Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 01

Nilipofikisha umri wa miaka 16, ndipo nilikuja kuambiwa na shangazi yangu Jemima kuwa mimi ni yatima!
Ndiyo siku niliyoshikwa na mshtuko mkubwa kuliko siku zote tangu nizaliwe.
Hakika siku hii sitokaa kuisahau katika maisha yangu…
Ilikuwa ni siku ya Jumapili nakumbuka ilikuwa ni desturi yangu kila siku ya Jumapili kuhudhuria ibadani kusali na kumuomba Mungu anisaidie katika maisha yangu, masomo na hata kuja kukutana na wazazi wangu ambao tangu utoto wangu nilikuwa nikidanganywa na ndugu zangu kuwa walikuwa mikoani kikazi lakini cha ajabu tangu kukua kwangu sikuwahi kuwaona sura zao.
Ingawa mitaani nilikuwa nikisikia fununu kuwa mimi ni yatima lakini sikutilia maanani wala sikutaka hata kuliweka akilini hilo swala.
Lakini wahenga walisema.
“Lisemwalo lipo na kama halipo basi laja”.
Ndicho kilichonikuta mimi Leylah.

Kwanza kabla ya siku hiyo nakumbuka siku moja niliwahi kuota ndoto ya kutisha mno.
Ndoto hii niliiota nikiwa kati kati ya msitu mmoja mnene sana ndani ya mkoa wa Iringa, ilikuwa ni ndoto fupi tu ambayo niliiota mara moja kisha usingizi ukapaa na kuniacha nikiwa macho na hofu juu!
Basi siku hii niliiunganisha na ndoto ile ambapo kichwani nilijenga taswira moja yenye picha ya kutisha na kuogopesha sana.
Japo nilijaribu kujizuia kulia lakini ilishindikana, nilijaribu kubana kilio lakini pia ilishindikana mwisho yowe kali lilinitoka!
Hakika hakuna kitu kinauma kama kumpoteza ndugu yako wa karibu kabisa hasa mzazi.
Kiufupi baada ya ile taarifa niliishiwa nguvu hata ibadani sikuweza kwenda, baadala yake niliishia kujifungia chumbani nikalia na mengi yaliyokuwa moyoni mwangu, nikalia na shida zangu zote, mwisho nilifuta machozi nikasali na kuwaombea wazazi wangu wapumzike kwa amani, pia niliomba baraka zao katika njia zangu zote nipitazo ili maisha yangu yawe marefu na yenye amani.

Wakati huo nilikuwa kidato cha nne pia mitihani ilikuwa inakaribia.
Kiukweli sikujua ni kitu gani kilichonifunga kichwa namna hiyo hata nikaishi miaka mingi bila kufuatilia taarifa kamili za wazazi wangu mpaka naelekea kuhitimu shule ya upili ndipo nakuja kuambiwa.
“Kwamba nililidhika sana na maisha ya shangazi yangu?”
Nilijiuliza hata sikupata jibu sahihi.
Lakini kipindi kile ni kama niliingiwa na msongo wa mawazo, saikolojia yangu ilivurugika hatimae uwezo wangu wa kimasomo shuleni ulishuka.
Hata siku ya mtihani wa mwisho ilipowadia nilikosa cha kujaza kwenye mtihani.
Nilipata robo ya mtihani wote, nikajikuta nimefeli vibaya nikaishia kurudi mtaani nikiwa sina ramani yoyote kichwani.

Vijana mtaani waliona wamepata fursa, walinong’onezana na kukonyezana kuwa sasa Leylah nimefeli kinachofata nitaondoka kwenda mikoani nisitoke hivi hivi ikiwezekana hata kubakwa nibakwe kuliko niondoke nikiwa kama dada mwenye heshima halafu nikifika mjini nibadilike na kuwa baamed, mdangaji, hivyo walitaka waanze wao.
Siku chache baada ya ule uvumi vijana walianza kuja kama nyuki nami nilijitahidi kupambana nao niliwakataa kwa sababu najua hila zao, niliwachukia na sikutaka kuwaona hata mmoja.

“Hivi Leilah kwanini unanifanyia haya, utaendelea kunitesa hivi mpaka lini au nikuulize tu kitu kimoja kwani muoaji huwa ana alama?”
Yalikuwa maneno ya Meddy Kigoe kijana mwenzangu ambae yeye sera zake zilionekana kuwa tofauti kidogo na za wenzie.
Nilimuangalia…nikamuachia tabasamu jepesi la kumweka njia panda, mwisho nilimuuliza swali.
“Kwani taratibu za kuoana mwanamke na mwanaume tangu enzi za mababu zetu huzifahamu?”
“Nazifahamu.”
Alijibu.
“Basi zifuate.”
Nami nilimjibu kifupi.
“Leylah siwezi kutafuta mshenga akapeleka posa kwenu angali mimi na wewe hatujaelewana, pagumu na hilo ndiyo tatizo kwangu.”
“Ok… Kwamba upo tayari?”
Nilimuuliza.
“Ndiyo.”
Alijibu.
“Sawa nenda kafanye hivyo.”
Nilimwambia.
Nilipomwambia vile Meddy aliondoka akaenda zake.

Kiufupi niliridhia kuolewa na mwanaume yule ambae sura na tabia zake za upole ziliniridhisha na kuniaminisha kuwa huenda akawa baba bora wa watoto wangu, nilijikuta nampenda kwa dhati.
Siku chache baadae posa ililetwa nyumbani, hata nilipoulizwa kama nilikuwa tayari kuolewa na mwanaume yule kwangu jibu lilikuwa jepesi mno!
Jibu lilikuwa ndiyo!
Basi baada ya hapo Meddy aliitwa nyumbani, akaja na ndugu zake kadhaa, kikao kikafanyika hatimae tarehe ya harusi yangu ikapangwa!
Nilifurahi sana, nilitamani kuolewa na Meddy baada ya kuona elimu imenikataa.
Siku hazikuganda… sekunde, dakika na saa, siku wiki hatimae tarehe lengwa iliwadia.
Siku ambayo siwezi kuizungumzia leo hii ingawa kwangu ilikuwa ni siku nzuri mno!
Sherehe haikuwa kubwa sana lakini waliokuwepo walifurahi na kuburudika sana.
Mwisho wa siku hiyo, jua lilinizamia nikiwa kwa wakwe zangu yaani wazazi wake Meddy.

Nilikwenda kuanzia maisha kwa wakwe zangu kwa sababu mume wangu Meddy hakuwa na nyumba ya kunifikishia.
Pale nilikutana na mawifi zangu watatu yaani dada zake Medy, Stella, Erica na Amina, lakini kati ya hao mawifi zangu watatu nilipatana na Amina tu wengine ukawa ni urafiki wa kawaida.
Mbali na hao dada zake Meddy alikuwa na Kaka yake mmoja alieitwa Joshua ingawa Joshua hakuwepo hapo alikuwepo mikoani kikazi.
Licha ya kuwa nimeolewa na kwenda kuanza maisha mapya, sikuweza kusahau nyumbani nilikwenda kusalimia mara kwa mara, huku pia mjomba na watoto wake nao wakinitembelea mara moja moja, isipokuwa shangazi yagu ndiye hakuwahi kunitembelea kabisa tangu siku yangu ya harusi pia aliondoa kabisa mazoea na mimi akawa yuko bize kabisa hata tukikutana popote hakuwa mchangamfu tena.
Sikujali sana badala yake namimi nilizidi kuangalia maisha yangu.

Miezi nane niliyoishi ndani ya ndoa ikanikuta nikiwa na ujauzito wa miezi sita!
Ndugu jamaa na marafiki hasa kutoka upande wa mume wangu walizidi kunijali, waliniletea zawadi mbali mbali ikiwemo nguo, vifaa vilivyohitajika hospitalini siku ya kujifungua na pesa, jambo lililozidi kuniletea hali ya kujiamini mno na hali yangu.
Meddy alizidisha upendo kwangu mara dufu, jambo lililopelekea na mimi kuipenda mimba yangu kupita kawaida hata nikahisi kulewa.

Hatimae miezi tisa ya mimba ikagonga! Kilichoanza kutazamiwa kuanzia wakati ule ilikuwa ni kukipokea kiumbe kipya duniani.
Ilikuwa ni siku ya Ijumaa jioni nakumbuka siku hiyo nilishikwa na uchungu wa ghafla nikiwa hospitali, ulikuwa ni uchungu wa kutisha, uchungu ambao sikuwahii kuumwa tangu nione jua!
Kutoka wodi ya wajawazito nilitolewa haraka nikaingizwa katika chumba cha kujifungulia.
Maumivu yalizidi kipimo kila sekunde iliyigonga na kupotea, mwisho nilihisi kuishiwa pumzi na nguvu, ghafla usinguzi wa ajabu ukanichukua.

Nilikuja kuzinduka siku ya pili Jumamosi asubuhi majira ya saa tatu asubuhi, kwanza nilishangaa kukutana na mazungira mengine tofauti na chumba nilichoingizwa jana jioni.
Sasa kujikagua vizuri nikakuta nimefungwa dripu la maji huku pembeni akiwepo mume wangu Meddy, mama mkwe na wifi yangu Amina walionekana kupoa kuliko kawaida.
Sijui kama waliona kama nimezinduka, ila nilivyomtizama mume wangu kwa makini niligundua alikuwa akilia kwani alikuwa akijifuta machozi.
“Meddy!” Nilimwita huku nikijaribu kunyanyuka! Nilikumbana na maumivu ya ajabu ya tumbo nikatulia kwanza.
“Tulia mke wangu utajitonesha mshono!”
Haraka Amina alimwahi mume wangu na kumziba mdomo.
“We Meddy nini sasa?”
Alimuuliza kwa ukali.
Niliposikia hivyo nilitoa shuka kwa kutumia mkono wangu wa kushoto.
Nilipigwa na butwaa baada ya kukutana na mshono wa kuogopeka tumboni, papo hapo akili ikaniambia nilijufungua kwa upasuaji, ila cha ajabu mtoto hakuwepo na ndugu waliokuwepo hapo wakiniangalia nyuso zao zilionesha simanzi kubwa mno! Jambo lililonishtua hadi nywele zikasisimka!.

Sehemu 2
0
0