Muonekano wa Giza:

Msaada

Angel - Sehemu ya Ishirini na Moja (21)

Rebeca alishtuka na kutoa goti kwenye kifua cha Angel huku macho yake akiwa kayaelekeza huko dirishani.
Kosa kubwa sana alilifanya Rebeca kwa kumsikiliza Angel...
Si kumbe alidanganya tu?
Alipotoa goti tu!
Haraka sana akainuka kwa Kasi ya ajabu huku akifanya tukio jingine la kumtandika John teke la sehemu za siri.
Rebeca anashtuka!
Akapewa ya uso mpaka giza!
Hapo sasa Angel akachachamaa kama mbwa mwitu!
“Hivi kumbe we kabinti kamalaya ee?”
John alikasirika sana kwa kupigwa teke la aina ile.
Alitamani hata kumuua Angel kwani maumivu aliyokumbana nayo hayakuvumilika kabisa!
Akataka kuiokota bastola yake, hata hivyo alishindwa kwani Angel alimwahi na kuiokota kisha akaitupa nje kupitia dirishani.
“Ku***ko umerudia tena?”
John akazidi kuwaka kama mbogo baada ya silaha yake kutupwa nje kwa mara nyingine tena!
Akarusha kofi zito alilolikadiria kumpata Angel sikioni...
Lakini Angel akawahi kuliona akalitolea nje kwa kulikwepa!
John hakukubali...
Akatuma lingine ambalo pia alilikwepwa!
Hakukubali pia!
Mtoto mdogo kama huyu amsumbue?
Akajikusanya tena huku safari hii akiwa amepanga kumchanganya na makofi mawili ili akikwepa moja lingine limpate...
Mara simu yake ikaita!
Doh!
Mipango yake ikaenda mrama, ikabidi apokee kwanza simu...
Akaiokota na kuipokea.

“Hallo!”
“Mr John.”
“Naam... Kiongozi.”
“Upo wapi? Kuna dili huku.”
“Dili gani hilo?”
Akauliza John huku akisogea pembeni zaidi.
Inaonekana kuna ishu nzito ilitarajiwa kuzungumzwa na huyo mtu wa upande wa pili.
“Kuna jiwe kubwa la Tanzanaiti limeibwa mererani sasa limeletwa Moshi.
Hawa jamaa wanataka kulipwa bilioni tatu pointi mbili njoo tulichukue mtu wangu.”

“Jiwe la Tanzanite? Lina ukubwa gani?”
Akauliza John huku akihaha.
“Sikiliza nikwambie... Hili tukilipeleka Cape Town tunaliuza pesa nyingi sana si chini ya bilioni kumi.”
“Wee!”
“Nakwambia.”
“Ok! Kwahiyo nini kiendelee?”
“Inatakiwa uje moshi mara moja.
Hawa jamaa tuwakatie chao, halafu na sisi tukate tiketi ya kwenda South Africa usiku huu huu kabla msako haujafika huku maana nasikia msako ulioko huko Arusha siyo wa nchi hii.”

“Ok sawa nimekupata... Nakuja.”
Simu ikakata, pale pale John akaanza kuvaa nguo zake haraka haraka.

“Sasa John...”
“Sikiliza Rebeca nimepata dharura ya kwenda sehemu na ni muhimu sana mimi kwenda, samahani kwa hilo.”
Akajibu John huku akifunga vyema mkanda wake.
Mmmh!
Rebeca sasa alianza kuingiwa na wasiwasi.
“Ninakwenda na nitarudi tena.”
John alimalizia kusema hayo kisha akaokota simu yake na kuondoka humo chumbani kwa mwendo wa haraka haraka kama mwanajeshi anaecheza gwaride.

Baada ya John kuondoka sasa!
Angel alimtizama Rebeca kwa macho flani hivi yasiyotabirika kwa muda usiopungua dakika tano!
Halafu baadae akayahamishia macho yake dirishani akawa anatizama nje gizani kupitia dirisani.
Wakati huo ukimya wa kutisha ukiwa umekitawala chumba kizima tangu John aondoke.

Alitizama nje kwa mda mrefu yaani kwa dakika zisizopungua mbili na sekunde zake.
Wakati huo Rebeca nae akiwa katulia tuliii kama hakuwepo vile.
Mwishowe Angel alirudisha macho ndani ya chumba na kumtizama Rebeca usoni ambapo alikutana na macho ya kikatili mno!
“Mmh!”
Angel aliguna kimoyomoyo kisha akapiga hatua kadhaa mbele na kulifikia begi lake lililokuwa linaning'ia ukutani.
Akalitungua!
Taratibu alitoa modo yake flani hivi ya mpira na kuivaa.
Wakati huo Rebeca akimtizama tu!
Akatoa T-shirt flani nyupe na safi kabisa ambayo kifuani ilikuwa na logo yenye maneno yaliyochorwa AS Kwa ustadi wa hali ya juu.
Akaitia mwili nayo ikamnata vyema kabisa!
Bado Rebeca aliendelea kumtizama tu, sijui alikuwa anafikiria nini?
Angel akavuta raba zake flani hivi za kufunga na kamba.
Akazitia miguuni na kuzifunga vyema kabisa.
Mwisho...
Akafunga begi lake lililokuwa na nguo kadhaa kisha akalitia mgongoni.
“Shangazi kwaheri.”
Alisema hivyo Angel huku akianza kupiga hatua za taratibu kueleka mlangoni.

“Wee! Hebu simama.”
Rebeca akanyanyuka kitandani kabisa.
Angel akasimama na kugeuka nyuma.
“Unaenda wapi?”
Akauliza Rebeca kwa ukali.
“Hupaswi kujua...
Na usitake tujibizane na wewe kwa sababu nina hasira sana na wewe...
Nakuchukia sana shangazi nitakuumiza bure niache niende.”

Akaongea Angel kwa ghadhabu mno.
“Usinitanie rudi huku.”
“Shang........”
Akamkatiza.
“Nimesema rudi huku we paka naona unataka kunipanda kichwani kumbe.”
Rebeca alizidi kufoka.
“Sirudi.”
Angel akapinga makusudi ili kuamsha ugomvi.
Ni kweli...
Rebeca alichukizwa sana na kauli ile, akajikusanya mazima kwenda kumvaa Angel.
Aloo! Akamkwepa...
Duuh!
Rebeca alikwenda kujigonga vibaya sana mlangoni huku nyuma Angel akatupa begi kitandani.
Rebeca akageuka huko na kuja akiwa amewaka kama mbogo!
Alipokelewa na teke saafi la kwenye kitovu lililomrudisha kinyume nyume mpaka akaenda kukita ukutani.
“Jumaaa! Jumaaa! We Jumaa!”
Rebeca alianza kuita hivyo kwa nguvu pindi akiwa kaegemea ukutani.

Dakika moja tu zilisikika hatua za mtu akija huko chumbani.
Bila shaka huyu atakuwa ni mlinzi wa usiku wa nyumba hiyo na inavyosadikika ni polisi kwani hatua zake zilibainika ni mtu alievaa buti za uhakika.
“Wapi?..wapi..wapi..wapi.”
Ilisikika sauti ya mwanaume huyo akiuliza kwa sauti huko sebleni, sauti yake ilijirudia rudia mara kadhaa kutokana kuakisiwa na jumba hilo.
“Hukuuuuu!!”
Rebeca akaitikia...
Wakati huo Angel akiwa anashangaa shangaa asijue nini afanye...
“Kuu! Kuu! Kuu! Kuu! Kuu! Kuuu.”
Zilisikika hatua zikija namna hiyo.
“Nimekwisha mimi.”
Angel alijisemea kimoyo moyo huku akitafakari cha kufanya kabla mambo hayahajaribika.
“Ngo! Ngo! Ngo! Ngo! Ngo!”
Hatimae mlango unagongwa kwa fujo kweli kweli.
Juma huyo hapo!
Angel akaona hapana, akakwapua begi lake na kupita nalo dirishani kisha huyoo akatua nje na kupotelea gizani...

Sehemu 20 Sehemu 22
0
0