Jabali - 02 
“Jabali lenye nguvu kubwa ya kimaajabu niliyokuwa naitumia katika utawala wangu ilitoweka tangu mke wangu atorokee mji wa wafu.
Jabali hilo nilililisi kutoka kwa baba yangu, na lilikuwa na nguvu kubwa ya kudhibiti mambo makubwa yaliyopangwa kutokea hapa Katesh
hasa katika vita.
Jabali hilo lilikuwa na uwezo wa kubadilisha tawira ya mji huu katika mboni za majeshi ya tawala zingine walipotumwa kuja
kutushambulia hawakuweza kuiona himaya hii zaidi ya kuona taswira nyingine ngeni kabisa!”
Maneno ya mfalme yaliwacha kila mmoja katika taharuki, wengi waliishia kuguna tu!
Mfalme aliendelea…
“Kwa maana hiyo himaya yetu ipo hatarini kuvamiwa na wapiganaji muda wowote na hata kutekwa kwa ardhi ya Katesh na kuwa katika
sehemu yao hasa Mfalme Kadevu jambo ambalo siyo jema hata kidogo, na ndiyo maana tumekusanyika mahali hapa tujadili na kufikia
muafaka tujue nini cha kufanya?”
Mfalme alisema na taratibu akakaa katika kiti chake kikubwa cha kifalme chenye mapambo ya manyoya ya ndege mbali mbali.
Bila shaka wananchi walishaelezwa kila kitu, na sasa ulikuwa ni wakati wa majadiliano kupatikana suluhu ya jambo hili.
Minong'ono mingi ikazuka kila mmoja akaanza kusema lake, baadhi ya watu waoga walianza kufikiria hata kuikimbia Katesh kwani hali hiyo
ilikuwa inatisha sasa, na kwa maana hiyo basi Katesh ilikuwa hatarini kuzukiwa na wafu ikiwa tayari Jabali hilo wanalo.
“Yeyote mwenye jambo la kuchangia kuhusu hili anaweza kufika hapa mbele.”
Malkia ambae ni mke wa mfalme alisema…
Watu walizidi kuchekecha akili.
Ukimya mkubwa ulitanda ukimbini kama hakukuwa na watu vile, hakika huu ulikuwa ni wakati mgumu kuwahi kushuhudiwa.
Muda mrefu sana uliyoyoma, hatimae mwanaume mmoja alinyanyuka kitini na kuanza kupiga hatua za taratibu kuelekea pale mbele.
Ukumbi mzima ulilipuka kwa mayowe na vifijo, makofi kwa wingi mpaka anafika mbele ya mfalme.
Aliinamisha kichwa chake chini kwa ishara ya kutoa heshima yake kwa mfalme, kisha akawageukiwa wananchi.
“Ndugu wananchi pamoja na mfalme wangu hapa!”
Alisema mwanaume huyo huku akigeuka na kumtizama mfalme ambae nae alimuunga mkono kwa kutikisa kichwa.
“Naitwa Mansol, nipo hapa kwaajili ya kuchangia hoja hii nzito yenye kuleta utata.”
Kelele ziliibuka kwa mara ya pili, ambazo hazikuendelea kwa mda mrefu baada ya ngoma kupigwa!
Utulivu ukajitokeza!
“Wazo nililoliona ni kwamba ingekuwa vyema kama mfalme angetuma jeshi kwenda kunako huo mji wa siri kufanya oparesheni
kali hatimae kulichukua jabali hilo.”
Mwanaume huyo aliacha hoja hapo kisha yeye akarejea kitini kwake.
Mfalme nae alisimama kitini ili kuichambua hoja hiyo kama inafaa au laa!
“Wazo lako ndugu Mansol liko sawa lakini pia kwa upande wa pili haliko sawa.
Kwanini nasema hivyo?
Kwanza tambua wafu ni watu hatari sana hawapigiki kizembe.
Pili Jabali hilo lina sharti moja kuu nalo ni kwamba yeyote atakaelishika tu! Huyo ndiyo anakuwa mfalme!”
Mfalme alisema… Lakini hakueleweka!
Maswali mengi yakawazonga watu wote mle ndani..
“Yoyote atakelishika tu ndiyo anakuwa mfalme?”
Kauli hiyo ilikuwa na utata, bado haikueleweka ilihitaji maelezo zaidi.
“Maanake ni kwamba...
Ni mwiko kwa yeyote asie mfalme kulishika jabali hilo, na ikitokea hivyo basi huyo ndiyo anakuwa mfalme na ili asiwe mfalme shart auawe na jabali hilo
lisiguswe na yeyote mpaka mfalme aliokote!”
Duuh!!
Hatimae Mfalme alitosheleza maelezo, lakini kila mmoja alitokwa na jasho kwani halikuwa jambo jepesi tena kulichukua
jabali hilo kutoka kwenye mikono ya wafu, halafu tena isipokuwa hivyo basi Katesh ipo hatarini kuvamiwa na wafu mda wowote!
Pia inasadikika kutoroshwa kwa jabali hilo ilikuwa ni sehemu ya njama kutoka kwa mfalme wa wafu ambae alilihitaji jiwe hilo
kwa udi na uvumba kwaajili ya kuja kuiangamiza Katesh pamoja na viunga vyake.
“Sasa ili kunusu Katesh na viumbe vyake kuvamiwa na watu na hata tawala jilani tufanyaje?”
Swali kutoka kwa mmoja kati ya wananchi liliulizwa.
“Kinachotakiwa kufanyika hapa ni mimi kuachia ngazi, kwanza wapatikane watu kadhaa watakaokwenda katika mji huo kufuata jabali hilo,
nitawapa namna ya kulipata, na atakaefanikisha kuja nalo ndiyo atakuwa mfalme wetu.”
Mfalme alisema…
Ufalme ni mzuri sana ila sasa mtihani huo nani atauweza?
Kila mmoja alikaa kimya.
Nani aende mji wa wafu, kwanza mji wenyewe haujulikani, je? Leo hii atapatikana mtu wa kwenda huko?
Baada ya muda watu watatu, ambapo wanaume wawili na mwanamke mmoja walijitokeza mbele!
Shangwe kubwa likalipuka ndani ya ukumbi, kila mmoja alijisemea nafsini kuwa wale ndiyo walikuwa ni wakombozi wao kwani
waliamini kuwa wao ndiyo wamejitoa mhanga kusafiri mji wa wafu kuchukua Jabali hilo kuja kuinusuru himaya yao iliyo hatarini mpaka mda huo.
Baada ya shangwe na vifijo kutulia ndani ya ngome, ndipo mfalme aliweza kuwauliza kama walikuwa tayari kusafiri kwenda
mji wa wafu kulifuata jabali na kuinusuru Katesh?
Jibu lilikuwa ni ndiyo!
Watu hao walikiri kuwa walikuwa tayari kwenda katika mji huo wa ajabu ili ikiwezekana waweze kuwanusuru wakazi wa Katesh
ambao walikuwa hatarini kupatwa na balaa muda wowote!
Furaha kubwa iliibuka upya ndani ya ukumbi huo! Watu walifurahi na kuruka ruka huku na kule!
Hakika hakuna kitu kinapendwa katika maisha ya binadamu kama amani na siyo mashaka!
“Tunashukuru ndugu zetu kwa kujitoa mhanga katika kujaribu kuokoa amani ya tawala yetu! Nami ninawaahidi ya kwamba yeyote
kati yenu atakaerudi katika ardhi ya Katesh na jabali hilo ndiyo atakuwa mfalme wa Katesh.
Lakini nawasihi, yeyote atakaekuwa wa kawanza kulikamata jabali hilo haruhusiwi kamwe kumpatia mwinzie! Endapo mtafanya hivyo litayeyuka na kuwapotea!”
Mfalme alisema! Maneno ambayo yaliwafanya watatu hao kusisimkwa na uoga!
Hakika ilikuwa ni zaidi ya maajabu, na walipata kujua kuwa kazi iliyokuwa mbele yao haikuwa ya kitoto!
“Pia kabla ya kuondoka! Itabidi muandaliwe kwanza! Mmenielewa?”
Mfalme aliuliza!
“Ndiyo tumekuelewa mfalme wetu mtukufu.”
Muda wote huo ukumbi mzima ulikuwa kimyaaa! Kana kwamba hakukuwa na watu kwani Mfalme tu ndiyo alisikika!
“Kongole kwa kunielewa! Lakini jambo la mwisho! Ningependa mjitambulishe ili umati huu uliopo hapa upate kuwajua!”
Naam ulikuwa ni wakati wa utambulisho sasa! Na alianza yule wa kike ambae kimwonekano ni bado binti.
Watu wote wakatega masikio yao kama antena!
“Naitwa Nkalo Nyakasi, natokea kabila la wahama!”
“Naitwa Mulah Ibrahim natokea kabila la Walongo!”
“Naitwa Sango Murha natokea kabila la Warha kama ubini wangu ujielezavyo!”
Naam!
Wote kwa pamoja walipata kujitambulisha namna hiyo!
Mflame alifurahia saana!
Hata wananchi pia kwa pamoja waliungana na mfalme wao katika kufurahia kile kilichokuwa kimetokea!
“Ndugu zangu hili ndilo lilipelekea tarumbeta kupigwa!
Na wote mkaitii na kukusanyika mahali hapa!
Na nafikiri kila mmoja amepata kujua hali halisi pia tumepata kujua nini kinaendelea!
Kwahiyo kufikia hapa ninaweza kusema mkutano unafungwa ili tuweze kuwaandaa vijana hawa waweze kwenda kusambaratisha njama
hatari ya mtawala wa mji wa wafu na tawala zingine ili tuweze kuishi kwa amani.”
Mfalme alisema na mkutano ukafungwa watu wakatawanyika, kuanzia siku hii kila mmoja alikuwa ametega masikio yake imara ili
asiweze kupitwa na yote yanayokwenda kutokea wakati vijana hao wanasafiri kwenda mji wa wafu.
Vijana hao watatu, Mulah, Sango na Nkalo wakachukuliwa moja kwa moja mpaka katika chumba kimoja hivi ndani ya ngome.
Chumba hiki kimwonekano tu kinaonekana ni cha kupigia ramli na mambo mengine ya kiganga ganga, kwa maana kilikuwa na tunguli kibao.
Walikalishwa katika kiti kimoja hivi kilichokuwa kimetengenezwa kwa ngozi ya mnyama ambae pia hakulikana kwani rangi ya ngozi kwao pia ilikuwa ni ngeni.
Waliambiwa ya kwamba walitakiwa kumngoja mtaalaam angewasili hapo mda si mrefu.
Na kweli, haikupita hata dakika kadhaa! Mtu mmoja ambae kivyovyote vile alionekana ni mganga aliwasili chumbani hapo!
Bila shaka alikuwa anajua kila kitu kilichokuwa kinaendelea,
kwani baada ya kuingia na kukuta kuna watu hakushughulika nao zaidi ya kuzisogelea tunguli zake!
“Ninawapatia Dawa.
Dawa ambayo itawasaidia kuuona mlango uendao katika mji wa wafu pindi mtakapofika eneo ulipo mlango huo.”
Aliongea mganga huyo huku akimimina kimimika flani hivi chenye asili ya mafuta katika kibuyu kingine kitupu.
Aliwapatia kibuyu hicho na kuwaelekeza kuwa walitakiwa kupakaa nyuso zao pindi watakapokuwa wamefika eneo ulipo mlango huo.
“Je? Tutajuaje kama tumefika eneo husika ikiwa mlango huo hauonekani kwa macho?”
Sango alihoji.
“Kabla ya kuanza safari rasmi mtakwenda kwa Mfalme kwanza hamtoondoka moja kwa moja kutoka hapa.”
Mganga alijibu…
Basi waliendelea kukamilishwa kamilishwa pale, kuna vijingozi pia walipewa wajifunge mikononi vikiwa na shanga moja moja.
Nkalo yeye alipewa kingozi kikubwa na kujifunga kichwani, nacho pia kilikuwa na shanga moja ambayo ilikuwa katika eneo la paji la uso.
Waliambiwa kuwa shanga zile zilizokuwa zimeshonewa katika ngozi hizo zilikuwa na kazi kubwa mno!
Hivyo walipaswa kuzilinda ngozi hizo wasije wakazipoteza hasa watakapokuwa katika mji wa wafu.
Na iwapo wangezipoteza basi nao wangeishia huko huko!
Duuh!
Wakaondoka na kwenda moja kwa moja kwenye chumba cha Mfalme, huko walipewa dhana na maelekezo ya kuwafikisha katika eneo
husika ambako ndiko uliko mlango uendao moja kwa moja katika mji wa wafu.
Mji ulio chini ya ardhi, mji ambao licha ya kuwa chini lakini ni mji usiojulikana!
Kwa rugha nyingine tunaweza kusema ni mji wa siri kwani hakuna mtu aliyewahi kwenda akiwa hai.
Mfalme aliwapa ramani iliyokuwa imechorwa juu ya kitambaa cheupe ramani ambayo ingewafikisha mahali mlango huo ulipo,
pia ingeweza kuwaongoza pindi wawapo ndani ya mji wa wafu.
Baada ya kila kitu kukamalika walibeba dhana zao na kuianza safari yenyewe safari ambayo unaambiwa kuufikia tu mlango huo ni siku 40,
kwani upo magharibi ya mbali sana kutoka himaya ya Katesh.
Ramani pamoja na maelezo ya kulipata Jabali hilo yalielekeza ya kwamba, watakapokuwa wamefika katika mji wa wafu walitakiwa kuwa makini sana wasije
kuonwa na yeyote mpaka pale watakapokuwa wamelipata Jabali hilo.
Pia jinsi ya kulipata, walielezwa kuwa kuna ndege angetumwa kuwafuata ndege huyo anauwezo mkubwa wa kuweza kuwafikisha katika ngome lilikohifadhiwa jiwe hilo.
Mfalme alisema kuwa ndege atakaewatumia amefanana kwa kiasi kikubwa na ndege waishio katika mji huo, hivyo isingekuwa rahisi kushtukiwa mapema.
Unaweza pia kusoma: