Angel - Sehemu ya Tano (05)
Babu alimuuliza mjukuwe huku akiwa kakaa stairi ya kuinama akimtizama usoni.
Angel alijibu kwa kutikisa kichwa akimaanisha ameelewa.
“Vizuri, sasa nakushauri hakikisha muda wote ukaokuwa ndani ya Dar es salaam usifuate ushauri wa mtu yeyote
zaidi ya huu ninaokwenda kukupa.. Tupo pamoja?”
“Ndiyo! Babu tupo pamoja!”
Angel alijibu.
“Cha kwanza! "Mapenzi" hakikisha hujihushi kimapenzi kivyovyote vile mpaka utakapotimiza miaka 26!”
Angel alishituka!
Mshtuko ambao haukuweza kujificha mbele ya macho ya babu na alimgundua vizuri tu sema akapotezea!
“Pili, Hutakiwi kuwa na marafiki hewa, wanafiki na wasio na msaada wowote kwako hata wa kimawazo!”
“Tatu... Anza kubuni njia sahihi za kujikwamua kimaisha...
Nasema njia sahihi na siyo haramu nafikiri umenipata!”
“Nimekupata vizuri kabisa... Lakini nina swali.”
“Karibu!”
“Umesema nisijihusishe kimahusiano mpaka nitimize miaka 26...
Sasa ikitokea kuna mwanaume anataka kunioa nikatae?”
“Najua unauliza swali hilo pasipo kujitambua!
Kwanza sasa hivi una miaka mingapi?”
“Nina miaka 13!”
“Mpaka utimize miaka 26 na utakapoanza mahusiano na kijana yeyote ni lazima uje kumtambulisha hapa sawa!”
“Ndiyo! Babu.”
“Vizuri kwa kunielewa...
Dare es salaam kuna kila aina ya ukatili hasa kwa watoto wa kike kama wewe ambae tayari ni yatima na ndiyo maana
nimekuita hapa kukupa mbinu kadhaa ambazo nina imani zitakusaidia katika kipindi hiki ambacho kwako hakifai kabisa!”
“Nashukuru kwa kunipa mawazo haya mazuri babu yangu sitoacha kukushukuru.”
Angel aliongea kwa sauti ya upolee!
“Na ndiyo maana nilitaka mjukuu wangu upitie hapa!
Natambua kabisa hakuna aliekwambia chochote kuhusu Jiji la Dar es salaam na wakazi wake!”
Mzee aliendelea kumwaga sera hapo, mara vikombe viwili vya kahawa vikaletwa hapo na mfanyakazi wa ndani wa nyumba hiyo.
Waligaiwa pale babu na mjukuu wake na kuanza kuinywa kahawa hiyo taratiibu.
Basi taratiiibu waliendelea kunywa kahawa huku wakiendelea kuhadithia mambo mbali mbali hususan
yahusuyo maisha na kadhalika.
Angel alifurahia sana mazungumzo yale kwani yalimpa mwanga fulani katika maisha yake.
Alipata kujua mengi ambayo hakuwa akiyajua.
Naam alipata kufunguka kwa namna moja au nyingine.
“Babuu.”
Angel aliita huku usoni akionekana wazi kuwa na swali.
“Naam mjukuu wangu!”
Babu aliitikia huku akitabasamu...
“Unalima sana nini?”
Aliuliza huku akicheka!
“Mmmh!! Kwanini?!”
Alihoji babu.
“Naona mwili wako siyo wa kizembe kizembe!”
Alisema Angel huku nae akijitikisa tikisa!
“Hahahaha.... Ooh! Yawezekana pia! Lakini kumbuka kulima si sababu ya mimi kuwa strong!”
Babu alicheka saana mpaka na “Mapengo” yakatokeza nje!
Kisha ndiyo akajibu!
“Ila?”
“Nafanya mazoezi sana!.”
Hatimaea Babu alijibu swali la mjukuwe!
Hapo ndipo Angel akakumbuka siku za nyuma kidogo kabla matatizo hayajamkumba, wakati alipokuwa akisoma darasa la tano.
Alikumbuka siku moja mwalimu wake wa Sayansi alivyokuwa akifundisha kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi kila siku.
Angel alikumbuka mengi sana mpaka akajikuta akitoka kabisa katika ile mudi ya hadithi walizokuwa wakihadithia na babu yake.
Ilikuwa yapata saa 12 jioni muda ambao bibi yake pia alirejea kutoka sokoni.
Nae pia alifulahi sana kumuona mjukuu wake Angel, alifurahi sana!
“Ooh! Mjukuu umekuja wewe!”
Bibi aliongea kwa hamasa!
“Ndiyo! Bibi yangu leo nipo kwako!”
Angel alijibu huku akitabasamu..!
“Hehehe!! Karibu ule mchele wa Morogoro!”
Bibi aliongea hayo pasipokujua kama alikuwa akimtoa mate mjukuu wake!
“Bibiiii... Mambo gani tena haya! Ujue wali nilikulaga sijui toka christmas!”
Angel alisema!
“Christmas? Heee! Basi leo wala mpaka uvimbiwe!”
Bibi alizidisha utani...
Angel akabaki akiugulia na kimuhe muhe cha kutaka kula tena wali kwa mara ya kwanza baada ya ukame wa kipindi kirefu
pasipo kula chakula hicho.
Basi bibi akaelekea zake jikoni huku akiwaacha Angel na babu yake nje wakiota moto kwenye karai kwani tayari usiku
ulishaanza kubisha hodi.
Wao waliendelea kuhadithiana mambo mengi sana!
Babu alianza kumuhadithia mjukuu wake mambo ya kale kidogo yaliyohusu maisha, wanyama, mazingira na kadharika.
“Babu umesema kwamba zamani hakukuwa na simu, wala barua, je mlikuwa mnapatanaje?”
Mada hiyo ndiyo mada iliyomkaa vyema Angel kichwani, hata akajikuta akitamani kuipatia maelezo zaidi.
“Ilikuwa kazi sana! Tena saaana! Ndiyo!
Unaweza penda na usimpate tofauti na sasa!”
“Kwanini?!”
Angel alihoji huku akikunja nne vizuri.
“Yaani enzi zile madomo zege walikuwa wanateseka sana!
Kwani mwanaume asipokomaa na maneno hapati kitu!”
Angel alicheka saanaa! Kisha akauliza...
“Halafu nasikia waschana wa enzi hizo walikuwa wagumu?!”
“We! We! We! Acha kabisa! Mwanaume akienda pupa ataoga matusi mpaka aloe!”
Mzee alitia fora hakika kwa Angel hata upweke ulimtoka!
“Uwii matusi tena?”
Alihoji Angel, huku moyo wake ukidunda dunda kwa furaha.
“Ayaa!! Unauliza hayo tena?! Mbona ilikuwa kawaida?”
Babu alijibu kwa staili ya kuchekesha mno!
“Hahahahaaa!! Babuu asa na wewe uliwahi kutukanwa?!”
“Siyo Kutukanwa tu! Yaani nilienda kuchongewa nyumbani...
Yaani nilikula kipigo cha mbwa! Mwizi.”
Dooh!
Angel alicheka saaanaa!!
“Ee!! e! e! We baba nanii... Rebeca utanivunjia mjukuu wangu mbavu huko!”
Ooh!
Bibi alitia nuksi soga za babu na mjukuu!
“Wee! Nae mama Rebeca nini huko?!”
“Hebu mje kula huku.”
Anhaa! Kumbe chakula kilikuwa tayari na ndiyo maana bibi huyo aliamua kuja kutia doa mazungumzo ya babu na mjukuu ili tu wakale.
Ilikuwa yapata saa mbili kasoro dakika kumi, usiku.
Angel na babu yake wananyanyuka na kuelea mezani kupata chakula cha usiku.
Dakika kumi na tano zinawatosha wao kutosheka kula bibi anainuka na kutoa vyombo mezani huku akisaidiana na mjukuu
wake Angel na kuvihamishia sehemu iliayopaswa.
Walirudi tena mezani na kuendelea kuzungumza mawili matatu ikiwemo maswali kadhaa ya bibi kwa mjukuu wake kuhusu safari na kadharika.
Baada ya mazungumzo hayo kufika tamati wanatawanyika kwenda kulala huku Angel akiwa kaoneshwa chumba chake.
“Kokolikooo!!!!”
Kelele za jogoo kuwika zilimtoa Angel usingizini...
“Kumekucha!”
Alijisemea Angel huku akijinyoosha nyoosha kitandani.
Sasa wakati akiwa katulia zake kitandani wakati huo akipiga mahesabu ya kuinuka ili avae masikio yake yalinasa
sauti za vishindo nje!
Vishindo hivyo vilikuwa vikibadili stairi kila wakati.
Kuna muda vilisikika kama mtu anakimbia!
Pia kuna wakati vilisikika kama mtu anaruka ruka lakini pia wakati mwingine vilisikika kama kitu kizito kikidondoshwa chini.
“Kitu gani tena hicho?”
Angel alijiuliza huku akiwa bado kalala chali kitandani kwake!
Mara! Akiwa bado anajaribu kusikiliza kwa makini vishindo hivyo kubaini ni kitu gani mlango wa chumbani kwake ukagongwa!!
“Ngo! Ngo! Ngo! Ngo! Ngo! Ngo!”
Mlango uligongwa mara sita mfululizo!
“Mmmh! Nini tena?”
Angel alijiuliza kimoyo moyo huku akiogopa kabisa kutoa sauti.
“Ngo! Ngo! Ngo! Ngo!”
Mlango uligongwa kwa mara ya pili safari hii mgongaji aliongeza nguvu kidogo katika ugongaji hii ni baada ya kuona mwanzo hakujibiwa!
“Mungu wangu! Nini hiki?”
Angel alianza kuhaha huku mapigo ya moyo yakianza kupanda kasi kila sekunde!
Unaweza pia kusoma: