Muonekano wa Giza:

Msaada

L and L (Msimu wa Kwanza) - Sehemu ya Kwanza (01)

Ndio kwanza alikuwa amerudi nchini kutokea nchini Russia katika mafunzo hayo ya upelelezi ingawa tayari alikuwa na uzoefu wa kazi alioupata miaka mitano iliyopita kabla hajapata nafasi ya kwenda kuongeza ujuzi katika nyanja ya upelelezi.
Lakini kazi aliyopewa aliiona ngumu kidogo.
Kilichomfanya aione ngumu ni kwamba tangu aanze kazi katika jeshi la polisi alisikia tuhuma hizo na mpaka wakati huo hazikuwa zimethibitishwa.
“Kama hakuna ushahidi si waache tu kufuatilia jamani.”
Lisa alilalamika pekeake.
Na kana kwamba mkuu wake wa kazi, mkuu wa upelelezi Mzee Issa Mwalukani, alikuwa akimsikia alimjibu.
“Vyanzo vya taarifa zetu zinamtaja huyu jamaa na sio chanzo kimoja lakini mpaka leo hatujawahi kupata ushahidi lakini haimfanyi asiwe mtuhumiwa kwasababu kama ni kweli hizi taarifa tunazozipata basi huyu ni mtu hatari sana.
Nakupa hii kazi kwasababu wewe ni mpelelezi hodari na umetoka mafunzoni hivi karibuni naamini tutafika mwisho wa hii kesi.”

Alijieleza kwa kirefu.
Bila kusubiri kujibiwa aliendelea.
“Sasa hivi umekabidhiwa ofisi kama mpelelezi wa kanda.
Hii ndio kesi utakayoanza nayo.
Faili lipo ofisini kwako ukihitaji msaada wowote tuwasiliane.”

Alimalizia na Afande Lissa alipiga salute na kutoka.

Alitembea kwa maringo huku akiutikisa mwili wake kwa madaha kana kwamba alikuwa kwenye mashindano ya walimbwende.
Ungemuona ungekiri kuwa hakustahili kuvaa gwanda za kipolisi na kukimbizana na wahalifu bali alitakiwa kuwa mwanamitindo au kazi zozote laini laini zinazowafaa wanawake wenye urembo kama aliokuwa nao Lissa.
Lakini yeye tangu utotoni alipenda kuangalia filamu za mapigano na upelelezi na alimuambia marehemu baba yake kuwa alitaka kuwa mpelelezi hapo baadae ijapokuwa mama yake alilipinga swala hilo kwa nguvu zote.
Baba yake Lisa alimuunga mkono na kumtengenezea njia ya kutimiza ndoto zake.

Na sasa Lissa Westley alikuwa ni askari mpelelezi na amepewa kesi ngumu ya kuanza nayo.
Masaa manne yaliyofuata alikuwa akipitia faili lililopewa jina la “TUHUMA”.
Alisoma maelezo na hitimisho za pelelezi za wapelelezi wenzake na aligundua kwanini bado upelelezi unaendelea ingawa pelelezi kadhaa zimeshafanyika tayari.
Pelelezi zote hazikutoa hitimisho zuri kwa kuelezea kwa ushahidi iwapo mtuhumiwa ni mhalifu ama laa.
“Kwahiyo wapelelezi wote wameshindwa kujua kama huyu jamaa ni mhalifu?
Mbona naskia ni mtu yupo open wala hajifichi inakuaje hajulikani?
Yani pelelezi zote zimeishia juu juu, huyu ni mtu wa namna gani au jini yani pelelezi zote hawajaweza kugundua chochote.
Sema sasa hivi kakutana na kiboko yao ni lazima ifahamike kama ni mhalifu ama hapana.”

Alijiwazia Lissa.
“Sawa nitatumia njia gani kupata taarifa za huyu mtu?
Maana wenzangu washatumia njia zote lakini ndiyo hivyo hawajaambulia kitu.”

Kutoka wakati huo akili ya Lissa haikutulia alikuwa akiwaza hili na lile njia hii na ile huku akisoma vitabu kadha wa kadha vya kipelelezi kutafuta mbinu huku akizipima hizo mbinu na kuzilinganisha na pelelezi zilizopita.
Huku pia akisoma Riwaya ya Patrick CK na Husein Tuwa.
“Inabidi nimsome nimtu wa tabia zipi.”

BAADA YA WIKI

“Ni mtu anayependa starehe kila siku lazima aende moja kati ya klabu hizi tatu na marafiki zake, atakunywa, atanunulia watu bia, saa sita usiku ataondoka.”
“Japo anapenda starehe lakini sio mtu wa kujichanganya na watu asiofahamiana nao na pia hapendi wanawake kwani hata mara moja haonekani kuchangamana na wanawake wala kuongea nao.”
Kufikia hapo Lissa hakuendelea kusoma ripoti hiyo aliyopata kutoka kwa askari aliyemuagiza kumfuatilia mtu wake.
“Oops! Kazi inaendelea kuwa ngumu sasa.”
Aliwaza Lissa.
“Lakini kwenye kamusi ya maisha yangu hakuna neno kushindwa.”
Alijipa moyo na kuendelea kuisoma ripoti hiyo.

Nusu saa baadae alikuwa ofisini kwa mkuu wake wa kazi akimueleza mpango wake wa utendaji kazi na mkuu wake huyo alionekana kuridhika nao.
“Lakini kuwa makini Lissa kazi hii ni hatari ukigundulika, na mimi sitaki kukupoteza kamanda wangu ndo kwanza umerudi mafunzoni.”
Aliongea mzee huyo anayekaribia kustaafu na Afande Lissa alimtoa hofu.
Baada ya kumtakia kazi njema Lissa aliondoka na kwenda kujipanga kuanza kazi yake.
Usiku wa saa nne Lissa alikuwa nje ya klabu moja maarufu jijini Dar Es Salaam iliyojulikana kama Wonderland night club.
Mavazi aliyoyavaa ambayo hayakuwa ya kawaida yake yalifanya baridi la usiku ule limshambulie bila huruma.
Alikata shauri kuingia ndani ya klabu ile na kutafuta sura ya mtu ambaye alimuona kwa picha tu.
Alikuwa akimkagua kila mtu na kisha akaangalia na picha husika iliyopo kwenye simu yake janja kutoka kampuni ya Apple “Iphone”.

“Ngoja nijifanye clubber ili mambo yawe mepesi huko mbele.
Muda umeenda na mtu mwenyewe simuoni.”

Alisema Lissa huku akiagiza smirnoff mbili alizozinywa haraka na kuchangamka.
Akaanza kucheza mziki huku aibu zikiwa zimeondoshwa mbali na pombe alizokunywa.
Ijapokuwa hakuwa mzoefu wa pombe hakulewa kiasi cha kupoteza uwezo wa kujiongeza.
Alijifanya amelewa ama vitu alivyovifanya vilikuwa kama geresha tu.
Alicheza mziki kiasi cha kuwavutia watu wengi ndani ya klabu hiyo na wanaume wakware wakimtolea macho kwa matamanio na baadhi yao wakijaribu bahati zao ambazo zilikuwa mbaya kwa kutokukubaliwa.
Klabuni hapo alionekana kama demu wa kishua alietokea geti kali ambaye amepata uhuru.

Saa nane kasoro Lissa aliondoka klabuni hapo huku akiwa hajapata nafasi ya kuonana na mtu aliyemtarajia.
Ijapokuwa kutokumuona mtu wake kulimfanya ajihisi ameanza vibaya kazi yake lakini alijitia moyo na kurudi kwake kupumzika na asubuhi aliingia kazini kama kawaida.
Jioni alienda klabu nyingine iliyojulikana kama Crystal pub ambayo kwa mujibu wa taarifa mtu aliyekuwa akimuwinda alipendelea kwenda.
Huko nako alikaa mpaka saa tano bila dalili yoyote ya mtu wake kuonekana.
Aliamua kurudi kwake. “Nikianza kuzunguka kwenye klabu anazopendelea kwenda nitapoteza hata chance ndogo ya kuonana nae.
Natakiwa nikae klabu moja hadi aje.”

Aliwaza Lissa akiwa kwenye gari lake kurejea kwake changanyikeni.
Alipofika alivua mavazi yale aliyoyanunua maalumu kwaajili ya kazi hiyo.
“Its hata tu kuonana nae, now nauona ugumu wa hii kazi.”
Aliwaza Lissa kiunyonge wakati akitafuta usingizi.

Sehemu 2
0
0