Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 30

Milango ikajifunga baada ya mimi kuketi sitini, Sam akalitia gari moto safari ya kuelekea nisikokujua ikaanza.
Nikiwa garini kuna hali ya usingizi ilianza kuninyemelea, kitu ambapo sikukipenda nilifumbua macho kwa nguvu huku nikifikicha macho ghafla hali ile ikatoweka lakini nikajikuta tupo sehemu ambayo ni uwanda wenye kijani kibichi kilichokolea rangi kama kuna mvua ilinyesha siku moja nyuma!
Hii sehemu haikuwa na majengo, isipokuwa kulikuwa na mlima wa ajabu sana mita kama sitini mbele yetu, nilishangaa imekuwaje, nahisi hata wewe unaweza kushangaa eti ule wakati nahisi kunyemelewa na usingizi inamaana nilikuwa nimesinzia kabisa sababu sikuona tulifika fikaje pale, ila nakumbuka tu wakati nafikicha macho kubishana na usingizi ile macho kufunguka ndo nakutana na hiyo jiografia.
“Tumefika!”
Aliongea Sam huku akibonyeza batan fulani kwenye dashboard nayo milango ya gari ikafunguka.
Nilishuka huku nikihisi mwili ukiwa umetawaliwa na ubaridi mkali mno.
Tulishuka garini kisha milango ya gari ikajifunga, tuliondoka tukatembea takriban hatua thelathini, mwisho wa safari yetu ya kutembea kwa miguu ikakomea mbele ya bonde kuuubwaa!
Hili bonde nahisi ndilo lililokuwa limetenganisha ule uwanda wa nyasi mbichi na ule mlima wa kimaajabu uliokuwa mbele yetu.
Tulisimama hapo huku tukiwa tunalitizama bonde lile kuubwa lisilo na miti wala kuonekana mwisho wake isipokuwa tu humo ndani lilitandwa na ukungu mwepesi uliokuwa ukipishana kama mawingu.
Pia kulikuwa na maji yaliyokuwa yakitoka kwenye mlima ulioonekana mbele yetu sehemu yalipokuwa yakitoka maji hayo yalitoka katikati ya mlima ule, sehemu iliyokuwa ikitoka maji hayo kuna mawe yaliyojipanga na kutengeneza taswira ya fuvu la binadamu, huku maji hayo yakitoka eneo la mdomo!
Siyo siri hili eneo linatisha ukilitizama.

Sam aliniacha nikatalii kwanza ndipo baadae akanistua!
“Leylah!”
“Abee!”
Niliitikia kwa kustuka.
“Unajiskiaje?”
“Aah!… Najisikia vizuri tu!”
Sam akatabasamu kisha uso wake akauelekeza chini.
“Nikuambie kitu?”
Aliongea saa hiyo akiinua uso wake na kunitizama.
“Ndiyo.”
Nilijibu lakini kuna kitu hakikuwa sawa moyoni.
“Mbona una wasiwasi na mawazo mengi sana… Kulikoni?”
Ni swali ambalo sikulitegemea kwa wakati ule hivyo likaniletea kigugumizi kwenye kulijibu, nikabaki nimeduwaa.
“Leylah…”
“Abee!”
Akanisogelea karibu zaidi akanishika bega kwa mkono wake wa kushoto, uso wake akausogeza karibu na uso wangu.
“Mbona una wasiwasi na mawazo mengi sana… Shida nini?”
Alirudia swali. “Hapana, niko sawa ila mazingira ndiyo yananitia ushamba kidogo ndiyo maana nazubaa sana.”
“Au siyo?… Sawa lakini nikuulize kitu kingine?”
“Ndiyo mume wangu?”
“Kuna kazi nikikupa utaweza kuifanya?”
“Hakuna kazi ya kunishinda kutoka kwako hata hivyo nielewa huwezi kunipa ambayo itanishinda.”
Sam alinitizama tena usoni huku akitabasamu, jambo lililozidisha uzuri wake wa usoni.
“Ni kazi ndogo sana… Siku utakayofanikisha kumuua Damson Mbarangu pia unatakiwa kumpoteza dunia Jr!”
Moyo ukapiga paaa! Papo hapo mnyama mwenye sauti kubwa kama simba aliunguruma juu ya kilele cha ule mlima ule wa kimaajabu.
“Fuuuuu!”
Nikashusha pumzi nzito maana nilihisi kifua kimejaa kwa ghafla pumzi ya moto!
“Vipi… Mbona umepatwa na hali ya sintofahamu? Halafu sikia wewe tembea na wanaume ovyo upate mimba sisi tutakutoa duniani kwa kigezo cha kushindwa kujifungua!”
Sam aliongea kwa sauti kavu kidogo jambo lililonishitua nikapeleka macho yangu usoni kwake!
Mamaaa!
Nilitamani kupiga yowe baada ya kuona Sam kabadilika na uso wake umefana na uso wa paka mweusi, duuuh nilipigwa na butwaa kubwa…

Mara nikajikuta nipo mahali nilipokuwa nimesimama awali huku nikiwa na simu yangu mkononi, niliachia pumzi kubwa huku nikiwatizama wapita njia wote waliokuwa wakipita eneo lile kama wananitizama au la?
Kila mmoja alionekana kutingwa na majukumu yake.
Simu yangu ikiwa mkono nikaitizama ajabu toka nitoe kufuli ya kioo haikuwa imejifunga tena cha kushangaza zaidi ni kwamba pazia la kioo chake ilikuwa ni ile picha ya zamani na siyo ile niliyoiona muda mfupi kabla sijahamishiwa dunia nyingine kimazingara.
Mmh! Ama kwa hakika yalikuwa ni mambo mazito sana, ni mambo ambayo tamani tu kusimuliwa yasije yakakuta!
Muda huo huo niliitafuta namba ya ofisi ya madalali niliiona nikapiga, simu ilipokelewa haraka sana tukasalimia na yule mtu aliepokea simu nikamweleza shida yangu nae akanieleza ni kwa namna gani ninaweza kufika ofisini kwao, basi nami bila kupoteza muda nilichukua usafiri wa bodaboda usafiri ulionipeleka moja kwa moja mpaka ofisi za madalali hao iliyopo Magomeni.
Ilikuwa ni ofisi nzuri iliyo ndani ya uzio mkubwa, nilifika ndani nikakutana na madalali na baada ya maongezi mafupi nilipelekwa mahali zilipoegeshwa gari zenyewe!
Bahati ikawa nzuri kwangu gari niliyokuwa nikiililia ilikuwepo! ‘Discover’ ya maana ambayo upande mmoja kuyoka usawa wa dirisha la katikati kuja mpaka kwenye pua ya injini mbele ilikuwa ya kijivu, halafu kuanzia pia dirisha la katikati usawa wa vioo kurudi nyuma mpaka kwenye bamba za usajili ilikuwa nyeusi! Halafu paa lote lilikuwa la kijivu.
Gurudumu za akiba nyuma zilikuwa mbili zikiwa na mifuniko yenye nembo ya ‘Toyota’ usajili wa “DZX” maana ake ilikuwa ni moja kati ya matolea ya mwisho kabisa kabla ya usajili wa ‘E’ kwa maana hiyo gari ilikuwa bado mpya saana!
Jamani…
Basi kwa kuwa sikutaka kupoteza wakati sana niliwapeleka mbio mbio kidogo tuafikiane kwenye bei, mara moja nikampigia Jr hewani kabla sijafanya malipo ili aanze kuja.
Malipo yalifanyika kwa njia ya mtandao, tukaandikishana pale nikapewa vibali vyote kuanzia kibali cha muuzaji, kibali cha dalali na kibali cha ununuzi pamoja na kadi ya gari.
Ilikuwa ni kama ndoto vile, kuna wakati akili iligoma kuamini hasa nilivyofikiria nilikotoka.
Nusu saa baadae Jr aliniambia amefika Magomeni center.
Hapo ilibidi niombe dereva aniendeshe mpaka center mahali alipo dereva wangu…
Hawakuwa na shida kuna mkaka akapewa ruhusa ya kuniendesha mpaka nilipohitaji kufikishwa!

Tukiwa garini…
“Ah! Dada unafanya kazi gani?”
“Mimi?”
“Ndiyo!”
“Mfanyabiashara tu wa mazao masokoni.”
“Doh! Inaonekana una jiwe sio poa!”
“Hahaha!… Kwanini?”
“We, hii gari imetangazwa kitambo na ni gari kali sana hapa bongo ila matajiri wamepwaya kuichukua ila nashangaa umefanya miamala haraka saaanaa!”
“Ila wanaume hivi mtaacha lini tongoza tongoza?”
Niliwaza akilini sababu nilishamsona anakoelekea.
“Hawajaamua tu mbona watu wanamiliki majengo ya bei ghali wana makampuni ya maroli ya kubeba mizigo ambayo kwa siku wanajikusanyia mabilioni ya pesa sasa mtu anashindwaje kununua gari ya milioni mia?”
Akabaki anacheka cheka tu…
Hatimae tulifika Magomeni center…
“Paki hapa dereva wangu yuko sehemu hii.”
“Sawa”
Aliegesha gari vizuri, ila kabla ya kushuka akaanzisha stori fupi mwisho kaniomba namba ya simu, kitu nilichohisi toka mwanzo.
“Unavoomba namba yangu hakikisha una ramani za biashara na siyo usumbufu...
Unanipigia unaniambia dada nina dumu mia za mafuta ya kula au nina tani 50 za sembe au tani kadhaa za mchele au maharage au gunua mia tano za mahindi, ila siyo uchukue namba kwa lengo la usumbufu sawa?”

Niliongea huku nikiwa nimemkazia macho hadi akaogopa!
“Aha! Dada samahani nilitaka tuwe marafiki tu, lakini poa!”
Akashuka bila hata kuaga, akaondoka!
Nilimtizama anavyotembea hadi anapotelea.
Nilitizama mazingira kisha nilimtafuta Jr hewani...
“Uko sehemu gani?”
“Nipo zebra hapa.”
“Mmh! Tatzo kupajua.”
“We upo maeneo gani au kuna nini hapo?”
“Apa nilipo, upande wa mashariki mwa barabara kuna duka kubwa la Alminium limeandikwa ‘MANGI ALMINIUM’ ndipo nilipo.”
“Ahaa!… Upo hapo kwa Mangi?,nipe dakika tano!”
“Sawa.”
Dakika mbili Jr alifika na kuingia kwenye gari akaliwasha na kuanza kuonesha fani yake, kazi ikawa ni kumuelekeza ni wapi aniepeleke nae ikawa ni kazi kunitii.

Siku hii nilimtafuta Erick hewani tukawa tumeongea kuwa mazoezi yatafanyika mchana na yatawahi kuisha, hiyo ikawa fursa kubwa sana kwangu sababu nilitamani sana siku hiyo nifike kanisani kwa Damson Mbarangu pia nilitarajia kuwahi kurudi Mbezi mapema ili nikapate muda mzuri wa kupumzika kisha nianze kupanga safari ya kwenda Njombe kama nilivyokuwa nimeelekezwa na mizimu ya ukoo wetu.
Tulikwenda hadi sehemu ya mazoezini huko tukafanya mazoezi takribani masaa matatu, hatimae ilipotimu saa nane na nusu tulitawanyika.
“Kwahiyo kumbe Leylah we ni mwigizaji na hukuwahi kuniambia?”
Jr aliniuliza swali hilo pindi tupo njiani kuelekea Manzese.
“Hahaha! Basi ndiyo kazi yangu hapa Dar es salaam.”
“Dah! Hongera sana kazi inakupendeza,utafisha sana kwenye kwenye picha lenyewe!”
“Au vipi?”
“Saana!”
“Asante kiikubwa ni dua tu!”
“Ni kweli.”
Kutokana na wepesi wa gari tuliyokuwa nayo tulifika Manzese mapema mno!
Tukawa moja kati ya waumini wa mwanzo kabisa kufika kanisa la Damson Mbarangu… Samahani sikulifatilia kanisa lile kujua ni dhehebu gani hivyo nilitumia jina la mmiliki wa kanisa.
Kufika pale Jr akatafuta sehemu nzuri akaegesha gari kisha tulishuka tukaingia bustanini na kuanza kuzurura tukivuta muda ili muda wa kuanza ibada ya jioni ufike tujumieke pamoja na mamia ya waumini waliokuwa wakifika kila kipindi cha ibada kusali.
Saa kumi kamili haikuwa mbali.
Hatimae alifika mchungaji aliwasiri kama ilivyokawaida yake akiwa kaambatana na mke wake pamoja na wababe wawili pembeni yao.
Kengele ya kuanza ibada iligongwa baadae kidogo, ndipo watu wote tuliokuwa tumekwishafika tuliingia ibadani, ibada iliyochukua takribani lisaa lizima, ibada iliyojaa kila aina ya miujiza na shuuda mbali mbali, hatimae ilifika tamati mida yaa saa kumi na moja unusu jioni.
Basi baada ya ibada mimi na Jr tulitoka tukapanda gari yetu tukaondoka zetu.

Kutoka tunatoka kanisani mpaka tunaingia barabara kuu licha kuwa tulikuwa tukiongea mawili matatu ndani ya gari lakini niliona mara kwa mara Jr macho yalikuwa hayabanduki kwenye kioo cha chepembeni yaani ‘side mirror’.
“Mbona unaagalia kwa makini sana tunakotoka kupitia kioo vipi?”
Niliamua kumuuliza.
“Kuna gari naiona hapa imefanana kwa kila kitu na gari iliyokufukuzia awali ila kasoro namba za usajili tu, tena siyo kwamba zimebadilishwa hapana! Ni kwamba haina plate number!”
“Mmh! Ni kina nani hawa kwani?”
“Hata mimi nashindwa kujua ile ngoja niongeze mafuta kidogo tukifika Ubungo nitaegesha sehemu tuone mwenendo wao.”
“Sawa.”
Jr akaipa gari mafuta ya kutosha, muda mfupi baadae tukawa tumefika ubungo, alichokifanya ni kuhamia upande wa pili wa barabara haraka kisha akashusha spidi mpaka tano kisha akaniambia nihamie siti ya dereva niendelee kuliendesha taratibu hadi mita saba mbele ambapo kulikuwepo na banda la vinywaji kisha niegeshe hapo.
Nikafanya hivyo kisha ye alirukia nje, mlango akausukuma kwa nyuma ukajifunga kwa nguvu nikaona wahuni nje wakimuangalia sijui walifikiri ni kibaka mwenzao kafanya yake ili nao wapate kula sijui?
Kwa mwendo wa taratibu niliendesha gari mpaka mahali lilipokuwepo banda la vinywaji banda hilo lilikuwa na turubai kubwa la bluu lenye tangazo la Pepsi bila shaka hao walikuwa ni Pepsi.
Nikaliegesha gari langu nikatulia kwanza, ile crown ikapitiliza wala haikusimama!
Ile gari nilianza kuipatia wasiwasi kwa kweli, kwanza nilitoa bastola yangu nikaikagua nikakuta ina risasi tatu.
“Mmh!… Inatakiwa iwe imejaa risasi muda wote hii.”
Nilijisemea kimoyo moyo saa hiyo nikivuta kumbukumbu kama nilikuja na risasi za kutosha kwaajili ya akiba?
Yes nilipata kukumbuka kuwa katika moja ya mabegi yangu ya nguo kulikuwepo na box la risasi risasi hizo nilipewa na Sam.
Nilitabasam nikarudisha silaha yangu mahala pake.
“Halafu sasa hivi ninatakiwa kubadili uvaaji isipokuwa tu wakati wa ibada.”
Niliwaza hivyo kubadili mtindo wa mavazi lengo ni kuhakikisha bastola inaishi kiunoni muda wote.
Bado niliendelea kuwaza na kuwazua nikiwa ndani ya gari, mara simu yangu ikapata kupigwa.
Kuangalia mpigaji nikaona ni Jr.

“Hallo.”
Nilipokea simu nikiwa katika utulivu mkubwa sana.
“Skia… Itoe gari hapo isogeze mita hamsini mbele.”
Nilivyoangalia mbele niliona kweli kuna uwazi umbali wa karibu mita sabini.
Nilichokifanya ni kuwasha gari taratibu nikawa naendesha nilitembea umbali mrefu kidogo mara simu ikaita tena safari hii nilipokea huku mkono mmoja nikiwa naendelea kuendesha kwa sababu gari ilikuwa katika mwendo wa taratibu sana.
“Hallo.”
“Egesha hapo mbele penye hilo jengo lililoandikwa twiga cement.”
Kweli nilivoangalia mbele nililiona hilo jengo.
Nilitembea taratibu hadi nikafika eneo hilo ile kabla hata sijaegesha Jr alifika haraka akafungua mlango wa katikati kisha akaingia.
Nilistaajabu!
Wepesi wa huyu mtu ulianza kunipa mashaka juu yake,asije kuwa jambazi aliekubuhu ndani ya mji mwisho wa siku nikaingia matatizoni.
“Siku utakayofanikisha kumuua Damson Mbarangu pia unatakiwa kumpoteza dunia Jr!”
Ghafla nilijiwa na kumbukumbu ile ya maneno ya Sam yaliyozungumzwa katika tukio moja la kutisha mno!
Pindi nimekumbuka maneno yale nilijikuta nikimtizama Jr ghafla kupitia kile kioo cha juu pale kwa dereva ambacho kazi yake ni kumwezesha dereva kuziona siri zote za nyuma.
Macho yakagongana!
“Vipi mbona kiwasi wasi sana unanitizama?”
Aliuliza saa hiyo akiwa keshafika kabisa karibu yangu.
Ikabidi nisinamishe gari kisha nikahamishia m siti ya upande wa pili.
Jr alikaa kitini akafunga mkanda akaiondoa gari.
“Hapa inabidi tufike Kimara mara moja hili eneo pia siyo salama sina imani nalo kabisa!”
“Kwani kuna nini?”
Niliamua kumuuliza sasa maana nilianza kuona mapicha picha tu halafu sielewi...
Kabla hajajibu mara gari ilizima ghafla ikasimama kabisa!

Sehemu 29 Sehemu 31
0
0