Dunia Ya Pili - 32
“Mbona uso wako umeonesha mshtuko mkubwa sana kwanini?”
Nikampa swali lingine angali bado kadata!
“No! Lakini ile haikuwa dawa ya usingizi.”
“Sasa unakataa nini wakati nilizidiwa na usingizi mzito?… Jr nachukia sana uwongo ujue!”
Nilimwekea ukauzu kidogo.
Alianza kuogopa!
“Lakini nakupenda Leylah.”
“Kubali dawa ya usingizi umeniwekea au haujaniwekea?… Nataka jibu na siyo maelezo.”
Akababaika.
Nilimtizama muda mreeefu nikajikuta naanza kupatwa na hasira ikabidi haraka nipotezee kuhusu ile mada nikaitoa kabisa moyoni kwani
niliona ninaokoelekea siyo kuzuri shetani alianza kucheza kwenye fikra zangu.
Ila sasa cha kushangaza wakati nafikiria kupotezea yale nilimwona Jr akiniangalia kwa makini sana usoni.
“Hivi mbona unapenda kuniangalia sana usoni kwangu?”
Nilimuuliza.
Akatabasamu!
“Ni kwa sababu ni mrembo sana ndiyo maana napenda sana kukutizama!”
Alijibu!
“Muongo huyo!”
Ghafla kuna sauti ilipiga akilini mwangu nikashituka na kujipa utulivu nisikie akili yangu inaniambia nini kuhusu mtu huyu?
“Anakuchota tu huyo tena ni jasusi na ni haka mkubwa!”
Nilitetemeka mwili mzima! Sikujua mawazo yale yalitokea wapi?
Niliinua macho nikamtizama tena Jr usoni nikashangaa yeye ndiyo kwaanza katulia ananitizama huku macho yake yakiwa yameanza kulegea sababu ya pombe.
“Mbona unawaza sana mrembo?… Sema nini usiwaze usiku sijakufanya chochote isipokuwa asubuhi napo kwa idhini yako, najua huwezi kuamini lakini huo
ndiyo ukweli kutoka moyoni mwangu Leylah naomba uniamini.”
Aliongea huku macho yakionekana kutia huruma sana, ni kweli Jr hakunifanya kitu usiku ule isipokuwa asubuhi, ila nilimtisha ili asinizoee
kingine nilitaka nijue adhimio lake haswa kuniwekea dawa ya usingizi kwenye kinywaji.
Hata hivyo baada ya kuelewa sikutaka kufanya mazungumzo kuwa marefu zaidi niliamua kuyatafutia njia yapuuzwe ili tuelelee na mada zingine.
“Nimekuelewa Jr lakini basi ninaomba ukiongeacho kiwe endelevu isiwe unaongea kutoka kinywani halafu ukasingizia kuwa yanatoka moyoni.”
“Dah!…Sijui nisemaje… Hivi unajua nini? Masikio yangu yanagoma kuamini kuwa yamesikia maneno haya kutoka kwako!”
“Kwanini?”
Akashusha pumzi...
Inavyoonekana alikuwa na mengi sana ya kutililika hivyo nami nikamwachia uwanja baada ya kuona muda unaruhusu.
Aliongea mengi sana kuhusu mahusiano kadhaa aliyoyapitia pamoja na changamoto alizopitia jambo lililopelekea azame kwenye pombe baada ya kuona mapenzi
sasa hayana maana zaidi ya miumizano tu!
Nikamuuliza kwanini?
Kwani wazazi wake wapo wapi?
Alijibu kuwa mama yake yuko Mvumi Dodoma wakati huo baba yake yuko Kilombero ya Morogoro.
Huku akielezea jinsi ndoa ya wazazi wake ilivyovunjika baada ya baba yake kupata kazi kwenye kiwanda cha sukari huko Kilombero kisha akaoa mwanamke
mwingine wa kirugulu halafu akamtelekeza mama yake Jr.
Alielezea mengi mno! Alielezea jinsi alivyoanza kutafuta maisha kwa kufanya kazi migodini kisha akakutana na wanawake kibao pindi yuko na pesa
nyingi sana za madini na jinsi wanawake hao walivyopotea pale alipoacha kazi ya uchimbaji na kuamua kufanya mishe zingine.
Hii kwa sababu alikoswa kufukiwa na kifusi cha mgodi ajali iliyoua jamaa zake wote.
Alisema baada ya mgodi huo kuvuja box karibu kumi na moja kisha kujifukia na kuua zaidi wachimbaji themanini huku Jr akiwa moja kati ya
manusura watatu waliokoswa na ajali hiyo.
Serikali ilifunga mgodi kisha Jr aliondoka na kutimkia Iringa kwa mara ya kwanza kabla ya kwenda Njombe, Mbeya kisha baadae Dar es salaam.
“Sasa hao jamaa zako walifukuliwa wakazikwa au ilikuwaje?”
Nilimuuliza.
“Ndiyo japo mi niliondoka siku ya pili, niliacha shuguli ya ufukuaji inaendelea kwaajili ya kuopoa maiti zilizofukiwa na kifusi.”
“Dah! Pole, lakini pesa si ulikuwa nayo?”
“Nilikuwa na pesa nyingiii saaaana! Kumbuka wakati mgodi unavunjika nilikuwa nje nimetoa mchanga wa madini sasa baada ya ajali ile vumbi kubwa
sana lilitimka eneo lile. Watu wakusanya ushuru pamoja na wanunuzi wa huo mchanga wa madini wakajivuta papo hapo nikatorosha viroba viwili
vya mchanga nikaenda kuficha kisha usiku niliosha mchanga huo lengo likiwa ni kupata madini kidogo ili niuze siku ya pili niweze kutimka zangu,
ndipo kwa bahati iliyoje katika kile kiroba cha kwanza nikakutana na vito vitatu vyenye thamani ya pesa ndefu sana! Niliuza kimoja kwa bei ya
shilingi milioni sabini ikiwa ni bei ya hasara mno! Ndipo nikatimkia Iringa kisha Njombe, baadae Mbeya hatimae huku Dar.”
“Sasa hizo pesa ulipeleka wapi?”
“Siyo hizo tu! Madini yote niliyofanikisha kutorosha kule mgodini niliuza na pesa zote ziliisha sababu ya…”
Alishindwa kumalizia anaangalia pembeni ni dhahiri machozi yalianza kujitokeza kwenye kope zake.
“Pole sana lakini ni changamoto tu kikubwa ujue ni nini unafanya ni wapi unaenda, kosa la kwanza siyo kosa ila kosa ni kurudia mara ya pili hayo huenda
yalikuwa ni matokeo tu ya balehe yako.”
Nilimfariji saa hiyo nikiokota glasi ya pombe nikanywa!
Nae aliokota yake akainywa mfululizo kisha alitia glasi mezani kwangu hata ikatoa mlio!
“Utapasua glasi ya watu wewe!”
Hakunijibu aliishia tu kutizama pembeni huku akichezea mdomo wake.
Kwa upande wa muda ilishatuma saa moja na dakika saba jioni,mataa yalianza kuwaka kila kona ya mji kiufupi usiku ulianza kuingia!
“Leylah kwahiyo tunarudi Ubungo au?”
Aliniuliza.
“Yaah! Ni lazima turudi nilikopanga.”
“Kwahiyo tunaondoka muda gani?”
“Kwani we unaishi sehemu gani?”
“Huko huko japo mitaa tofauti na pia kuna umbali kidogo.”
“Kuna kipi cha muhimu zaidi? Kodi umelipa ya muda gani?”
“Vya kisela tu! Kodi umebaki mwezi mmoja.”
“Kwani ukivitelekeza?”
“Labda begi”
“Tupitie tukalichukue.”
“Sawa.”
“Lakini tule mitungi kidogo mke wangu jamani…Nakupenda wewe?”
Niligundua keshaanza kulewa huyu.
Ili alewe vizuri niliagiza konyagi kubwa na vichanganyio!
Tulikunywa mpaka mzinga unakata ilishatimu saa mbili na robo.
“Tuondoke zetu!”
Aliongea Jr huku akiyumba yumba!
“Nyie si mlale tu mtaodoka kesho.”
Aliongea meneja wa bar hiyo.
“Hakunaa! Twende zetu mke wangu… Halafu huyu simbilisi mbona simuelewi eti? Au ndo chawa?”
“Wewe hebu twende zetu… Kaka samahani tunafika.”
Yule meneja hata hakujibu ni wazi alikasirishwa na maneno ya Jr yaliyokuwa yamejaa kila aina ya shombo.
Tulitoka Jr akang’ang’ania kuendesha gari, nami nikamwachia!
Akalitia moto hiyo rivasi yake sasa nusura agonge magari ya watu.
Lakini hakugonga!
Akakaa vizuri akafunga mkanda!
Barabara akaiona, muda mfupi tukawa barabara kuu alitembea sipidi kali mpaka nikaanza kuogopa, tulivyofika sehemu ambayo sikufahamu
alichepuka akaingia Barabara fulani ya uchochoro huko alizidi kutembea mwendo mkali utafikiri jambazi anaefukuziwa na polisi.
Mara mbele tuliona watu watatu wakiwa wameshikana mibega huku wakitembea wakiyumba mithili ya walevi waliozidiwa na pombe!
Jr akawatizama kwa makini, kitendo tunataka kuwapita wale wawili wa pembeni ghafla walisukuma mwenzao wa kati kati ili aangukie
barabarani tumgonge!
Jr akawahi kuwashitukia!
Aliyumba kwa nguvu upande wa pili hadi nikama siti! Mara kishindo kikasikika!
“Tiiii…”
Unaweza pia kusoma: