Muonekano wa Giza:

Msaada

Angel - Sehemu ya Kumi na Moja (11)

Vyombo vikaondolewa mezani na wale wafanyakazi wa ndani huku utambulisho ukifuatia.
“Angel.”
“Abee.”
“Huyu ni mume wangu, ambae ni mjomba wako anaitwa Patrick.”
Rebeca alimtambulisha mumewe kwa Angel, baada ya hapo akamgeukia mumewe pia.
“Patrick.”
“Naam mke wangu.”
“Huyo ndiyo Angel aliefiwa na mama yake, haya baba yake pia hajulikani alipo mpaka sasa kwahiyo mimi kama shangazi yake nimepewa jukumu la kuishi nae kama nilivyokuwa nimekuelekeza hapo awali.”
“Nashukuru sana kukufahamu Angel, jiskie kuwa huru hapa ni sawa na kwenu umenielewa ee?”
Wakapeana mikono.
“Asante sana Anko nashukuru sana.”
Baada ya utambulisho kwa mumewe kukamilika Rebeca aliwageukia na watoto wake na kusema.
“Secy, Asha, Lucy na Imani.”
Aliwaita kwa pamoja...
Nao wakaitikia kwa pamoja!
“Mnamuona huyu?”
Akauliza...
“Ndiyo mama tunamwona.”
Wakajibu.
“Anaitwa Angel, ni binamu yenu na tutakuwa tunaishi nae hapa sawa?”
“Ndiyo mama.”
Baada ya hapo akamgeukia na Angel pia.
“Angel.”
“Abee shangazi.”
“Hawa ndiyo watoto natumai unawajua.”
“Ndiyo shangazi ninawajua kwani umekuja nao mara nyingi sana kule mbeya kwahiyo nawajua vizuri tu.”
“Enhee na hao wawili ni wafanyakazi wetu wa ndani ambao wanatusaidia kazi ndogo ndogo za humu ndani, hapo kuna Bakari na Agnes.”
“Nashukuru kwa kuwafahamu.”
Akajibu Angel.
“Haya.. Hapa nafikiri kazi imekwisha ikiwa umechoka sana unaweza kwenda kulala.”
“Asante sana shangazi, ni kweli nina uchovu mwingi sana mwilini kwahiyo ninahitaji kupumzika.”
“Kumbuka kuoga, bafu lipo kwa upande ule kule.”
“Sawa.”

Angel akanyanyuka na kuwaacha wenyeji pale pale sebleni wakiendelea kuburudika kwa kuangalia season mbali mbali kwenye televishen baada ya chakula cha usiku.
Angel akanyoosha moja kwa moja mpaka bafuni.
Huko alioga na kisha kuelekea chumbani kwake alikofikia na kukabidhiwa kuwa ndiyo chumba chake atakachokuwa akilala.
Pindi Angel alipokanyaga mlangoni tu ile ndoto mbaya aliyoiota muda mfupi uliopita ilianza kujirudia kichwani kwake kama mkanda wa filamu ya kutisha.
Angel aliganda kwa mda pale mlangoni huku akihisi kuliona tukio lile laivu kwa jinsi ndoto lilivyokuwa ikitililika kichwani kwake bila mawenge ya aina yoyote.
Angel akavuta pumzi ndefu kisha akaishusha na kuingia ndani.
Akafunga mlango kwa ufunguo uliokuwa unaning'ia pale pale kwenye kitasa kisha akaondoka na ufunguo huo mpaka kitandani akauhifadhi sehemu aliyojiridhisha kuwa ni sahihi na asingeisahau pindi ambapo angekuwa akiuhitaji ufunguo huo tena.
Taratibu akatungua begi lake na kutoa makopo matatu ya mafuta na kuyaweka kitandani kisha akaanza kufungua moja akajipaka.
Aliporidhika na hilo akalifunga na kuliweka pembeni, akachukua lingine.
Hilo lilikuwa ni kopo lenye mafuta ya kudhibiti mwili kuvuja jasho nyakati za usiku hasa sehemu nyeti za mwili mfano makwapani na sehemu zingine zingine...
Baada ya kumalizana na hilo akalifunga na kuliweka kando.
Akachukua lingine tena, hayo yalikuwa ni marashi, akajipulizia pulizia mpaka pale yeye mwenyewe aliporidhika.
Baada ya hapo aliyarudisha makopo hayo begini na kulifunga kisha akalitundika mahali pake.
Mwisho akapanda kitandani na kuvuta shuka, usingizi mzito ukamchukua na kumsafirisha alfajiri...

Ilikuwa ni asubuhi mpya baada ya Angel kuamka.
Alijongea bafuni kuoga huku kichwani akiwa anafikiria kuwa siku ile ni lazima angepelekwa shule kama shangazi yake alivyokuwa amewaahidi bibi na babu yake alipokuwa kule Morogoro kuwa alitakiwa kufika Dar es salaam mapema sana ili akaendelee na masomo haraka sana.
Basi ndicho alichokuwa anafikiria Angel kuwa siku hiyo asubuhi anapelekwa katika shule aliyoandaliwa kuendelea na masomo.
Wakati Angel anatoka bafuni, baada ya kuoga aliitwa na Rebeca aliekuwa sebleni.
Bila kupoteza muda Angel alifika haraka kutii wito moyoni akitegemea kusikia habari njema.
“Ah! Umekwisha oga ee?”
Lilikuwa ni swali la kwanza kutoka kwa Rebeca baada ya Angel kufika mbele yake.
“Ndiyo shangazi nimekwisha oga.”
Akajibu.
“Vizuri... Sasa nataka niwatume sokoni. Hela hii hapa.. Nunueni samaki, mafuta, nyanya, vitunguu na mapochopocho mengine kibao mtakuwa na Agnes yeye atakuelekeza vile ambavyo vinahitajika na sijavitaja ili mnunue umenielewa?”
“Ndiyo shangazi nimekuelewa.”
Angel alijibu huku akili ikimkaa njia panda.
“Mimi ninakwenda kazini, kikapu cha kubebea mapochopocho kile palee.”
Akaongeza Rebeca na kunyayuka huku akiwa na mkoba wake akatokomea nje.

Angel akabaki hewani, alianza kujiuliza.
Sasa mbona habari ya mimi kwenda shule haigusiwi? Au muda bado?
Aaah wenda ni mapema ngoja nisubili kwanza shule nitaenda tu.
Angel alirudi kwanza chumbani kwake akaenda kujiandaa na kuvaa vizuri mpaka pale alipojiridhisha kuwa sasa anafaa kutoka nje machoni kwa watu.
Saa kubwa ya ukutani iliyokuwa chumbani kwa Angel ilikuwa inasoma saa 1:40 asubuhi.
Akazichukuwa zile hela na kuzikumbatia kwenye mkono wake wa kushoto kisha akatoka mpaka sebleni.
Akachukua na kile kikapu alichokuwa ameagizwa kukibeba kwaajili ya kwenda kubebea mapochopocho sokoni kisha akawa anatoka nacho.
“Angel.”
Mara akaitwa, haraka akageukia kule sauti ilikotokea.
“Abee.”
Akaitikia baada ya kumuona mwitaji ambae alikuwa ni Agnes aliekuwa chumba kingine lakini alikuwa akimtizama kupitia dirishani.
“Sasa unaniacha tena?”
Akauliza Agnes.
“Hapana nipo hapa nje we fanya upesi tu.”
Akajibu Angel.
“Sawa, ndiyo nipo navaa sasa hivi nipatie dakika tano.”
“Sawa nipo hapa nje.”
Akajibu Angel.
Angel akatoka mpaka nje.

Hakika kwa siku hii ya leo Jiji la Dar es salaam lilikuwa linapendeza sana katika swala la hali ya hewa Angel mwenyewe alipenda baada ya kutoka nje.
Siku hii kulikuwa na joto kiasi lililopumbazwa na upepo kwa umbaali.
Jua pia lilichoma kidogo na ikichangia ilikuwa bado ni asubuhi, basi jua lilipendwa na wengi sana mmojawapo Angel pia hata akatamani kuliota.
Wakati anaendelea kumsubili Agnes pale nje alijongea sehemu nzuri ambayo hakukuwa na kivuli.
Akajianika hapo na kuanza kuotea jua mpaka pale Agnes alipotoka.
“Twendezetu.”
Alisema Agnes na bila kupoteza wakati waliianza safari.
Kutoka pale nyumbani kwa Rebeca mpaka sokoni hapakuwa mbali sana hivyo basi walitumia dakika chache tu wakawa wamefika.

Sehemu 10 Sehemu 12
0
0