Muonekano wa Giza:

Msaada

Angel - Sehemu ya Nne (04)

“Ee...e..ee.. Tumefika anti?!”
Angel alijikuta akibabaika na mwisho akajishitukia akiuliza swali bovu kabisa!
“Unaota? Kwani nimekwambia Dar. tunafika saa ngapi?”
“Saa 12 Jioni.”
Angel alijibu.
“Na sasa hivi saa ngapi?”
Rebeca alimswalika!
Angel hakuwa na jibu zaidi ya kuinua mkono wake wa kushoto na kutizama saa yake ya mkononi.
“Saa 3:25 asubuhi.”
Alijitamkia yeye mwenyewe moyoni huku akirejesha mkono wake mahali ulipokuwa awali.
“Anti ni saa tatu na dakika ishirini na tano asubuhi.”
Angel alisema...
“Sasa ndio tufike sasa hivi? Iringa yenyewe bado.”
Rebeca aliongea.
Angel akakaa kimya, wakati huo basi walilopanda likielea barabarani acha kabisa!

Mnamo majira ya saa 4:10 walitimba ndani ya Igumbilo Terminal bus, Iringa.
Ilikuwa ni stendi nzuri sana ingawa ilikuwa bado haijakamilishwa lakini kwa sehemu ilipokuwa imefikia kimatengenezo hakika ilikuwa inapendeza sana!
“Hii ndiyo stendi ya Iringa!”
Rebeca alisema, akimwambia Angel...
“Panapendeza japo ni pembeni sana na mji.”
Angel alijibu huku akitabasamu.
“Ndiyo inavyotakiwa...
Stendi kubwa za mikoa ni lazima ziwe nje kidogo ya mji.”

Rebeca alijibu huku akichezesha kichwa chake kurekebisha nywele.
Kufikia Hapo Angel hakuwa na la kuongea tena zaidi ya kuendelea kuitizama kwa makini stendi hiyo mpya iliyokuwa ikiendelea kukarabatiwa.
Basi hilo waliokuwa wakisafiri nalo halikupoteza muda sana ndani ya stendi hiyo, ni baada ya kupakia abiria waliokuwa wamekata tiketi katika ofisi za basi hilo, waliondoka.

Safari ilianza kuiva upya, na wakati huo mkoa uliokuwa unafuata ni Morogoro.
Kutokana na kuwa ndiyo mara yake ya kwanza kusafiri safari ndefu Angel alijikuta akipata wakati mgumu ndani ya gari kwani alichoka kukaa hata akaanza kuhisi makalio yake yanawaka moto na miguu kufa ganzi...
Hatimae alianza kuhangaika mfano wa mtu anaeshambuliwa na siafu...
“Mmmh!! Nini tena?!”
Rebeca alimuuliza Angel baada ya kuona hatulii sasa!
“Anti mi nimechoka.”
Angel alitoa jibu ambalo lilimkera sana Rebeca.
Lakini baadae akatambua kuwa ni kweli hakuwa akifanya makusudi kwani inawezekana tangu kuzaliwa kwake hakuwahi kusafiri umbali mrefu kwa gari.
Akaona ili asiendelee kuleta ghasia akafanya jambo.
Akampa soda ya coca_cola ya kwenye kopo (take way).
Angel alipokea na kisha kumtizama shangazi yake usoni...
“Kunywa.”
Rebeca alisema!

Kiulafi ulafi Angel akaibwia yote kwa mara mbili tu, kikopo akatupa nje!
Oohoo!
Kwani muda ulikwenda? Wakati huo huo Angel alianza kujihisi uchovu mkubwa sana ukiambatana na usingizi vilivyoanza kumzonga kwa pamoja!
Macho yakawa mazito, taratibu alianza kurembua kama mlevi.
Mwishowe akarudi nyuma taratiiiibu akaiegemea kisha kichwa chake kikaenda kuegemea bega la shangazi yake.
Usingizi mzito sana ukamchukua Angel akalala fofofo!!
Rebeca yeye hakuwa na habari yaani ndiyo kwaanza alikuwa akiburudika na muziki mnene kupitia foni zake alizokuwa ameunganisha kwenye simu yake kubwa ya smartphone.
Mpaka inatimu saa nane kasorobo walianza kuitafuta Msamvu.
Sehemu ilipo stendi kuu ya mabasi ya mkoa wa Morogoro.
Hapo sasa ndipo Rebeca alipoanza kupiga hesabu za kumwamsha Angel kwani walitakiwa kushukia Morogoro kama baba yake alivyokuwa amemwamuru...

“Angel..! Angel..! Angel..!”
Rebeca aliita mara kadhaa huku akimtikisa bega Angel hatimae akakurupuka usingizini.
“Mmmmh!!”
Angel aliitikia kivivu huku akifumbua macho yake mekundu yaliyotawaliwa na ulegevu kutokana na usingizi aliokuwa anauchapa!
“Tunakaribia Msamvu kwahiyo jiandae tunashuka hapo!”
Rebeca alimwambia hivyo Angel, wakati huo ye akipiga miayo na kujinyosha nyosha.
“Inamaana tumekwishafika Morogoro?”
Angel alitupia swali...
“Ndiyo!”
Rebeca alijibu!
“Sawa.”

“Haya wale abiria mnaoshuka msamvu, msamvu, msamvu.. Tunakaribiaaa.”
Alisikika kondakta akisema hayo huku taratiibu basi lilianza kupunguza mwendo kwa sababu mbele kulikuwa na kibams/tuta.
Rebeca na Angel walianza kutungua mabegi yao na kuyashika mikononi kwani tayari walishafika msamvu wanapotakiwa kushukia.
Wakashuka baada ya basi lao kusimama.
Angel alikuwa akijinyoosha nyoosha sana kutokana na uchovu mkubwa wa safari uliokuwa umeuvaa mwili wake.
“Leo ndiyo mara yako ya kwanza kusafiri safari ndefu ee?!”
Rebeca alimuuliza kwa kumtania Angel...
“Ndiyo! Anti yaani nimechoka mimi loo!”
Angel alijibu...
“Hahaha... Njoo huku sasa tuangalie bajaji ya kutufikisha huko kwa babu yako.”
Rebeca alisema.
Basi wakatoka pale na kutembea hatua kadhaa mbele mara bajaji hii hapa!
“Wapi kinadada?!”
Dereva bajaji aliuliza kwa uchangamfu.
“Hapo bondeni.”
Rebeca alijibu.
“Karibuni niwawahishe dada zangu.”
“Shilingi ngapi itakuwa?”
“Aah! Dada zangu nipeni buku niwakimbize.”
Maana ake hapo kila mtu angelipia shilingi mia tano.
Aaah!
Nauli ya kawaida kabisa hiyo, hawakusita wakaingia ndani ya bajaji kisha safari ikaanza.
Sehemu yenyewe anapoishi baba yake Rebeca siyo mbali sana hivyo hawakupata tabu kufika muda huo huo..

“Oooh! Mjukuu wangu Angel karibu, karibu sana katika makazi ya babu yako!”
Walimkuta huyo mzee yupo nje na alipowaona tu alifulahi sana hasa kumuona Angel alifurahi mno!
Hata akamkaribisha kwa hamasa kubwa sana!
“Asante babu! Mimi pia nafurahi kufika hapa!”
Angel nae aliupokea ukaribisho huo kwa mbwembwe kede kede...
Basi ikawa ni zaidi ya furaha walikaribishwa ndani ya nyumba kisha maongezi ya hapa na pale yakafuata baada ya wawili hao kupata maji...
“Habarini za safari jamani.”
Babu aliuliza!
“Ni salama baba za tangu majuzi mwenyewe!”
Rebeca alijibu na kisha kumrudishia kijiti tena!
“Aaah! Mi mwenyewe ni njema kabisaa!
Na ninashukuru kuona nanyi mmefika hapa mkiwa salama.”

“Tunashukuru baba... Aaah mama yupo wapi kwani?”
Rebeca alihoji.
“Huyo nafikiri yupo sokoni huko maana ana kabiashara siku hizi.”
“Atachelewa kurudi?”
“Sijajua kama atamaliza saa ngapi mzigo wake, kiufupi hana muda maalumu wa kurudi nyumbani.”
“Eh! Sasa mi likizo yangu inakwisha kesho na nikilala huku Morogoro nitavuruga mambo mengi sana.”
Aliongea Rebeca.
“Mimi shida yangu ilikuwa ni huyu mjukuu wangu tu!
Kwa kuwa sasa umemfikisha we hata ukiondoka sasa hivi nenda tu, utakuja kwa muda ambao utakuwa na nafasi kazini kwako.”

Babu alisema!
“Ni kweli kabisa baba nitakuja siku za weekend.”
Rebeca alijibu huku akijiweka sawa tayari kwa kuondoka!
“Hakuna shida, huyu mjukuu atakapoanza kuja huko nitampakia kwenye basi na tutawasiliana ili umpokee.”
“Sawa baba, ngoja mimi niwahi mabasi ya jioni jioni hii.”
“Haya safari njema mwanangu.”
“Sawa baba asante sana!”
Rebeca baada ya kuaga akaondoka zake kuelekea tena Stendi ya basi ya Msamvu.

Huku nyuma wakabaki Angel na babu, wao wakaendeleza gumzo.
“Mjukuu wangu sasa unakwenda kwenye jiji la wahuni upo?”

Sehemu 3 Sehemu 5
0
0