Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Real Love - Episode 03

Mama Charles akinyanyuka bila ubishi na kumpisha Salim aliyemlaza vizuri Charles pale kitandani na kumfuta Machozi na kisha kuwakusanya wazazi wa Charles na kutoka nao nje.
Walifika sebuleni na kuketi mama Charles, Gertrude alikuwa bado akipiga kwikwi alikuwa amemuegemea mumewe kifuani na Salimu alienda kuketi kwenye sofa jingine lililokuwa pembeni kati ya masofa mazuri yaliyokuwepo mule sebuleni.
“Baba kilichomkuta Charles ni kwamba...”
Hakupewa nafasi kumalizia.
“Tumesikia yote.. tulikuwa hapo mlangoni. Kwakweli kijana wetu ana mtihani mzito sana.”
Salim alitoa leso na kujifuta machozi.
“Nachoomba muacheni apumzike atakavyo atarejea tu kuwa kawaida au kama inawezekana apatikane mwanasaikolojia kwa ajili yake.”
“Sawa asante Salim imekuwa rafiki mwema kwa kijana wetu nasisi tunakufurahia.”
Alisema baba Charles aliyekuwa muongeaji.
Salim aliaga na kuondoka huku baba Charles akishindwa kumsindikiza kutokana na mkewe kugoma kutoka kifuani kwake.
“Tufanyaje mke Wangu.”
“Tutafute psychologist kwanza kabla ya chochote.”
“Okay.”

Mwanasaikolojia alitafutwa na kuanza kumtibu Charles ambaye alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa.
Mwanasaikolojia yule alitambua maendeleo hafifu ya Charles hata hivyo alijipa moyo na kuendelea kumtibu kwa namna mbalimbali.
Haikuwa mpaka mwezi mmoja na nusu ndipo Charles alionesha kuimarika.
Salim alienda kumtembelea na kufurahishwa na maendeleo yake.
“Bro naomba nisaidie kitu.”
Charles alianza.
“Naomba ukamtembelee Happy mama yake ataona nmemtelekeza inakaribia miezi miwili hatumi hata meseji wala sijawasiliana nao, naomba please.”
“Duuuh.”
Aliguna Salim aliwaza sana hata hivyo hakuona shida kumkubalia rafiki yake huyo.
“Poa nitaenda weekend.”
Alisema Salim na alienda kweli mwishoni mwa wiki.
Alikaribishwa na mdogo wake Happy wa kiume na wa mwisho, Wisdom, akaingia mpaka sebuleni hapakuwa na uchangamfu mahali hapo.
Palipooza kana kwamba hakuna watu kama asingeambiwa na Wisdom kuwa mama yupo ndani basi angeng’amua kuwa mahali hapo hamna watu.
Aliketi huku akizungusha macho yake mule sebuleni.
Macho yake yaligota kwenye picha nzuri na kubwa ambayo hakushindwa kuitambua kuwa ni Happy.
Aliitazama na kusifu moyoni kuwa hakika happy ni mzuri sana Charles ana haki ya kuchanganyikiwa.
Akiwa bado anasadifu mandhari na picha zilizopo mule ndani, mama Happy aliwasili.
Salim aligutushwa na ujio wake, alisimama na kumsalimia na baada ya salamu waliketi wote.
“Najua hunifahamu naitwa Salim...”
Alisita kuendelea mpaka mama Happy alipomshtua aendelee.
“Mimi ni rafiki wa Charles na amen...”
Aliona mama huyo akigeuka pembeni huku ametua sura kwa huzuni.
“Mama Charles amenituma nije kuwasalimia na kumjulia hali mrembo wake Happy na...”
“Alikuwa wapi siku zote?”
Aliuliza mama happy kwa jazba.
“Mama kusema kweli Charles alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa na muda wote alikuwa akipatiwa matibabu kwa mwanasaikolojia.”
Mama happy alitaka kuongea neno lakini akashindwa akabaki tu kimya.
Dakika kadhaa za ukimya zilipita huku kila mtu akiwaza lake.
“Mwanangu nenda kamwambie tunaendelea vizuri na Happy anaendelea vizuri kabisa kwahiyo asiwe na wasiwasi aendelee na matibabu na aishi maisha yake atusahau kabisa.”
“Mama sio hivyo kwa Charles kuniagiza hapa hamaanishi kuwa anataka kuwatelekeza hapana...”
“Charles...”
Sauti kutoka nyuma yao ilisikika.
Salim aligeuka kwa haraka kuisikiliza na kukuta akitazamana na kiumbe ambacho akilini kwake alijua ni mzimu aliruka pembeni na kusogea mbali na pale.
“Happy nani kakwambia utoke nje jamani.”
“Hapana mama nimesikia jina la Charles.”

Salimu akiendelea kuwatazama kama vile ameona mzimu akimtazama mwanamke yule ambaye aliyejibainisha kama Happy ndipo alipogundua msiba wa rafiki yake ni mkubwa zaidi ya alivyofikiria.
Robotatu ya uso wa Happy ilikuwa hautamaniki jeraha la moto ambalo sasa lilikuwa limepona na kuacha kovu baya lilifunika uso wake mzuri wote jicho moja liliharibiwa vibaya sana huku uwezo wake wa kuona ukipungua na kubakiwa na jicho moja tu lenye kuona vizuri.
Hakuwa na nywele hata moja kichwani zaidi ya ngozi mbaya iliyorundikana kichwani kwake.
Ni kipande kidogo tu cha mwili wa Happy ambacho hakikuungua ambacho kilihusisha jicho moja, pua, mdomo na sikio moja sehemu zingine zote ziliungua na makovu mabaya yalimtambaa.
Hata pale alipokuwa alimshuhudia Happy alitembea kwa shida kutokana na ngozi kukamatana kutokana na kuungua sehemu za miguuni.
“Utajiumiza bure tu em rudi ndani mama.”
Alisema mama Happy akimshika Happy na kumkokota kuelekea ndani.
Salim alibaki na bumbuwazi alitoka kimya kimya mpaka kwenye gari lake alifunga milango yote na kupandisha vioo na alikaa akilia.
Sio kwamba alilia kwasababu ya rafiki yake, roho ya ubinadamu ilimuingia na kujikuta akimhurumia Happy mno.
Hakujua kama rafiki yake Charles atakubali hata kuja kumuona akija kusikia kuhusiana na hali ya Happy.
Kioo cha gari lake kiligongwa hakutazama ni nani anayegonga alitia moto gari lake na kuondoka kwa kasi.
Alienda nyumbani kwake moja kwa moja alikokuwa akiishi na mkewe na mwanaye mwenye miezi saba, Shaila.
Mkewe alitambua kuwa Salim ana shida akimuacha apumzike mpaka jioni walipopata kujadili.
“Sasa utafanyaje?”
Mariam mkewe Salim alimuuliza.
“Sina jinsi ni kumueleza tu Charles.”
“Jamani hapo tu umenisimulia nimeogopa sijui itakuaje nikimuona.”
“Acha tu mke wangu.”
“Namhurumia Charles lakini namhurumia Happy zaidi.”
Salim alikuwa na mawazo mengi akiwa kazini aliwaza sana jinsi atakavyopeleka taarifa kwa Charles.
Kila saa alikuwa akivuta pumzi na kuzishusha kwa sauti.
Kazi hazikufanyika kabisa.
Charles amekuwa akimsumbua sana kuhusiana na safari ya kwa akina Happy kwa kuwa hakupata majibu yoyote.
Jioni ile Salim alienda.

“Ukapotea kabisa bro.” Charles alianza baada ya maongezi ya hapa na pale.
“Hamna bro hali niliyomkuta nayo Happy sio nzuri kwakweli.”
“Kwanini?”
“Daaah....nashindwa pa kuanzia.”
“Anzia popote pale.”
“Nimefanikiwa kuonana na mama yake Happy analalamika kwanini hujaenda kumuona mwanaye...na...”
“Nilijua tu.”
Alisema Charles huku akinyoosha mkono wake kuchukua simu na kumkabidhi rafikiye ambaye aliipokea na kuitazama aliweza kuona meseji iliyotumwa kwa namba iliyoseviwa kama “Mama Happy.”
“Mwanangu Charles tunashukuru Mungu tu wazima na asante kwa kumtuma mtu kutusalimia.
Ningependa uendelee na maisha yako Charles usihangaike na sisi wewe ni kijana mdogo sana.
Naomba usikanyage hapa kwangu kabisa na umsahau happy.”

Salim alimaliza kuisoma meseji ile na kumtazama Charles aliyekuwa akitoa tabasamu hafifu.
Hakujua kama ni tabasamu la huzuni au furaha hali iliyompa wakati ngumu kumueleza hali ya Happy.
“Sijui umesemaje kule mpaka mama kapaniki hivi ndomaana ulikuwa unakimbia kuja hapa.”
Alisema Charles akimalizia na kicheko.
“Well nitaenda mwenyewe najua jinsi ya kuongea naye akanielewa.”
Charles aliongea na kunyanyuka, Salim hakujua anapotaka kwenda hata hivyo alimzuia.
“Nini?”
“Happy anaendelea vizuri lakini robo tatu ya mwili wake umeungua vibaya na ana makovu makubwa mno kiufupi Happy amekuwa kiumbe wa kutisha.”/
Charles alibaki kimya.
“Nimemuona Happy kiukweli nimeshindwa kuzuia hofu na masikitiko yangu juu yake Happy sio yuleyule unayemfahamu Happy wa sasa hana tofauti na zombie na pia has...”
Ukosi wa shati alilolivaa salim ulishikwa kwa nguvu kiasi cha kumnyanyua kidogo kwa kuwa hakutarajia tukio hilo.
“Unasemaje wewe mwendawazimu...Happy ni zombie??... Chezea kila kitu changu nitakuacha lakini sio Happy.”
“Niachie Charles najaribu kukuelezea hali halisi.”
Akiwa kama amepigwa butwaa Charles akimuacha.
“Jicho lake moja halioni vizuri kwa kuwa limeharibika sana na hawezi kutembea vizuri kwa kuwa ngozi za miguu zimeungana kutokana na kuungua. Sura yake karibia yote umeungua na hana unywele hata mmoja kichwani zote zimeungua..... kiukweli hali yake ni mbaya....”
“How bad..........Salim...how baaaaaaaaaaaaad.”
Charles alipayuka kana kwamba ameshikwa na wazimu.
Alishika kichwa chake kuashiria maumivu na hapo mlango wa chumbani kwake ulifunguliwa kwa nguvu.
Wazazi wake waliingia ndani kwa pupa.
“Charles.”
Charles akipepesuka kidogo kiasi angeweza kudondoka kama wazazi wake wasingeingia na kumuwahi na kumketisha kitandani kwa vile Salim alikuwa mbali asingeweza kumdaka.
“Salim Charles hajapona bado unawezaje kumpa taarifa mbaya bila kuchukua tahadhari.”
Kimya.
Salim alifuta Machozi yaliyokuwa yakimchuruzika alishindwa cha kufanya.
“Niondoke au nibaki.”
Aliwaza.
Ghafla Charles aliinuka kwa nguvu na kuelekea mlangoni.
“Charles......we cha.....”
Alichelewa mlango ulijibamiza kwa nguvu na Charles aliishia.
Wote watatu walikimbia kwenda nje walikuta Charles akipita getini huku akitumia gari la salim.
Mama Charles alitikisika kidogo huku akitoa mguno hafifu mzee Katesh alimuwahi kabla hajaanguka.
Ilibidi amsaidie kurudi ndani kwani ilionekana wazi afya yake sio nzuri.
Waliketi kimya sebuleni kila mtu aliwaza lake.
“Balaa gani tena kwa mwanangu Charles.”
Mama Charles aliwaza.
“Maskini Charles anatia huruma.”
Salim naye aliwaza.
“Mungu naomba umlinde mwanangu Charles na umpe moyo wa ushujaa.”
Ndivyo alivyokuwa anawaza baba Charles, mzee Katesh.
Saa moja baadae mlango ulifunguliwa kwa kasi, mdogo wa Charles binti pekee wa Katesh Careen akiingia kwa wahka.
“Baba mbona pako kimya sana hapa kuna nini?”
“Em kuwa na adabu huwezi kusalimia eenh.”
Careen alipoa na kutulia hata kusalimia aliacha.
Alikuwa akitokea kigamboni alipokuwa akisoma chuo cha IFM na pia alikuwa na saluni ya kike huko kigamboni.
Alipenda sana mambo ya urembo na ndio kitu kilichopelekea kufungua saluni hiyo, hivyo alikuwa akisoma huku akisimamia biashara yake ambayo nayo haikumuangusha.
Alikuwa amepanga huko kigamboni mji mwema na alirejea nyumbani wakati ambao alikua huru.
Ukimya uliendelea kutawala mpaka ulipokatizwa na sauti ya injini ya gari iliyoingia ndani ya geti hilo kwa nguvu kila mtu aligeukia mlangoni kutazama aliyekuwa akiingia.
Kabla mlango haujafunguliwa kilio kilisikika “Hiiiihiiiihiiihihii” hakuna aliyenyanyuka.
Mama Charles alikuwa akilia kwa sauti ya chini huku mumewe akimbembeleza.
Charles akiingia ndani huku akilia kwa sauti, mishipa yote ya uso na shingoni ilisimama sio siri alitia huruma.
Careen ndiye aliyekuwa wa kwanza kwenda kumkumbatia kaka yake.
Kabla hajajua hata kilichomsibu naye alikuwa akilia kwa sauti.
Baba na mama Charles hawakunyanyuka mama Charles alikuwa akiongeza sauti ya kilio kadri alipokuwa akisikia watoto wake wapendwa wakilia.
Ilibidi Salim awe na moyo mkuu, aliwanyanyua Charles na Dada yake na kuwaketisha akijaribu kumpoza Charles huku akimzuia Careen kulia.
Muda ulizidi kwenda na kidogo Charles alionekana kupunguza kilio japo alikuwa akipiga kwikwi.
Sasa wote walikuwa kimya huku sauti za kwikwi zikisikika.
Salim alichukua nafasi hiyo kuelezea matatizo ya Charles mbele ya familia ile.
Alipofika kwenye kuelezea jinsi Happy alivyoharibika Charles alizidisha kilio kiasi kukawa hakuna maelewano tena.
Sasa familia ilimsogelea Charles na kumpa pole huku wakimfariji kwa maneno mbalimbali, hakuwa na jinsi ila kuelewa tu.
Aliongozwa chumbani kupumzika baada ya kuonekana ametulia kidogo.

Salim ilimbidi kulala hapo nyumbani kwa vile muda ulikuwa umeenda na hapakuonekana mtu anayeweza kusikilizwa na Charles zaidi yake.
Alipoamka alipitiliza moja kwa moja kazini bila kurejea nyumbani.
Charles aliamka saa tano siku iliyofuata japo alikuwa na unyonge, lakini alijiwa na nguvu kutokana na faraja za familia yake.
Dada yake, Careen alimhudumia kwa upendo huku akimtaniatania.
Salim alirejea nyumbani kwake baada ya kutoka kazini akiwa na uchovu mwingi.
Alimkuta mkewe amefura kwa hasira.
“Kwahiyo unatumia matatizo ya rafiki yako kuchepuka na kuamua kutorudi nyumbani na kurudi unapojiskia wewe? Umekosa aibu kabisa mwanaume wewe mtchieeeew.”
Salimu alishindwa cha kujibu alimuacha mkewe aendelee kuongea huku yeye akijawa na mawazo lukuki.

Ndani ya siku tatu Charles alionekana kukubaliana na hali na alijipa ujasiri hata wa kurejea kazini baada ya kutokuwepo kwa takribani miezi miwili.
Alipofika kwa katibu muhtasi wake salamu ilikuwa ndefu sana baadhi ya wafanyakazi wenzake walikuja kumsalimia huku wakiuliza kuhusu hali yake tangu ameondoka kazini wengine walitania kuwa amekonda sana.
“Mxsiiiiiieeew.”
Kila mtu aligeuka kuona ni nani aliyesonya.
Yvonne alipita kuelekea ofisini kwake.
Kila mtu alimshangaa Charles alibaki kimya baada ya salamu sasa kila mtu alienda ofisini kwake kuendelea na kazi.

Baada ya masaa ya kazi kuisha Charles aliamua kwenda tena kwa akina Happy.
Alikaribishwa na wadogo zake Happy, Wisdom na Glad waliokuwa wakicheza nje.
Akiingia sebuleni na kumkuta mama Happy akiangalia televisheni huku akiwa na mawazo mengi.
Salamu ya Charles ndiyo iliyomgutusha kutoka katika Lindi la mawazo.
“Karibu.”
Alikaribishwa.
“Asante.”
Kimya kilitawala hakuna yeyote kati yao aliyeonesha kutaka kuanza kuongea.
“Nmekuja kumuona Happy.”
Charles aliamua kuvunja ukimya.

“Charles hukuona meseji niliyokutumia siku aliyokuja rafiki yako?”
“Niliiona lakini mam...”
“Lakini nini we Happy umemuona unadhani ni yule msichana unayeweza kwenda naye mlimani city tena? Tafadhali mwache mwanangu ataishi maisha yake yaliyobakia hapahapa nyumbani..”
“Lakini mama nlishakuja nkamuona mbona??...Hata nilisema nijaribu kuishi mwenyewe nashindwa nampenda sana happy sijui tu nifanyaje.”
Mama happy alibaki kimya hakuwa na habari kuwa Charles aliwahi kuja na alitoka baada ya kumuona happy katika hali ile na alilia kama mtoto akikataa kuamini kuwa yule ndiyo happy wake.
Ni takribani siku tatu zimepita tangu aje wakati huo yeye alikuwa kazini.
“Charles......”
Happy aliita huku akijitahidi kutembea kutokana na maumivu aliyokuwa akiyasikia magotini ilimlazimu kujikunja kidogo.
Charles alinyanyuka na kwenda kumsaidia kutembea na kisha kumkalisha kwenye kiti na kukaa pembeni yake.
Alishamzoea sasa ingawa ilikuwa kama anamtazama mtu mwingine.
Ni sauti na mdomo mzuri na pua ndogo pamoja na jicho moja ndivyo vilivyomtanabaisha kuwa huyu ni Happy.
“Charles..sijisikii vibaya kuwa hivi ila at least napumua namshukuru Mungu. Naomba umsikilize mama anachokwambia kwasababu mimi maisha yangu yote yatakuwa hivi na nimekubaliana na hali siwezi kubadili. Mi nitakuelewa tu ukiacha kunitafuta ukaendelea na maisha yako hakuna namna.
Usijefanya unanipenda baadaye ukashindwa kunitunza ukaanza kuninyanyasa kwakweli sitakusamehe Charles.
Katafute mwanamke mwingine mzuri muanze familia mimi sina pingamizi wala lalamiko.”

Aliongea Happy kwa upole na utulivu akionesha kumaanisha anachokisema Charles alitulia huku amepakata uso wake kwa kiganja cha mkono alichokiegemeza kwenye paja lake.
“Lakini Happy mbona mimi sikukupendea uzuri wako hayo mawazo yako ndio yaliyonivuta kwako. Kama ningetaka wanawake wazuri nisingeridhika na wewe kwa sababu wazuri wapo wengi na wanazidi zaliwa. Mi nilivutiwa na mtu aliyeko ndani yako wala sio nje.
Moto umemharibu mtu wa nje lakini wa ndani bado anaishi na mimi ndiye ninayemtaka.
Kwakweli hakuna hata nukta ya mapenzi yangu yaliyopungua juu yako bado nakupenda kwa namna na kiwango kilekile tena na zaidi naomba usinikatili.”

Sehemu 2 Sehemu 4
0
0