Mzimu Uliorudi Kulipiza Kisasi - Sehemu ya Kwanza (01) 
Saida anaolewa na Patrick ambaye ni mwanaume masikini wa kutupwa.
Lakini licha ya hali hiyo Saida anamkubali kwa moyo mmoja wenye upendo tele.
Siku zinakatika na hali ya maisha inazidi kukaza kila uchwao.
Kutokana na ushauri wa marafiki wa vijiweni, Patrick ana shawishika kutafuta utajiri kupitia nguvu za giza.
Naye anaenda kumshawishi mkewe mpendwa ambaye hana jinsi zaidi ya kukubali wazo hilo.
Kwa pamoja wanaenda kwa mganga ambaye anawahakikishia kuwa watapata mali na kuwa matajiri, ila kwa sharti moja gumu…
Ndiyo!...
Sharti Saida atolewe kizazi.
Patrick na mkewe wanawaza na kujadili kwa muda, ila kwakuwa maji wamesha yavulia nguo wanakubaliana kizazi kitolewe…
Wanafanikiwa kuwa matajiri.
Waswahili walisema kuwa Masikini akiokota matako hulia mbwata!...
Patrick anaanza mambo ya umalaya bila haya mbele ya mkewe waliosota pamoja.
Mkewe aliyekubali kupoteza kizazi ili tu waishi maisha ya kifahari anasalitiwa wazi wazi!
Ananyanyaswa kwa kila hali hadi anapoteza maisha.
Ila jino kwa jino moto kwa moto…
Katika eneo moja la makazi liitwalo Kihesa lililopo ndani ya mkoa wa Iringa.
Ndani ya eneo hili kulikuwa na familia moja ijulikanayo kama familia ya bwana Patrick.
Ni kijana wa makamo kidogo ni kijana mwenye miaka 32.
Bwana Patrick alikuwa na wake wawili mke wa kwanza anajulikana kwa jina la Saida.
Huyu ndiyo mke alieanza nae maisha tangu bwana Patrick akiwa maskini mpaka leo hii anamiliki magari, majumba, mahoteli na mali zingine kibao.
Zote hizo kachuma akiwa na mkewe wa kitambo sana ajulikanae kwa jina la Saida.
Leo ikiwa ni majira ya asubuhi na mapema bwana Patrick anaamshwa na kengere ya alarm ya simu yake.
Bwana Patrick anaamka na kuingia bafuni kwaajili ya kuoga wakati huo kichwani akiwa na haraka.
Alioga na kurudi mezani.
Alikuta mkewe Saida akiwa amemuandalia chai kwa vitumbua.
Patrick alikunywa chai hiyo kisha akaagana na mkewe na kumwambia kuwa alikuwa akielekea katika hotel yake ya PATRICK HOTEL na angeludi saa saba mchana.
Saida hakuwa na pingamizi lolote kwani hiyo ni kawaida.
Alimtengenezea chai mumewe kisha akamkisi na kumtakia safari njema.
Gari moja kali ya kitajiri sana aina ya prado taratibu inaondoshwa pale nyumbani huku nyuma ikisindikizwa na macho ya Saida.
Baada gari hiyo kuondoka mlinzi wa geti alifunga geti na kurudi kibandani kwake.
Wakati huo Saida akiwa sebleni akiwa bado anaisindikiza gari hiyo kwa macho kupitia dirishani mpaka inapotelea…!!
Taratiibu Saida machozi yaliyoanza kumlenga lenga hatimae aliangua kilio ambacho hatujui ni cha nini?
Tukija huku kwa Patrick, ni kwamba baada ya kutoka nyumbani kwake alinyoosha mpaka katika nyumba yake moja maarufu sana ambayo ni
maarufu kwa wapangaji matajiri.
Alifika pale na kupaki gari yake nje ya geti la nyumba hiyo, ambapo punde tu geti la nje lilifunguliwa nae akazama ndani baada ya geti kufunguliwa.
Alitoka mwanadada mmoja makini sana ambae kwa kumtizama tu huenda ukahisi ni jini kwa jinsi alivyobalikiwa kuwa mzuri wa sura.
Umbo na shepu kiujumla alikuwa ni mwanadada ambae kwa umri wake siyo chini ya miaka 23-25.
Mwanadada huyu baada ya kutoka alitembea kwa mwendo wa madaha huku kila umbo likisapoti kila hatua aipigayo.
Patrick nae alifungua mlango wa gari yake na kushuka chini kitu cha kustaajabisha.
Mwanadada huyu ajulikanae kwa jina la Ashura alikwenda moja kwa moja kujaa kifuani mwa Patrick.
“Saida mbona unalia dada yangu??”
“Ha.. Ham...mmm...na...”
“Tafadhari naomba uniambie huenda nikawa msaada dada yangu…”
“Emanuel naomba uniache sipo sawa kwa sasa hivi.”
“Lakini hujaniambia nini tatizo dada ujue unapokuwa huna furaha hata mimi nitakosa amani niwapo kazini.”
“Tafadhari nitakwambia niwapo sawa.”
“Daah! Sawa dada sasa chai yangu vipi mbona mpaka sasa hivi saa mbili hii?”
“Ahaa ok uende pale jikoni utaikuta pamoja na chapati pale juu ya kabati..”
“Sawa , asante.”
Yalikuwa ni maongezi kati ya mlinzi wa geti la Patrick na Saida mke wa Patrick.
Mlinzi huyu aliamua kwenda ndani kumuangalia mke wa Patrick kwani leo hajamletea chai tangu bosi wake atoke asubuhi mpaka sasa hivi inaelekea saa mbili
asubuhi mke wa bosi wake huyo hajatoka ndani kumletea chai hivyo Emanuel aliamua kufuata mwenyewe ndani kwani kashindwa
kuvumilia kwa jinsi baridi ilivyojaa tumboni.
Lakini kitu kisicho cha kawaida anakutana na kilio sebleni.
Mke wa Patrick akiwa kajiinamia mezani analia kilio kisicho cha kawaida huku machozi yakichururuzika kutoka mezani kudondoka chini.
Emanuel mlinzi wa geti alipigwa na butwaa baada ya kukutana hali ile.
Haraka hisia zake zikamtuma kuwa Saida amepatwa na msiba.
Alijisogeza mpaka pale na kujaribu kumdadisi lakini majibu aliyoyapata hata hakuridhishwa nayo.
Emanuel aliamua kumuacha bosi wake huyo na kufuata maelekezo yake akiingia mpaka jikoni.
Kweli aliikuta chai japo tayari ilishapoa kwa kukaa muda mrefu kwenye kikombe.
Hii ni baada ya Saida kuiandaa kwaajili ya mlinzi huyo halafu hakuipeleka.
Emanuel aliibeba chai hiyo hivyo hivyo huku ikiwa imepoa kwani hakuwa na jinsi tena.
Akachukua na vitafunio kisha kwa hatua za kivivu akaanza kutoka nje huku akiwa na mawazo mengi mno kichwani kwake kuhusu bosi wake Saida kapatwa na nini.
Mara nyingi mlinzi huyu wa geti alihisi huenda bosi wake huyo wa kike kapatwa na msiba.
Emanueli alijiwekea asilimia mia kuwa Saida kapatwa na msiba.
Je ni kweli Saida kapatwa na msiba?
Emanuel mlinzi wa geti la tajiri Patrick alijongea taratiibu mpaka katika kijibanda chake cha mlinzi wa geti na kuweka mazaga zaga yake chini kisha akaweka
mikono yake mashavuni akiwaza ni jambo gani linalomsumbua mke wa bosi wake.
Emmanuel ni mtu wa imani sana na ni mtu mwenye huruma kupita maelezo hivyo kitendo cha Saida kuwa katika majonzi kilimpa mawazo mengi sana mlinzi huyo
wa geti ambae yeye alihisi huenda amepatwa na msiba.
Tukija huku ndani hali ilikuwa ni tete kabisaaa unaambwiwa kilio alichokuwa analia mwanamama huyu unaweza kusema kapatwa na msiba wa mwanae wa pekee.
Hii hali imeanza kujitokeza humu ndani takribani wiki moja iliyopita.
Patrick amekuwa ni mwanaume wa ajabu ajabu sana.
Katika siku za nyuma walikuwa wakisafiri pamoja na mke wake huyu Saida katika gari moja pindi
wanapokwenda kutembelea miradi yao mbali mbali.
Lakini hali hii imebadilika gafla Patrick kawa mkali kila akirudi kutoka safari mara kadhaa anarudi akiwa amelewa na mkewe kuchezea
kipigo kila anapojaribu kumlaki.
Hali hii ilimuumiza sana Saida.
Katika siku za mwanzo alijua huenda ikawa ni hasira za stress za mawazo kwa mumewe huyo lakini alipojaribu kumchunguza
mwenendo alijua wazi kabisa kuna kitu nyuma ya pazia.
Siku moja Patrck aliudi jioni akiwa amelewa chakarii kiasi kwamba hata gari ilikuwa ikimshinda kuendesha kwani alilazimika
kumkodi mtu amrudishe nyumbani.
Hali hii ilimuumiza sana Saida kwani alijua laiti kama mumewe asingemkataa kutembea pamoja yeye ndiye angemuendesha pindi hajiwezi.
Baada ya yule jamaa aliemleta mumewe kupewa chake na kusepa Saida alimwendea mumewe wakati huo yupo chumbani anavua suti zake.
“Patrick mume wangu…”
“Nini wewe?”
“Lakini kwanini umekuwa hivyo?”
“Hebu fata yako.”
“Lakini…”
“Nimekwambia fata yako we mwanamke mbona hujielewi?”
“Patrick huo ujasili umetoa wapi wewe jamani?”
“Hebu nitokee hapa kwanza hujui tu! Kila neno unalolitamka nahisi kama mdomo wako unatoa funza yaani matapishi yananijia mpaka kooni.”
“Patrick...!!!!”
“Toookaa!! Na ukiendelea kujibizana na mimi utachezea vitasa sasa hivi oooohoo!!!”
Kiukweli maneno yale yalikuwa ni kama kaa la moto kati kati ya kidonda kibichi.
Mapigo ya moyo wa Saida yalianza kwenda mbio kiasi kwamba alihisi kama moyo unataka kuchomokea mdomoni.
Tumbo lilikuwa likimvuruga kama mtu aliekunywa mafuta ya kondoo.
Machozi ya uchungu yalianza kumwagika Saida kwa kasi kweli kweli.
Hata hivyo hakutaka kubishana nae kwani alijua nini kitafuata.
Alichokifanya ni kuchukua suti za Patrick na kuzikunja vizurii kisha akaziweka kwenye begi wakati
huo Patrick alikuwa amekwenda bafuni kuoga.
Saida alichokifanya ni kupanda kitandani na kuvuta shuka lake na kulala.
Usiku huo ulikuwa ni usiku wa majonzi kwa Saida.
Mawazo mengi yalikuwa yakipita kichwani kwake.
Mpaka inatimia saa kumi na moja alfajiri alikuwa macho naweza kusema kwa usiku huo Saida hakupata hata lepe la usingizi.
Asubuhi ya siku hiyo ndiyo siku hiyo kama unakumbuka katika sehemu ya kwanza ya simulizi hii Patrick aliaga kuwa anakwenda
kuangalia moja kati ya miladi yake hivyo Saida alimwandalia nguo zake kisha akaondoka na baada ya Patrick
kuondoka tunashuhudia mkewe Saida akimsindikiza kwa macho mpaka anapotelea kishaa akaangua kilio kisicho na mfano
kilio ambacho mlinzi wa geti Emanuel alihisi huenda ni msiba umempata mwanamama huyo.
Jambo ambalo halikuwa la kweli...
“NAAM HUO NDIYO MKASA MZIMA UNAOMLIZA MWANAMAMA SAIDA.”
Unaweza pia kusoma: