Angel - Sehemu ya Kwanza (01)
Angel, ni mschana wa miaka 20 aliezaliwa na kukulia katika familia ya kimaskini sana huko mkoani Rujewa, Mbeya.
Ni mschana aliekulia katika maisha magumu mno.
Mikasa ya ajabu na isiyosahaulika aliipitia msichana huyu...
Anaitwa “Angel”.
Hakika katika haya aliyoyapitia na tunayokwenda kuyasoma yanaumiza kwa kiasi fulani lakini pia yana mafundisho ndani yake...
Okay!
Simulizi ipo hivi...
Mwaka 1998 Tarehe 5, October alizaliwa Angel huko Rujewa Mbeya.
Wazazi wake walikuwa ni watu maskini sana watu ambao uchumi wao ulitegemea mvua kwa kiasi kikubwa.
Kiufupi Angel alikuwa ni mtoto pekee katika familia hiyo.
Kitu ambacho kiuhalisia hakikuwa cha kawaida kwani wanandoa hao walikuwa wameoana kwa muda mrefu sasa iweje
ndani ya miaka mitano ya ndoa aje kuzaliwa mtoto mmoja, tena awe kifungua mimba na kitinda mimba pia?
Basi ilikuwa ni zaidi ya furaha kwa Bi. Aneth mama mzazi wa Binti Angel pamoja na kwa baba mzazi bwana Taison.
Maisha yakazidi kusonga katika familia hiyo, japokuwa walikuwa ni maskini lakini hawakuwa tayari kuona mtoto
wao huyo wa pekee akiishi maisha ya tabu.
Walijitahidi sana kumtimizia kila hitaji lake muhimu kama vile mavazi, matibabu na kadharika jambo lililopelekea
Angel akue kwa afya njema kabisa.
Mwaka 2003 Angel aliandikishwa shule ya mshingi hapo hapo Rujewa, darasa la kwanza ili aanze rasmi masomo yake.
Kwa kuwa alikuwa ni mtoto wa pekee wazazi wake hawakupata tabu kumnunulia vifaa vya kusomea kwani gharama yake ilikuwa ni
ndogo sana ukilinganisha na baadhi ya familia zenye watoto wengi mashuleni.
Masomo yakaendelea vyema huku tayari binti huyo akiwa ameanza kujiwekea ndoto fulani kichwani kwake
kuwa siku moja angekuja kuwa nani...
Miaka mitano baadae Mama yake Angel alishikwa na maradhi ambayo yalianza kumsumbua kwa kiasi kikubwa kipindi hicho Angel akiwa darasa la tano.
Maradhi haya yalianza kama utani lakini baadae tatizo lilizidi kuwa sugu.
Bwana Taison alihangaika sana kuzunguka mahospitali mbali mbali kujaribu kunusuru uhai wa mkewe lakini licha
ya kuhangaika kote huko Bi Aneth hakuonesha dalili zozote kuwa angepona.
Pesa nyingi sana ziliteketea katika matibabu yake hata kupelekea umaskini kuongezeka mara dufu.
Siku moja Angel akiwa ndiyo ametoka shuleni alimkuta mama yake akiwa kalala sebleni machozi yakimtoka na kuushukia
ule mkono aliokuwa kalazia kichwa mkekani.
Angel baada ya kufika sebleni kumkuta mama yake katika hali hiyo, alimuuliza...
“Mama leo unajiskiaje?”
Angel aliuliza swali ambalo kwa mama yake lilikuwa ni kama mkuki moyoni.
Aliumia sana lakini hakutaka kuionesha hali ile mbele ya mwanae huyo kipenzi.
Hivyo aliamua kumjibu kwa kusema.
“Najiskia ahueni.. Vipi za masomo mwanangu.”
“Njema kabisa mama.”
Angel alijibu.
“Hayaa! Vizuri sana sasa uende ukabadili nguo ili uende jikoni mwanangu.”
Mama huyo alijibu.
Angel hakutaka kupoteza muda pale alipitiliza mpaka chumbani kwake huko alibadili nguo zake na kuvaa za nyumbani.
Nguo za shule alizihifadhi vizuri kwenye sanduku na kuzifungia kabisa.
Moja kwa moja akaelekea jikoni ambako aliandaa chakula na kwa sababu ilishakuwa jioni aliamua kuandaa chakula cha moja kwa moja.
Yeye na mama yake walikula kisha cha baba yake alikihifadhi vizuri.
“Mama ni miezi mitano sasa unaumwa kwani tatizo ni nini lisilosikia dawa?”
Jioni hiyo Angel aliamua kumuuliza mama yake baada ya chakula cha jioni.
Alichokuwa anakijua Angel ni kwamba mama yake alikuwa ni mgonjwa ila hakujua alikuwa akisumbuliwa na nini?
Sasa leo aliamua kuuliza.
“Ooh! Vizuri mwanangu!
Umefanya la maana kuuliza, ili hata siku nikifa na watu wakakuuliza mama yako alikufa na nini uwe na jibu la kuwapa!”
“Kufa!!
Mama mbona sikuelewi?!”
Angel alitaharuki...
“Sijamaanisha ninakufa leo mwanangu!”
“Ila?”
“Mama yako nasumbuliwa na saratani ya kizazi.”
“Umesema?”
“Haijaanza leo ni ya muda mrefu na ndiyo maana hata kwenye uzazi imenisumbua mbaka nikakuzaa wewe peke yako!”
Angel alijikuta akiangusha machozi kwani katika sayansi huko shuleni tayari alikwisha kusoma mada zihusuzo maradhi sugu
ikiwemo saratani moja kati ya magonjwa hatari zaidi ulimwenguni...
“Mama unaumwa saratani?
Kwahiyo unakufa?
Je mimi nitakuwa mgeni wa nani?”
“Sitokufa mapema mwanangu cha msingi ni kukazana kufanya maombi tu!”
Mama alijitahidi kumliwaza mwanae lakini wapi.
Angel alishajua kuwa uyatima unamnyemelea sasa angekuwa mgeni wa nani?
Alilia sana licha ya mama yake kujitahidi kumbembeleza lakini wala.
Angel alilia sana mpaka usingizi ulikuja kumnyamazisha akiwa miguuni mwa mama yake pale pale sebleni.
Siku hiyo Mume wake Aneth hakurudi tangu alipoaga mapema kuwa alikuwa na safari ndogo lakini angerudi, lakini hakurudi.
Angel ndiyo alikuwa mtu wa kwanza kutoka usingizini, ikiwa ni siku ya pili...
Alikuja kugundua kuwa walilala sebleni na mama yake tangu jana jioni mpaka asubuhi.
Kitu cha kwanza baada ya Angel kutoka usingizi hakutaka kumsumbua mama yake kwa kumuamsha kwani yeye alikuwa bado amelala.
Hivyo alichokifanya ni kwenda jikoni kuandaa uji.
Lengo lake lilikuwa mama akiamka akute kila kitu kipo sawa.
Huko alikoka moto, na kupika uji safi wa lishe.
Ulipokamilika aliusogeza pale pale alipokuwa amelala mama yake.
Muda huo ilikuwa inakaribia saa moja kasorobo, mama huyo alikuwa bado amelala, jambo ambalo halikuwa la kawaida kabisa.
Hapo ndipo Angel akajipa jukumu la kumuamsha.
“Mama... Mama... Mama.. We mamaaa...”
Angel alimwita mama yake mara kadhaa huku akimtikisa lakini hata hakushtuka!
“Mmmh! Mama leo kalalaje tena?”
Angel alijiuliza huku akifikiria labda mama yake alizidiwa usiku?
Alimwamsha sana bila mafanikio mwishowe aliamua kuchukua jukumu la kwenda chumbani kwao kwenda kumgongea mlango
baba ake ili aje kuona hilo!
Cha ajabu kufika kwenye mlango wa chumba hicho alikuta kimepigwa komeo kwa nje kana kwamba ndani hakuna mtu.
“Ina maana jana baba hakurudi?”
Alijihuliza Angel wakati huo alikuwa amepata wazo la kwenda kuangalia kama chakula chake kimeliwa ili apate
uhakika kama alirudi au laa!
Uhakika aliupata kuwa baba ake hakurejea tangu aondoke jana kwani chakula kilikuwapo kama alivyokihifadhi mwenyewe jana jioni.
“Atakuwa alipata safari ya dharura ambayo imemfanya asirudi jana hiyo.”
Alijisemea moyoni Angel wakati huo akirudi tena mahali alipokuwa mama yake na kuendelea kumuamsha tena na tena bila mafanikio!
“Hivi mama kalala usingizi kwelii au?”
Alijiuliza Angel huku wasi wasi mwingi ukianza kumtawala moyoni hata akapata wazo la kusikiliza mapigo ya moyo
kama yalikuwa yanafanya kazi.
Wazo hilo hakutaka kulipuuzia...
Taratibu anasogeza kichwa chake na kukilaza kifuani kwa mama yake upande wa kushoto.
Baada ya kuhakikisha sikio lake limekita katika ziwa la mama, alitulia kwa muda kubaini kama kulikuwa na mdundo wowote!
Unaweza pia kusoma: