Foolish Age - Msimu wa Kwanza - Sehemu ya Kwanza (01) 
***** Wakati Uliopo *****
Asubuhi ya siku ya jumamosi ilikuwa na kibaridi na mawingu kiasi kuonesha kwamba kungekuwa na mvua
wakati wowote ule katika mji wa Shinyanga.
Huku ndege wakizunguka huku na huko kufurahia siku mpya iliyokuwa imeingia.
Alfajiri ya saa kumi na mbili ilinikuta njiani nikitembea huku nikiwa na mawazo mengi.
Miaka kadhaa ya kuishi kwangu ilinibadilisha kutoka msichana mwenye thamani hadi kuwa mama asiye na
mbele wala nyuma.
Nilitembea hali nikiwa na kipochi changu kidogo ambacho kilikuwa kimezoeleka sana kubebwa na wakina mama waliokuwa wakiuza mboga mboga.
Nilijifunga kitenge kikuukuu ambacho hata rangi yake haikuweza kujulikana kwa kuwa kilikuwa
kimechujuka sana na shati langu ambalo wakati nalinunua lilikuwa na rangi ya njano.
Mpaka wakati huo rangi yake ilikuwa inaelekea kwenye rangi ya maziwa.
Kichwani nilikuwa na nywele tano ambazo zilikuwa zimepauka na huku zimefumuka fumuka.
Miguuni nilikuwa nimevaa viatu vya wazi ambavyo navyo vilikuwa vimechoka sana.
Kila aliyeniona nadhani aliweza kujua kwamba ninapitia maisha magumu sana.
Nilitembea hatua za haraka haraka asubuhi hiyo huku nikijaribu kuwahi kufika kuikwepa mvua ambayo
ilionekana kutaka kunyesha muda wowote ule.
Kutoka Ibinzamata nilitembea kwa hatua za haraka haraka na haikuchukua muda mrefu sana tofauti na
ambavyo ingekuwa hadi kufika majengo mapya.
Nilianza kukata mitaa ya Majengo mapya na ndipo hofu ya moyo wangu ilipozidi kuongezeka,
moyo ulikuwa ukipiga kwa kasi sana.
Ni miaka kumi sasa imepita niko Shinyanga hii hii lakini sijawahi kukanyaga huu mtaa.
Niliondoka kwa kebehi, kwa dharau na sasa ninarudi kinyonge sana.
Saa kumi na mbili hiyo watu wengi walikuwa bado hawajaamka.
Nilipishana na baadhi ya madereva daladala wachache waliokuwa wakiwahi shughuli zao zinazowapatia
chakula cha kila siku.
Nilitembea kwa uwoga huku nikiwa na hofu kama ningewakuta wale ambao nilikuwa nikiwaendea
asubuhi wakiwa tayari wameshaamka.
Na ghafla nilipaona mahali ambapo nilitaka kufika asubuhi hiyo.
Nyumba ilionekana kama mpya, ilikuwa nzuri sana iliyozungushiwa geti ambalo lilinakishiwa vizuri sana.
Nilisimama kwa muda huku nikitafakari kumbukumbu nyingi zilipita katika macho yangu.
Nilifumba macho huku nikijaribu kuzipoteza kumbukumbu hizo.
Machozi yalianza kunilenga kidogo kidogo.
Nilifungua upande wangu wa kanga na kisha kujifuta machozi yaliyokuwa yakianza kunianguka.
Na kisha nilipiga hatua za kichovu kuelekea kwenye geti hilo.
Nilipofika getini nilichungulia ndani ilionekana ni wazi kwamba bado hawajaamka wenyeji wangu.
Nilinyanyua mkono wangu nikiashiria kutaka kupiga hodi hata hivyo nilisita,
“Sijui nitakuwa nawasumbua.”
Nilijiuliza.
“Aanh ngoja tu nisubiri waamke.”
Niliendelea kuwaza.
“Mmmh, sasa mvua ikinikuta hapa itakuwaje? Lakini ni sawa mie sitastahili kwanza sijui hata wameniitia nini.”
Nilivuta ndala zangu na kisha kuzikalia pale pembezoni mwa geti.
Kadri muda ulivyokuwa ukizidi kujongea ndivyo upepo ulivyozidi kuongezeka na mawingu yalizidi
kuwa meusi.
Mara nilisikia kilio cha mtoto mchanga akilia kutoka ndani ya hiyo nyumba.
Nilishituka.
“Mmmh!”
Nilinyanyuka kwa mshituko na kubaki nimekodolea macho ndala zangu pale chini kana kwamba zimefanya
tukio la kustaajabisha.
Mawazo yaliyochanganyika na hofu yalinifanya nizidi kujikunyata pale mlangoni.
Hata hivyo nilisikia sauti ambayo kwa mbali nilihisi kuifahamu.
“Hello.”
Niligeuka haraka haraka na kuchungulia kutoka pale pembezoni mwa geti.
Unaweza pia kusoma: