Muonekano wa Giza:

Msaada

Foolish Age - Msimu wa Kwanza - Sehemu ya Pili (02)

Moyo ulinipiga paa...
Nilimfahamu mwanamke huyo.
Alipiga hatua za haraka na kisha kuja mlangoni kunifungulia.
Nilikuwa nimejikunyata huku mvua ikiwa imeshaanza kunyesha.

“Karibu ndani, kwanini hukugonga mlango?”
Aliongea kwa upole kama ambavyo alikuwa siku zote.
Nilishindwa cha kujibu nilibaki nikimtazama kana kwamba ndiyo nakutana naye siku hiyo.
“Ingia ndani mama.”
Aliniongelesha kwa upole tofauti na nilivyotarajia.
Niliingia ndani na moja kwa moja nikaelekea kwenye veranda ili kujikinga na mvua ambayo ilikuwa ikizidi kuongeza kasi kadri muda ulivyozidi kwenda.
Sauti ya mtoto mchanga iliendelea kurindima humo ndani.

“Karibu.”
Mara baada ya kufunga geti alinikaribisha ndani.
Niliingia mpaka sebuleni, kwa miaka kumi iliyopita sebule hiyo ilikuwa imebadilika sana ilizidi kuongezeka hadhi kana kwamba anaishi mfalme ndani ya nyumba hiyo.
Kulingana na maisha ambayo nilikuwa nikiishi mimi sehemu hiyo ilikuwa ni sehemu ya kifahari kuliko zote.
Nilipatazama kwa huzuni na uchungu sana.
“Ningekuwa nikiishi hapa mimi.”
Niliongea na nafsi yangu.
Nilibaki tu nimesimama nikishangaa.
Kilichonivutia zaidi ni picha ya binti mzuri sana aliyekuwa akichekea kamera.
Nafsi iliniuma mpaka kufikia chozi kunidondoka.
“Karibu ukae.”
Aliongea.
Nilichagua kiti kilichokuwa pembeni yangu na kisha kukaa.

Mwanamke huyo alipita na kuelekea moja kwa moja mahali ambapo nilidhani ni chumbani kwake.
Rangi ya nyumba hiyo ilikuwa imebadilishwa, marumaru zake pia zilikuwa zimebadilika na zaidi ya sana ziliongezwa marumaru nyingine ukutani.
Kulikuwa na vitu vingine vya thamani ambavyo vilikuwa vimeongezwa.
Hakika palikuwa panavutia sana.
Nilikaa nusu saa nzima nikiwa peke yangu huku nikiwa kama sijiamini.
Nilitamani kuita mtu lakini hata nilihisi kwamba sistaili.
Baada ya muda mrefu kidogo kupita mwanamama yule aliyenifungulia mlango alitoka akiwa amebeba mtoto.
Mtoto ambaye kwa kumkadiria alikuwa na kiasi kama cha miezi tisa.
Alikuja naye moja kwa moja mpaka nilipokuwa nimekaa na kisha akanikabidhi yule mtoto.

Nilikuwa nikitetemeka mwili mzima.
Nilimshika yule mtoto huku nikijaribu kumchekesha kwa namna yoyote niliyojua.
Mwanamke yule aliyenikabidhi mtoto aliondoka tena.
Nilisikia baadhi ya vitu vikigongana, mahali ambapo bila shaka nilipatambua kama jikoni.
Na baada ya muda alikuja kumchukua yule mtoto.
“Twende ukanywe chai.”
Nilibaki tu nimetoa macho.
Wakati nimesimama huku nikiwa sijiamini kabisa kupiga hatua alitokea kipande cha mwanaume.
Pamoja na woga niliokuwa nao nilitembea kwa hatua za harakaharaka na kisha kupiga magoti mpaka chini na kumsalimia kwa kisukuma.

“Mwadela bhabha.”
“Mwadela mayo.”
Baada ya salamu hiyo nilinyanyuka.
“Za siku.”
Alinisalimia.
“Nzuri.”
Nikiongea huku nikikwepesha macho yangu kumtazama usoni.
Nilikuwa nikiangalia chini muda wote.
Mwanamama alidakia.
“Amenenepa, amekua mama sasa hivi.”
Nilishindwa kugeuza uso wangu.
Nilitabasamu tabasamu lenye uchungu sana, huku nikitazama chini.
“Twende tukapate kifungua kinywa.”
Tulielekea moja kwa moja mezani na kisha kupata kifungua kinywa.
Mwanamama yule alikuwa ameandaa vitu vingi sana kiasi kwamba sikuamini kama hivi vitu ni kwa ajili yangu au nimevikuta tu kwa bahati mbaya.
Baada ya matatizo yote, shida zote ambazo nilisababisha kwenye ile familia leo hii wana ujasiri wa kuniandalia chakula kizuri hicho.
Sikutaka kuamini kama ni maalumu kwa ajili yangu.

Sehemu 1 Sehemu 3
0
0