Angel - Sehemu ya Kumi na Nne (14)
“Kwani hupajui?”
Mmojawapo aliuliza huku akionekana kumshangaa...
“Hapana sipajui dada zanguni.”
Akajibu kwa sauti iliyojaa unyonge.
“Hata hivyo inaonekana hukuulizia tangu huko nyuma mbona umekwisha pita tena mbali kweli kuleeeee!”
Ayaaa!
Angel alikosa nguvu kabisa kwani sehemu aliyokuwa akioneshea yule mschana palikuwa ni kitambo kidogo kwa mwendo wa miguu
ulikuwa ni mwendo wa zaidi ya dakika 30 au zaidi.
“Asanteni sana mbarikiwe.”
Akajibu huku akianza kugeuka...
“Asante we ukifika mtaa ule ulizia watakuonesha nyumba yake.”
“Haya jameni siku nyingine panapo majaliwa.”
Wakaagana namna hiyo kisha Angel akaondoka na kugeukia usawa ule.
Hapo sasa alianza kuchapa mguu kweli kweli kujaribu kwenda na wakati uliokuwapo.
Angel alitembea kweli kweli yaani ndani ya dakika ishirini na upuuzi alikwishatia mguu ndani ya mtaa ule.
Hapo hakuzubaa tena aliulizia ulizia wakamwoneshea, bila kupoteza muda akanyoosha mpaka pale.
Kutokana na kutumia muda mrefu sana kuzurura baada ya kupotea, alimkuta shangazi yake Rebeca alikuwa amekwisha rudi na
walikuwa wakila chakula cha mchana na mfanya kazi wake wa ndani Agnes pamoja na watoto wake kasoro mumewe tu ndiyo hakuwepno.
Ile Angel kutia mguu mlangoni tu!
Alikutana na mjicho huo! Balaa!
Rebeca alimtizama Angel kwa macho makali zaidi ya sekunde arobaini bila kupepesa wala nini.
Hii iliashiria ni kwa kiasi gani alikuwa ameshikwa na hasira kwa kitendo cha Angel kurudi muda huo tangu asubuhi...
“Saa ngapi saa hizi?”
Rebeca alimtupia swali Angel, swali ambalo sauti yake ilikua imejaa ukakasi mno!
Angel alijikuta akikosa jibu la moja kwa moja na kujikuta akiishia kufikicha vidole tu.
“Ni saa saba kasoro.”
Angel alimjibu shangazi yake huku wasi wasi mwingi ukiwa umemjaa moyoni.
“Saa saba kasoro, enhe na hapa nyumbani mmeondoka saa ngapi?”
Akauliza Rebeca.
“Asubuhi.”
“Asubuhi ee? Unaweza kuniambia masaa yooote haya ulikuwa wapi?”
Kimya.
Angel alikosa jibu la moja kwa moja, hakujua aanzie wapi mpaka Rebeca amwelewe na kibaya zaidi Agnes
aliemuuza yeye karudi zake kitambo kwani yeye mwenyeji na anazijua njia za mikato hivyo baada ya kumaliza shughuli zake
akawahi kurudi.
“Angel wewe ni bubu?”
Rebeca alikuja juu baada ya kuona hajibiwi...
“Shangazi.. Aa.. Aaa......”
“Jibuuu! Puumbavu mkubwa wewe ulikuwa wapi?”
Rebeca aliongea kwa ghazabu huku akipiga meza kwa kiganja mpaka Angel akashtuka!
“Nilipotea!”
Angel alijibu kifupi huku akijitahidi kupambana na ile hali ya uoga uoga iliyokuwa imeweka makazi moyoni mwake.
“Ulipotea?”
“Ndiyo nilipotea njia wakati narudi hapa nyumbani.”
Rebeca akamgeukia Agnes mfanyakazi wake wa ndani na kumuuliza.
“Kwani we Agy hapa si mliondoka pamoja?”
“Ndiyo tuliondoka pamoja anti".”
“Sasa imekuwaje tena?”
“Anti mimi mwenyewe Angel alinitoroka bila kuniaga.”
“What? Angel ulikuwa wapi we mtoto?.”
Rebeca alianza kuwaka kama mbwa mwitu.
“Shangazi baada ya wewe kututuma sokoni ni kweli tulikwenda sokoni na tulifanikiwa kununua vitu
ulivyotuagiza lakini baada ya hapo Agnes alinipeleka sehemu nyingine ambayo mimi sikupendezewa nayo ndipo nikaamua
kuachana nae kwa lengo la kurudi hapa lakini kwa bahati mbaya nikapotea njia.”
Angel akajitetea hivyo...
“Uache kuongea uwongo mbele ya shangazi yako wewe!
Sema ukweli ulikokuwa na usinisingizie uwongo mimi.”
Agnes alimruka futi mia!
Yeye mwenyewe hakuamini...
Hao ndiyo watoto wa mjini bwana!
Rebeca baada ya kuona wanaanza kutupiana mpira hakutaka mabishano nao zaidi ya kukaa kimya huku akimwambia
Angel aende kuchukua chakula chake jikoni huko.
“Chakula chako kipo jikoni huko nenda kakichukue.”
Angel akaondoka huku akiwa kakumbata mikono yake kifuani.
Tayari alishaanza kumchukulia Agnes kama adui yake mkubwa asiepaswa kukaa nae karibu.
“Kwa hali hii yanipasa huyu mtu nitengane nae kabisa, atanisababishia matatizo Agnes siyo mtu mzuri hata kidogo.”
Alikuwa akijisemea yeye mwenyewe nafsini kwake.
Akafika mpaka jikoni, huko alikikuta chakula chake kwenyo hot pot kikiwa kimefunikiwa.
Angel hakuona haja ya kwenda Seblen tena mezani akaona ni vyema alie kule kule jikoni.
Basi akafungua zake hot pot na kuanza kukila chakula chake bila shida yoyote.
Mara! Mlango ukasukumwa!
Kugeuka, anakutana na Agnes nae alikuwa akiingia huko jikoni.
Angel yeye akaendelea kula wala hakushughulika kujua Agy kafata nini kule.
“Hebu wacha ushamba wa bush wewe uliona nani analia chakula jikoni?”
Agnes akaanza uchokozi.
“Agnes tafadhari sana niache na ushamba wangu sawa?”
“Hehehee halooo! Hebu nenda mezani huko achana na ushamba wa bush mi nataka kufagia huku.”
“Sasa kama ulikuwa unataka kufagia si ungeniambia tu kuliko kunidhihaki kiasi hicho Agy?”
Angel aliongea kwa sauti iliyojaa unyonge.
“Aha! Ulitaka nikunyenyekee kama mfalme ee? Hebu toka nenda mezani huko!”
“Umesema?”
Angel akasimama kabisa neno "Toka" lilimuuma vibaya mno aliona ni kama alitukanwa tusi la nguoni kabisa!
“Hivyo ulivyosikia ndivyo nilivyosema kwahiyo watakaje?
Sasa kama nakuambia unipishe nifanye usafi haunielewi wataka nikuambiaje?”
Bado Agnes aliendelea kujibu kwa nyodo na jeuri bila kujali kama Angel hakupendezewa na majibu na alikuwa
amebadilika sana usoni kwa kujawa na hasira.
“Agy tafadhari usitake ugomvi na mimi sawa?
Kuwa makini na majibu yako kama hujiskii kuongea na mimi ni afadhari ukakaa kimya.”
“Kwendraaa!
Nikukalie kimya ukiwa kama nani?
Bosi mwenyewe najibizana nae sembuse manzi kama wewe?”
“Mi manzi ee?....
Taaaaaaaaaas!
Uvumilivu ukamwishia Angel akajikuta akimtandika Agnes kofi zito lililonata vyema kabisa katika shavu la kulia la
Agnes mpaka chumba kizima kikapokelea daah!
Agnes akapandwa na mapepo.
Hakuamini kabisa kama Angel angekuwa na ujasiri wa kumpiga kofi la namna ile...
Aisee!
“Wee! Mtoto wa kahaba unanipiga mimi ee?”
Aliongea kwa ghazabu Agnes kisha bila kupoteza muda akarusha ngumi nzito kweli kweli akiwa ameikadilia ikampate Angel jichoni.
Angel akaiona!
Akaipangua ngumi ile kisha akamtumbukizia ngumi ya titi mpaka Agnes akaguna mmmh...
Make ngumi ilikubali kweli kweli...
Agnes hakukubali kabisa kupigwa na Angel, pale pale akaja na pigo jipya.
Kwanza alimuuza kwa kutishishia kumpiga kofi la sikio.
Angel alipotaka kulipangua kofi lile akajikuta akila ngumi saaafi ya pua mpaka akapiga chafya...
Huyu mwehu ni mtaalamu wa kupiga ngumi balaa!
Sijui kafundishwa wapi?
“Wee! Mtoto wa kahaba unanipiga mimi ee?”
Ile sauti ilijirudia kwenye kichwa cha Angel jambo lililompandisha balaa!
“Mimi ni mtoto wa kahaba?
Yaani huyu malaya anamwita mama angu kahaba?”
Angel alijiporomoshea maswali kibao kichwani kwake yaliyokosa majibu.
Wakati huo wakila kambaliga za hatari.
“Agnes unamwita mama yangu kahaba? Agy! Agy! Agy!”
Unaweza pia kusoma: