Muonekano wa Giza:

Msaada

Angel - Sehemu ya Kumi na Mbili (12)

Yaani kwa jinsi soko lilivyokuwa limechanganya Angel alijikuta akianza kuogopa kuingia maana ake hili lilikuwa ni soko la uhakika na siyo kigenge.
Ndani ya soko kulikuwa na kila aina ya watu, wakubwa kwa watoto, mavuta bangi ambao walikuwa ndiyo makuli walikuwa mule.
Aisee kwa jinsi soko lilivyokuwa limefurika watu ilikuwa ni zaidi ya mzinga wa nyuki.
“Twende wewe mbona unaanza kubaki nyuma?”
Agnes alimuuliza Angel baada ya kuona mwendo umepungua.
“Wewe mi naogopa!”
Akajibu Angel kwa aibu...
“Unaogopa? Hebu wacha masihara basi.”
“Walai vile ninaogopa sana.”
Akazidi kusisitiza.
“Sasa kigeni cha kukutisha hapa ni kipi?”
“Watu, ninaogopa sana watu.”
“Hivi Angel.”
Agnes aliita huku akirudi nyuma na kumsogelea zaidi.
(Huku akimtizama usoni) “Hivi unataka kuniambia ya kwamba ni kweli unaogopa watu au?
Hebu niambie huko kwenu ulikuwa unaishi vipi?
Hakukuwa na watu? Au haukuwahi kwenda masokoni?”

Agnes alihoji kwa msisitizo zaidi.
Angel akajibu.
“Siyo kwamba kule nilikokuwa naishi hakukuwa na watu, hapana isipokuwa sehemu kama hizi sijawahi kutia mguu.”
“Ahaa! Twende sasa... Uache ushamba utaniaibisha twende mwaya.”

Akamshika mkono kisha taratibu wakawa wanaelekea ndani ya soko hilo.
Muda wote Angel alikuwa siyo mtu wa kujiamini.
Alikuwa ni mtu mwenye wasiwasi mno hakuwa na amani kabisa kuwa ndani ya umati mkubwa wa watu namna ile.
Ni halali Angel awe hivyo kwa sababu ni mtu ambae alizaliwa vijijini na kukulia huko huko.
Shule alianzia kusoma huko huko vijijini, kiufupi Angel tangu anazaliwa kule Rujewa, Mbeya vijijini hakuwahi kukanyaga mjini.
Dar es salaam ndiyo jiji lake la Kwanza kukanyaga mjini na kuingia sehemu za umati kama zile.
Kwahiyo kiufupi ni kwamba hakuwahi kutembea katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu wa kila aina kama sehemu aliyokuwa ametembelea siku hiyo.
Kwahiyo ilikuwa ni halali kwake kuwa katika hali ile.

Wakaingia ndani ya soko ambapo kulikuwa na kila aina ya vyakula, matunda, viungo, mboga na kadharika.
Agnes alianza kutaja mahitaji muhimu waliyotakiwa kununua hapo sokoni huku mlipaji akiwa ni Angel sababu yeye ndiye aliepewa pesa ya kununulia mahitaji hayo.
Baada ya muda wakawa wamekamilisha kila kitu...
“Kuna kingine anti kakuagiza zaidi ya hivi?”
Aliuliza Agnes ili kuhakiki kama wamekamilisha mahitaji yote muhimu kabla ya kutoka sokoni hapo.
“Hakuna cha zaidi alichoniagiza, kama mahitaji muhimu ya jikoni yamekamilika basi hakuna cha zaidi.”
Akajibu.
“Umebakiwa na shilingi ngapi?”
Akauliza Agnes.
“Elfu sita.”
Akajibu Angel.
“Sasa hiyo twende tukaile tu.”
“Wewe Agy mimi sijaambiwa hivyo bwana, turudishe hela ya watu.”
“Acha ushamba wewe... Anti hana noma na vichenji kama hivi twende tukale sambusa bwana.”
Agnes alizidi kumshawishi mwenzake waende wakaitumie kwa kuila ile chenji iliyokuwa imebaki.
Huku akimwaminisha Angel kuwa shangazi yake hanaga time na vichenji kama hivyo.
“Agy usije ukaniingiza mjini bila viatu wewe?”
“Hapana ni uoga wako tu! Lakini kile nikwambiacho ndivyo ilivyo Angel.”
“Mmh...”
Aliguna Angel.
Ukweli ni kwamba Angel moyo ulikuwa unasita kufanya kile Agnes alikuwa akimshauli kwani anatambua fika mchezo wa kula chenji zilizobaki kwenye ununuzi wa mahitaji unakuwaga siyo mzuri.
“Twende wewe acha kuguna...
Hivi Angel kwa akili yako unafikiria kabisa Rebeca anaweza kuvifuatilia vijisent hivyo?”

“Agy! Samahani… Pesa ni pesa tu! Kwahiyo hata iwe ndogo kiasi gani lakini thamani yake haipungui upo?”
“Ah! Hebu wacha kuwa mshamba kiasi hicho…
Skia hivi ulishawahi kula pilau la pwani ya bahari ya hindi?”

“Pwani ya bahari ya hindi?”
Angel alijibu katika mtindo wa swali huku na taharuki ikiwemo.
“Sasa sikia hilo pilau linakuwaga tamu hilo achaaa...
Mbona utakula na vidole nakwambia!”

“Acha uongo!”
Taratibu Angel alianza kuingia laini mwenyewe.
Kwa maana hio porojo aliyoitumia Agnes sijui alisomea wapi?
Jaman.
“Twende ukaonje.”
Agnes akasema.
“Ah! Ila chenji za watu hizi Agy.”
“Angel.. Hebu kuwa mjanja basi, kuwa mtoto wa mjini mambo ya kibush vua.”
Agnes akasema huku akimshawishi kwa kumshika mkono na kujaribu kuondoka nae.
Akamfuata!

Angel msimamo wake ukawa umeishia pale moja kwa moja wakatoka sokoni pale na kuanza kufuata barabara flani iliyokuwa ikielekea mahali ambako Angel hata hakujua ilikuwa inaelekea wapi?
Lakini Agnes aliongoza huko na yeye alimfuata tu nyuma nyuma.
Wakakaribia sehemu moja ambapo kimwonekano palikuwa ni pazuri mno.
Kulikuwa na nyumba nzuri sana ambayo kwa nje kulikuwa na bustani yenye maua mchanganyiko na yatunzwayo vyema kwa kumwagiliwa na kuyafanya yang'ae na kupendeza sana.
Angel alishituka akauliza...
“Sasa Agnes ndiyo tunaenda wapi huku?”
“Usiwe na shaka.”
Agnes akajibu kifupi huku akizidi kusonga mbele kuikaribia zaidi nyumba ile.
Angel na hakuwa na jinsi zaidi ya kumfuata mpaka wakakaribia mlangoni mwa kuingilia ndani ya jengo lile.
Ndani ya jengo lile kulikuwa na watu wengi sana vile vile kulikuwa na burudani ya muziki.
“We Agy...”
Angel aliita lakini akasita kusema kitu baada ya kumuona Agnes akitoa simu yake kisha akaipalaza palaza na kuiweka sikioni.
Ilikuwa ni smartphone na ilionekana kuna mawasiliano alikuwa akitaka kuyafanya.
Angel akabaki kimya huku akimtizama.
“Hallo! Baby nipo hapa nje!”
Agnes aliongea maneno yaliyomwacha kinywa wazi Angel pindi simu ilipokuwa imepokelewa.
“Sawa nakungoja hapa hapa.”
Akajibu tena, ni wazi maongezi yao mafupi yalifika tamati, lakini Angel hakuweza kumsikia huyo wa simuni kwahiyo yeye alimsikia Agnes pekee.

Baada ya Agnes kumaliza maongezi yake na kukata simu Angel alimuuliza.
“Agnes nilichokisikia hapa ndicho ulichokizungumza hapa au?”
(Huku akibinua mdomo kwa kejeli) “Ndiyo nilichokizungumza kwani kuna kipi kigeni hapo?”
“Agy tafadhari nipatie hicho kikapu mi niende nyumbani.”
“Sikia... Huu ni mgahawa sawa? Mimi nitakuja kuchukuliwa na mchumba wangu hapa naenda kula vitamu huko ndani kwa hiyo we tumia hiyo chenji wala hakuna tatizo.
Lakini ukitaka mwanaume wa kukulisha huko ndani wako kem kem, unaweza chagua mmoja na mambo yakawa poa tu.”

Agnes alizungumza maneno yaliyomkata maini Angel yaani hakutegemea kabisa kama Agnes angekuwa ni mpuuzi kiasi hicho.
“Anaenda kudanga?
Kwani alichokikosa haswa ni kipi?
Mshahara hapewi?
Chakula hali?
Au tatizo ni nini?”

Angel alizama katika lindi kubwa la mawazo lenye maswali lukuki yasiyo na majibu.
“Angel.”

Sehemu 11 Sehemu 13
0
0