Angel - Sehemu ya Tisa (09)
Alijisemea Jr huku akijiweka sawa ili kumpa nafasi Angel alale vizuri begani kwake!
Safari ikawa inaendelea...
“Baba Angel amesafiri na basi gani?”
Aliuliza Rebeca kwa njia ya simu.
“Anakuja na NGANGA.”
“Amendoka muda muda”
“Saana... Yaani inabidi usogee stendi kabisa.”
“Sawa baba.”
Rebeca alijibu kisha simu ikakata.
Bila kupoteza muda Rebeca alianza kujiandaa ili kusogea Ubungo kwaajili ya kwenda kumpokea Angel.
Kitu ambacho hakikutakiwa kutokea kwa Angel ni kulala.
Angel hakutakiwa kulala kabisa lakini ndio hivo tena alijikuta analala mpaka anajisahau.
Wanaita ‘kulala fofofo’.
Ilifika muda usingizi umemkolea kisawa sawa, mdomo wake ukaachana kidoogo!
Saa ngapi macho ya Jr hajafika pande hizo?
“Mmmh! Mwanya?”
Jr alijisemea huku akichomoa foni upande mmoja ili aone vizuri.
Aisee...
Angel alikuwa na mwanya mzuri sana uliokuwa katika meno ya upande wa juu jambo lililofanya uso wake kupendeza mno.
Hasa pindi akitabasam.
Na hapo alikuwa akitabasam baada ya kuwa katika usingizi mzito sana wenye ndoto.
Jr akaendelea kumtalii mpaka pale alipolizika mwenyewe akaguna kimoyomoyo kisha akaendelea kuburudika na muziki mnene kupitia foni zake.
Mpaka wanakaribia Dar es salaam bado Angel alikuwa akiuchapa usingizi yaani ndiyo kwaanza hata dalili za kuamka alikuwa hana.
“Sasa kama atalala hivi mpaka ubungo si atachanganyikiwa pindi atakapoamshwa?”
Alijiuliza Jr huku akipiga hesabu ya kumwamsha.
“Angel... Angel... Angel... Angel…”
Aliita huku akimtikisa karibu mara nne ndiyo Angel anakuja kushtuka!
“Mmmh... Mmmh!!”
Aliguna guna huku akifumbua macho yake yaliyokuwa yamekolea kwa usingizi na kuwa mekundu kama nyanya.
“We! Unalala utafikiri upo chumbani kwako eti?”
Aliuliza kiutani.
“Angalia mpaka umevujia jasho kwenye bega langu!”
Akaongozea!
“Hee! Kwani nimelala kuanzia wapi?”
Aliuliza Angel kwa taharuki...
“Karibia Tanga kwa mbele uko.”
“Hee!”
“Yaah!”
“Loh! samahani kwa...”
“Usijali... Hakuna tatizo lolote.”
Alimkatiza kwani alijua anataka kuomba msamaha kwa kumpaka jasho begani kwake.
Angel akakosa neno na kukaa kimya...
“Nimekuamsha maana tunakaribia ubungo sasa!”
Akaongezea...
“Ubungo? Unataka kuniambia tumefika Dar es salaam sasa hivi?”
“Ndiyo!”
“Jr hebu wacha utani, mara hii tupo Dar? Hapana!”
“Lakini Angel nimekwambia nini, umelala muda mrefu hujanielewa!”
“Hata kama Dar saa hizi?”
“Eboo! Hebu tizama nje kwanza!”
Angel akaelekeza macho yake nje ambapo bila kutarajia alikutana na msongamano mkubwa wa watu magari na nyumba nyingi sana!
“Umeona?”
Akauliza Jr...
“Mmmh! Dar kweli hapa?”
Bado hakuamini...
“Ubungo sasa jiandae mama.”
Ooh!
Angel kusikia hivyo tumbo moto...
Alianza kujifikiria kama Rebeca atakuwa amefika kweli?
“Una uhakika mwenyeji wako atakuwa amefika?”
Yaani ile anawaza na kuwazua Jr nae akaulizia mule mule.
“Kufika atafika ingawa sina uhakika kama kwa sasa hivi atakuwa amekwishafika.”
Angel alijibu.
“Ungewasiliana nae kabla hatujafika ingekuwa vyema zaidi.”
“Ningefanya hivyo ila sina simu sasa.”
“Ah! Usijali, kama una namba yake nipatie!”
Akazidi kuchangamka huku akitoa simu yake.
“Hata namba yake sina pia...”
“Hee! Basi hakuna namna... Utamkuta au atakukuta kama anatambua basi unalosafiri nalo.”
Jr alijibu huku akirudisha simu yake begini akafunga zipu na kulibeba kabisa maana tayari walishakaribia ubungo
stendi kuu ya mabasi Dar es salaam.
Jr alifikiria sana ni njia gani angetumia ili kumpatia Angel namba yake?
Ukweli ni kwamba alitokea kumwelewa sana Angel lakini shida ilikuja jinsi ya kumwingia.
Angel alionekana ni mschana mchangamfu sana lakini kimwonekano alikuwa ni mschana mwenye msimamo mkali sana.
Jr alilitambua hilo kwa kumtizama mboni za macho, aligundua fika Angel hakuwa mschana wa kimchezo mchezo.
Mpaka wanaingia ubungo Jr hakuwa amefanikiwa kumpatia Angel namba yake kama alivyokuwa amedhamiria.
“Angel mimi nashuka!”
Jr aliaga baada ya basi kupaki mahala husika na abiria wote kuanza kushuka.
“Hata mimi pia!”
Angel alijibu huku akilishika vyema begi lake!
“Chukua namba yangu!!”
Jr alinong'ona kwa mbaali, kwanza Angel hata hakuskia chochote!
“Sasa we unashuka wakati hauna uhakika kama shangazi yako keshafika?”
Akauliza...
“Kama hajafika basi nitakaa katika ofisi za basi hili atanikuta hapo!”
Akajibu...
Angel na Jr wakawa wanashuka chini taratibu baada ya umati wa abiria kupungua ndani ya basi hilo.
Jr roho ilikuwa ikimuuma sana kwa kuona kuwa anaanza kuachana na Angel pasipo hata kumpa namba zake.
Roho ilikuwa ikimuuma vibaya mno.
“Angel... Nifanye nini uelewe kama nimekupenda? Hebu ntizame usoni kwanza mwenzako maini yanaungulia
kwa kuona tunaanza kuachana pasipo kukueleza kilicho ndani ya moyo wangu ingawa ni mapema mno lakini tambua
ya kwamba mapenzi ni hisia, na hisia hazizuiliki...”
Alijisemea kimoyo moyo Jr wakati huo wakimalizia kushuka ngazi ya mwisho na kukanyaga sakafu ya Ubungo!
Hayo yote aliyafikiria mwenyewe tu, Angel hakuwa na habari kabisa kwanza yeye ndiyo kwaanza alianza kuzitafuta ofisi
za kampuni ya Nganga ili apumzike hapo.
Kwanza alishamsahau Jr hakujua kama alikuwa ameendelea na safari yake? Au alikuwa akimfata nyuma?
Sasa kabla Angel hajafika kwenye ofisi alizokuwa akienda mara akashtukia akiguswa bega, haraka akageuka!
“Ahaa! Shangazi ni wewe?”
Kumbe alikuwa ni Rebeca.
“Ndiyo, sasa ulikuwa unaenda wapi?”
“Nilitaka kwenda kukaa kwenye ofisi za kampuni ya basi nililokuja nalo baada ya kuona we hauonekani.”
Akajibu Angel.
Unaweza pia kusoma: