Unseen - Episode 02 
Niligonga mlango na nilifunguliwa mlango na sura mpya bila kuuliza nilijua huyu ni rafiki yake Tessa
ambaye nilikuwa nikitambulishwa.
Alikuwa mzuri kama Tessa ingawa kuna baadhi ya vitu ambavyo alizidiwa na Tessa.
Tessa alitoka ndani wakati huo bado nilikuwa nimesimama mlangoni lakini niliweza kumuona kwa vile Tessa alikuwa kwenye nyumba
ambayo ilikuwa ina chumba na sebule.
“Eti nimependeza?”
Alikuwa akimuuliza rafiki yake.
“Ndiyo umependeza.”
Mimi ndiye niliyejibu.
Alishangaa.
Alikuja kunikumbatia.
“Karibu… Umewahi tofauti na nilivyotegemea.”
Dakika hii Tessa alikuwa amebadilika hakuwa yule aliyekuwa akinifokea wakati nipo nyumbani.
“Ndiyo niliona niwahi kidogo ili nisiwacheleweshe.”
“Ok fine.”
“Karibu.”
Alinikaribisha ndani.
Nilikuta wameandaa vyakula vizuri vya aina mbalimbali hasa vile ambavyo nilikuwa nikivipenda.
Walinikaribisha mezani na tulianza kula huku tukipiga stori mbili tatu.
Tuliongea mambo mengi hadi tulipomaliza kula na baada ya hapo tuliwasha runinga huku tukipiga stori mbalimbali.
Wakati mazungumzo yakiwa yanaendelea Tessa alitopea katika kuangalia tamthilia ya kikorea ambayo alikuwa akiifuatilia
mara nyingi na huo ndiyo ulikuwa muda wake.
Hivyo aliendelea kuangalia akiachana kabisa na habari za kupiga soga ambazo zilikuwa zikiendelea hapo sebuleni.
Wakati huo Robert na rafiki yake Tessa ambaye alikuwa akiitwa Jacqueline walikuwa wakiendelea na mazungumzo ambayo
Tessa hakuyaelewa vizuri kwasababu kwanza akili yake ilikuwa imetawaliwa na tamthilia iliyokuwa ikiendelea.
Aliendelea kuangalia wala hakujishughulisha na mazungumzo.
Takribani dakika arobaini na tano zilipita huku Tessa akiwa kimya kabisa.
Hadi tamthilia ilivyoisha Tessa aligeuka na kuangalia alimkuta Robert akicheka na rafiki yake Jack ingawa walikuwa mbali na yeye
Tessa ndiye aliyekuwa akiwatenganisha kitendo hicho kilimchukiza sana.
“Mnacheka nini?”
“Stori zimenoga.”
Alijibu Robert.
“Stori zimenoga…!”
Aliongea huku akiwa amebana pua.
Jack alikuwa ameishatulia ni kama alihisi hali ya hatari.
“Wewe si ulikuwa bize unaangalia runinga.”
“Usinijibu mimi hivyo.”
Tessa aliongea huku sura yake ikionesha haina chembe ya utani.
Alianza kufoka.
“Yani mmekaa hapa mnajiongeleshaongelesha mnajichekacheka kama watoto, hamna akili nyie mnachekacheka kama matahira.”
Aliongea Tessa.
Robert alikunja uso kwa ishara ya kutoelewa maana halisi ya kile alichokuwa akikizungumza Tessa.
Wakati kimya kimeendelea kutawala huku Robert akiendelea kushangaa tabia iliyooneshwa na Tessa na wakati huo Jack akiwa
amebaki kimya tu asijue nini cha kuongea Tessa alizidi kushikwa na hasira.
“Kwahiyo nyie mnashindwa kunijibu?”
Aliendelea kufoka huku akitukana.
Hali hiyo ilimchanganya sana Robert.
“Umeshanikera Robert nyanyuka uondoke.”
Robert aliendelea kushangaa.
“Nyanyuka utoke…”
Akiwa bado ameendelea kuduwaa akishangaa hali ilivyokuwa.
Tayari Tessa alikuwa ameshanyanyuka na kuja kumnyanyua kwa nguvu na kisha kumsukumia nje.
“Toka…”
Alimfukuza.
Robert alijikuta yuko nje huku akirushiwa viatu, alishindwa kuelewa maana halisi ya kile alichokuwa akikifanya Tessa.
“Ana matatizo gani Tessa?!!”
“Na wewe…”
Tessa alimgeukia Jack mara baada ya kurudi ndani Jack alikaa vizuri.
“Sitaki mazoea na watu usiowajua.
Sijui mkoje mshaniharibia siku yangu naenda zangu kulala.”
Alisema Tessa na kisha kuingia kulala.
Robert alivaa viatu vyake akiwa nje huku baadhi ya watu wakimuangalia.
Aliondoka kiunyonge sana na kisha kuelekea nyumbani kwake.
Mawazo mengi yaliniandama sana.
Nilipiga hatua za kinyonge sana kuelekea nyumbani kwangu.
Mimi na Tessa tulikuwa hatuishi mbali.
Tessa alikuwa akiishi maeneo ya mpakani.
Nilitembea nikiwa na mawazo mengi wala sikujua hata nilikuwa nikielekea wapi.
Nilichokuwa nikikijua nilikuwa nikinyoosha moja kwa moja barabarani niliweza kujua kwamba nimekata kona ya njia ya kuelekea
kwangu makumbusho.
Mawazo yalinizidia hata nilishindwa kuelewa ni saa ngapi nilifika makumbusho.
Nilitembea kutoka kwa Tessa mpaka makumbusho na hapo nilipogundua nimetembea umbali mrefu sana.
Nilikatiza mitaa na kisha kuelekea kwangu huku nikiwa nimechanganyikiwa nilipoingia chumbani kwangu.
Nilijitupa tu kitandani na viatu vyangu nilipitiwa na usingizi kabisa.
Niliamka ikiwa ni siku ya pili yake huku kichwa kikiwa na mawazo mengi sana.
Roho iliniuma sana kwa alichonifanyia Tessa.
“Kama hanipendi si aseme.”
Kwa akili nyingine ilikuwa ikiniambia mara ngapi Tessa aliniambia tuachane.
“Inawezakana mimi namlazimisha.”
“Ndiyo.”
Nilijiuliza na kujijibu mwenyewe.
Niliamua kuvaa moyo wa kiume kutomtafuta.
Nilienda kazini huku nikiwa na mawazo mengi sana.
Kazi hazikufanyika hiyo siku nilisitisha huduma kwa wateja wangu wote.
Nilirudi nyumbani jioni huku nikiwa sijafanya kitu chochote.
Nilipofika nyumbani niligundua kwamba sijala kitu chochote tangu usiku uliopita nilipokula nyumbani kwa Tessa.
Akili yangu ilikuwa ikipingana na mawazo ya kumuacha Tessa lakini pia moyo ulishindwa.
Hapo ndipo nipogundua kwamba njaa inaniuma.
Sikuwa hata na hamu ya kupika chakula niliamka na kisha kuelekea kwenye vibanda vilivyokuwepo nje karibu na nyumbani kwangu na
kisha kununua chakula.
Nilinunua chipsi kuku na soda na kisha kurudi nyumbani.
Nilivifakamia vyote.
Hapo nilihisi afueni.
Niliwasha runinga huku nikipoteza mawazo.
Siku hiyo ilipita bila mawasiliano yoyote yale kati yangu na Tessa.
Asubuhi niliamka nikiwa nimechoka sana.
Sikuweza hata kunyanyuka.
Sikuwa na nguvu ya kufanya chochote.
Machozi yalianza kunilengalenga kila nilipofikiria kuachana na Tessa nafsi iligoma kabisa.
“Haaa.. Tessa.”
Niliongea huku nikivuta pumzi.
“Wa ajabu sana kama jina lako, unanitesa tu.”
Mara nilisikia hodi.
Nilienda kufungua alikuwa ni rafiki yangu Idrisa.
“Oy vipi weekend hii.”
“Karibu ndani bwana.”
Nilimkaribisha kinyonge.
“Vipi una matatizo?”
“Daa aisee mimi simuelewi kabisa shemeji yako Tessa.”
“Kafanyaje tena?”
“Mimi sielewi kabisa yani daa.”
“Sasa kama mwanamke umuelewi si unampiga chini.”
“Yani hapo ndiyo penye ugumu mimi simuelewi lakini kumuacha pia siwezi. Nimejitahidi sana kutomtafuta tangu juzi
sijaongea naye hapa naona naye ameninyamazia.”
“Aanh huyo hakupendi huyo, halafu kwanini umng’ang’anie mwanamke wewe mbona uko vizuri, una kazi nzuri, unaishi vizuri,
una pesa zako unashida gani ya kumng’ang’ania mwanamke achana naye bwana fanya mambo mengine.”
“Kila nikijaribu nashindwa rafiki yangu.”
“Aanh usilete umama bwana utaweza tu usijali.”
Nilivuta pumzi na kushusha.
“Umekula sasa?”
“Hata sijala, nilikula jana usiku.”
“Aanh wewe umekaa kiboya sana changamka mtoto wa kiume unaliliaje mapenzi cheki jamani ulivyonyong’onyea
ngoja niingie jikoni basi nikuandalie chai.”
Akili yangu ilizidi kupambana na mawazo mapya aliyoyaleta rafiki yangu.
Aliingia jikoni na kubandika chai huku akitafuta kitu chochote cha kupika humo ndani na mara simu yangu iliita nilikurupuka
fasta na kuangalia ni nani alikuwa akipiga.
Alikuwa ni mfanyakazi wangu.
“Boss samahani kuna mteja amesema kama akija utakuwa kazini, kwasababu hii wiki yote haukuweza kufanya kazi.”
“Wiki nitakapoanza nitawajulisha.”
Nilijibu kiufupi na kisha kukata simu sikutamani tena kufanya kazi.
“Kijana changamka.”
Rafiki yangu aliropoka akiwa jikoni.
Nilikaa huku nikiendelea kutopea kwenye mawazo yangu.
Simu iliita tena nilijua tu ni mfanyakazi wangu akihitaji maelezo zaidi.
Niliacha ikaita mpaka ikakatika.
Ikaita mara ya pili nikaiacha.
Mara ya tatu nilikasirika.
Nilipokea kwa hasira.
“Haloo si nimeishakuelekeza.”
“Umenielekeza nini?”
Ilikuwa ni sauti ya Tessa.
Nilikurupuka na kusimama wima.
Huku nikionesha nidhamu kana kwamba Tessa alikuwa akinitazama.
“Tessa…”
Rafiki yangu alishituka kule jikoni alikuja moja kwa moja na kisha kuniangalia nadhani alishangaa sana kunikuta
nimesimama vile.
“Hallo Tessa hujambo? Mambo.”
Nilijikuta nikiropoka kwa sauti.
Rafiki yangu alibaki amesimama tu huku amenishikia kiuno.
“Sijambo kwanini hujanipigia simu tangu juzi?”
“Aanh, nimebanwa tu na majukumu nimekumisi sana Tessa wangu. Uko salama?”
“Ndiyo niko salama.”
“Nilikuwa nafikiria nije kukuona nikajua unaumwa.”
“Hapana mimi siumwi.”
“Kwahiyo utakuja kwangu?”
“Nitakuja.”
“Ok nakusubiri nimekumiss sana.”
“Usijali nitakuja.”
“Unileteee na zawadi.”
“Sawa mama.”
Niliongea na kisha kukata simu.
Nilibaki nikivuta pumzi tu kana kwamba nimetoka kukimbia katika mashindano ya riadha.
“Hivi mwanangu wewe una matatizo gani?”
“Mimi sielewi kabisa.”
“Aanh, wewe mwenyewe si ndiyo umesema unamuacha lakini sasa hivi amekupigia simu unatetemeka kweli.”
“Kila nikipanga kumuacha huyu Tessa nashindwa.”
“Aisee pole sana rafiki yangu.”
Nafsini mwangu wala sikuwa na hatia kwamba Tessa alikuwa akinisumbua kiasi hiko.
Lakini Idrisa alitamani sana kunifanya nione hatia.
Aliandaa chakula na mimi nilikula kiunyonge.
Nilifikiria safari ya kurudi tena kwa Tessa.
Niliwaza itakuwaje endapo atanifukuza tena.
Nilijipa ujasiri wa kwenda.
Ilipofika jioni nilijiandaa vizuri na kisha kwenda.
Tessa alinipokea vizuri sana.
“Nilikumiss sana mume wangu jamani siku nyingine usirudie kufanya hivyo.”
Aliniambia hivyo na maneno mengi sana ya kunifariji na kunitia moyo nilisahau vyote ambavyo alinifanyia.
Usiku ule aliandaa chakula kizuri.
Tulikula na kufurahia na kisha tulilala wote.
Usiku wetu ulikuwa mzuri sana hakika nilifurahia.
Nilisahau kila kitu ambacho kilipita katikati yetu.
“Tessa nakupenda sana mke wangu.”
“Nakupenda pia mume wangu.”
“Vipi swala la kwenda kuwaona wazazi wangu?”
Aliniangalia tu kana kwamba ananitafutia kitu cha kuniambia.
“Usiku mwema ulale salama.”
Alisema na kisha kuvuta shuka na kugeukia upande wa pili.
Unaweza pia kusoma: