Dunia Ya Pili - 11
Muda mfupi baadae Amina alifika, alinipokea kisha tuliondoka kuelekea nyumbani.
Huko nilipokelewa na mawifi zangu Stella na Erica, ukarimu ulikuwa ni mkubwa mno kiasi kwamba ungetuona usingeweza kuhisi kama kuna kitu kimetokea.
Baada ya mambo yote ya kikarimu kuisha niliingia kwangu tulipokuwa tukiishi na mume wangu marehemu Meddy.
Kitu kisichokuwa cha kawaida ni kwamba baada ya kuingia ndani kwangu kuna fikra za ajabu zilinijia!
“Hivi hapa kuna ndugu yangu?”
Nilijiuliza!
Jibu lake.
Ikaja,
“Hapana!”
“Kama ni hapana, je ni kipi nakisubili hapa haswa?”
Nilijiuliza.
Jibu likaja,
“Hakuna!”
Kufuatia fikra zile, kuna wazo lilinijia kichwani, wazo hilo lilikuwa ni kuondoka tu kwenye familia ile kwani hakukuwa na cha kuniweka tena.
Basi baadae usiku uleule nilichukua jiwe langu la dhahabu kwenye tranka kisha niliondoka zangu hata pasi na kuaga.
Baada ya kutoka nyumbani kwa wakwe zangu, nilitembea nikakata mitaa usiku kwa usiku hadi nikaja kutokea kalenga njia panda ikiwa yapata saa mbili usiku.
Hapo nilichukua bodaboda iliyonikimbiza moja kwa moja hadi mjini, baada ya kufika mjini usiku uleule nilitafuta bar nzuri yenye vyumba vya kulala wageni.
Niliipata!
Nayo ilikuwa ni bar ya Five Stars, ni bar kubwa iliyo katikati ya mji, pia ni Night club, yaani ni bar inayotoa huduma kwa saa 24.
Niliingia humo.
Nikalipia chumba kwanza, nikaweka mizigo yangu likiwemo jiwe kubwa la dhahabu iliyokuwa mali yangu, kisu pamoja na bastola niliyokuwa nayo.
Baada ya hapo niliingia bafuni kwanza nikaoga, nikatoka nilibadilika kisha nikaingia rasmi ukumbini mahali ilipo bar yenyewe ya Five Star Night club.
Ama kwa hakika ilikuwa ni sehemu iliyochangamka tena kwa kiasi cha kutosha na palivutia mno.
Kama ilivyokuwa desturi yangu nilijongea mpaka sehemu palipokuwa tulivu, huko niliketi peke yangu nikiwa na meza yangu, punde si punde mhudumu alifika kunisikiliza.
“Niletee Castle lite tano na mzinga mdogo wa konyagi.”
Niliagiza.
Mhudumu huyo aliondoka na baadae alirudi akiwa na vinywaji nilivyomwagiza, pamoja na glasi.
Alivitenga mezani akaniwekea na opena yangu kabisa kisha alinikaribisha akaondoka zake.
Cha kwanza nilichokifanya nilichukua ule mzinga mdogo wa konyagi nikaufungua nikamimina kwenye glasi hadi ikafika nusu nikaufunga na kuulaza mezani
nikachukua castle lite moja nikaifungua na kuimimia kwenye glasi hadi ikajaa kisha nikaitua ile chupa mezani.
Nikanyanyua glasi nikapiga funda tano za maana hata nikahisi mwili mzima umepokelea!
Nikatikisa kichwa kwa nguvu kuondoka msisimko mkali wa pombe uliongia mpaka mashavuni.
Nilitua glasi mezani kisha nilichukua simu yangu na kuiwasha kioo, nilikutana na missed call siyo chini ya tano, simu ilikuwa silent ndiyo
maana sikusikia pindi inaita.
Missed call mbili zilikuwa za Amina, moja ya Erica na mbili kutoka kwa Shangazi.
Kuona missed call zile nilianza kujishauri je? Nipige au nipotezee?
Nilijiuliza zaidi ya mara tatu bila kupata jibu la moja kwa moja mwisho niliokota glasi kwa mara ya pili nikanywa na kuitua mezani tena.
Nilipotezea kwanza nikawasha data na kuingia facebook huko nilikutana na ujumbe mpya kwenye inbox.
“Mambo!”
Ulikuwa ni ujumbe uliosomeka hivyo.
Kwanza nilimwangalia huyo alienitumia ujumbe huo kama alikuwa hewani muda huo.
Yes alikuwa hewani, nami nikamjibu muda huohuo.
“Poa mzima?”
“Mi mzima… pande zipi?”
Alijibu muda huohuo.
“Nipo Iringa, vipi wewe uko wapi?”
“Mimi nipo Dar es salaam.”
“Ahaa! Sawa, nambie.”
“Samahani dada hiyo picha ni ya kwako?”
Aliuliza.
“Ipi?”
Nilimuuliza.
“Kwenye profile na ile nyingine uliyopost siku za hivi karibuni.”
“Ndiyo ni za kwangu.”
“Woow! Nice uko vizuri… Kama unaweza kufanya kazi za filamu karibu tufanye kazi pamoja kupitia sura yako unaweza kupata mafanikio makubwa sana kupitia uigizaji.”
Ujumbe ule ulinifanya nitulie kidogo, nilichokifanya niliingia kwenye profile yake nikakagua picha zake, kweli mkaka yule aliyeingia kwenye mtandao wa
facebook kwa jina la Erick Mdoe picha zake nyingi sana alipost akiwa amepiga na waigizaji maarufu wa tamthilia moja nzuri sana iliyokuwa imeshika umaarufu
karibu nchi nzima iliyofahamika kwa jina la Heart yaani moyo.
Siyo kupiga nao picha tu, Erick alionekana hata kwenye baadhi ya picha za jarada la tamthilia ile akiwa kama mhusika fulani.
Kuona vile haraka nilirudi inbox nikamjibu.
“Yes!… Napenda sana hiyo kazi na ilikuwa ni ndoto yangu.”
Nilijibu.
Haraka Erick alijibu.
“Kweli?”
“Ndiyo.”
“Ooh!… Basi uje Dar kuna tamthilia tunaiandaa, karibu tufanye kazi.”
“Sawa basi nipe muda kidogo nijiandae kisha nitakujulisha pindi nitakapoweka mambo sawa na kupanga safari ya kusafiri kuja huko.”
“Sawa.”
Tulihitimisha hivyo.
Nilitoka inbox nikaingia kwenye taarifa huko nilikagua kagua nikaona hakuna jipya nikatoka na kuingia WhatsApp.
Huko nilikutana na status za hapa na pale nazo nilizipuuza nikatoka ile nataka kufunga data nikaona simu ya video ikiingia kwa njia ya WhatsApp,
kuangalia nikaona mpigaji ni Samweli.
Nilipokea na kuiweka katika mkao wa kujirekodi video.
“Hallo Sam…”
“Nambie mrembo Leylah.”
“Safi naona upo apo kwenye bar ile niliyokunywa hadi nikazama eti?”
“Kama kawaida bata kama lotee.”
Alijibu Sam saa hiyo nikona watu waliokuwa pembeni yake wakinyonyana denda huku wakiwa na kila dalili za kutaka kufanya mapenzi hadharani.
Nilitabasamu.
“Kweli hata mimi naona!”
Nilimjibu.
“Naona umefanikisha yale malengo ee?”
“Ndiyo nimefanikisha dear.”
“Sawa, na kule usirudi tena.”
“Kule siwezi kurudi tena, nitaenda kufanyaje tena?”
“Yeah, halafu tutaonana ili tupange ni lini tutausafirisha huo mzigo.”
“Sawa.”
Wakati najibu sawa tayari niliona mtu kashika ukuta.
Duh!
Simu ilivyokata nilijikuta naingia na mawazo ya kutamani niwe kule aliko Sam nilitamani sana niwe kule tuwe na Sam tule bata pamoja
ila sasa mimi binafsi sikuwa na uwezo wa kwenda kule isipokuwa kwa nguvu zao.
Niliweka simu mezani nikaokota konyagi nikaifungua na kuimiminia yote kwenye glasi iliyokuwa imesalia kisha nilichanganya na castle lite nikaendelea kunywa.
Mawazo ya kuwa kule aliko Samweli yalizidi kuchukua nafasi kichwani hata sikujua ni kwanini nilitamani kuwa huko, niliendelea kuwaza hata baadae
nikajikuta uchangamfu ule wa unywaji ukapotea nikakosa hamu ya kuendelea kunywa tena nikatamani kwenda kupumzika tu.
Hata zile bia sikumaliza niliamua kuondoka zangu nikaenda chumbani huko nilipanda na nguo kitandani nikalala chali huku nikiisikia konyagi kwa mbali ikianza kunivizia.
Mara nilianza kuhisi kama usingizi fulani hivi tena siyo usingizi, ulevi siyo ulevi yaani kichwa kikawa kizito, mara nikajikuta nipo mjini natembea bila kuwa na mwelekeo.
Simu yangu iliita muda huohuo kuangalia niligundua mpigaji ni Sam.
“Abee.”
Nilipokea.
“Uko sehemu gani hapo?”
Aliuliza.
Nikaangaza macho yangu nikaona mnara mrefu umeandikwa blood tower mitaa nilipokuwepo.
“Nipo blood tower hapa.”
Nilijibu hivyo nikiamini kabisa lazima mtaa huo unaitwa hivyo.
“Blood tower kwa upande gani hapo?”
Aliuliza.
“Hapa barabarani natizamana na geti la kuingilia ndani ya uzio wa mnara huu.”
“Nimekuona, geuka nyuma yako utaniona.”
Sam aliongea hivyo,na ni kweli nilivyogeuka nilimwona akija kwa kutokea katikati ya majumba makubwa na marefu yalikuwa yamepangana katikati ya mji
ule ambao hata sikujua unaitwaje.
“Mambo Leylah.”
Alinisalimia Sam baada ya kufika kwangu.
“Safi mzima?”
Nilimjibu saa hiyo nikimpa mkono kwa maana ya kusalimia kwa kushikana mikono, nae aliupokea tukasalimiana kwa furaha.
Baada ya salamu na maongezi ya hapa na pale Sam aliniambia kuwa siku ile kulikuwa na sherehe kubwa sana kwao hivyo ilikuwa ni muhimu sana mimi na yeye kuihudhuria.
“Kwahiyo tunaenda saa ngapi?”
Niliuliza huku moyoni nikiwa na shauku kubwa mno ya kuishuhudia sherehe hiyo kwani licha ya kutowahi kuhudhuria wala kuona ila nilisikia viumbe wale
sherehe zao huwa ni kubwa sana.
“Sasa hivi tunaondoka.”
Alijibu Sam, na tuliondoka muda huohuo.
Tulitembea kwa mguu mpaka tunafika mahali palipokuwa na bar moja kuuubwa, nje ya bar hiyo ziliegeshwa gari za adabu sana za kutembelea.
Sam alinyoosha moja kwa moja mpaka kwenye egesho la magari, nikashangaa akifungua mlango wa Land Rover moja nzuri mno! Ilikuwa ni mpya na
toleo la kisasa kabisa tena usajili wa E, nikabaki nalitizama gari lile kwa matamanio.
Sam baada ya kuingia ndani ya gari aliliwasha na kuligeuza kisha akiliendesha taratibu mpaka nilipokuwepo, akalisimamisha mlango wa upande wa
pili ukajifungua wenyewe nami nikaingia huku nikiwa ndani ya mshangao wa kipekee kwa jinsi gari ile ilivyokuwa nzuri.
Nao mlango ukajifunga, nguu!
Safari ilianza, sikuwa najua ni wapi tunaelekea lakini nakumbuka mara ya mwisho niliona tunatoka kabisa nje ya mji ule ila kilichotokea mara ya mwisho ni
kwamba wakati safari inaendelea nilipitiwa na usingizi wa ghafla usingizi ambao sikujua hata ulidumu kwa muda gani? Kwani kuisha kwake uliisha pale
nilipokuja kuamshwa na Sam kuwa sasa tumefika.
Kufumbua macho nilishangaa kukuta tupo ndani ya ngome moja kubwa, ilikuwa ni ngome iliyozungukwa na ulinzi mkubwa, ulinzi ulioimarishwa na viumbe wa
ajabu kabisa wakiwemo misukule, mizuka na viumbe wengine wa kutisha sana wakiwemo skeleton wenye uhai.
Nakumbuka si mara ya kwanza kufika pale, ila si kwa kiasi cha kuwa mwenyeji, lakini sasa kilichonishangaza na kuniogopesha ni wale viumbe walinzi.
“Sam nini hiki?”
Nilijikuta nauliza swali lililotawaliwa na hofu wakati tupo ndani ya gari.
“Usiogope ni hali ya kawaida sana.”
Alijibu, mara milango ya gari ikajifungua yenyewe.
Pale wenye gari tuonekana ni sisi pekee, usafiri mwingine niliouona ni wa farasi pekee ambao niliwaona wakiwa wamefungwa sehemu wamewekewa na chakula.
Kitendo cha milango ya gari kufunguka nikashangaa kuona misukule yenye silaha za kutisha tisha wamefika na kulizingira gari letu, niliogopa mno nikamtizama
Sam huku nikimeza mate mepesi.
“Usiogope hao ni walinzi tu wamekuja kutuimarishia ulinzi… Tushuke.”
Bila kujibu chochote nilishukia mlangoni kwangu huku nikitetemeka mwili mzima.
Sam nae alishukia mlangoni kwake kisha alizunguka kuja kunichukua, milango ya gari ikajifunga yenyewe huku si tukiwa tunaondoka ilihali
tumeshikana mikono huku nyuma tukiwa tunafuata na kundi dogo la misukule wenye silaha.
Tuliingia mpaka ndani ya ngome ile kubwa huku tukisindikizwa na ulinzi nyuma mpaka tunaketi vitini, ni kweli siku ile kwa nchi ile kulikuwa na
karamu kubwa sana, na ndipo nilipokuja kugundua kuwa sikuwa peke yangu na wala sikuwa mtu wa kwanza kufika ulimwengu ule bali ulimwengu ule
ulikuwa umekaliwa na kutawaliwa na watu wenye nguvu kubwa sana kiuchumia kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Katika ukumbi ule niliweza kuwaona maelefu ya watu wakiwemo matajiri wakubwa sana duniani, wakiwemo pia watu maarufu na waliopendwa zaidi na
makundi ya watu duniani walikuwepo kule.
Ajabu sasa ndani ya ukumbi ule mkubwa kulikwepo na maskrini makubwa sana na yalikuwa yakiendelea kuonesha kama kawaida,tena nilishangaa hata kuona
habari kutoka baadhi ya vyombo vikubwa vya habari duniani zikirushwa kwenye runinga zile.
Pia mule ndani kuna agenda tuliikuta inaendelea, kiongozi mkuu na msimamizi wa mkutano ule kiumbe Soul aliekuwa kaketi kwenye kiti chake cha
kifalme ndani ya ukumbi akiendelea kuhutubia maelfu ya watu waliofika kuhudhuria sherehe zile zilizoambatana na mikutano mkubwa ndani yake.
“Nafikiri sasa tunaelekea kufika nusu ya lengo letu ingawa bado kuna vingine vingi sana kwenye njia yetu ya kufanikisha lengo lakini nina imani tutashinda tuuu!”
Ilikuwa ni sauti ya kiumbe Soul, nao ukumbi mzima ulilipuka kwa yowe la furaha huku wengi wakiunga mkono kwa kusema,
“Ndiyo mkuu… lazima tushinde tena kwa kishindo.”
Kiumbe yule alicheka.
“Hahahaha!”
Kisha aliendelea kuongea.
“Tutatengeneza pombe mpya yenye chembechembe za madawa ya kulevya ndani yake, pombe itakayopendwa sana na vijana pindi itakapoingia kwenye
soko la dunia la pombe, tutaweka sumu ya kulegeza viungo kwenye pombe hii kila atakaekunywa jioni basi siku ya pili lazima aamke saa
tatu au saa nne huko hii itapelekea vijana wengi kuharibika, nguvu kazi itashuka na umaskini utaingia hapo ndipo hapo tutakapoingizia mpango wetu…
Nina imani tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani vijana watakuwa na uhitaji mkubwa wa pesa lakini hawatakuwa na uwezo wa kuzitafuta kwa jasho hivyo ni
lazima sera yetu ipite kwa mafanikio makubwa na huo utakuwa ni mwanzo wa kuiteka dunia hahahaaha!”
Kama alivyoanza na kicheko ndivyo hivyo pia alimalizia na kicheko kiumbe yule alieketi juu ya kiti cha kifalme.
Ukumbi wote ulilipuka kwa makofi na vifijo, huku mimi nikibaki nimeduwaa kama sanamu hadi pale Sam aliponishitua na kofi la mgongo.
Unaweza pia kusoma: