Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Unseen - Episode 03

Nilibaki tu nikiwa na mawazo yasiyoisha.
“Sasa tutaendelea hivi mpaka lini jamani?! Mimi natamani tufunge ndoa lakini huyu mtu anaweka vikwazo.”
Niliendelea kuwaza na kuwazua. Haukupita muda kabla sijaanza kusikia kelele.
Tessa alianza kulalamika akiwa usingizini. “Aanhhh…. aaanh….”
Alipiga kelele huku akijigeuzageuza huku na kule.
Nilisogea pembeni ili kumpa uhuru zaidi aendelee kujigeuza geuza.
“Sitaki…”
Alianza kuongea.
“Sitaki nimesema toka…”
Alianza kuongea kwa sauti ya kipole ambayo baadae ilielekea kukaza alikuwa akionesha msisitizo zaidi.
“Sitaki nimesema kwani lazima?...”
Aliongea.
Nilivuta shuka na kisha kukaa kabisa kitandani.
Nilinyanyua mto wangu na kuuegemea huku nikimuangalia Tessa alivyokuwa akiniigizia pale kitandani.

Sio mara ya kwanza mimi kulala na Tessa lakini ilikuwa mara ya kwanza kabisa usiku kukosa usingizi nikiwa na Tessa na kumshuhudia akiwa usingizini.
Alijigeuza huku na huko huku akijishika sehemu mbalimbali.
“Nimeshasema sitaki mtu asinilazimishe…”
Aliendelea kuongea kwa sauti kiasi kwamba mtu angekuwa chumba cha pili angeweza kusikia.
Nilibaki nikimshangaa.
“Hataki nini?”
Nilijiuliza maswali yasiyo na majibu.
“Nimeshasema siendi.”
Alikuwa akiongea na kisha kupumzika kidogo.
Bado niliendelea kushangazwa na vitimbwi vya Tessa.
“Siendi…”
Aliongea na kisha kutulia kama dakika tano hivi na kisha kuendelea tena.
“Sitaki kwenda kwa mama yako.”
Nilishituka sana nilisogea hadi kwenye kingo ya kitanda na kisha kukaa huku nikijiinamia.
“Anamaanisha nini?! Inamaanisha vitu vyote anavyovifanya uwaga anaviongea usiku!!... Aanhaaa…”
Nilivuta pumzi na kuzishusha.
“Ngoja niendelee kumsikiliza.”
“Siendi mimi kwa mama yako.”
Aliongea.
Na hapo ilichukua nusu saa nzima bila kumsikia akiongea chochote.
Usingizi na mimi ulianza kuniingia.
Ulikuwa usiku mnene sana mishale ya saa saba.
Nilipitiwa na usingizi na kulala.
Saa kumi na moja niliamka.
Tessa alikuwa bado amelala.
Niliendelea kumuangalia, niliangalia sura yake nzuri, niliangalia jinsi alivyokuwa amelala kwa amani kabisa pale kitandani.
Kumbukumbu ya tukio la usiku ilinijia.
Akili yangu iliendelea kuwa na mawazo mengi.
Nilijilaza tu pale kitandani nikiwa sina usingizi wowote.
Tuliendelea kulala mpaka ilipofika takribani mida ya saa mbili.

Tessa alijigeuza huku na huko kabla ya kuinuka kitandani.
Alijishika kichwa huku akikunja sura.
Niliendelea kumuangalia pale huku nikijifanya nimelala.
“Kichwa kinaniuma.”
Alinyanyuka huku akisema.
Alienda kuchukua dawa zilizokuwa pembeni ya kitanda kwenye meza ambayo alikuwa akiweka vitu vyake vya kujirembea maarufu kama dressing table.
Alichukua vidonge vya kupunguza maumivu viwili huku nikimtizama.
Aliziangalia na kisha aliongezea nyingine mbili.
Alisonya na kisha kuongeza mbili nyingine.
Nilishangaa sana.
Dawa hizo zilifika sita.
Alizinywa zote kwa mara moja.
Nilibaki nimetumbua macho tu pale kitandani sikutaka Tessa aone kama nilishuudia hicho kitendo.
Baada ya kunywa alikunja sura kidogo na kisha alitulia.
Alitikisa kichwa na kisha kuweka tena mikono kichwani kwa ishara ya kwamba maumivu yalikuwa yakizidi kuongezeka.
Alichukua vidonge vya kupunguza maumivu vingine vinne na kisha kumeza.
Kwa maana hiyo ni kwamba alimaliza dozi nzima ya vidonge vya kupunguza maumivu kwa mara moja.
Nilishangaa sana.
Huku nikiwa na mawazo.
“Si anaweza kufa?!”

Alinyanyuka na kisha kurudi tena kitandani alikaa kwa muda mfupi alinyanyuka tena na kuelekea nje.
Nilikaa nikiendelea kuwa na mawazo.
Nilimsikia Tessa akiongea huko nje.
Katika nyumba ile kulikuwa kuna wapangaji wawili tu pamoja na mama mwenye nyumba.
Mama mwenye nyumba alikuwa akiishi nyumba ya mbele ambayo ilitengana kabisa na sehemu ambayo wakina Tessa walikuwa wakiishi.
Ni aghalabu sana kukutana na mama mwenye nyumba katika hiyo nyumba ya kina Tessa.
Tessa alikuwa akiishi sehemu ya nyuma pamoja na mpangaji mwenzie ambaye alikuwa ni mwanaume.
Naye muda mwingi hakuwepo sana nyumbani.
Tessa alikuwa akizozana na mtu huko nje.
Nilisikia kwa mbali sauti ya Tessa.
Mwanzoni ilikuwa ni ya taratibu lakini kadri muda ulivyozidi kwenda ilizidi kupanda na kuwa kubwa.
Ilionesha ni dhahiri kwamba anagombana na mtu huko nje.
Nilinyanyuka na kusogea dirishani ili niweze kusikiliza vizuri kilichokuwa kikitokea.
Nilisikia Tessa akitamka maneno makali sana kwa huyo mgomvi wake.
“Sitaki unizoee, usinishobokee wala mimi sitaki shobo na mtu ushanielewa? Umekuja hapa usianze kufatilia mambo yasiyokuhusu.”
Ni moja kati ya maneno makali ambayo Tessa alimtamkia huyo msichana.
“Huna hata haya mwanamke hujisikii vibaya muone kwanza.”
Aliongea na maneno mengine mengi.
Kilichonishanganza zaidi ni kwamba yule mgomvi wake hakuwa akijibu chochote.
Nilifunua pazia na kisha kuangalia.
Kama alivyotoka ndani Tessa alikuwa amejifunga kanga mbili huku ameshika kiuno akiendelea kuongea.
Ni dhahiri kwamba aliamua kushusha sauti ili nisiweze kusikia kile kitu ambacho alikuwa akikiongea.
Aliendelea kumsema yule mwanamke kiasi kwamba mama mwenye nyumba aliamka na kisha kutoka nje.
Alisimama tu mlangoni na kuangalia kilichokuwa kikiendelea.
Tessa aliendelea kuongea bila kujali uwepo wa mama mwenye nyumba.
Alimchamba akachambika.
Nilibaki nikimshangaa.
Kiukweli sikuficha mshangao wangu juu ya Tessa.
“Kwanini haogopi hata watu wazima?!”
Nilijiuliza.
“Mama mwenye nyumba si anaweza kumfukuza. Kwanini Tessa ana tabia za ajabu hivi?!”
Hasira zilinipanda.

Safari hiyo sikutaka kumlazia damu nilimsubiri hadi aje.
Nilikaa takribani dakika tano nzima.
Kisha Tessa aliingia ndani huku akiwa amekunja sura.
Alikuja moja kwa moja mpaka chumbani na kuanza kuzungukazunguka mule ndani.
“Tessa…”
Nilimuita.
“Nimeshavurugwa hapa naomba usiniongeleshe chochote.”
Aliongea.
“Hivi unadhani uko sahihi kweli?”
Nilimuambia.
Alinikata jicho kali wala hakujibu chochote.
“Hata kama mtu kakukosea unafikiri una haki ya kugombana naye kivile. Unamtamkia maneno makali kiasi kile, kweli Tessa?”
Aliendelea kunikazia jicho kana kwamba hasikii nilichokuwa nikimwambia.
“Si naongea na wewe hutaki kunijibu?
Lazima uwe na heshima Tessa.
Hata kama mtu kakukwaza kiasi gani kwanini usimuite kiustaarabu ukaongea naye, unagombana, unapayuka kiasi kwamba mpaka mama mwenye nyumba yako anasikia, akikupa notisi je? Unatakiwa ujiheshimu jifunze kuishi na watu vizuri kwanini unakuwa hivyo Tessa?”

Niliongea kiuanaume huku nikiwa nimepaniki.
Tessa aliniangalia tu bila kujibu chochote.
Alivuta pumzi na kushusha.
Nilihisi amenielewa na hapo alikuwa akitafuta maneno ya kuniomba msamaha.
Hapo nilijiona kweli nimeuonesha uanaume wangu mbele ya Tessa.

Alipiga hatua za kinyonge sana na kisha kuelekea kwenye kabati yake.
Alifungua kabati na kisha kujifikiria.
Niliendelea kumuangalia tu alichokuwa akikifanya.
Na hapo tabasamu la ushindi lilinitoka.
“Hatimaye kwa mara ya kwanza nimemuweza Tessa.”
Niligeukia pembeni huku nikiachia tabasamu la ushindi.
“Toka…”
Tessa alinishitua katika furaha niliyokuwa nayo.
Alikuwa amenishikia nguo zangu pamoja na viatu vyangu.
“Ondoka…”
Alisema.
“Tessa… Kwanini?!!”
“Ondoka nyumbani kwangu…”
“Kwahiyo Tessa wewe ni mtu gani usiyetaka kupewa ushauri usiyetaka kukosolewa.”
“Nimeshasema toka, si una kwako.”
Alisema.
“Ok fine. Leta nguo zangu nivae.”
“Utaenda kuvalia kwako…”
Mwilini wangu wakati huo nilikuwa na boksa tu niliyokuwa nimevaa.
Nilishangaa sana.
Tessa anataka kunifukuza huku nimevaa boksa.
“Sikia naomba uondoke humu ndani sitaki kuiona sura yako tena na usinitafute tena sijui unanielewa?”
“Sasa Tessa, kwani kosa langu mimi ni nini?”
“Nimeshasema ondoka.”
Nilichanganyikiwa sana sikutegemea kama hali ingekuwa hivyo.
Nilipiga magoti na kisha kuomba msamaha.
Kilikuwa ni kitendo kisichotarajiwa sikutegemea kabisaa kufanya hivyo hata hivyo nilijikuta kwamba sina namna.
“Tessa samahani mama yangu nilikuwa najaribu kuweka hali sawa. Ulichokifanya hakikuwa kizuri.”
“Kwahiyo wewe unajiona wewe ndiyo mkamilifu sana? Wewe kama nani mpaka uniambie hivyo, unanikemea na kunikaripia, who are you? Mimi sitaki kabisa mtu anisumbue. Najua mwenyewe ninachokifanya.”
“Basi mama yaishe.”
Nilijikuta tu nikiomba msamaha.
Kwanza kabisa nafsi yangu iliniambia kwamba natakiwa niombe msamaha niepushe aibu ya kutolewa nje nikiwa na boksa tu.
Nafsi iliniuma kweli nilijiona mimi ni mume bwege.
“Hivi kanifanyia madawa huyu mwanamke mbona nafanya vitu ambavyo sijategemea kabisa kufanya.”
Niliendelea kuwaza na kuwazua.
Hatimaye alininyanyua pale na kunikumbatia huku amekunja sura kuonesha kwamba bado ana hasira na mimi.
Nilijifanya tu nimefurahia lakini bado akilini kwangu sikuwa sawa kabisa.

Baada ya hali ya hewa kutulia nilioga, aliandaa chai, nilikunywa na kisha kumuaga.
“Baby si tushinde wote leo.”
Tessa alisema.
“Hapana inabidi niende ofisini nikashughulikie baadhi ya vitu.”
“Utarudi tena usiku? Nataka kulala na wewe tena.”
“Nitaangalia mama nikipata muda nitakuja.”
“Usiniambie nitaangalia nipe uhakika kabisa.”
“Ok fine nitakuja.”
“Ok baby.”
Alinikumbatia na kunibusu.
Niliondoka.
Na wala sikuelekea ofisini kwangu nilirudi moja kwa moja nyumbani nilijifungia mule ndani huku mawazo yakinijia.

Nilikuja kushituka muda umeshaenda sana.
Ilikuwa ni takribani saa tatu za usiku na wala sikuwa nimekula chochote tangu nitoke nyumbani kwa Tessa.
Na pia cha kushangaza sikuhisi njaa kabisa.
“Tessa…”
Nilijikuta nikiwaza na kuwazua.
Simu yangu iliita.
Niliogopa kupokea nilihisi anaweza kuwa ni Tessa akinikumbushia ahadi yangu ya kurudi kwake usiku huo.
Nilivuta huku nikiangalia kwa mbali hata hivyo hakuwa ni Tessa alikuwa ni rafiki yangu Idrisa.
Nilipokea simu huku nikiongea kiuchovu.
“Hallo…”
Niliongea huku nikivuta pumzi.
“Vipi mwanangu mbona hujatokea kazini leo?”
“Aanh nahisi uchovu naumwa.”
“Usiniambie kwamba ni mwanamke wako bado anakutia wazimu.”
“Daah, mwanangu acha tu.”
“Nini kimetokea?”
“Yani nimeenda kumtembelea leo anagombana na watu hatari anawatukana matusi.”
“Hivi mara ngapi nikuambie kwamba huyo mwanamke hakufai.”
“Aisee Idrisa naomba niache naomba usiongelee kabisa kuhusu hili swala kama hauna ushauri mwingine zaidi ya huo naomba ukae kimya.”
Nilisema.
“Aanh mwanangu ushafanyiwa madawa.”
“Vyovyote vile mimi mwenyewe nimeridhika, wewe niache hata kama nikiwa mume bwege niache hivyohivyo.”
“Sawa basi hamna shida ila mimi usiniambie tena kuhusu habari za Tessa.”
“Sitakuambia tena na wala usiniulize.”
Nilijibu kiubabe na kisha kukata simu.
Nilivuta pumzi ndefu na kisha kuendelea kubaki hapo.

Sehemu 2 Sehemu 4
0
0