Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 07

Sikujali niligeuka nikaendelea na safari yangu hatimae nilitoka nje ya duka lile kubwa la mabegi na mikoba.
Kufika nje nilikutana na machinga muuza vyombo nae akiwa katika harakati zake.
“Mambo?”
Nilimsalimia alikuwa ni kijana wa miaka 22 hivi tuseme alikuwa lika langu tu.
“Poa dada karibu… nauza vyombo vya jikoni, karibu.”
“Kwani mimi nimekuuliza unauza nini?”
Nilimhoji, kitendo chake cha kusalimiwa yeye akanadi biashara yake kilinikera.
Nilivyompiga swali akanywea!
“Haya una visu apo?”
Nilimuuliza.
“Ndiyo ninavyo dada karibu.”
Nlijibu haraka huku akifungua fungua vyombo akanionesha visu.
Niliangalia angalia pale nikachagua kimoja nilichopendezewa nacho, nikakagua makali nikakuta kipo vizuri.
“Shilingi ngapi?”
Niliuliza bei.
“Elfu mbili tu dada.”
Nilikiweka kwenye mkoba wangu kisha nikatoa noti ya shilingi elfu kumi nikamkabidhi halafu nikaondoka zangu.
“Dada chenji yako umesahau.”
Nilisikia sauti nyuma.
“Utanywea chai hiyo.”
Nilimjibu pasi na kugeuka nikatokomea.
Nilikuja kutokea mshindo, nilikuwa nikitembea tu hata nisijue naelekea wapi cha ajabu hata sikuwa na wasiwasi wala nini yaani hata sijui roho yangu ilikuwaje.
Nilivyofika mitaa ya kanisa la Roma mshindo hapo nilikatiza nikaiacha barabara kuu nikaingia vichochoroni lengo langu nipite njia za mikato nije kutokea VETA kisha mlandege.
Nilitembea na kukata mitaa karibia mitatu nikaja kutokea car wash moja iliyoandikwa ‘KUKAYE CAR WASH’ hapo nilipitiliza mbele kidogo kulikuwa na uchochoro ambao upande ulikuwa na pagala halafu upande mwingine kukawa na nyumba nzuri tu halafu njia ilipita katikati.

Kitendo cha kufika katikati ya uchochoro ule kuna vijana watatu walitoka kwa kasi kwenye lile pagala wakanizoa kwa namna ambayo hata mimi sikuelewa nimebebwaje wakaingia nami ndani ya pagala lile, huko walinitua na kunitaka nitoe pesa zote nilizokuwa nazo ili waniachie vinginevyo wangenitoa uhai.
Nilishangaa na kuogopa sababu kwanza mmoja alikuwa na upanga.
“Mmh!”
Sikuwa na jinsi ilibidi nisalimu amri kwa kukubali kuwapa pesa nilizokuwa nazo ili kuokoa uhai wangu.
“Toa hela haraka dada vipi wewe?”
Aliongea kijana yule alieshika upanga saa hiyo akiwa kanisogelea karibu zaidi.
Basi nikafungua mkoba wangu nikaingiza mkono humo huku nikimtizama yule kijana mwenye upanga kwa jicho lile la nionee huruma.
“Toa hela wewe, unatia huruma nini? Mimi siyo ndugu yako bwana.”
Aliongea kwa nyodo, ghafla akashitukia kisu kikizama kooni alishindwa hata kupiga yowe akaanguka chini kama gunia puu!
Haraka nilichomoa kisu, mwingine nae akanijia kasi kwa lengo la kunidhibiti, nikamtuliza!
“Nakuua!”
Yule mwingine baada ya kuona mwenzie pia kadhibitiwa kwa kuwekewa kisu shingoni alipotea ghafla kwenye pagala.
“Wewe ni kibaka siyo?… Sasa utamfata huyu mwenzio ambae hata sauti hakutoa.”
“A…as…aa, usiniue dada ni… Ni… Nimee… Etuu… Mwa.”
Aliongea kwa shida huku akiwa kanyoosha mikono juu.
“Na nani?”
Nilimuuliza saa hiyo nikiwa nimemtolea kisu shingoni.
“Aliekuuzia mkoba ndiye alietutuma.”
“Ooh! Kamwambie hivi nitakuja tu nimpe hizo pesa wala hakuwa na haja ya kuwatuma nyie angesema kama shida ni zile pesa alizoziona basi angesema nimpe…
Nenda kamwambie nitaenda kumpa mimi mwenyewe sawa?”

“Ndiyo.”
“Haya potea.”
Yule kijana alitoka huku akigeuka mara mbilimbili asiamini kama kweli ameachiliwa akiwa hai wakati mwenzie kitambo sana alishakuwa marehemu.
Alivyotoka nilipukutia kisu changu kwenye nguo za yule mwenzie aliyekufa pale kisha nilikirudisha kwenye mkoba nikatoka zangu.
Hakuna mtu aliekuwa ameshituka kwa lile tukio kwani kila mtu alioneka yuko bize tu.
Hatimae nilivuka ule uchochoro nikaikamata barabara itokayo mashine tatu kwenda mlandege kupitia VETA, nikaunga nayo hiyo.

Wakati nikiwa natoka pale kwenye duka niliponunua mkoba, kuna kitu nilikisoma kwenye macho ya muuza duka pindi naziweka zile pesa kwenye mkoba pamoja na simu.
Kwa jinsi alivyonitizama na alivyozitizama zile pesa na simu machale yalinicheza ndiyo maana nilitoka kimachale pia.
Masikio yalikuwa makini kusikiliza nyuma ndiyo maana niliposikia neno,“Ee uko wapi?” niligeuka nyuma nikaona kweli yule muuza duka anaongea na simu.
Simu ile niliitilia shaka ndiyo maana nilivyotoka nje tu niliamua kununua kisu na kuanzia hapo nilianza kutembea kwa tahadhari kubwa.
Mpaka nafika Mshindo tayari nilishagundua kuwa nafuatiliwa ndiyo maana nilijilengesha sehemu ambayo niliamini kabisa wale watu wangenikamatia pale.
Nilifanya hivyo kwa kuamini wasingeweza kunifanya chochote kwani nilishakuwa nimejipanga bila wao kujua.
Na kweli kilichotokea mmoja alikufa, mwingine nikamdhibiti mwingine alikimbia lakini hata huyo sikumuua nilimuonea huruma ila nikampa tu ujumbe.

Saa tatu na dakika hamsini asubuhi ilinikuta mitaa ya VETA hapo nilianza kujisikia njaa, hivyo nilianza kuangaza macho huku na kule nikitafuta mgahawa.
Niliuona, lakini nilivyotoka kuchepuka nilikumbuka kuwa mbona nimekaribia Miami night club nikakumbuka pale huwa wanauza na vyakula safi.
Nilivyokumbuka hivyo tu nikaghairi kwenda kwenye mgahawa niliouona nikaendelea na safari.
Hapakuwa mbali kutoka hapo, nilikatishia kwenye stendi ya mabasi ya mlandege nikazunguka na kuja kutokea Miami ikiwa tayari imetimia saa nne kamili asubuhi.
Moja kwa moja baada ya kuingia nilitafuta sehemu tulivu nikaketi na kutulia.
Muda mfupi baadae mhudumu alifika kunisikiliza.
“Niletee supu ya utumbo wa ng’ombe na chapati tatu.”
Niliagiza.
“Ni shilingi elfu nne.”
“Sawa kaniletee.”

Haikuchukua muda supu ilifika ikiwa na viungo vya kila aina hata vingine vikiwa pembeni kwamba nitajiongezea mwenyewe pale nitakapojiskia.
Nilikunywa supu ile hadi nikajisikia sasa tumbo limekuwa zito.
Nikaagiza Kilimanjaro mbili za baridi nikaletewa na glasi, ilikuwa ni siku yangu ya kwanza kunywa pombe ukiachana kule nilikoanzia.
Nilikunywa taratibu zile bia hadi nikajikuta sasa nimechangamka, sikutaka kuendelea kukaa hapo nililipa bili nikatoka zangu, ile natoka nje nilikutana na kurupushani watu wakikimbizana kuelekea round about ya pale mlandege huku nikisikia watu wakisema.
“Nasikia amechomwa kisu cha shingo alivyokufa wakamtupia kwenye pagala.”
Nilivyosikia hivyo nilijua nini maana yake.
Nilivyotizama huko walikokuwa wanakimbilia watu niliona karandinga ya polisi ikiingia barabarani huku ikifuatiwa na gari ya kubeba maiti nyuma.
Sikujali niliendelea na safari zangu nilitembea mpaka nafika mitaa ya mwisho wa lami hapo nilichepuka nikaingia kushoto, nikatembea mita saba mbele nikavuka barabara tena nikaingia upande wa kulia huko nikaingia kilabu maarufu cha zebra.
Huko nilikutana na mkusanyiko mkubwa wa watu, wazee kwa vijana wadada kwa wamama, hii ni kwa sababu ya upatikanaji wa pombe ya kienyeji kwa wingi eneo hilo kingine pombe katika klabu ile bei yake ilikuwa rafiki sana kwa kila mnywaji aliefika eneo hilo kupata kileo.
Cha kwanza baada kufika kwenye ukumbi wa klabu hiyo nilitulia kwanza ukumbini nikaangalia na kujishauri ni chumba kipi niingie?
Yaa! Jibu nikalipata, kuna chumba kilinivutia nikaingia huko.
Nilikutana na pombe mbalimbali za kienyeji ukiwemo ulanzi, mbege ya wachaga, kangala ya wamasai, wanzuki ya wagogo, komoni ya wahehe, kimbumu cha wabena bila kusahau kihambule cha wakinga, yaani mule ndani kulikuwa na pombe za kila aina hadi bia zilikuwepo.
Ooh! Ni raha iliyoje kwa walevi?
Watu walikuwa wamelewa hatari, halafu chumba kile kilipendwa sana na vijana na ndiyo waliokuwepo kwa wingi sana mle ndani.

Baada ya kuingia niliketi kitini nikatulia hadi muuzaji akafika kunisikiliza.
“Karibu… Kuonja ni buree!”
Aliongea muuzaji ambae alikuwa ni mdada wa makamo kiasi.
“Naomba safari mbili.”
Niliagiza.
Yule mhudumu aliondoka, akarudi na bia mbili za safari pamoja na glasi.
“Karibu.”
“Asante… Hawa vijana wanakunywa pombe gani hapo?”
Niliuliza.
“Hawa? Labda tuwaulize… Eti nyie hebu msikilizeni huyu dada hapa.”
Wote waligeuka kuniagalia mimi, nikatoa shilingi elfu kumi nikampa yule muuza pombe.
“Wasikilize wao.”
Nilisema.
Wale vijana walifurahi mno, walinipa asante zisizo na idadi mwisho waliagiza debe la komoni wakaendelea kuserebuka wenyewe.
Nilikunywa bia zangu taratibu hadi zikaisha nikaagiza mbili zingine.
Nilipoelekea kumaliza moja nilihisi kulewa jambo ambalo sikutaka linitokee mchana ule hivyo nilisitisha kunywa pombe nikatoka na kuagiza nyama ya kitimoto kilo yenye mafuta.
Nyama zilikuwa zinachomwa mulemule ukumbini.

Nilirudi, baada ya dakika kumi na tano nyama ilikuja, nikala nyama ile nyenye mafuta mengi ilivyoisha nilihisi pombe imeshuka kichwani, hapo nikaendelea kunywa.
“Dada mambo.”
Nilisikia nasalimiwa, ikabidi nigeuke kwanza nimuone anaenisalimia.
“Ooh! Poa kijana vipi?”
“Safi… Mimi naitwa Farid.”
Alijitambulisha kwa maana ya kwamba na mimi nijitambulishe.
“Naitwa Irene.”
Nilidanganya jina.
“Vizuri… Jina zuri lakini mbona kama inaonekana mgeni mlandege hii ingawa inaonekana mwenyeji Iringa.”
“Ni kweli, mimi ni mzaliwa wa mkoa huu ingawa sijakulia hapa ila leo nimeamua nije kutembelea mlandege, hasa soko lake sababu tangu lijengwe sikuwahi kuliona hivyo nimekuja kutembea mlandege ili nilione na soko lake.”
“Sawa karibu sana.”
“Asante sana nimekaribia, nimefurahi sana kutembelea mlandege.”
“Asante pia kwa kutujali, nimefurahi sana kwani ni wachache wenye moyo kama wako.”
Aliongea Farid, nikamtizama usoni niliona kweli uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu la furaha japo ulevi pia ulikuwepo ndani yake.
“Usijali… Lakini naweza kupata dalali huku?”
“Unataka kiwanja au nyumba ya kupanga ama chumba?”
“Vyovyote vile ikiwezekana.”
Farid kusikia hivyo alitoa simu yake akampigia mtu akaongea nae na kumwambia aje zebra.
Kweli ndani ya muda mfupi alifika, kuna mwanaume wa makamo alifika hapo.
Farid akamwoneshea kwangu yule mwanaume akaja.
Tukasalimiana kisha alijitambulisha kwa jina la Ally Matata, pia alijitambulisha kama dalali wa eneo hilo la mlandege na hata nje ya mlandege.
Basi nami nilipata wasaa wa kumueleza shida yangu, nimimueleza kuwa nilikuwa ninahitaji nyumba nzuri ya kununua ambayo isingekuwa mbali na mjini.
Dalali huyo akaniambia ilikuwa ni kama bahati vile kwani wakati akiwa njiani anakuja pale zebra alipigiwa simu na mkurugenzi wa taasisi ya mikopo ya Saccos Iringa mjini akamwambia kuna nyumba imetaifishwa baada ya mwenye nyumba kushindwa kurejesha mkopo aliokopa kwenye taasisi hiyo hivyo nyumba hiyo ilikuwa sokoni, uzuri dalali huyo alisema nyumba yenyewe anaifahamu.
Kilichofuata hapo niliwaaga wote mle ndani tukatoka na kuchukua bodaboda iliyotukimbiza moja kwa moja mpaka eneo la tukio, kweli nyumba ilikuepo niliiona na nikaridhika.
Ilikuwa yapata saa saba mchana, muda ulikuwa ni mwingi mno, haraka taratibu za malipo zilianza kufanyika na kwa kuwa pesa nilikuwa nayo hilo likaniwia urahisi zaidi, ni ndani ya muda mfupi tu tukawa tumeuziana nyumba na Saccos, dalali akalamba chake, vibali vyote nikapewa pale nyumba yangu nikawekea kufuli mpya mambo yakawa yameisha.
Nyumba ilikuwa maeneo ya orofea karibu na mnada.
Katika kibunda nilichopewa na Sam ilibaki milioni mbili tu baada ya kununua nyumba ya thamani ya milioni mia sita.
Baada ya kununua nyumba wazo la kwenda nyumbani kule nifate lile jiwe la dhahabu likanijia.
“Lakini nikienda kule sitakamatwa kweli?”
Nilijiuliza.
Lakini nikaona siyo shida, wacha niende tu hakuna wa kunikamata.
Kitendo cha kupitisha wazo lile tu simu yangu iliita kwenye mkoba.

Sehemu 6 Sehemu 8
0
0