
Ukuaji na maendeleo ya mtoto wa miezi sita (6)
Baada ya kujifungua shauku ya wazazi ni kujua au kuona maendeleo na ukuaji mzuri wa mtoto.
Katika makala hii tufahamu kuhusu ukuaji na maendeleo ya mtoto wa miezi sita.
Kipindi cha miezi sita katika ukuaji wa mtoto ni kipindi cha kufurahisha kidogo.
Mtoto anaendelea kukua kwa kasi sana kulinganisha na miezi iliyopita.
Upande wa kushoto wa ubongo wa mtoto unaanza kuunganisha mawasiliano na upande wa kulia.
Hali hiyo inamfanya mtoto kuwa na uwezo wa kudhibiti matendo yake.
Wewe pamoja na mwanao sasa mnaanza kuelewana vizuri.
Watoto wanaanza kuonesha hisia zao na unaweza kuwajua kama wana furaha au wana huzuni, pia wanaanza kuonesha muitikio kwa maneno wanayoyasikia.
Mpaka kufikia miezi sita watoto wanakuwa na uelewa mpana kuhusu wao wenyewe na ulimwengu wao wanaoishi.
Watoto pia wanakuwa na uelewa mzuri wa kutofautisha wazazi wao, ndugu na watu wengine na wanaweza kuwa uwoga kwa watu wasiowajua.
Miezi sita ni umri sahihi unaoshauriwa kuanza kumpa mtoto vyakula vingine tofauti na maziwa ya mama.
Ni muhimu kumpa mtoto vyakula vyenye lishe mbalimbali ikiwa pamoja na madini chuma ili kusaidia kuimarisha misuli ya taya.
Misuli ya taya itamsaidia kutafuna vizuri na kuongea.
Anza na vyakula vilaini kidogokidogo angalau mara moja kwa siku huku ukiendelea kumnyonyesha.
Na unapoanza kumpa vyakula vigumu pia ni muhimu kumpa maji safi ya kunywa.
Watoto wa miezi sita sasa wanakuwa na uwezo wa kushika vitu vizuri na kuvivuta na wanaweza kuamisha kitu kutoka mkono mmoja na kushikia mkono mwingine.
Kwa umri huu bado ni vigumu kutambua kama mtoto anatumia mashoto au mkono wa kulia.
Mikono yote miwili anaitumia sawa.
Kwa miezi sita watoto wanakuwa na uwezo wa kugalagala chini hivyo umakini unahitajika sana kama utakuwa umemlaza mtoto juu ya vitu au kitandani.
Watoto wanaanza kujisukuma chini wakijaribu kutambaa, wanaanza kujinyanyua kama Utajaribu kuwasimamisha na wanakuwa na uwezo wa
kujigeuza upande wowote anaoutaka mwenyewe.
Kwa mtoto wa miezi sita anaweza kukereka anaapoachwa peke yake kwa muda mrefu.
Watoto wanaendelea kufurahia kushika vitu tofautitofauti na kuviweka mdomoni.
Watoto wa miezi sita wanafurahia uwepo wako karibu yao na wanajifunza jinsi ya kukuelezea nini wanachokitaka kwa njia tofauti na kilio.
Baadhi ya watoto katika umri huu wanaanza kuelewa baadhi ya maneno na kuyajua majina yao.
Pia watoto wanakuwa na uwezo wa kutambua hisia zako kwa namna unavyozungumza, kama utawaongelesha kwa ukali au kwa upole.
Uwezo wa watoto kujifunza kuongea unakua kwa kasi, unaweza kuanza kumsikia akitoa sauti tofautitofauti na kurudirudia baadhi ya maneno kama vile bababa.
Unaweza kurudia na wewe maneno anayoyasema ili kumsaidia kuendelea kujifunza kuongea.
Ili kumsaidia mwanao kukua na kuwa na maendeleo mazuri:
Hakikisha vitu vinavyokuwa karibu yake ni salama kwasababu mtoto anashika kila kitu anachokiona na kukipeleka mdomoni.
Msikilize na ongea na mwanao kwa kuangaliana usoni, muoneshe hisia tofautitofauti na umjibu sauti zake anazozitoa.
Watoto wanapenda kusomewa vitabu hasa vitabu vyenye picha za kung’aa.
Mfanye mtoto ajihisi yuko salama kama yuko na watu ambao hawajui.
Watoto wana ukuaji tofauti kuna watoto wanawahi na kuna wengine wanachelewa kuonesha hatua hizi.
Ila unaapoona mambo haya kwa mwanao ni muhimu kumuona daktari kwa msaada zaidi.
- Mtoto anaonekana kama hawajui wazazi wake na wala hana ishara yoyote hata kwa watu wake wa karibu.
- Mtoto haoneshi kuvutiwa na kitu chochote karibu yake wala kutaka kuvishika.
- Kama mtoto hajaanza kutoa sauti yoyote.
- Mtoto anashindwa kukuangalia usoni.
- Na kama mtoto anasumbua kwa muda mrefu na anashindwa kutulizwa hata na mzazi au mlezi wake.
Ukuaji na maendeleo ya mtoto wa miezi saba (7)
Ukuaji na maendeleo ya mtoto wa miezi mitano (5)
Ukuaji na maendeleo ya mtoto wa miezi minne (4)
Ukuaji na maendeleo ya mtoto mchanga wa miezi mitatu (3)
Ukuaji na maendeleo ya mtoto mchanga wa miezi miwili (2)
Ukuaji na maendeleo ya mtoto mchanga wa mwezi mmoja (1)
Unaweza pia kusoma: