Unseen - Episode 01 
Alionekana kama mwenye kusubiria ugeni uliokuwa na umuhimu kwake.
Alizunguka kila pande za chumba chake.
Alienda mlangoni, alisogea karibu na kabati, alienda dirishani huku akiangalia saa yake na punde si punde hodi iligongwa
alienda kufungua haraka haraka.
Aliingia msichana mrembo sana ambaye alikuwa na rangi nyeusi ya kuvutia, macho yake makubwa na nywele zake za asili alizokuwa
amezibana vizuri.
Alipendeza katika mavazi aliyokuwa amevaa yalimkaa vyema kwenye maungo yake hakika alionekana kama malaika.
Aliingia na kwenda kukaaa kwenye sofa moja la pekee lililokuwepo humo ndani.
Robert alivuta pumzi na kushusha na kisha akamsogelea.
“Nikuletee kinywaji gani?”
“Aanh niambie ulichoniitia.”
“Aanh… Hapa ni kwako.”
“Ndiyo ni kwangu nitakunywa nikijisikia, sema umeniitia nini?”
Robert alijikuta amekosa cha kuongea.
Alivuta pumzi na kisha kusogea pembeni na kukaa.
“Kwahiyo hutaki kuongea ulichoniitia?”
Tessa aliendelea kuongea kwa sauti kavu.
“Lakini Tessa kwani unashida gani?”
“Sina tatizo lolote.”
“Aanh mbona sioni kama uko kawaida.”
“Niko kawaida kabisa.”
“Kuna nini?”
“Mimi sioni kama kuna tatizo lolote, sijafanya kosa lolote sasa nashangaa unavyokuwa hivyo.”
Tessa aliongea.
“Tessa nimekuuita kwenye sherehe nikutambulishe marafiki zangu uwaone, ulichokifanya pale sijakipenda kabisa,
kwanini uliondoka kabla sijakutambulisha?
Wewe unadhani mimi ningewaambia nini marafiki zangu pale? Yani umenitia aibu sana.
Kwanini umefanya vile, ile sherehe ilikuwa kwaajili yako mimi nimegharamia kila kitu ili wewe uonane na marafiki zangu
lakini unafanya kitu kama hicho kwanini?”
Tessa alinyamaza kimya kana kwamba alikuwa hajasikia.
“Tessa naongea na wewe.”
Alivuta pumzi na kuzishusha.
“Ndiyo hilo?”
“Ndiyo.”
“Wewe unaona hilo ni kosa kubwa sana kiasi cha kunifokea kiasi hicho?”
“Hivi Tessa ni wewe kweli ama ni nani?”
“Sikia nikwambie Robert, mimi maswala ya kunipeleka kwa marafiki zako halafu wanakaa pembeni wananisema wananiangalia kwa
jicho baya siwezi, kwani kuna ulazima gani wa kutambulishana kwa marafiki zako, kwani wao ndiyo wachungaji au wao ndiyo Mungu.
Sikia kama hatuwezi kuendelea na mahusiano yetu bila marafiki zako kujua basi tuachane lakini kama tunaweza kuishi vizuri tu bila
marafiki zako bila sijui akina nani its ok, kwanza marafiki zako kwanini wawe wasichana?”
“Aahaa Tessa usiseme hivyo, marafiki zangu wapo wasichana wapo wavulana si pale walikuwepo wote.”
“Sikia hilo zoezi la kutambulishana kwa marafiki zako wasichana naomba liishe na liishie hapa. Sitaki kuwajua wewe endelea kuwa nao.”
“Unamaanisha nini?”
“Namaanisha kwamba sitaki kuwajua hao marafiki zako.”
“Mimi bado sikuelewi.”
“Nimesema sitaki.”
“Marafiki zako wananiangalia, wananisema, wananikata jicho baya mi niko tu eti nawafurahia, nikae pale ninalipwa au kuna nini?
Sikia Robert nilichokiongea nimeshakiongea sibadilishi wala sifanyi nini, kama hilo ndiyo uliloniitia basi tumeshafikia
mwisho naondoka.”
Tessa alinyanyuka na kisha kubeba pochi yake.
Robert alishindwa kuelewa kama ni kweli Tessa alikuwa akifanya hivyo.
Aliondoka kweli wala hakugeuka nyuma.
Alibaki mwenyewe amechanganyikiwa.
“Hivi ni huyu Tessa kweli au ni mtu mwingine. Mbona kama siamini.”
Alikosa raha hiyo siku alishindwa hata kula.
“Au anafanya hivyo kwasababu anajua nampenda. Aaanh mapenzi gani sasa haya.
Kwanini hataki kuwajua marafiki zangu hasa wa kike au anahisi mimi ninamahusiano nao? Ngoja nimpigie.”
Alijaribu kupiga simu haikupokelewa alipiga zaidi ya mara nane lakini simu haikupokelewa alituma meseji nyingi tu hazikujibiwa.
Aliamua kumuacha.
“Nimuache labda ana hasira nitamcheck kesho asubuhi.”
Alilala akiwa na mawazo mengi sana kichwa kilimuwia kizito.
Usingizi ulimpata kwa shida.
Aliamua kunyanyuka na kisha kuelekea kwenye grocery iliyoko karibu na kisha alinunua bia mbili na kuelekea nyumbani.
Aliamua kuzinywea hapohapo nyumbani.
Alikunywa na wala hakuweza kuzimaliza zote alipitiwa na usingizi mzito.
Robert aliamka ikiwa ni asubuhi ya siku ya pili na kilichomshitua kilikuwa ni mlio wa simu.
Alimtazama mpigaji alikuwa ni Tessa ambaye kwenye kioo cha ile simu alikuwa akisomeka kama “sweetheart”.
Alipokea huku mkono ukitetemeka.
Kumbukumbu za siku iliyopita zilimuijia.
“Hello sweetheart I miss you.”
Alikuwa ni Tessa mara baada ya kupokea simu.
Huyu ndiye aliyekuwa mwanamke ambaye nilimpenda sana.
Tessa Felix.
Nilijuana nae wakati wote tuko mwaka wa mwisho chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Mimi nilikuwa nikichukua Sheria wakati yeye alikuwa alikuwa akisomea mambo ya biashara.
Alikuwa msichana mzuri sana, mcheshi na mpole.
Nilipokutana nae tu siku ya kwanza nilimpenda ingawa watu wanasema unapomuona mtu kwa mara ya kwanza unamtamani
lakini mimi nilimpenda sana Tessa, hata nilivyoanza maongezi naye wala hakuwa akiringa kama wasichana wengine hasa waliokuwa
wakitoka katika kitivo chao.
Tulianza urafiki wetu, ilichukua muda mrefu sana kubadilisha urafiki wetu kuingia kwenye mapenzi.
Ni takribani miaka miwili sasa tangu nimjue Tessa na takribani mwaka mmoja wa mahusiano yetu.
Tessa ni mfanyakazi wa kampuni iliyokuwa ikijihusisha na maswala ya burudani iliyokuwa ikiitwa L.L.A FAME.
Alikuwa ni mmoja wapo kati ya wafanyakazi wazuri sana kwenye hiyo kampuni na hii ilipelekea kupendwa sana na wafanyakazi wenzie.
Ucheshi wake pia ulimsaiidia na uzuri wake ulimbeba.
Katika kipindi hiki cha kujuana kwangu mimi na Tessa nadhani bado sikuwa nikimfahamu vizuri Tessa.
Hakuwaga na wakati wa kwenda kusalimia familia kama jinsi ilivyokuwa kwangu na kwa watu wengine wakati wa sikukuu alibakia
hapahapa Dar hakwenda sehemu yoyote.
Kila mara nilipomuuliza kuhusu swala la familia yake hakuwa tayari kulizungumzia.
Tessa amekuwa ni msichana asiyeishiwa na vituko mara nyingi nilikuwa nikifikiria kumuacha lakini moyo wangu unakataa kabisa.
Alikuwa ni kiumbe wa ajabu sana kuwahi kukutana naye wakati mwingine nilijuta hasa kwanini nilimpenda hata hivyo sikuweza kuuzuia
moyo wangu kumpenda.
Mbali na vituko vyake vyote Tessa alikuwa ni moja kati ya wasichana ambao ninaweza kuwaita ni bora zaidi.
Nilimpenda sana Tessa na niliamini kabisa katika maisha yangu ndiye atakayekuja kuwa mke wangu.
Ni jambo la kushukuru Mungu kwamba tangu nilipomaliza chuo hatukupata shida kupata ajira.
Tessa aliajiriwa mapema kuliko mimi na alikuwa akinisapoti kwenye mambo mengi na hata hii kazi niliyoipata Tessa alisaidia sana
ili niweze kuipata.
Nilifanikiwa kuwa mwanasheria katika kampuni fulani binafsi iliyokuwa ikijihusisha na maswala ya kibiashara ya kuchukua bidhaa nje ya nchi na
kuziingiza nchini, katika kampuni binafsi iliyokuwa ikiitwa KOK.
Niliweza kufahamiana na watu wengi sana na niliweza kufungua ofisi yangu binafsi hata hivyo sikuwa na mtu ambaye nilikuwa na kazi nyingi kama
ilivyokuwa kwa Tessa.
Mapenzi yaliendelea kuimarika siku hadi siku.
Niliipokea simu ile huku nikiwa nimepata afueni kidogo.
“Umeamkaje Tessa?”
“Nataka ukakutane na rafiki yangu.”
“Nilibaki nimetumbua macho.”
“Rafiki yako?”
“Yah, ni rafiki yangu mkubwa sana, tulikuwa tukisoma wote shule ya sekondari yeye alipangiwa kusoma UDOM sasa amekuja
alikuwa kwao Mwanza ila amekuja saa hizi Dar nataka ukutane nae umuone na amehamia hapa Dar saa hizi atakuwa anafanya
kazi hapa Dar ameajiriwa.”
“Sawa… Hamna shida. Anafanya kazi gani?”
“Subiri bwana tukikutana naye ndiyo utajua vizuri.”
Aliongea na kukata simu.
Niliamka na kisha kwenda kuoga mara baada ya kuoga nilifungua friji yangu kutafuta kitu chochote cha kula.
Friji lilikuwa limejaa maji tu.
Nilichukua glass na kisha kunywa maji na baada ya hapo niliingia mtaani kutafuta chakula.
Mara nyingi sikupenda kupika ni mara chache chache sana ilinikuta niko jikoni.
Nilipata supu na chapati mbili na kisha kuelekea ofisini kwangu.
Mimi ndiye nilikuwa mmiliki wa ofisi yangu iliyokuwa ikiitwa ROCKS Advocates.
Ofisi yangu ilikuwa maeneo ya Mwenge wakati mimi nilikuwa nikiishi Morocco.
Nilipofika ofisini kwangu nilimkuta mteja mmoja.
Tuliongea mazungumzo mafupi na kisha aliondoka akiniachia kazi ya kufanya hata hivyo akili yangu haikuwepo hapo kabisa mara
zote nilikuwa nikimfikiria Tessa.
Niliamua kumpigia simu.
“Baby…. Za saa hizi.”
“Nzuri nitakupigia simu baadae si nimekuambia kwamba tutakutana baadae una shida gani tena?”
“Aanha nimefikiria sana nataka twende tukamuone mama yangu.”
“Unasemaje?”
“Tessa nataka nikupeleke kwa wazazi wangu wakakujue, wakakutambue. Hizi ni hatua za mwanzo kabisa kuelekea kwenye kufunga ndoa.”
“Uko wapi?”
“Huu wakati sio wa kupaniki, niko ofisini.”
“Naomba tukutane nyumbani kwako.”
Alisema Tessa.
Kutoka uko ofisini kwake mpaka nyumbani sio mbali.
Nilitoka nikiwa na mawazo mengi lakini cha kushangaza nilimkuta Tessa mlangoni akiwa ananisubiri.
“Funguo uko wapi?”
Nilitoa mfukoni na kisha kumkabidhi alifungua mlango na kisha kuingia ndani.
Alionekana ni mtu aliyepaniki sana.
“Unajielewa kweli?”
Hilo ni neno la kwanza aliongea pia nilishangaa.
“Kwanini unasema hivyo!?”
“Wewe umenipigia simu ukaniambia nini?”
“Nimekwambia twende tukamuone mama yangu nataka kukutambulisha kwa mama yangu nataka akujue.”
“Sidhani kama una akili za kutosha. Huyo mama yako ana umuhimu gani mpaka mimi nikamuone?”
“Lakini hatuwezi kufunga ndoa bila kukutambulisha kwa mama.”
“Sasa sikia kama ni lazima kwenda kumuona mama yako basi hakuna ndoa, mimi kwa mama yako siendi.
Huyo mama ako amekuwa Mungu hiyo ndoa tunamfungia yeye?
Kama kuna ulazima wowote wa kwenda kumuona mama yako basi swala la ndoa naomba ulisahau.”
“Lakini Tessa huu ni utaratibu unaofanyikaga kote.”
“Siyo kwangu, mimi siendi kwa mama yako. Kama unafikiri huwezi kufunga ndoa mpaka uende kwa mama yako nenda mwenyewe.”
“Lakini Tessa tunaenda kupata baraka.”
“Baraka gani? Kama unaziitaji hizo baraka za mama yako fata mwenyewe mimi sizitaki halafu hilo swala sitaki tena kulisikia.”
“Lakini Tessa nimekuita nikakutambulishe kwa marafiki zangu umeondoka, nimekuita nikakutambulishe kwa mama yangu unapaniki
sasa unataka nini?”
“Sitaki kutambulishwa popote.”
“Mimi nashindwa kukuelewa.”
Robert aliendelea kulalamika.
“Kama hatuelewani basi kamtafute mtu ambaye mnaelewana tuachane.”
“Haaa sasa mbona umefika mbali.”
“Nimesha ongea na nimemaliza swala la kwenda kutambulishana kwa mama yako limeishia hapa.”
Aliongea.
“Na sitaki tena kulisikia na jioni naomba uje nakupeleka ukamuone rafiki yangu.”
Aliondoka na kunibamizia mlango.
Kweli nilishangaa sana.
“Huyu ana matatizo gani? Wasichana wengi wanafurahia kwenda kutambulishwa kwa wazazi lakini kwanini
yeye yuko hivi!?”
Nilidhani ningemfurahisha sana kumuambia hivyo lakini yeye hakuonekana kufurahia hiko kitu.
“Aanh huyu mwanamke bwana.”
Nilishindwa tena kurudi ofisini nilikaa nyumbani nikiwa na mawazo mengi nilishindwa kujua nimetumia muda gani
kuwaza hata hivyo nilikuja kushituka simu yangu ilikuwa ikiita.
“Umeshajiandaa?”
Nilipokea bila kujua ni nani ambaye alikuwa akinipigia.
Niliposikia hiyo sentensi ya kwanza na sauti niliweza kujua kama ni Tessa.
“Ndiyo najiandaa.”
“Ufanye haraka uje kwangu.”
“Sawa.”
Nilijibu kiunyonge.
Nilinyanyuka pale na kisha kuelekea bafuni kwa ajili ya kuoga.
Niliporudi nilikuta simu yangu ikiita, niliangalia mpigaji alikuwa rafiki yangu na mfanyakazi mwenzangu pale KOK, Idrisa.
“Oy mbona nimekupigia sana simu hupokei?”
Huyo alikuwa akitoka nilikokuwa nimeajiriwa kama mwanasheria.
“Nakupigia simu muda mrefu hupokei una matatizo?”
“Aanh hamna mwanangu.”
“Sasa mbona hupokei simu?”
“Aanh mambo mengi nilikuwa mbali na simu.”
“Fresh nilikuwa nataka tukutane jioni vipi una muda?”
“Hapana kwa kweli sina muda mambo yameingiliana.”
“Basi sawa hakuna shida siku nyingine au siyo.”
“Sawa.”
Nilikata simu na kisha kwenda kuchagua nguo ambayo nilidhani Tessa angeipenda.
Niliondoka kiunyonge kuelekea nyumbani kwa Tessa.
Kadri nilivyozidi kukaribia ndipo furaha yangu ilipozidi kupungua.
“Yeye mbona anataka anitambulishe kwa marafiki zake kwanini mimi hataki nimtambulishe, hivi ni kweli ana malengo na mimi huyu?”
Nilijiongelea.
Unaweza pia kusoma: