Unseen - Episode 04 
Nyumba yangu ninayokaa ina wapangaji wengi kidogo kuliko Tessa.
Mama mwenye nyumba ana mabinti takribani wanne na wote walikuwa wakiishi hapo nyumbani.
Mmoja kati yao alikuwa amezaa mtoto mmoja na alikuwa akikaa hapohapo nyumbani.
Sikuwa na mazoea nao sana lakini mara nyingi sana wanawake waliokuwa wakikaa kwenye ile nyumba walikuwa wakikutana nje na kisha kupiga
stori mbili tatu.
Sikuzoea kujiunga katika vikao vyao ukizingatia kwenye ile nyumba tulikuwa wanaume wawili tu na wengine wote waliobakia
walikuwa ni wanawake.
Nilikuwa kidogo nimemzoea mpangaji mwenzangu.
Ilikuwa ni nyumba ya kisasa kabisa ambayo usingeweza kuhisi kama ndani yake kuna mambo ya kiswahili.
Sehemu ambayo nilikuwa nikikaa ilikuwa ikijitegemea kabisa tofauti na wapangaji wengine wote.
Ilikuwa na vyumba viwili sebule nzuri na kubwa choo na bafu vya ndani pamoja na jiko.
Huku vyumba vingine vikiwa vimejipanga katika msururu mmoja.
Na nyumba kubwa ambayo alikuwa akiishi mama mwenye nyumba pamoja na watoto wake.
Jioni ya siku hiyo nilisikia sauti zao hapo nje kama ilivyoada wakiongea mambo mbalimbali.
Wala sikujishughulisha na pia nilikuwa nikiona aibu sana kupita katikati yao kwa maana ili nitoke nje ilikuwa ni lazima nipite
kwenye kibaraza ambacho walikuwa wakitumia mara nyingi kukaa.
Wakati nikiendelea kuwaza hayo ghafla nilisikia vurumai huko nje.
“Hivi hamna sehemu nyingine ya kukaa isipokuwa hii mnataka mkae hapa ili mpate nini?
Mnashindwa kukaa mkafanya mambo yenu kazi kukaa kwenye milango ya watu mnataka msikie nini au mnataka mpate nini?”
Bila hata kupepesa akili nilijua kabisa aliyekuwa akiongea maneno hayo alikuwa ni Tessa.
“Mungu wangu Tessa amekuja na huku tena kuniharibia.”
Nilivuta pumzi na kuzishusha.
“Tessa… Tessa… Why?!”
Nilinyanyuka kitandani kwangu na kuanza kuzungukazunguka kama kichaa.
“Mungu wangu… Mungu wangu… Leo ndiyo nafukuzwa hapa.”
Nilifungua pazia na kisha kuchungulia kidogo.
Wanawake wale waliokuwa wamekaa pale nje walikuwa wakimshangaa Tessa alionekana kama mwendawazimu fulani hivi.
Nilichanganyikiwa huku nikishindwa cha kufanya ilinibidi tu kushikwa na moyo wa ujasiri.
Nilitoka nje harakaharaka na kisha kuelekea pale Tessa alipokuwa, nilimshika mkono na kisha kumvuta ndani.
“Niache niwaambie ukweli.”
Tessa aliendelea kuongea.
Nilimuingiza Tessa mpaka ndani.
Hata hivyo niliogopa sana kuongea.
Niliogopa kumuambia kwa maana ningemuudhi.
“Aya na wewe niambie sababu ya kutokuja nyumbani.”
Aliongea kwa sauti kiasi kwamba sikuwa na shaka kule nje walikuwa wakisikia.
“Si ulisema utakuja, ulienda kazini kweli wewe? Hizo nguo ndiyo umetoka nazo nyumbani na mpaka saa hizi bado unazo
unanidanganya siyo, umeanza lini kunichezea?”
Aliongea Tessa.
“Basi tulia mama tuongee.”
“Uongee nini na mimi? Yani unaniona mimi nishakuwa mpuuzi saa hizi kwasababu nakuangalia kila kitu unachokifanya,
unajielewa kweli?”
Tessa aliendelea kupayuka.
Nilimuacha aongee kila alichokuwa akitaka kukiongea.
“Yani na hao wanawake huko nje hawana kazi za kufanya?”
Aliongea kwa sauti kubwa.
“Tessa tulia basi watakusikia.”
Niliendelea kumsihi.
“Wanisikie ili wabadilike wanakaaje kwenye milango ya watu yani huyo mtu asipite wamuangalie anapoenda mpaka anapoishia.
Hawana shughuli za kufanya?
Hawana wanaume? Hawana kazi? Si kama hawana kazi si wakakae huko wakaangalie TV au hata TV kwao hawana?”
Kiukweli maneno aliyokuwa akiongea Tessa yaliniudhi sana.
Lakini hata hivyo sikuwa na namna ya kumzuia aliendelea kuongea.
Ilinibidi tu nimzibe mdomo.
“Tessa tulia basi.”
Nilifoka.
Aliniangalia huku akinikata jicho.
“Kwanini hujaja nyumbani?”
“Aanh Tessa unanichanganya.”
Alinipiga kibao kimoja.
Nilihisi kuona nyota.
“Usinijibu upuuzi mimi.”
Kwa mara ya kwanza nilikuwa nimepigwa kibao na mwanamke.
Nilishikwa na hasira nilitamani kumrudishia hata hivyo nilimuonea huruma kwa hasira nilizokuwa nazo ningeweza kumpiga sana
mpaka nikamvunja nilitulia tu huku nikijaribu kuziongoza hisia zangu nilimtazama tu na kisha kukaa kitandani.
Alikuja na kupiga magoti mbele yangu.
“Una nini?”
Aliniongelesha kiupole kana kwamba siyo yeye yule aliyekuwa akifoka dakika mbili zilizopita.
“Tessa kwanini inakuwa hivyo?”
“Nakuwaje?”
“Yani Tessa sasa kwa mfano mimi nikifukuzwa hapa naenda wapi?”
“Unakuja kukaa kwangu.”
Aliongea.
Niliona anajibu majibu marahisi kwenye maswali magumu.
“Hebu kaa kwanza hapa.”
Nilimnyanyua kutoka pale chini alipokuwa amepiga magoti na kisha kumuweka kitandani.
“Umekula?”
Nilijikuta nikibadilisha mada.
“Sijala, nimepika na nikawa nakusubiri wewe urudi sasa hujaja mpaka saa hizi na hujapiga hata simu,
na kwanini hujaenda kazini?”
Aliniuliza maswali mengi ambayo niliona kabisa sina majibu.
Nilibaki tu nimejiinamia nikiwaza na kuwazua.
Mara ghafla mlango wa chumba changu ulibishwa.
“Subiri… Subiri kwanza. Nani huyo?”
Aliniuliza.
“Sijui sasa mimi na wewe tuko ndani unaniuliza nani mimi nitajuaje.”
Aliitikia na mimi kisha nilinyanyuka nilifungua mlango na kukutana na mmoja kati ya mabinti za mama
mwenye nyumba.
“Mama anakuita.”
Alisema na kisha kuondoka.
Niliondoka kiunyonge sana kisha kuelekea nyumbani kwa mwenye nyumba.
Nilibisha hodi na kisha kukaa.
Mama mwenye nyumba alikuwa mpole sana.
“Kuna nini mwanangu?”
Aliniuliza.
“Samahani mama kwa kilichotokea.”
“Nimeshangazwa sana. Huyo msichana ndiyo kwa mara ya kwanza namuona lakini amekuja kufanya vurugu nimeshangaa.
Ni nani yako?”
Aliniuliza mama sikuona sababu ya kumficha.
“Mama huyu mimi ni mchumba wangu.”
“Sasa inaonekana ana matatizo.”
Mama aliniambia.
Hapana mama ndivyo alivyo.
“Mmh sawa, kwasababu tu ni wewe mimi nimeelewa na nimesamehe yote lakini jaribu kukaa na mwenzio umuonye umwambie
jinsi ya kuishi na watu.”
“Sawa mama nitafanya hivyo, samahani kwa kilichotokea mama naomba samahani kwa watoto zako wote na kwa wapangaji wote sijadhamiria.”
“Hata wao pia wameshangaa siku zote umekuwa mtu mzuri halafu mtu mgeni tu anatokea anaanza kufanya hivyo sidhani kama watakuwa na
shida tena na wewe muhimu kama umeomba msamaha mimi nitaongea nao.”
“Sawa nashukuru.”
“Aya sawa nenda ukamuwahi mgeni wako.”
Mama alisema na kisha kuniruhusu kuondoka.
Niliondoka kiunyonge sana kisha kuelekea chumbani.
Hata hivyo huko nje ngurumo zilikuwa zimeanza kuonesha kwamba mvua zingeweza kunyesha wakati ule.
Niliingia ndani.
“Eenhe walikuwa wanasemaje?”
Tessa aliongea huku amenishikia kiuno.
Hakuna kitu kilichonishangaza zaidi na kunishitua kama jinsi ambavyo Tessa alikuwa akiweza kubadilisha hali yake.
Sasa hivi amekasirika, saa hiyo hiyo anabadilika na kuwa mwenye furaha na saa hiyohiyo anaweza kubadilika na kuwa mwenye
huzuni hakika alikuwa ananishangaza sana.
“Aanh, wameniita tu wameniambia kwamba hawajapenda kitendo cha wewe kuwafokea.”
“Sasa mimi si nilikuwa nawaambia ukweli.”
“Sikia Tessa kila sehemu ina taratibu zao hapa utaratibu wao ndiyo huo wanakaa pale kila siku wanaongea hata mimi nimehamia
nimewakuta wanafanya hivyo hasa unakuja unaanza kuwafokea tu halafu kibaya zaidi ndiyo kwa mara ya kwanza wanakuona lazima
umewapa hali fulani hivi ya kushituka.”
“Kwahiyo hawasikilizagi watu mpaka wawe wanamjua?”
Aliongea Tessa.
Niliona sasa akinipeleka nje ya mada.
Alichokuwa akikiongea kilikuwa hakileti maana ya kile ambacho nilikuwa nikimuuliza niliamua kuacha maana ni sawa natwanga maji
kwenye kinu, mtu niliyekuwa nikiongea naye alikuwa hanielewi kabisa.
Na mara radi kubwa ilipiga.
Tessa alipiga ukelele wa nguvu na kuja kunikumbatia.
“Mamaaa…”
Nilimdaka na kisha tukaangukia kitandani.
“Tessa…”
Alivuta shuka na kujifunika mwili wote.
“Tessa…”
Nilifunua.
Alikuwa amelingangania lile shuka na wala hataki kuliachia.
“Tessa…”
Nilifungua ile shuka na kumkuta Tessa akilia.
“Unalia nini?”
Tessa alianza kulia kwa kwikwi.
Niliogopa sana nikihisi labda radi imemdhuru.
Mvua kubwa ikiambata na upepo mkali iliendelea kunyesha Tessa alijikunja kama mtu anayeogopa kitu fulani,
alijikunyata hadi mwisho wa kitanda na kujifunika shuka gubigubi.
Alinishangaza sana.
Alishika shati langu akatae kuniachia nilizidi kushangaa matendo ya Tessa.
“Tessa tulia basi.”
Alianza kupiga kelele kwa sauti ya chini ilibidi nisogee pale alipokuwa na kumkumbatia.
Akiwa ndani ya shuka niliyahisi mapigo ya moyo wake kabisa, ulikuwa ukipiga kwa kasi kubwa.
Nilimkumbatia kwa nguvu zote kuonesha kwamba ninamlinda.
Hapo kidogo niliona hali yake ikitulia nilimkumbatia kwa muda mrefu sana mpaka alipopitiwa na usingizi.
Hata hivyo sikumuachia niliendelea kumkumbatia hivyo hivyo.
Hakika hali iliyokuwa ikitokea hapo ilinichanganya.
“Tessa wewe ni kiumbe gani?!”
Niliendelea kujiuliza.
“Unanishangaza sana ila siyo bure wewe utakuwa na matatizo.”
Niliwaza na kuwazua.
Usiku huo hatukuweka neti, hatukula wala sikuzima taa niliogopa kumuachia Tessa.
Tulilala hivyohivyo mpaka asubuhi ya siku ya pili.
Tessa aliamka akiwa na uchovu mwingi, alipoamka tu aliniamsha.
“Amka…”
Niliamka huku na mimi nimechoka.
Tulilala tukiwa na nguo zetu tena Tessa akiwa ndani ya shuka mimi nikiwa sijajifunika nadhani mbu walinifanyia sherehe usiku huo.
Niliamka nikiwa na uchovu mwingi zaidi ya Tessa.
“Yani wewe umezubaazubaa kweli, sasa umeamka unaanza kujivutavuta.”
Tessa aliniambia.
Sikumshangaa tena kwa maana alivyokuwa akinifanyia vilikuwa ni vya kushangaza vya kutosha hilo kwangu
sikuona kama lilikuwa linashangaza.
Nilijitahidi tu kuonesha nimechangamka.
“Mgeni anakuja kwako muandalie basi hata chakula cha asubuhi, jana umenilaza njaa, saa hizi umeamka na kuanza
kijivutavuta.”
Tessa aliongea.
Niliamka na kutoka nje.
Niliingia jikoni huku nikipiga miayo mirefu nilijaribu kutafuta kitu cha kupika asubuhi hiyo.
“Sijui nipike nini?”
Nilivuta muayo mrefu na kisha kurejea chumbani.
Nilimkuta Tessa bado amekaa kitandani.
“Tessa…”
Nilimuita.
Wala hakugeuka kuniangalia.
“Simu yangu iko wapi?”
Aliniuliza.
“Aanh sijui.”
Nilienda mpaka mezani na kisha kuichukua simu yangu.
“Yani wewe mimi nakuambia uamke asubuhi uniandalie chai unaamka na kuanza kuwasha simu,
unajielewa kweli?”
“Aanh Tessa si nakupigia ili uipate simu yako!”
“Kwani nimekwambia nina shida sana na simu yangu hebu kaandae chakula njaa inaniuma. Lete simu yako hapa nijipigie mwenyewe.”
Tessa aliongea.
Nilimrushia simu na kisha kutoka.
Nilienda jikoni.
Nilifungua friji langu hata hivyo hakukuwa na chochote cha kupika zaidi ya nyama.
Nilichukua nyama hiyohiyo na kuamua kuitengeneza.
Niliikaanga vizuri na baada ya hapo nilitoka nje.
Niliwaza nitafute kitu gani cha kuilia na hiyo nyama.
Nilirudi ndani na kisha kunawa uso wangu vizuri kabisa nilibadilisha nguo na kisha kutoka kuelekea soko lililokuwepo
karibu tu hapo na kwangu.
Nilitafuta ndizi mzuzu mbichi nzuri nikanunua nyanya na baadhi ya vitu vingine nilivyokuwa nikivihitaji na kisha kurejea nyumbani.
Nilizikaanga zile ndizi na ndani ya lisaa lizima nilikuwa nimeshamaliza hadi kukata kachumbari nikaweka mezani.
Nikachemsha chai na kisha kuiweka mezani.
“Tessa umeoga?”
Nilimuuliza.
“Nimeoga saa ngapi sasa?”
“Basi kaoge chakula tayari.”
Alienda kuoga huku akivaa baadhi ya nguo zake ambazo nilikuwa nazo hapo nyumbani.
Na mara baada ya kumaliza kuvaa alitoka na kuingia sebuleni.
Nilinyanyuka na kisha kuelekea bafuni na mimi kwaajili ya kuoga.
Nilitumia muda mrefu sana kuoga huku nikifikiria hili na lile.
Nilipomaliza nilirejea na kuvaa kiuvivu na kisha kuelekea sebuleni kuungana na Tessa kwa ajili ya kifungua kinywa cha asubuhi.
Unaweza pia kusoma: