kama anataka kupumzika atawaambia wazazi wake wasimsumbue ila ale.
Charles alikubali kwa kutikisa kichwa.
Salim aliamua kuondoka huku akiwahusia wazazi wa Charles kutomsumbua aliwaambia wampelekee chakula kilaini na kile ambacho Charles alipendelea kula bila kumlazimisha.
Aliwaambia inawezekana ana tatizo kwahiyo anahitaji kupumzika na kufikiria hivyo atakapokuwa sawa atasema wasimlazimishe.
Pia aliwaambia wamuombee ruhusa kazini kutokana na matatizo yake na aliahidi kuja kumuona kila akitoka kazini kwake.
Wazazi wa Charles walijitahidi kufuata alichosema Salim hata hivyo mara nyingi walikuta chakula walichomuwekea Charles hakijaliwa hata kidogo. Hali hii ilimuumiza sana mama Charles alikuwa akijifungia chumbani na kulia mwenyewe.
Salim hakupata nafasi ya kuja kumuona tena rafikiye kwa kubanwa na majukumu ya kazini na familia.
Mpaka baada ya wiki ndipo alipopata wasaa kumtembelea rafikiye.
Charles alimkuta rafikiye amedhoofu sana, sura yake ilionesha amelia kwa muda mrefu.
“Huli kama tulivyokubaliana? Una nini rafiki yangu? Sema kisije kukuua bure tuone namna ya kukusaidia, ona upo wiki nzima ndani hujapata nafuu si bora utuambie tukushauri, au huniamini hata Mimi?”
Alisema mfululizo.
“Daaah...”
Aliongea Charles huku machozi yakimlenga lenga.
Salim alijua kuwa rafiki yake amekabiliwa na tatizo kubwa alitoa leso mfukoni kwake na kumfuta machozi.
Charles aliipokea leso na kujifuta mwenyewe.
Alipomaliza alikaa kitandani vizuri na kuanza kuongea kwa uchungu huku sauti ikikatakata.
“Bro, sielewi cha kufanya nimewaza mpaka nimefika mwisho sijui nitafanyaje...”
Sauti yake ilielekea kilio.
“Endelea bro..nakusikiliza.”
“Najua unamjua mpenzi wangu Happy....”
“Kafanyaje?...kakuacha??”
Salim Aliongea kwa jazba sana.
“Bora ingekuwa hivyo bro.”
“Niambie bro usinifiche.”
“Pia nilikuelezea kuhusu Yvonne yule dada wa kazini kwetu ... Sasa Happy akawa ameona meseji za yule dada akakasirika nikamuita nimuombe msamaha akaja kweli tukakutana mlimani city..... Salim..ndo... ndo ile siiiisikuuu paliwaaaakhaa...Haaapy alikuwa mlangoooni ameungua Broo kaunguaaaaaaa.”
Charles aliongea kwa uchungu sana Salimu alimvutia begani kwake na kumkumbatia huku akimpigapiga mgongoni kumtia moyo.
Happy alikuwa akimfahamu japo hakumuona uso kwa uso lakini alionyeshwa picha zake na sifa nyingi alizisikia kutoka kwa Charles.
Alijua kuwa Happy ndiye mwanamke pekee ambaye Charles anataka kumuoa.
Na alijua kuwa Happy ni mwanamke mzuri na mwenye moyo mzuri.
Taarifa ile hata yeye ilimuumiza na chozi lilimtoka.
Akijitahidi kujifuta ili aoneshe ushujaa mbele ya rafiki yake yule mwenye msiba mzito.
“Pole sana rafiki yangu...kwa hiyo ndo kusema Happy hatunaye??”
Aliuliza kwa upole.
Charles alipendelea kulia kwa sauti kuu alilia mno.
Salim alipata shida kumbembeleza.
Alijua kuwa Happy amefariki kwa kuwa mamia ya watu waliokuwepo Mlimani city waliripotiwa kufa.
“Broo Happy yupo hai lakini...lakini(kilio)happy sio happy yule nnayemjua....ameunguaaaaa mwili wote umeungua.”
Charles sasa alikuwa akilia kama mtoto huku kamasi, machozi na jasho vikitiririka.
Uso ulishabadilika na kuwa mweusi zaidi ya alivyo macho yalikuwa mekundu huku mdomo wake ukilowa pamoja na fulana nyepesi aliyokuwa ameivaa.
“Tulia Charles cha msingi hajafa unaweza hata kumuona....”
“Broo huwezi kumtazama huweeeezi..anatisha....Happy wangu jamani ni nini hili.”
Sasa Charles alikuwa kama aliyechanganyikiwa.
Wazazi wa Charles waliingia kwa pupa.
Mama Charles aliyekuwa ametangulia huku akilia alijibwaga pembeni ya Charles na kumkumbatia kwa nguvu.
Ikawa ni kilio juu ya kilio.
Salimu alimshuhudia mzee Katesh akitokwa na chozi Salim alinyanyuka na kupisha sehemu kwa ajili ya familia hiyo kufarijiana.
Alisimama kando akiwatazama jinsi walivyokuwa wakilia hata yeye Machozi yalimtoka.
Alisubiri kwa dakika kama tano na kurejea pale kitandani.
“Mama muacheni apumzike kwanza.”
Alisema Salim huku amkimnasua mama Charles kutoka kwenye mwili wa Charles aliyekua akilia huku akishika kichwa kuashiria alikua akisikia maumivu.

Sehemu 1 Sehemu 3
0
0