Dunia Ya Pili - 19
Nilikuja kuzinduka siku ya pili asubuhi nikiwa hospitalini Government hospitali ambayo pia ni ya rufaa kwa mkoa wa Iringa.
Baada ya kufumbua macho nilimwona Sam pembeni yangu wakati huo pia nikiwa nimefungiwa dripu mkononi.
Sam alikuwa kavalia sare zake za kazi kama ilivyokawaida yake kwa siku mojamoja.
“Sam…”
Nilimwita sababu alikuwa ametingwa na simu yake.
“Naam… Haa! Umezinduka mke wangu? Vipi unajiskiaje?”
Alikuja na maswali mfululizo huku akiweka simu kando akanisogelea karibu zaidi.
“Najiskia vizuri, halafu vipi imekuwaje nipo hapa?”
“Skobe!”
Alitaja tu hilo jina, nikagundua nini maana yake.
Kwanza mwili ulisisimka msisimko wa aina yake, nilihisi hasira sana hata sijui kwanini lakini nilitamani tu kuona mwanaume yule akiwa
kapotea duniani tena kwa kupigwa risasi na mkono wangu.
“Mlimkatamata?”
Nilimuuliza.
“Hapana, hatukuweza kumkamata kwani kama ilivyokuwa mwanzo ndivyo ilikuwa mara ya pili tena!
Alitoroka kwa namna ileile…
Mbaya zaidi alikuwa amekwisha kuchoma sindano yenye sumu kali ndiyo maana tulighairi kuendelea kumfukuzia ikabidi tutumie gari yetu kukukimbiza hapa hospitalini.”
“Shiit… mkoba wangu?”
“Bahati nzuri sana mtu wa kwanza kumfikia nilikuwa mimi huenda nilifika ndani ya muda wake, kwani pindi anajiandaa kutoroka nilimpunyua na risasi
kwenye koti mkoba ukamponyoka akiwa katika harakati za kujibu shambulio kwa lengo la kujitetea.”
Nilishusha pumzi huku kichwani nikiwa na maswali mengi sana juu ya mwanaume yule, nilijiuliza sana ni nini anakitaka kwangu?
Je, ile sumu ni sumu gani aliyonidunga? Halafu katika kumbukumbu zangu sindano ya aina ile si mara moja kuona ni mara mbili sasa nanusurika
kuchomwa au kuwekewa kwenye kinywaji sumu hiyo, sasa nikawa najiuliza ni sumu gani ile na ilikuwa na lengo gani kwangu?
Nilijiuliza pasipo kupata jibu.
“Sasa ni sindano gani niliyochomwa na ni kwaajili gani nilifanyiwa hivyo?”
Nilimuuliza Sam.
“Hata mimi sijui lakini ni sumu yenye kuleta usingizi kwa mujibu wa vipimo, hata hivyo madaktari walijitoa kwa kiasi cha
kutosha sana kwako hadi ukarudi kwenye hali yako ya kawaida ni jambo kubwa sana wamelifanya.”
Kufuatia maelezo yale nilikosa cha kuongea nikatulia kuupa nafasi ubongo kutafakari.
“Hii sindano ni ya nini?”
Ni swali lililotembea akili zaidi ya dakika kumi.
Nilimkumbuka yule mwanaume aliesadikika kufa palepale Miami na hakufahamika alikuwa ni nani?
Zaidi ya kujua kuwa ni mfanyakazi TANROAD kwa mujibu wa vyeti vyake lakini cha ajabu hata baada ya kifo chake hata fununu tu hazikutoka alipotea
kimyakimya nae alikuwa na hiyo sindano na alinusurika kunidhuru kwenye kinywaji bahati mbaya kwake nilimshtukia mapema.
Mara ya pili ni kule Mwangata wakati nilipokunywa nikalewa hata nikaanza kucheza na kijana mchafu na mvuta bangi akataka kujimegea tunda
nilivyoshituka nikamkataa kwa nguvu akatoa sindano hiyo nikawahi kuiona nikapiga yowe, kijana Farid alipojitoa mhanga kunitetea akadungwa
mwenyewe baadala yangu na tangu hapo sikujua hali yake hata leo.
Hatimae mara ya tatu Skobi anafanikiwa kunidunga sindano ile… sasa nikawa najiuliza ni sindano ya nini ile?
“Hapanaaa!
Sikubali ni lazima nimsake Skobe kivyovyote vile ikiwezekana hata kwa njia ya mapambano ni lazima nimsake ataniambia tu ile sindano ni ya nini?”
Nilijisemea kimoyo moyo.
“Kwanini unataka upambane na mtu usiyemfahamu?”
Nilishangaa sana kusikia Sam akiniuliza kwa sauti, nilishangaa!
“Kwani nimesema nataka kupambana na mtu?”
Nilimuuliza ilihali nikiwa katika hali ya taharuki.
“Si umesema ni lazima umsake Skobe kivyovyote vile? Sasa wewe polisi tunashindwa kumkamata wewe pekee yako uweze?”
“Wewe Sam kwani nimeyasema saa ngapi hayo?”
Nilimhoji huku nikirudisha kumbukumbu nyuma nikafatisha mazungumzo hayo mpaka kipengele tulichofikia lakini sikukumbuka kama hilo
nililiongea kwa sauti zaidi ya kujiongelea tu kimoyomoyo nalo lilikuwa kama wazo tu.
“Hivi Leylah siku hizi una mawazo gani? Halafu ujue wewe bado mtoto mdogo sana mbona unakuwa na mawazo mengi hadi yanakuchanganya ubongo hadi
unakuwa msahaulifu kiasi hicho? Kitu unaongeza na unakikana mwenyewe?”
Yaani nilishindwa kumwelewa Sam hata hivyo sikutaka tena kubishana nae nikampotezea kabisa.
Nayo ikawa imetimia saa mbili na dakika arobaini asubuhi, jua nalo likawa linapanda taratibu nayo joto ikawa inaongezeka taratibu huku nayo ile baridi
sumbufu mwilini ya nyakati za asubuhi ikawa inauaga taratibu mkoa wa Iringa.
Muda huo Sam aliondoka na kwenda kumwita muuguzi mmoja ambaye punde si punde alifika na baadhi ya vifaa vya kupimia afya, basi akanipima pima pale
akaniruhusu niondoke maana kwa mujibu wa vipimo vya afya vilionesha sasa mwili wangu umetengemaa.
“Sasa dokta hii sumu ambayo nimechomwa ni sumu gani kwani hamjaweza kuibaini?”
Nilimuuliza muuguzi yule wakati hatujaondoka.
“Ile haikuwa sumu… bali kwa mujibu wa vipimo vya afya imebainika kuwa ile ni dawa ya usingizi ambayo haijathibitishwa na mamlaka husika
zinazosimamia mambo ya madawa hivyo dawa ile ni haramu inayotengenezwa vichochoroni kwaajili ya kuwasaidia wahalifu katika kazi yao,
dawa ile ni kali sana na ina asili ya sumu iwapo mtu atadungwa sindano hiyo dawa ikiwa imezidi basi akilala anaweza kulala moja kwa moja.”
“Toba!”
Nilishituka.
“Ndiyo hivyo lakini kwa sasa ndugu nani?”
“Leylah…”
“OK ndugu Leylah kwa sasa mwili wako uko safi kabisa hivyo kuwa na imani.”
“Asanteni sana ndugu zetu mwenyezi Mungu aendelee kukulipa kwa kazi yako nzuri ya kunusuru watu kwenda kwenye mauti.”
“Amina!.. Tupo pamoja.”
Basi tukiwa na Sam tuliondoka ndani ya hospitali hiyo kwa kupitia njia ya gerezani.
“Leylah kwa sasa hivi mimi bado nina majukumu ya kikazi hivyo natakiwa kuelekea kituoni.”
“Kwahiyo?”
“Nafikiri jioni tutaonana, kwani we una ratiba gani leo?”
“Leo najiandaa na safari ya Dar es salaam si unajua tena? Ninatakiwa kufika kule mapema kwa sababu nina kazi nyingine pia.”
“Sawa… Fanya maandalizi halafu tusisite kuwasiliana.”
“Sawa.”
Tulishafika maeneo ya kituoni hivyo tuliachana pale, Sam aliingia kituoni huku mi nikipitiliza mpaka Miyomboni madukani.
Nikiwa huko nilichagua nguo nyingi nzuri na za kila aina, nikanunua begi kubwa la magurudumu kisha zile nguo nikazipanga zote
kwenye begi kisha nilipiga kiasi cha shilingi laki nne na nusu nikajikuta nimebakiwa na hela kidogo sana halafu sikuwa nimekamilisha
mahitaji yote hivyo ilibidi nimtafute wakala wa huduma za kibenki haraka sana nikatoa kiasi cha shilingi milioni moja na nusu kisha
nikazichimbia mkobani, hapo nikatafuta duka la viatu.
Huko nilinunua siyo chini ya pea tano za viatu vipya vilivyogharimu kiasi cha shilingi laki tatu.
Hapo nikawa nimeridhika sasa, kilichofata sasa nilikodi tax iliyonikimbiza moja kwa moja katika ofisi za mabasi ya kampuni ya Majinjah Express
zilizopo Iringa mjini stendi ya zamani.
Huko nilikata tiketi ya kuondoka na basi la kwanza kabisa la asubuhi siku inayofata, nililipia nauli nikakatiwa tiketi yangu kisha mizigo nikaiacha pale ofisini.
Nayo ikawa imetimia saa nne na dakika hamsini asubuhi, yaani ilikuwa saa tano kasoro dakika kumi asubuhi.
Nilitoka ofisi zile muda huo nilianza kuhisi njaa hivyo ilibidi nitafute sehemu ambayo ningeweza kupata kifungua kinywa.
Nilipaona.
Nikachepukia hapo, ilikuwa ni sehemu nzuri kiasi, ilivutia sababu supu ilikuwepo ya kila aina na vitafunwa tele.
“Niletee supu nzito na chapati tatu.”
Niliagiza pindi mhudumu amefika kunisikiliza.
Nilihudumiwa kama nilivyoagiza nikapata kifungua kinywa njaa ikatulia.
Nilinawa mikono kisha nilitoka sehemu ile.
Nayo ikawa imetimia saa tano na robo, nilipotoka sehemu ile nilitoa simu yangu na kumpigia Erick.
Simu iliita mara mbili ikapokelewa!.
“Hallo!”
“Habari ya asubuhi.”
“Poa mzima?”
“Mi mzima hofu kwako.”
“Safi habari za Iringa.”
“Njema habari za Dar es salaam huko.”
“Huku pia kwema.”
“Sawa… Sasa Erick kesho nakuja Dar.”
“Haa! Unasema kweli?”
“Ndiyo!”
“Waoo! Karibu sana ni wakati mzuri mno! Utawahi hivyo hata kazi utaichukulia uzoefu mapema karibu sana.”
“Sawa, na ndicho nilichokuwa nakutaarifu hicho.”
“Aah.. haina shida, mawasiliano yawepo kwa kila hatua ili pindi utakapowasili stendi nije kukupokea.”
“Sawa.”
Mazungumzo yalifika tamati nikakata simu saa hiyo nikiwa nimerejea tena eneo la stendi ya zamani Iringa mjini.
Nayo ikawa imetimia saa tano na nusu, wazo la kulewa likanijia!
Pale pale niliita bodaboda.
“Nikimbize Serengeti bar.”
“Elfu tatu kutoka hapa.”
“Twende.”
Niliikumbuka Serengeti bar kwani ni siku nyingi kidogo nilikuwa sijaitembelea bar hiyo na cha kushangaza zaidi nilipendelea sana kunywea
baa za Mlandege na si sehemu nyingine sijui ni kwanini?
Kutokana na mwendo wa mwendesha bodaboda kuwa wa kasi kidogo tulitumia dakika tano tu kutoka Iringa mjini mpaka Mlandege mahali ilipokuwepo bar yenyewe.\n
Nilishuka nikamlipa dereva bodaboda ujira wake akaondoka zake kisha mimi nikaingia zangu bar.
Nilikuta ndiyo kwaanza wahudumu wameanza kufanya usafi na hakukuwapo na mteja hata mmoja.
Licha ya wao kuwa kwenye majukumu ya usafi mimi sikujali niliingia na kutafuta sehemu ambayo tayari imeshafanyiwa usafi na kupangwa viti vyema nikaketi huko.\n
Punde si punde mhudumu alifika kunisikiliza.
“Niletee Castle Lite bando tatu.”
Niliagiza, siku hii sikutaka kulewa mapema.
Kama nilivyoagiza ndivyo nilivyohudumiwa, Castle zilifika nikaanza kuipunguza ya kwanza.
Kwa sababu nilijua siku inayofata nina safari na inatakiwa simu iwe hewani, nilichukua chaja yangu kutoka kwenye mkoba kisha nikaichomeka kwenye
soketi iliyokuwa ukutani palepale nilipoketi.
Nilichomeka simu yangu ikaanza kupeleka chaji nikaiweka mezani kisha nikaendelea kunyonya mtungi.
Namna Skobe alivyoingia mule ndani sikuelewa ila nilishangaa namuona anatembea ndani ya ukumbi wa bar hiyo, tena alivyoniona ndiyo
akanyoosha kuja kwangu huku akitabasamu.
Mwili mzima ulinisisimka hadi nywele..!
Taratibu nilisogeza simu yangu karibu zaidi kisha nikaupapasa mkoba wangu uliokuwa mapajani sababu ilikuwa desturi yangu
nikiketi basi mkoba nausukumia mapajani.
Taratibu nikapapasa mahali ilipo zipu nikaishika na kutulia.
Alifika!
“Oohw! Leylah!”
Huku nikimtizama usoni nikamjibu.
“Vipi?”
“Poa mzima?”
Alijibu huku akivuta kiti akasogea na kuketi meza niliyoketi mimi.
Wakati huo mimi niliwaza kuwa iwapo angefanya chochote cha kunishtua tu! Angekutana na shaba ya kichwa.
“Mi mzima!”
Nilimjibu saa hiyo nikifungua zipu ya mkoba taratiiiiiiibu! Lengo langu niishike bastola iliyokuwa ndani ya mkoba.
“Aah! Samahani kwa kile kilichotokea jana! Kifupi nina uhasama mkubwa na jeshi la polisi tena ni uhasama mkubwa sana lakini wao
kunikamata si rahisi… Lakini nisamehe nilifanya vile kujihami kwani ningechelewa hata wao wangenifyatulia risasi.”
Aliongea akaweka kituo.
“Lengo la kukutafuta ni kukuomba msamaha kwa kile kilichotokea, kuomba kampani kwako baadae nikakutishia usalama tena! Nisamehe kwa hilo.”
Sikumjibu chochote sababu kila nilivyozidi kumtizama nilizidi kuchafukwa.
“Skobe!”
“Naam.”
“Kwa usalama wako naomba uondoke mara moja kabla mambo hayajawa mabaya kwako.”
“Leyl…”
“Ondoka tafadhali.”
“Lakini tunaw…”
“Skobeee!”
Nilimtolea bastola nikamwonesha mara moja kisha nikaificha kabla wahudumu hawajaiona, nikabaki namtizama kwa jicho
kali kutokana na hasira nilizokuwa nazo juu yake.
Licha ya kumwonesha bastola baada ya kushituka alitabasamu kana kwamba kaona mrembo wa kuvutia na si chombo cha mauti.
Unaweza pia kusoma: