Muonekano wa Giza:

Msaada

Angel - Sehemu ya Tatu (03)

Kufikia hapo hakukuwa na namna.
Ikizingatia Angel alikuwa ni mtoto wa pekee katika familia ya wanandoa hao ilitakiwa apate wa kumtunza baada ya mama yake kufariki na baba yake kutonekana tena.
Siku mbili baadae kilifanyika kikao cha kifamilia ili kujadili na kuafikiana kujua nini kifanyike na nani akaishi na Angel?
Mjadala ulikuwa mrefu sana.
Mwishowe wakaafikiana kuwa Angel aende kuishi na shangazi yake alieitwa Rebeca aliyekuwa akiishi Dar es salaam.
“Rebeka unakabidhiwa binti huyu, kamtunze na umpe malezi bora kama jinsi alivyokuwa akitunzwa na mama yake.
Iwapo kutakuwa na tatizo lolote usisite kutujuza.”

Ndugu mmoja ambae alikuwa ni mjomba wake Angel alisema...
Rebeka hakukataa alikubali kuondoka na mschana huyo kwenda nae Dar pia aliwaahidi wanandugu kuwa angekwenda kumuendeleza Angel kimasomo pamoja na ahadi zingine kem kem...
Basi baada ya maafikiano kikao kiliisha na wanandugu kuanza kutawanyika kurejea makawao kuanzia siku hiyo...

Angel pia aliambiwa aanze maandalizi kwani siku iliyofuata walitakiwa kusafiri kwenda Dar es salaam...
Rebeca alikuwa ni mwalimu wa secondary hivyo alikuwa na haraka ya kurudi Dar es salaam kuendelea na kazi.
Angel alianza maandalizi kwa kufua nguo zake pamoja na kuzipanga katika begi lake, pia aliweka sawa viatu vyake ikiwa ni pamoja na kuzifanyia usafi soksi.
Angel alikuwa na pea mbili ya viatu pamoja na soksi zake.
Sasa wakati yupo katika harakati za kufua soksi kuna kitu siyo cha kawaida aligundua katika moja ya pea ya soksi.
Hili lilijitokeza katika soksi zilizokuwa katika ile pea ambayo hakuvaa siku ile anakwenda shule, ambayo pia ndiyo ilikuwa ni mara yake ya mwisho kwenda shule.
Pia ilikuwa ni mara yake ya mwisho kuongea na mama yake.

“Kitu gani tena hiki?”
Angel alijiuliza huku akiingiza mkono ndani ya soksi kukitoa!
Ilikuwa ni karatasi iliyokuwa imekunjwa vizuri sana na kutumbukizwa katika soksi yake.
Angel alishituka sana na kujiuliza ni nani alieweka ile karatasi ndani ya soksi yake?
Jibu hakulipata!
Sasa ikabidi aikunjurue haraka haraka asome kilichoandikwa ndani yake.
Alikutana nacho!
Hakika yalikuwa ni maneno yaliyomwacha kinywa wazi mschana huyu pindi alipoanza kuyasoma!

Nayanukuu....

-HAKIKISHA USOMAPO HAYA MTU YOYOTE ASIONE-
Kilikuwa kama ndiyo kichwa cha habari, Haraka Angel aligeuka huku na kule kuona kama kulikuwa na mtu yeyote alikuwa akimtizama?
Hakukuwa na mtu yeyote.
Hata hivyo aliona haitoshi akaamu kukimbilia chumbani kwake ili akasome kwa uhuru zaidi...

Mimi ni baba yako mpendwa mwanangu Angel, samahani kwa haya unayokwenda kuyasoma!
Mama yako amekuwa ni mgonjwa kwa muda mrefu sana, amekuwa ni mtu asie na furaha muda wote kwa sababu ya maradhi yaliyokuwa yakimwandama.
Mimi baba yako nimehangaika nae kwa kipindi kirefu sana nafikiri wewe mwenyewe ni shahidi.
Nimehangaika mpaka kufikia hapa ninaweza kusema ni dakika za mwisho ambazo ndiyo dakika ambazo baba yako nimenyoosha mikono juu na kusalimu amri kwa maradhi kuwa nimeshindwa na yamenishinda.
Na sijashindwa mimi bali madaktari wameamua kuniambia kuwa mama yako siyo mponaji na bado kidogo afariki kwa sababu tayari hitlafu imefika sehemu mbaya sana ya mwili itakayopelekea mauti yake wakati wowote.
Baba yako siwezi kushuhudia mke wangu mpendwa niliempenda mpaka mwisho wa mapenzi yangu akate roho mbele ya macho yangi.
Hata mimi naweza kufa ni afadhari nikapumzike mahali kwanza, kuna baadhi ya ndugu zako wanatambua wapi nipo, na wao ndiyo watashughulika na mazishi ya mama yako, mi nitakuja kuliona kaburi lake tu.
Ishi salama mwanangu, nitasikia mahali ulipo na nitakufuata na kuja kukusalimu.
Nina imani utaishi vizuri kama ulivyokuwa mikononi mwetu.

-PIA HAKIKISHA KARATASI HII HAUMUONESHI MTU YEYOTE-

Huo ndiyo mwisho wa nukuu.
Angel alijikuta akishikwa na uchungu wa gafla moyoni machozi yake akashindwa kuyazuia kilio kikali kikamkumba alilia sana chumbani kwake mpaka pale hasira zake zilipokwisha ndipo akatoka kuendelea na kufua.
Sasa wakati anafua, shangazi yake akapita pale, sura yake ya huzuni haikuweza kumficha Angel mbele ya mtu yeyote alietizamana nae na asigundue kama alikuwa mwenye majonzi hivyo basi hata shangazi yake alimgundua ikabidi amuulize...

REBECA: “Angel...”
ANGEL: “Abee... Ant.”
REBECA: “Mbona kama hauko sawa vipi una tatizo?”
ANGEL: “Hapana! Ila tu mawazo ya mama yangu yananisumbua wakati mwingine.”
REBECA: “Pole na tambua wewe siyo mtu wa kwanza kufiwa.”
ANGEL: “Natambua hilo Anti lakini mimi kwangu ni too much...
Naachwa mimi kama mimi?
Sina hata mdogo wangu kweli?”
Angel alijibu huku machozi yakianza kujaa tena kwenye kope zake!

REBECA: “Pole na jitahidi basi usahau kwani ukiendelea kuyaweka mawazo hayo utakonda.”
ANGEL: “Ah! Nitajaribu japo nahisi kama moyo unawaka moto!”
Alijibu Angel huku akiendelea kufua baadhi ya nguo na soksi zake.
Wakati huo matone ya machozi yakimtoka na kundokea ndani ya beseni alilokuwa akifulia...
Hakika hakuna kitu kiumacho kama kufiwa na mmoja kati ya wazazi wako...

Siku ilipowadia Angel pamoja na Shangazi yake Rebeca waliondoka Mbeya kwa basi kuelekea Dar es salaam.
Lakini walipokuwa njiani Rebeca alipigiwa na baba yake ambae kwa wakati huo alikuwa amekwisha rudi Morogoro alikokuwa akiishi baada ya mazishi kukamilika kule Mbeya.
Alimpigia Rebeca na kumwambia kuwa alikuwa akimhitaji mjukuu wake Angel apitie kwake kwanza.
“Lakini baba mimi nina haraka sana kuwahi kazini, huoni kama nitachelewa?”
Rebeca alilalama kwenye simu.
Aliboeka sana na kitendo cha mzee huyo kuhitaji wao wapitie kwake ilihari tayari alikuwa amekata tiketi za moja kwa moja!
“Nimesema hiviii namhitaji mjukuu wangu apitie hapa!
We kama una haraka pitiliza!”

Mzee huyo aliongea kibabe kwa kutumia nafasi ya uzazi.
Rebeca hakuwa na jinsi alikubaliana na matakwa ya baba yake.

“Angel tutashukia Morogoro kwanza kwani babu yako anakuhitaji.”
Rebeca alimwambia Angel.
“Sawa Anti...”
Angel alijibu kwa sauti iliyojaa upole na unyonge...
Basi safari ikawa inaendelea na wakati huo walikuwa wanaitafuta Iringa.
“Halafu anti nasikia Iringa kumejengwa stendi mpya ya mabasi ni kweli?”
Angel aliuliza huku akijaribu kujitoa upweke.
“Ndiyo!”
Rebeca alijibu...
“Ni nzuri? Na inaitwaje?”
Angel aliuliza tena!
“Ndiyo ingawa bado ipo matengenezoni...
Inaitwa IGUMBILO TERMINAL.”

“Ahaa! Halafu pia nasikia hii barabara imepita nje ya mji huo?”
Bado Angel alizidi kujichangamsha!
“Tena mbaali sana... Kutoka huko ilikopitia mpaka mjini ni parefu unapanda bajaji.”
Rebeca alijibu.
“Sawa anti nimeelewa.”
Angel alikosa cha kuuliza ikabidi aishie hapo!

Safari ikawa inasonga ndani ya basi kuna nyimbo ilikuwa inapigwa mara kwa mara iitwayo ‘Mirros’ yake mwanamziki ‘Justin Timberlake’.
Hii nyimbo imekaa kihuzuni sana, ni nyimbo ambayo Angel alipoisikiliza kwa muda mrefu alijikuta akishikwa na sononeko moyoni mwishowe alianza kutokwa na machozi bila yeye kuwa na taarifa.
“Haaa.... Wewe nini tena!”
Rebeca alimshtua!
Halafu alishituka vibaya!

0
0