Muonekano wa Giza:

Msaada

Angel - Sehemu ya Saba (07)

Rebeca alisema kwa njia ya simu.
“Tutaangalia, na tutakujulisha.”
“Sawa baba.”
Maongezi ya simu kwa siku hiyo yakawa yamekomea hapo.
“Itabidi keshokutwa usafiri kwenda Dar es salaam shangazi yako Rebeca anasema amekwisha kuandalia shule.”
Aliongea babu yake Angel baada ya simu kukata.
“Sawa babu ila nitawakumbuka sana!”
Angel alisema.
“Ah! Sasa kwani unakwenda jumla?”
Bibi aliuliza.
“Hapana ila siwezi jua mambo ya shule inawezekana nisipate muda wa kuja huku tena.”
Angel alijibu.
“Hakuna kitu kama hicho! Likizo zipo.”
Babu aliunguruma!
“Sawa babu nitakuwa nakuja kuwatembelea siku za likizo.”
Angel akaunganishia kauli ya babu yake.

Siku iliyofata Angel alianza maandalizi ya safari ya kwenda Dar es salaam aliyotarajia kuifanya siku iliyofata.
Alifua nguo zake zote na kuzipiga pasi vizuri kisha kuhifadhi kwenye begi lake la nguo pia hata yeye mwenyewe alijiweka sawa kimwili mpaka pale alipojiridhisha kuwa sasa anafaa kukanyaga ardhi ya Dar es salaam kwani alikuwa anang'aa ng'ari ng'ari.
Angel siku hiyo kwake ilikuwa ni siku ya furaha sana kwake.
Naam alikuwa na furaha kubwa sana furaha yake ilikuwa ni kwaajili ya kwenda kuliona jiji la Dar siku iliyofuata.
“Eti babu kwani safari ya kutoka hapa Morogoro mpaka Dar es salaam ni masaa ngapi?”
Angel alimuuliza babu yake jioni ya siku ile ambayo alitarajia kuamkia safari.
“Inatokana na mwendo wa gari, siyo masaa mengi saana ni kati ya manne au matano.”
Babu alijibu.
“Sawa babu.”
“Mbona una furaha sana? Unafurahia kwenda Dar es salaam ee?”
“Saana babu yaani.”
Angel alijibu huku akiwa na fulaha kubwa sana moyoni.
“Hahaha, ni kuzuri lakini pia ni kubaya sana.”
“Ubaya wake nini babu?!”
“Hiyo ndiyo bongo mjukuu wangu kuna kila aina ya vishawishi nakusihi kuwa makini.”
“Kuhusu hilo usiwe na shaka kabisa.”
Angel alijibu kwa kujiamini kabisa.

Tiketi ya kusafiria Angel kwenda Dar es salaam iliandaliwa siku ile jioni.
Tiketi ilikatwa kwenye ofisi ya kampuni ya mabasi ya NGANGA EXPRESS na alitakiwa kuripoti tena katika ofisi za kampuni hiyo siku ya pili saa nne asubuhi.
“Mjukuu wangu sasa unakwenda kwenye uso wa Tanzania.”
Bibi aliyasema hayo, siku ile jioni wakati Angel analalia safari.
Ilikuwa ni baada ya chakula cha usiku.
“Una maana gani bibi kusema hivyo?”
Angel aliuliza huku usoni akionekana kuwa na tabasam pana mno.
“Usipokuwa makini utaishia kuwa changudoa na usijijue!”
Bibi alisema.
“Kweli kabisa mama Rebeca.”
Babu nae pia aliunga mkono point hiyo.
“Hapana babu na bibi ninawahakikishieni kuwa nitakuwa makini sana.”
Angel alisema...
“Yetu macho!”
Bibi alijibu kwa staili ya msuto flani hivi...
“Na pia usisahau kuja kututembelea pindi uwapo na nafasi.”
Babu nae aliongezea...
“Sitowasahau bibi na babu zangu, nitahakikisha nakuja kuwasalimia kila niwapo na nafasi.”
Angel alijibu huku akipekecha viganja.

Siku iliyofata ndiyo ilikuwa siku ya Angel kusafiri kwenda kwa shangazi yake Rebeca aishie jijini Dar es salaam.
Siku hii Angel aliamka mapema sana huku akiwa na furaha kubwa sana moyoni.
Alikuwa na shaukuu kubwa mno ya kuliona jiji hilo.
Yaani hakupata jibu kama angejisikiaje pindi atakapokuwa ndani ya Dar es salaam.
Bado hakupata jibu kabisa!
“Hivi nitajiskiaje pale nitakapokanyaga sakafu ya Ubungo?”
Angel alijiuliza wakati huo akiwa jikoni akiandaa chai.
Kuna muda Angel nywele zilimsisimka pindi alipofikiria kuwa kufikia saa sita angekuwa ndani ya gari akielekea Dar.

“Angel... Tunakupa wosia wa mwisho, kuwa makini na Dar es salaam unasikia wewe!”
Bibi alikuwa akimsisitiza pindi Angel amekwisha kaa mkao wa safari.
“Bibi nakuhakikishia kuwa ninakwenda kule kufuata kinipelekacho tu! Vingine vyote nitaviacha kama vilivyo.”
Alijibu Angel.
“Kumbuka! Wewe ndiyo ulikuwa mtoto wa pekee kwa mama yako, haya mama yako kafariki kwa maradhi, sasa watu wote tumeyaelekeza macho yetu kwako tunaangalia nini unakifanya?”
Bibi aliongezea...
Papo hapo Angel alikumbuka kitu.
Alikumbuka siku moja kabla ya kuondoka Mbalizi na shangazi yake Rebeca kuna barua aliisoma ambayo aliikuta katika moja ya soks zake.
Alikumbuka kuwa katika barua ile kuna mahali alisoma palikuwa pameandikwa kuwa baba yake alikua hai isipokuwa sehemu alipokuwa ndugu wengi hawakupajua ingawa siyo wote.
Pia alikumbuka kuwa kuna mahali paliandikwa kuwa yeye Angel angechukuliwa na mmoja kati ya ndugu na kuishi nae.
Ambapo baba yake huyo alimwahidi Angel kupitha barua kuwa siku moja angekuja kumtembelea huko.
Angel alipolikumbuka hilo alijikuta akiangusha machozi mbele ya bibi yake pasipo kutarajia.
Bibi kumuona mjukuu wake katika hali ile alitaharuki vibaya mo!
“Unalilia nini tena?”
Bibi aliuliza kwa taharuki huku akimsogelea Angel kwa karibu zaidi.
“Bibi kwani baba yangu yupo wapi?”
Aliuliza Angel huku machozi yakiendelea kumtoka...
“Aah!”
Bibi alidata na kujikuta akitoa sauti isiyo na maana yoyote yaani hakutoa neno lolote zaidi ya kusema 'Aah!'.
Hapo ndipo alipozidi kumtia taharuki mjukuu wake!
“Niambie! Mbona unababaika?”
Akamkazania.
“Yupo!”
Bibi alijibu...
“Yupo wapi?”
Akahoji.
“Hatujui alipo ila yupo.”
Bibi alijibu tena!
“Lakini bibi mbona umebabaika mwanzo?”
“Mjukuu wanguu... Baba yako yupo hai isipokuwa kasafiri kidogo na atarudi tu!”
Babu alidakia...
Angel aligeuza shingo yake na kumtizama babu yake.
Alijaribu kumsoma usoni kuona kama kile alichozungumza kilikuwa cha kweli au alikuwa anamraghai?

Sehemu 6 Sehemu 8
0
0