Ukuaji na maendeleo ya mtoto wa miezi saba (7)
Baada ya kujifungua shauku ya wazazi ni kujua au kuona maendeleo na ukuaji mzuri wa mtoto.
Katika makala hii tufahamu kuhusu ukuaji na maendeleo ya mtoto wa miezi saba.
Watoto wanaendelea kukua kwa kasi katika umri huu.
Wanaanza kukaa wenyewe na kula vyakula tofauti ila kuendelea kumnyonyesha maziwa ya mama ni muhimu kwasababu ni chanzo kikuu cha virutubisho vyake.
Katikati ya mwezi wa 5 mpaka wa 7 unaweza kuona jino linaaza kuota, ila hauna haja ya kuwa na wasiwasi kama haijatokea hivyo
kwasababu ni kawaida pia kwa meno kuchelewa mpaka miezi 12.
Na kama meno yameanza kuota tarajia kumuona mtoto anazidisha kutoa mate.
Kwa miezi saba uwezo wa mtoto kufanya mambo mbalimbali unaongezeka, anakuwa na uwezo mzuri wa kushika vitu kwa mikono yote miwili.
Anakuwa na uwezo wa kuvuta vitu kwa vidole kuvisogeza karibu yake anavichunguza kwa ukaribu au kuviweka mdomoni.
Miezi saba watoto wengi wanakuwa na uwezo wa kukaa chini peke yao bila kushikiliwa.
Ila ni muhimu kuchukua tahadhari kumuwekea vitu vilaini pembeni kama ataanguka asiumie.
Watoto wanakuwa na uwezo wa kugeuka mwenyewe upande wanaotaka na wengine wanakuwa na uwezo wa kujikalisha wenyewe kama watakuwa wamelalia tumbo.
Baadhi ya watoto wa miezi saba wanakuwa na uwezo wa kujigalagaza chini na kuna wengine wanaanza kutambaa.
Uwezo wa mtoto kutunza kumbukumbu unaanza kuongezeka, anaanza kutafuta kitu kilichofichwa au kilichodondoka.
Mtoto anakuwa na furaha sana anapokuona unaingia ndani na anakosa furaha unapokuwa mbali nae.
Mtoto anaanza kupata uwoga wa kutengana na mzazi ila hali hiyo inaweza kupotea taratibu kadri mtoto anavyokua.
Watoto wa umri huu wanaweza kuanza kukujaribu na kukataa kufanya unachowaambia ili kuona mamlaka yako, haimaanishi kuwa ni kiburi ila ni hatua ya ukuaji wake.
Mtoto anaendelea kutoa sauti mbalimbali na kujaribu kurudia rudia maneno anayoyasikia.
Wanaanza kutamka maneno kama mama au dada japokuwa hawaelewi nini maana yake.
Wanaanza kutumia makelele kama njia ya kukuita ili uwasikilize na wanaonesha hisia tofauti kwenye sura zao.
Ili kumsaidia mwanao kukua vizuri na kuwa na maendeleo mazuri:
Jitahidi kuwa na muda mwingi na mtoto msomee na kumuelezea picha mbalimbali inamsaidia kukuza uelewa wake wa mambo.
Zungumza na mwanao muda wote mnapokuwa pamoja, muelezee kuhusu mazingira yanayomzunguka na muelezee nini unafanya ukiwa nae.
Umri huu mtoto anapenda sana mazingira ya nje kuliko kukaa ndani.
Kwa kawaida ukuaji wa watoto ni tofauti kuna wanaowahi na kuna wengine wanachelewa kuonesha hatua hizi.
Kwa miezi saba unapoona mambo haya kwa wanao ni muhimu kumuona daktari kwa msaada zaidi.
- Mtoto hajifunzi wala hajaribu kutoa sauti yoyote.
- Haoneshi muitikio wowote anapoona watu anaowajua au anaposikia sauti zao.
- Anashindwa kugalagala unapokuwa umemlaza chini.
- Na kama mtoto anashindwa kuchezesha miguu yake na anashindwa kuhamisha kitu kutoka mkono mmoja kushika na mkono mwingine.
Ukuaji na maendeleo ya mtoto wa miezi nane (8)
Ukuaji na maendeleo ya mtoto wa miezi sita (6)
Ukuaji na maendeleo ya mtoto wa miezi mitano (5)
Ukuaji na maendeleo ya mtoto wa miezi minne (4)
Ukuaji na maendeleo ya mtoto mchanga wa miezi mitatu (3)
Ukuaji na maendeleo ya mtoto mchanga wa miezi miwili (2)
Ukuaji na maendeleo ya mtoto mchanga wa mwezi mmoja (1)
Unaweza pia kusoma: