Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Jabali - 05

“Wanatakiwa askari mia tano na farasi wawatoshao askari hao, Tarishi nakupa kazi hiyo chagua askari wenye uwezo mkubwa na farasi wenye kuweza kuhimili kukimbia kwa kasi umbali mrefu ndani ya mda mfupi.”
Mfalme alisema.
Mjadala haukuwapo tena, mara moja Tarishi aliianza kazi hiyo mara moja.
Ndani ya nusu saa tu! Askari wapatao mia tano walio na afya ya uhakika na ujuzi wa hali ya juu walikuwa wameshateuliwa na kuweka pembeni.
Madume mia tano ya farasi yaliletwa mahali hapo.
Mfalme ndipo alipoweza kuwaeleza ya kwamba walikuwa na safari ndefu sana ya kuelekea katika mlango uingiao katika mji wa wafu.
Walitakiwa kufika katika mlango huo ndani ya siku saba pekee kwani kuna uzembe ulikuwa umekwisha tendeka na ungeigharimu Katesh kama kusingefanyika jambo mapema.
Askari wote kusikia hivyo wakatambua kwamba wapo kazini kweli na siyo utani.
Walijua fika kuwa vita inakwenda kupiganwa huko, tena mbaya zaidi wanakwenda kupigana na wafu majitu hatari zaidi.
Na kabla ya hii inayotokea ipo iliyowahi kutokea kabla miaka ya nyuma ambapo kuna miiko ilikwenda kuvunjwa katika mlango huo jambo lililopelekea wafu kupanda duniani.
Vita kali sana iliendeshwa na askari wengi waliuawa na kuliwa.
Wafu walikuja kukoma kupigana baada ya kuliona jabali la ajabu likiwa mikononi mwa mfalme wa enzi hizo.
Jabali hilo lilikuwa likiogopwa sana na wafu, na ndiyo maana waliweka silaha chini pindi walipoliona hata wakasalimu amri ya kurudi katika mji wao.
Na sasa inakwenda kutokea kwa mara ya pili, askari wengi walikuwa na wasiwasi mkubwa sana juu ya safari hiyo, walihofia huenda ndiyo mwisho wa uhai wao.
Baada ya safari kuwa imekamilika askari hao wakiongozwa na Mfalme wao waliondoka na kuianza safari.
Farasi walianza kukimbizwa kwa kasi kubwa ili kujaribu kwenda na mda.

Walipelekeshwa umbali mrefu sana kwenda chini utelezi ule waliamua kukubali yote kwani hata sehemu ya kushika haikupatikana ilibidi kutulia tu kuona mwisho kutakuwaje!
Walipelekwa kwa spidi kali gafla! Lile jiwe likafika mwisho! Tena lilishia hewani Halafu chini kulikuwa na shimo! Hakukuwa na namna waliweza kupitiliza na kwenda kupita ndani ya shimo lile kwa kasi kama upepo! Shaaa! Wakajikuta wametua sayari nyingine!
Ilikuwa ni juu ya kilele cha mlima ambapo hakukuwa na miti ya aina yoyote!
Kitu cha kushangaza ni kwamba eneo lile kwa jinsi lilivyokuwa likionekana lilikuwa ni tofauti kabisa na mazingira ya Duniani.
Walijaribu kutizama kwa makini kubaini kama kuna kitu chochote ambacho kinaweza kuwa kinafanana na vitu vya duniani.
Hapana!
Hawakuweza kukipata!
Vyote vilikuwa ni vigeni kwao!
Waliendelea kushangaa mno vijana hao lakini pamoja na kushangaa kote huko hawakuweza kugundua chochote zaidi ya kuona mazingira yenye utata.
Yaani mazingira ambayo kamwe duniani hayapo!
“Nini tufanye mtu wangu!”
Sango alimuuliza mwenzake Mulah.
“Aisee! Hapa nahisi ramani ndiyo itatuongoza!”
Hapo ndipo walipoikumbuka ramani, bila kupoteza mda Mulah akashusha begi lake dogo la ngozi kuitoa ramani hiyo!
Ajabu! Hakuweza kuiona..!
“Mmmh!”
“Mulah nini?”
“Ramani haipo ndugu yangu.”
“Eh! Umesema?”
“Kosa kubwa la kizembe tumeshalifanya, kwanza licha ya ramani ilitakiwa tufunge kamba kule nje itakayotusaidia katika jiwe lile lenye kuteleza wakati wa kurudi je? Kama tumetua huku kichwa kichwa tutarudi na nini?”
“Aah!!”
Wote walichanganyikiwa, ni kweli walichokuwa wamekifanya kilikuwa ni makosa makubwa ambayo yatapelekea wao kukwama katika mji huo wa wafu na hata kugeuzwa kitoweo!
“Lishakuwa tatizo hili Mulah daah!”
“Yaani kichwa kishakufa kabisa! Ramani hakuna, kamba hatujafunga sasa je?
Nini hatma yetu?”

Mulah alilalama.
“Hakuna jinsi tukomae wenyewe tushalikoroga hili lazima tulinywe tu hakuna namna.”
Baada ya majadiliano mafupi vijana hawa waliamua kupiga moyo konde na kuruhusu akili zao kuwaongoza japo uhakika wa kutoka katika mji huo wakiwa salama ulishakuwa ni mdogo.
Waliyatizama mazingira hayo kwa mara nyingine tena kujaribu kubaini hata pande kwamba ni wapi mashariki na wapi magaribi hata hivyo hawakuweza kubaini hilo kutokana na mazingira yenyewe.
Kilichofuata hapo ni kwamba walijiweka sawa na kuianza safari mpya sasa baada ya kuingia katika mji huo mpya ambao haukulikana kama ndiyo huo mji wa wafu au la?
Taratibu walianza kushuka kimlima hicho kuelekea chini ambako kulionekana kuwa na tambarale.
Walifanikiwa kushuka mpaka chini, baada ya hapo waliyainua macho yao juu na kutizama angani ambako wishoni mwa kilima kile kwenda juu kulionekana ukungu mwepesi ambao ni mweupee kama mawingu ya kiangazi. Hata mlango walioingilia hawakupata kuuona tena!
Duuh!
Sasa walianza kwenda kwa kukisia kisia, hawakujua watatokea wapi, Wala kutakuwa na nini?
Walichokifanya ni kuzipa akili zao nafasi ziwaongoze.
Walitembea umbali mrefu sanaa pasipokuona makazi yoyote zaidi ya tambarale yenye mti mmoja mmoja!
Halafu kitu cha kustaajabisha mji huu haukuwa na mwanga wa jua.
Anga la mji huu lilikuwa ni anga lililopumbazwa na hali ya hewa yenye ukungu uliotanda juu, kwahiyo haikujulikana kama kulikuwa na jua au laa!
Waliendelea kwenda!
Lakini mwishowe sasa walichoka! Walihitaji kupumzika.
Hapo ndipo walipotafuta mahali ili waweze kupumzika na ikiwezekana waweze kutengeneza chakula wale.
Yah!
Walifanikiwa kupata sehemu ambayo wao walihisi patawafaa, ilikuwa ni chini ya m'buyu mkubwa.
Mbuyu huu ulikuwa umejitenga kidogo na miti ya kawaida nina maana ya kwamba miti mingine ilikuwa mbali kidogo, umbali ambao miti mingine ya kawaida haikuwa imeachana umbali kama huo.
“Hapa tutapata kuni kweli?”
Mulah aliuliza wakati huo akishusha mazaga zaga yake chini.
“Hebu tuangalie angalie tukipata hata vigogo viwili vitatosha.”
Sango alijibu wakati huo akigeuza shingo yake huku na kule kuona kama ataweza kuona kuni ya aina yoyote.
Naam! Kwa mbali kidogo alipata kuona ukuni mmoja ukining'inia juu ya mti mkubwa!
“Kuni ile pale ngoja nikailete!”
“Sawa fanya hivyo.”
Sango alijiweka sawa kisha akaanza kupiga hatua za haraka haraka kuelekea mahali pale.
Alifanikiwa kufika!
Alizungusha macho pande zote kuhakiki usalama kwanza!
Alipojiridhisha na usalama wa chini aliyainua macho yake juu kuuvunja ukuni huo!
Gafla akasita!
Kwani macho yake yaliona kiumbe kisicho cha kawaida! Mmmh! Akaduwaa kwanza!
Kiumbe huyu alikuwa akifanana kwa asilimia kubwa na pakaa!
Lakini yeye alikuwa mweusi tiii halafu pia macho yake yalikuwa ni meupe yasiyo na mboni, pia alikuwa na makucha marefu mno! Yaliyomfanya kiumbe huyo kunasa bara bara katika moja ya tawi la mti huo!
“Mmmh!”
Sango aliachia mguno wa kimoyomoyo huku akivuta upanga wake na kukamata vyema mkononi.
Akaukamata ukuni huo na kuuvunja kisha akaondoka zake na kuanza kurudi nyuma huku kila mara akiutizama mti huo kuona kama kiumbe huyo atashuka kumfuata au la.
Lakini pia yule kiumbe hakuweza kumfuata alibaki kule kule juu ya mti.
Sango alirudi mpaka pale chini ya m'buyu alipomwacha mwenzake, shughuli ya kukoka moto ikaanza.
Sango aliweza kumsimulia mwenzake kuhusu kiumbe aliemwona juu ya mti wakati anavunja ule ukuni.
Hata hivyo wote kwa pamoja walionekana kumpuuzia kiumbe huyo na kujipa matumaini kuwa wenda walikuwa ni viumbe waliokuwa wakiishi ndani ya mji huo.
Basi wakaendelea na shughuli yao pale chini ya m'buyu.
Mara gafla hali ya hewa ilibadilika! Kulitokea kama muungurumo flani chini ya ardhi, mungrumo huo wenye kutetema mfano wa tetemeko ulivuma ndani ya dakika moja mfululizo na kukata gafla!
Kila mmoja alimtizama mwenzake usoni. Na kabla hawajakaa sawa! Walishuhudia vidole vya mikono ya binadamu vikichomoza ardhini kwa wingi huku vikicheza cheza!
Weee!
Walidata!
“Mulah!! Mulah!! Angalia angalia!”
Sango alipayuka kwa taharuki na uoga mwingi..!
Vidole vilizidi kuwa vingi ardhini hali iliyozidi kuwapa mashaka zaidi.
“Tukimbie!”
Mulah aliamuru watimue mbio! Lakini kabla hawajafanya hivyo ardhi ilitetemeka!
Na kusababisha crerck kila mahali, mwishowe mikono ya wafu ilianza kuchomoka ardhini kwa wingi, sambamba na vumbi jingi kuanza kutimka ardhini jambo lililoathili uwezo wa kuona vyema kwa vijana hao!
Ilibidi watimke sasa!
Mbio kali walianza kukimbia huku kila mara wakigeuka nyuma, aisee! Nyuma kilikuwa kivumbi.
Sauti za ajabu zilianza kusikika sambamba vishindo vya watu kuja kwa kasi mahali walikokuwa Sango na Mulah.
Kitu cha ajabu kabisa ni kwamba watu hao waliokuwa wakija kwa kasi na vishindo walikuwa hawaonekani, kwani kila walivyozidi kuja wingu la vumbi nalo lilizidi kuwazingira na kuwafanya wasionekane.
“Tujitahidi mtu wangu tunakufa!”
Sango alimhimiza mwenzake wazidishe mwendo maana nyuma kilikuwa ni kivumbi, wingu zito la vumbi lilizidi kuwafuatilia huku likiongezeka mara dufu, na pia ndani yake vinasikika vishindo vya watu wakiwafukuzia.
Hali ilizidi kuwa tete! Baada ya kukimbia sana mwishowe walichoka!
Hata wakakata tamaa na kutaka kusimama ili liwalo na liwe maana kama ni kukimbia wamekimbia mpaka na pumzi zinataka kuwaishia! Walianza kuhisi vifua vinawaka moto!
Lile wingu nalo lilizidi kuwasogelea tu!
Tena kadri lilivyodhidi kuwasogelea walianza kuhisi kama sauti za wanyama wa ajabu wakitoa milio ya kutisha ndani.

Mfalme Katesh akiwa na jeshi kubwa lenye askari wapatao mia tano, walikuwa msafarani kuwafuatilia vijana wao waliokuwa wametumwa kusafiri Mji wa wafu lakini kwa bahati mbaya kuna makosa makubwa wamekwisha kuyatenda na wapo hatarini kuuawa.
“Huyo ndege anasema nini?”
Mfalme aliuliza baada ya kumuona ndege aliekuwa ametumwa na mtaalamu wake amerudi na kutua begani kwake.
“Anasema tayari vijana wamefika katika mji wa wafu lakini wapo katika matatizo makubwa!”
Mtaalamu huyo alijibu.
“Matatizo gani hayo? Hebu muhoji vizuri.”

Sehemu 4 Sehemu 6
0
0